Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/8 uku. 29
  • Mbona Machozi Yote Hayo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mbona Machozi Yote Hayo?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Sisi Hulia?
  • Yale Machozi Mengine
  • Kwa Kupepesa Jicho
  • Machozi Yako ya Ajabu
    Amkeni!—2014
  • Masomo Tunayojifunza Kutokana na Machozi ya Yesu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2022
  • Machozi Yako Yana Thamani kwa Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2024
  • “Tazama! Ninafanya Vitu Vyote Kuwa Vipya”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/8 uku. 29

Mbona Machozi Yote Hayo?

NI LINI ulipolia kwelikweli mara ya mwisho? Je, ilikuwa kwa sababu ya furaha au huzuni? Kwa sababu ya ushindi wa kibinafsi au ushinde mbaya sana? Kwa sababu ya kupata kitulizo au kwa sababu ya kukata tumaini? Kuzaliwa kwa mtoto au kufa kwa mwenzi, kukumbuka jambo zuri au kukumbuka jambo lenye kuumiza, kumkaribisha rafiki umthaminiye sana au kuaga mtu? Hali tofauti, hisia tofauti, hata hivyo mara nyingi zaonyeshwa katika njia ileile—kwa machozi.

Lakini ni kwa nini sisi hulia kwa sababu ya hisia-moyo nyingi? Je, kulia hutimiza jambo lolote? Au je, tungeweza kukaa bila kulia?

Kwa Nini Sisi Hulia?

Hakuna yeyote aliye na uhakika juu ya hilo. Wanadamu na wanyama hutoa machozi ya aina mbili: Machozi yanayotoka sehemu ya chini, au kwa kuendelea, hulowesha jicho, na machozi yanayotoka yenyewe hutokea jicho linaposumbuliwa na kitu fulani kigeni. Lakini yaonekana binadamu pekee ndio hutoa machozi ya hisia-moyo—nayo hayaeleweki sana.

Mtafiti William Frey adokeza kwamba kulia kwa kihisia-moyo hutoa mwilini vitu vyenye madhara na vinavyozidi kiasi, kama vile tu figo, utumbo mpana, mapafu, na vinyweleo. Kitabu chake Crying—The Mystery of Tears hufafanua uchunguzi wake ambao ulilinganisha machozi yasababishwayo na kisumbufu (kitunguu) na machozi yasababishwayo na hisia-moyo (yatokanayo na kutazama sinema zenye kuhuzunisha). Machozi ya hisia-moyo yalikuwa na protini nyingi zaidi—yapata asilimia 24 zaidi. Sababu haijawa wazi bado, lakini kwa wazi mwili hutokeza aina fulani ya machozi kwa sababu ya hisia-moyo, machozi ambayo yatofautiana na yale yasababishwayo na kisumbufu.

“Ninalia kama mwanamke. Jicho langu, jicho langu latiririka maji,” akaandika nabii Yeremia. (Maombolezo 1:16, NW) Je, kwa kweli wanawake hulia zaidi kuliko wanaume? Kulingana na takwimu, ndio—mara nne hivi zaidi (mara 5.3 kwa mwezi kwa kulinganishwa na mara 1.4 kwa wanaume). Kulingana na Frey, wavulana na wasichana hulia kwa kiasi kilekile wakiwa wachanga, ingawaje huenda ikachukua siku au majuma kadhaa tangu kuzaliwa kabla ya mtoto kutoa machozi ya hisia-moyo. Hata hivyo, tofauti huanza kusitawi katika utineja. Huenda hilo likawa kwa sababu ya uvutano wa kijamii. Lakini homoni iitwayo prolactin (isababishayo kutokezwa kwa maziwa) yapatikana katika kiwango kilekile katika watoto wa jinsia zote mbili hadi wanapofikia miaka ya utineja. Kipindi fulani kati ya miaka 13 na 16, kiwango hicho huongezeka katika watoto wa kike.

Homoni hiyo hupatikana katika machozi. Hiyo huongezeka pia katika mwili wakati wa mkazo. Hivyo, wanawake wangeweza kuwa na viwango vya juu hata zaidi vya homoni hiyo kuliko wanaume wanapokuwa chini ya mkazo. Je, hiyo ingeweza kuwa sababu inayofanya wanawake walie kwa urahisi zaidi na mara nyingi zaidi kuliko wanaume? Dakt. Frey aamini kwamba kulia kwa sababu ya hisia-moyo ni jitihada ya mwili ya kupata tena usawaziko wa kikemikali. Huenda hizo homoni zikachochea kulia, naye atoa nadharia ya kwamba hiyo ndiyo sababu mara nyingi sisi huhisi vizuri zaidi baada ya kulia.

Uchunguzi mwingine uliofanywa na daktari wa saikolojia, Margaret Crepeau, ulivumbua uhusiano uliopo kati ya kulia na “kiwango cha juu zaidi cha matatizo ya ndani yanayosababishwa na mkazo kama vile vidonda vya tumbo na uvimbe wa utumbo mpana.” (Gazeti Seventeen, la Mei 1990) Watafiti wengine walipata uthibitisho ulio kinyume cha huo. Gazeti Health liliripoti kwamba Dakt. Susan Labott na Dakt. Randall Martin waliwachunguza watu ambao hulia kwa ukawaida na ambao hawalii kwa ukawaida. Ugunduzi wao ulionyesha kwamba mkazo haukupunguzwa na kulia na kwamba watu ambao hulia kwa ukawaida “walielekea zaidi kuhangaika na kushuka moyo.” Walikata maneno kwamba kulia hakuna faida yoyote wakati ambapo kulia “hutukengeusha kutokana na tatizo lenyewe.” Hata hivyo, kulia kwaweza kuwa sehemu ya maana ya kukubali jambo lenye kufadhaisha, kama vile kifo cha mpendwa.

Yatosha kusema kwamba, bado sababu na kusudi la machozi ya kihisia-moyo halijajulikana.

Yale Machozi Mengine

Twajua mengi zaidi juu ya kazi ya machozi yenye kuendelea, machozi uliyo nayo sasa hivi machoni mwako. Hayo hufanya mambo mengi zaidi ya kuyaloweza macho yako tu. Acheni tuzungumzie mwendo wa umajimaji huo wa ajabu ufanyizwapo, uenezwapo, na kutolewa kupitia mfumo wa machozi.

Tezi kuu ya machozi hupatikana katika mbonyeo ulio juu kidogo ya pembe ya nje ya jicho lako. Tezi hiyo iliyo kama sponji, pamoja na nyingine 60, hufanyiza utando wenye safu tatu—ute, maji, na mafuta.

Safu ya ndani, ute, hulainisha sehemu ya nje ya jicho ili kigubiko kiteleze juu ya sehemu ya jicho iliyo wazi. Safu yenye maji ndiyo nene zaidi kati ya safu zote tatu, yenye vichanganyiko vingi vya maana kutia ndani oksijeni, iliyo muhimu kwa konea. Pia kuna kiasi fulani cha lysozyme na vimeng’enya vingine 11 vipatikanavyo katika machozi. Lysozyme ni mpigana na bakteria aliye bora kabisa. Hudumisha jicho likiwa jeupe na safi.

Sehemu ya mwisho ya chozi itaandaliwa na tezi 30 za Meibom, yale madoa madogo ya manjano yaliyo kwenye laini moja nyuma ya kope. Tezi hizo hutoa safu ya mafuta, iliyo nyembamba sana hivi kwamba haibadili mwono wako, hata hivyo hudumisha utando wa chozi usivukizwe na kusababisha visehemu vikavu kwenye jicho visivyostarehesha wakati wa kupepesa jicho. Kwa hakika, watu fulani wana kiasi kisichotosha cha mafuta, nayo machozi yao huvukizwa haraka zaidi ya ilivyo kawaida.

Kwa Kupepesa Jicho

Kigubiko ndicho hicho, kikifunika haraka, kikileta vichanganyiko vinavyofaa, na kuvieneza sawasawa juu ya jicho katika safu tatu. Vigubiko hukutana sawasawa hivi kwamba jicho zima hufunikwa na mwosho huo wenye kuburudisha.

Machozi yaliyotumika huenda wapi? Kulichunguza jicho lako kwa makini zaidi kutaonyesha shimo dogo katika pembe ya ndani ya jicho, ambalo hutoa machozi ya ziada na kuyaingiza kwenye kijia kinachoelekeza kwenye mfuko wa machozi. Tokea hapo machozi hayo hupita sehemu ya nyuma ya pua na koo, ambapo machozi hayo hufyonzwa na tando zenye ute. Kupepesa jicho husababisha mfuko wa machozi utende kama pampu, ambayo huyasukuma machozi yaingie kwenye kijia hicho na kuteremka.

Uanzapo kulia, huenda ukapepesa jicho haraka zaidi kisilika, ukitendesha pampu hiyo haraka zaidi ili kuyachukua machozi hayo ya ziada. Hata hivyo, machozi yanapofurika, pampu hiyo hujaa mno, mfuko wa machozi ulio katika kijia cha pua hufurika, na machozi yanatokea puani. Nawe huenda ukatafuta kitambaa chako cha mikono kwa sababu kufikia sasa machozi yaliyosalia yanamwagika nje ya vigubiko na kutiririka kwenye mashavu.

Kwa hiyo yawe yanasababishwa na nini—pongezi ya kutoka moyoni au tukano lenye kuumiza, kicheko au kushuka moyo, ushindi mkubwa au kukata tamaa vibaya sana—machozi ya kutosha yasubiri kuonyesha hisia zako.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki