Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 9/8 kur. 4-7
  • Kutafuta-Tafuta Kusudi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutafuta-Tafuta Kusudi
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutafuta-Tafuta Kusudi
  • Ni Nini Hufanya Uhai Uwe Wenye Kusudi?
  • Kufadhaika na Kutamaushwa
  • Nani Awezaye Kutuambia?
    Ni Nini Lililo Kusudi la Uhai?
  • Kufuatia Kusudi Lenye Maana Maishani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kusudi Lenyewe la Uhai
    Amkeni!—1992
  • Je! Uhai Una Kusudi?
    Ni Nini Lililo Kusudi la Uhai?
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 9/8 kur. 4-7

Kutafuta-Tafuta Kusudi

TANGU wakati wa Charles Darwin, kumekuwako na msongo mkubwa mno kutoka kwa wanabayolojia wa kuweza kukubali wazo la kwamba kwa sababu ya mageuzi, maisha kwa msingi hayana kusudi. Hata hivyo, wengi hukataa hilo kisilika. Wenzi wawili wachanga waliooana, wanaotazama mtoto wao mwenye uzuri aliyetoka tu kuzaliwa, wangeliona kuwa jambo gumu kuamini kuwa uhai huu mpya hauna kusudi. Kwa hao, ni muujiza, ni ajabu inayofanya maisha zao kuwa zenye maana na zenye kuridhisha.

Hata baadhi ya wanasayansi hawakubali kwamba uhai ni aksidenti isiyo na maana. Kwa nini sivyo? Kwa sababu ya yale The Encyclopedia Americana huita “kiasi cha kustaajabisha sana cha utata na utaratibu katika viumbe vinavyoishi.” Americana huendelea kusema: “Uchunguzi wa makini zaidi wa maua, wadudu, au mamalia huonyesha mpangilio hususa wa visehemu mbalimbali ulio wa kustaajabisha.”

Kwa kufikiria utaratibu huo ulio tata na wenye uzuri—ambao huonekana hata katika viumbe sahili zaidi—mwanasayansi wa Afrika Kusini Dakt. Louw Alberts alinukuliwa na gazeti Cape Times akisema: “Mimi hupata uradhi zaidi wa kielimu kwa kukubali kwamba kuna Mungu badala ya kukubali tu kwamba huo [uhai] ulitokea kwa nasibu tu.” Akizungumzia mfanyizo wa kikemikali wa viumbe vilivyo hai, mstadi wa elimu ya nyota Mwingereza Sir Bernard Lovell aliandika: “Uwezekano wa . . . tukio la kinasibu linaloongoza kwenye mfanyizo wa molekyuli ya proteni iliyo duni sana ni mdogo mno. . . . Hasa haiwezekani.”

Akiwa na wazo hilo hilo, mstadi wa elimu ya nyota Fred Hoyle aliandika: “Muundo mzima wa biolojia sanifu bado hushikilia kwamba uhai ulitokea kwa nasibu. Hata hivyo wanabiolojia-kemia wanapovumbua zaidi na zaidi utata wenye kustaajabisha wa uhai, ni wazi kwamba uwezekano wao kuwa ulitokea kwa aksidenti ni duni sana hivi kwamba waweza kukataliwa kabisa. Uhai haungeweza kuwa ulianza kwa nasibu.”

Hilo linamaanisha nini? Ikiwa uhai haukutokana na aksidenti, lazima uwe ulitokana na ubuni. Na ikiwa ndivyo, lazima uwe ulikuwa na Mbuni. Na lo! yeye ni Mbuni aliyeje! Mtunga Zaburi alisema vema hivi: “Nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.” (Zaburi 139:14) Lakini hilo latuambia nini kuhusu kama uhai una kusudi au la?

Wanadamu pia hubuni na kufanyiza vitu. Wao hufanyiza eropleni. Hufanyiza vituo vya kusafisha mafuta. Hufanyiza vituo vya kutokeza nguvu za umeme. Na hufanyiza vitu vingine vingi vya muundo tata zaidi au usio tata sana. Lakini wanadamu hawabuni na kujenga vitu tata bila sababu. Kila kitu hufanyizwa kwa kusudi fulani akilini.

Kwa kuwa hakuna kitu kilichofanyizwa na wanadamu ambacho hata hukaribia kuwa sawa na viumbe hai walio tata na wenye kustaajabisha, bila shaka Mbuni wa uhai hangeumba uhai bila kusudi fulani kwao. Ni kukosa kutumia akili vizuri kuamini kuwa ‘tuliumbwa kwa jinsi ya ajabu’ kisha tukaachwa bila mwongozo na mwelekezo na bila kusudi.

Kutafuta-Tafuta Kusudi

Kwamba Muumba aliumba wanadamu ili atimize kusudi fulani huungwa mkono sana na jambo la kwamba sisi wanadamu hutafuta kwa kisilika kusudi la uhai wetu. Msaikolojia Gilbert Brim, alizungumzia uhitaji wa kisilika wa mwanadamu kupata kusudi aliposema: “Watu wengi hupata fursa ya usitawi na shughuli ya kibinafsi yenye kupendeza mahali pao pa kazi. Lakini wale wasiopata hayo hutafuta-tafuta uchocheo wa kipekee katika shughuli ziwapendezazo na uradhi kwingineko: kupunguza uzani wao, kuwa stadi wa mchezo wa gofu kwa kuupiga mpira wakiwa kwenye sehemu iliyoinuka, kufanyiza andazi la mayai (kimanda) lililo bora kabisa au kufuatilia mambo ya kusisimua—iwe ni mchezo wa kubembea hewani kwa tiara au kujaribu vyakula vipya.” Viktor Frankl, daktari wa akili hata alidai: “Jitihada ya kutafuta maana ya uhai wa mtu ndiyo kani ya msingi yenye kuchochea katika binadamu.”

Ebu tuchunguze baadhi ya miradi ambayo watu hujiwekea maishani.

Ni Nini Hufanya Uhai Uwe Wenye Kusudi?

Tineja mmoja mchanga, alipoulizwa kuhusu kusudi lake maishani, alijibu: “Ndoto yangu ni kupata tu nyumba yangu nzuri, gari zuri, na mvulana rafiki wa kuandamana nami kwenye gari. Mimi nitatimiza tamaa zangu mwenyewe. Mimi hupendezwa na ‘mimi binafsi’ kwa hiyo ninakuwa wa kwanza maishani. Ninataka yale yatakayonifanya niwe mwenye furaha, si yale yatakayofanya jumuiya nzima iwe yenye furaha.” Ikiwa wafikiri kuwa hilo lasikika kuwa ubinafsi, haukosei. Ni kweli. Hata hivyo, ni sikitisho kwamba mwelekeo huo ndio wa kawaida.

Hata hivyo, je! kufuatia tu vitu vya kimwili na anasa huridhisha uhitaji wa kuwa na maana maishani mwa mtu? La. Anasa inapokuwa ndiyo tu kusudi letu, inakosa kuridhisha. Watu mmoja mmoja wanaoifanya iwe mradi wao wa pekee maishani mara nyingi hujipata baadaye wakirudia moyoni mwao maneno ya mfalme mwenye utajiri wa nyakati za zamani aliyetumia uwezo na utajiri wake kufuatilia namna mbalimbali za anasa zilizopatikana wakati huo. Sikiliza mkataa aliofikia:

“Tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana. . . . Na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo.”—Mhubiri 2:8, 11.

Wengi hupata uradhi katika kazi-maisha au kwa kutumia uwezo wao wa akili au wa kimwili kutimiza ile inayoonekana kuwa miradi inayostahili. Hata hivyo, baada ya muda, kazi-maisha hairidhishi kikamili uhitaji wa kuwa na kusudi maishani. Peter Lynch, aliyeelezwa kuwa “bingwa wa kuweka dhamana kwa kampuni,” aliacha kazi-maisha yake yenye ufanisi alipogundua kuwa kitu fulani kilikosekana maishani mwake. Kitu gani? Uhusiano wake na familia yake. Yeye alikiri: “Nilipenda yale niliyokuwa nikifanya, lakini nilifikia mkataa, na ndivyo na wengine kadhaa: Haya yote . . . tunayafanya kwa ajili ya nini? Mimi sijasikia mtu yeyote ambaye, akiwa kitandani akikaribia kufa, alitamani kwamba afadhali angetumia wakati zaidi ofisini.”

Hivyo, msichana mmoja tineja alionyesha kadiri fulani ya usawaziko alipofikiria miradi yake maishani na kusema: “Moja kati ya ndoto zangu ni kuwa na kazi-maisha. Lakini ninafikiri kwamba ndoto yangu kubwa ni kuwa na familia yenye furaha.” Ndiyo, familia yetu yaweza kufanya uhai wetu uwe na maana na kusudi. Mwanamke mmoja mchanga aliyeolewa alisema: “Mapema sana maishani mwangu niliona kule kuwa mzazi ni jambo moja kati ya mengine ambayo mtu alizaliwa ayafanye, na ni moja ya makusudi ya uhai, na huwa sina shaka juu ya hilo.”

Wengine hutafuta kusudi la uhai katika mambo mengine. Wengine—sana sana kutia ndani wanasayansi wanaodai kuwa uhai ni aksidenti isiyo na maana—hutafuta kusudi katika kufuatilia maarifa. Mwanamageuzi Michael Ruse aliandika: “Tuna kiu cha kupata ufahamu, na hilo hutufanya tuwe bora zaidi ya wanyama. . . . Kati ya mahitaji na wajibu wetu ulio mkubwa sana ni ule wa kuwapitishia watoto wetu maarifa mengi ya wakati uliopita, pamoja na furaha yetu na matimizo yetu. . . . Tamaa ya maarifa, na mafanikio, hufanyiza moja ya tabia zenye kutokeza zaidi katika asili ya binadamu.”

Wengine hupata kwamba kufanya jitihada katika kutegemeza kanuni fulani hufanya uhai wao uwe na kusudi. Wao hujitoa kwa uhifadhi wa jamii ya wanyama wasio rahisi kupatikana. Au wanapinga uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Watu wenye kujali hutetea haki za watoto au hujitoa kwa ajili ya wale wasio na makao au walio maskini. Au hujitoa kukinza mweneo wa uzoevu wa dawa za kulevya. Watu mmoja mmoja kama hao wakati mwingine hutimiza mambo mengi yaliyo mazuri, na yale wafanyayo hufanya uhai wao uwe wenye kusudi.

Kufadhaika na Kutamaushwa

Hata hivyo, ni lazima tukubali kwamba wanadamu hufadhaika mara nyingi katika kufuatilia kwao miradi hata ikiwa miradi hiyo inastahili. Wazazi wanaotoa upendo mwingi na kufanya jitihada katika kulea watoto wao wakati mwingine huwapoteza katika aksidenti, uhalifu, ugonjwa, au uzoevu wa dawa za kulevya. Au watoto wanapokua, huenda wakaambukizwa roho ya ubinafsi ya ulimwengu huu na kukosa kurudisha upendo wa wazazi wao.

Wale wanaojitoa bila ubinafsi ili kustawisha mazingira hufadhaika mara nyingi kwa sababu ya mapendezi ya kibiashara au kwa sababu ya jambo la kwamba wengine hawajali. Wale wanaojitoa kwa ajili ya masilahi ya maskini hushindwa na ukubwa wa kazi hiyo. Mtu ambaye kazi-maisha yake humletea uradhi hufadhaishwa wakati anapolazimika kustaafu. Mtafiti ambaye hupata uradhi kikamili kwa kufuatilia maarifa hufadhaishwa wakati maisha yake yakaribiapo mwisho wayo na bado maswali mengi yanabaki bila kujibiwa. Mtu ambaye ametumia maisha yake kupata utajiri hupata kwamba, hatimaye, hulazimika kuwaachia wengine utajiri huo.

Mfalme wa kale aliyenukuliwa mapema alieleza baadhi ya kufadhaika huko alipoandika: “Nikaja kuchukia kazi yangu yote na jasho nililotoa chini ya jua, kwa sababu nitapaswa kuachia mwandamizi wangu matunda yake. Yule atakayeniandama atakuwa mtu wa aina gani, ambaye hurithi yale ambayo wengine wamejipatia? Ni nani ajuaye kama yeye atakuwa mtu mwenye hekima au mjinga? Na bado yeye atakuwa bwana mkubwa wa matunda yote ya kazi na ustadi wangu.”—Mhubiri 2:18, 19, New English Bible.

Basi, je! uhai hauna kusudi kabisa, kama vile maneno hayo ya ukweli mtupu yanavyoonekana yakimaanisha? Je! miradi mbalimbali ambayo wanadamu hufuatia ni msaada tu wa kuwapitisha miaka ya maisha yao ya 70, 80, au 90 ambayo wengi hujaliwa? Zaidi ya hiyo, je! miradi hii kwa msingi haina maana yoyote? La. Kwa kweli, inaonyesha jambo la maana sana juu ya vile sisi tuliumbwa, na hutoa ithibati kwamba kweli kweli, uhai una kusudi la ajabu. Lakini twawezaje kupata kusudi hilo?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wengine hupata kwamba kufuatilia maarifa hufanya uhai wao uwe na maana na kusudi

Wanadamu hawafanyizi vitu tata bila kuwa na kusudi fulani akilini

[Hisani]

picha ya NASA

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki