Mitaa ya Hali ya Chini—Nyakati Ngumu Katika Matatizo ya Maisha ya Mjini
Na mleta habari za Amkeni! katika Afrika
MTOTO wa mtaa wa hali ya chini atembea barabarani miguu mitupu katika mji mmoja wa Afrika ya magharibi. Kichwani mwa msichana huyo mna sinia la mviringo lililo tambarare lenye machungwa mengi. Juu ya mwili wake mwembamba mna kanga ya manjano iliyokwisha kutumiwa na wengine. Anatokwa na jasho.
Akishindana na watoto wengine kutoka familia maskini, yuko barabarani akiuza. “Nunua machungwa!” ndiyo sauti ya kawaida. Lakini mtoto huyu ni kimya; labda ana njaa au ni mgonjwa au amechoka tu.
Kutoka upande ule mwingine, waja wasichana wawili wa shule waliovaa unifomu (sare) za shule za zambarau-buluu. Kila mmoja wao amevaa soksi nyeupe na viatu vyeupe. Kila mmoja ana mfuko wa vitabu ulio na vitabu vingi. Wasichana hao watembea upesi-upesi, wakizungumza pamoja kwa furaha. Wao hawamwoni mtoto yule, lakini yeye awaona. Yeye awatazama kwa macho makavu.
Hatimaye wasichana hao wa shule wafika kwenye nyumba zao zenye starehe na usalama. Lakini wakati yule mtoto aendapo nyumbani mwishoni mwa siku, yeye aenda kwenye ulimwengu ulio tofauti kabisa. Makao yake ni msongamano wa nyumba za mbao na mabati.
Mtaa wa Hali ya Chini
Barabara kuu hapa ni kijia cha udongo uliogandamana. Wakati wa kipindi cha mvua, hiyo hugeuka kuwa matope. Ni nyembamba sana kwa gari kusafiria. Kando yayo hutapata stesheni ya polisi, kituo cha wazima moto, hospitali, au mti hata mmoja. Juu yayo hakuna kamba za stima (umeme) wala za simu. Chini yayo hakuna mifereji ya maji machafu wala ya maji safi.
Watu wamejaa tele. Hewa imejawa na kelele za masemezano. Mazungumzo yanachanganyika na kicheko, mabishano, kilio, na nyimbo. Wanaume wenye majoho meupe wameketi kwenye benchi ndefu, wakizungumza. Wanawake wakoroga mchele unaopikwa katika vyungu juu ya moto wa kuni. Watoto wako kila mahali—wakicheza, wakilala, wakifanya kazi, wakiongea, wakiuza. Wengi wao, kama yule mtoto mwenye machungwa, hawatapata kamwe kuzuru makao ya wanyama, kuendesha baiskeli, au kukanyaga shuleni.
Katika nchi ambamo wastani wa matarajio ya muda wa kuishi wakati wa kuzaliwa ni miaka 42 tu, watu katika eneo hili hufa wakiwa wachanga sana. Mtoto akiwa na miaka tisa tayari yeye anakuwa ameokoka, hata ingawa uwezekano wa kuokoka miaka minne ya kwanza ya uhai ni mmojawapo ya chini sana ulimwenguni. Katika wakati huo alikuwa anaelekea kufa kwa kadirio la mara 40 au 50 zaidi ya ikiwa angalikuwa amezaliwa katika taifa lililositawi. Wengi waliozaliwa naye hawakuishi zaidi ya miaka mitano. Ikiwa ni msichana na anaishi muda mrefu vya kutosha, ataelekea zaidi kufa wakati wa ujamzito au wa kuzaa kuliko mwanamke wa Ulaya au Amerika ya Kaskazini—uwezekano wa mara 150 zaidi.
Mamia ya mamilioni huishi katika mitaa ya hali ya chini inayopanuka upesi kama hii. Kulingana na tarakimu ya Umoja wa Mataifa, watu bilioni 1.3 wamesongamana katika miji ya mataifa yanayositawi, na wapatao milioni 50 wanaongezwa kila mwaka.
Maisha Katika Nchi Zinazositawi
Je! nyumba yako ina kiasi fulani cha faragha, maji ya mfereji, choo? Je! mtu fulani huzoa takataka zako? Mamia ya mamilioni ya watu katika nchi zinazositawi hawana mambo hayo.
Katika miji mingi maeneo ya maskini yana watu wengi sana hivi kwamba ni jambo la kawaida kwa familia ya watu kumi kuwa katika chumba kimoja. Mara nyingi, watu wana nafasi ya kuishi iliyo chini ya mita moja kwa mraba. Katika sehemu nyingine za mji katika Mashariki, hata vyumba vidogo vimegawanywa ili kuwa na wakazi wengi, kukiwa na vitanda vilivyozungushiwa waya ili kuwa na usiri na usalama dhidi ya wevi. Katika nchi nyingine, mpango wa “kitanda-kimoto” huwezesha watu kukodi vitanda saa baada ya saa hivi kwamba watu wawili au watatu wanaweza kulala kwa zamu kila siku.
Kulingana na ripoti ya kila mwaka ya 1991 ya UNICEF (Hazina ya Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Watoto), watu bilioni 1.2 ulimwenguni pote wana maji yasiyo salama kwa uhai. Mamilioni hulazimika kununua maji yao kutoka kwa wachuuzi au kuyachota kutoka kwa vijito au vyanzo vingine vya maji vilivyo wazi. Mahali ambapo maji ya mfereji yapatikana, nyakati nyingine watu zaidi ya elfu moja hung’ang’ania mfereji mmoja wa maji.
UNICEF pia inakadiria kwamba watu bilioni 1.7 hawana njia ifaayo ya kuondolea mbali kinyesi cha binadamu. Ni jambo la kawaida kwa asilimia 85 ya wakazi wa mitaa ya hali ya chini kukosa vyoo. Katika miji mingi ya Afrika na Esia, kutia na ile yenye watu zaidi ya milioni moja, hakuna mfumo wowote wa kuondolea maji machafu. Kinyesi cha binadamu huingia katika vijito, mito, mitaro, mifereji, na michirizi.
Takataka ni tatizo jingine. Katika miji ya mataifa yanayositawi, kuanzia asilimia 30 hadi 50 ya takataka haizolewi. Sehemu za maskini ndio hupuuzwa zaidi. Sababu moja ni kwamba maskini hutupa takataka chache zaidi zinazoweza kutumiwa kwa faida au kutumiwa tena na wazoa takataka au biashara zinazozitengeneza tena. Sababu ya pili ni kwamba kwa kuwa makao mengi ya maskini hayatambuliwi kuwa yamethibitishwa kihalali, serikali huyanyima utumishi wa umma. Tatizo la tatu ni kwamba, ni vigumu na inagharimu kutumikia sehemu nyingi za maskini, kwa sababu ya mahali zilizoko, na wingi wa watu.
Na takataka hiyo huenda wapi? Hutupwa kuozea barabarani, kwenye sehemu zilizo wazi, mitoni na katika maziwa ya maji.
Hatari kwa Afya
Hali ya maskini waishio mijini hutofautiana mahali-mahali. Na bado, mambo matatu yako karibu kila mahali. Jambo la kwanza ni kwamba nyumba zao si kwamba tu hazistareheshi, bali pia ni zenye hatari. Kitabu The Poor Die Young husema hivi: “Angalau watu milioni 600 wanaoishi katika maeneo ya mijini ya Ulimwengu wa Tatu huishi katika yale yanayoweza kuitwa makao na ujirani wenye kuhatarisha uhai na afya.”
Makao yasiyofaa yanaweza kuhatarishaje afya? Msongamano wa watu katika sehemu za maskini mijini husaidia kuchochea mweneo wa magonjwa, kama vile kifua kikuu, homa ya mapafu, na homa ya utando wa ubongo. Msongamano pia huongeza hatari ya aksidenti za nyumbani.
Ukosefu wa maji safi ya kutosha huongeza maambukizo ya magonjwa yanayoenezwa kwa maji, kama vile homa ya matumbo, mchochota wa ini, na kuhara damu. Pia hutokeza ugonjwa wa kuhara uuao mtoto kila sekunde 20 kwa wastani, katika nchi zinazositawi. Ukosefu wa maji ya kutosha ya kuoshea na kuogea hufanya watu waelekee zaidi kupata maambukizo ya macho na magonjwa ya ngozi. Na wakati watu maskini walazimikapo kulipa bei ya juu kwa maji, pesa za chakula huwa hazitoshi.
Kuchafuliwa kwa maji na chakula hutokeza magonjwa ya mdomo na matumbo na minyoo, kama vile safura, mchango duara, na tegu. Takataka isiyozolewa huleta panya, nzi, na mende. Maji yaliyokusanyika ni mahali wanapozaana mbu wanaobeba malaria na filariasi.
Janga la Umaskini
Jambo la pili linalopatikana katika maisha ya mitaa ya hali ya chini ni kwamba ni vigumu sana kwa wakazi kuondoka katika maisha hayo. Wengi wa wale wanaokuja mjini ni wahamiaji wanaolazimika kutoka mashambani kwa sababu ya umaskini. Wakiwa hawawezi kulipia nyumba zifaazo, wao huanza kuishi katika mitaa ya hali ya chini na mara nyingi wanazeekea humo.
Wengi wa watu hao ni wenye bidii ya kazi na wanataka kufanya kazi, lakini hawana la kufanya ila kukubali kazi za saa nyingi na malipo haba. Wazazi wenye shida mara nyingi hutuma watoto wao kufanya kazi badala ya kwenda shule, na watoto wenye elimu ndogo ikiwa wana yoyote wana matarajio madogo ya kufanikiwa maishani kuliko wazazi wao. Hata ingawa vijana hupata pesa kidogo sana, mara nyingi zile wanazochuma huwa za muhimu sana kwa familia zao. Hivyo, kwa maskini wengi wa mijini, hakuna tumaini la kuinua hali yao ya maisha; mradi wao ni kupata mkate wa kila siku.
Wasiopendwa, Wasiotakwa
Jambo la tatu katika maisha hayo ni kwamba hakuna uhakika wa kuishi makao hayo muda mrefu. Kwa serikali nyingi, mitaa ya hali ya chini ni aibu. Badala ya kujitahidi kuinua hali ya mitaa hiyo, jambo ambalo halifanyi kazi nyakati zote, mara nyingi serikali mbalimbali hupeleka tingatinga za kubomoa.
Huenda serikali mbalimbali zikajitetea kwamba kuondoa mitaa ya hali ya chini ni jambo la muhimu ili kufanya mji uwe maridadi, kuondoa wakora, au kusitawisha sehemu hiyo. Hata sababu iwe nini, maskini ndiyo huumia. Mara nyingi hakuna mahali pengine pa wao kwenda na ikiwa wanalipwa chochote, wao hulipwa kiasi kidogo sana. Lakini matingatinga yanapoingia, hawana la kufanya ila tu kuondoka.
Jukumu la Serikali
Kwa nini serikali huwa haziandai nyumba zifaazo zenye maji, mifereji ya maji machafu, na utumishi wa kuzoa takataka kwa watu wote? Kitabu Squatter Citizen kinajibu: “Mataifa mengi ya Ulimwengu wa Tatu yana upungufu mkubwa sana wa nyenzo na uwezekano mdogo sana wa kusitawisha jukumu lenye nguvu na maendeleo katika soko la ulimwengu hivi kwamba inawezekana kushuku sana uwezo wazo wa kuwa mataifa mazima. Mtu hawezi kulaumu serikali kwa kushindwa kutimiza mahitaji ya raia zayo wakati taifa zima lina upungufu mkubwa sana wa nyenzo, hivi kwamba katika hali za sasa, hakuna nyenzo za kutosha za kutimiza mahitaji ya msingi.”
Katika nchi nyingi hali za kiuchumi zinazoroteka. Mwaka jana, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyestaafu aliripoti hivi: “Hali ya mataifa mengi yanayositawi katika uchumi wa ulimwengu imekuwa ikizoroteka kwa muda fulani. . . . Zaidi ya watu bilioni 1 sasa huishi katika umaskini hohehahe.”
Namna Gani Kuhusu Msaada wa Kutoka Nje?
Kwa nini mataifa tajiri hayafanyi mengi zaidi kusaidia? Ikizungumzia kuhusu tokeo la msaada kwa umaskini, Ripoti ya Maendeleo ya Banki Kuu ya Ulimwengu inakiri hivi: “Watoa misaada wenye kufaidika [wanaotoa asilimia 64 ya msaada wote wa kigeni] . . . hutoa msaada kwa sababu nyingi—za kisiasa, kijeshi, kibiashara, na kibinadamu. Kupunguza umaskini ni lengo moja tu, na mara nyingi si lililo la maana zaidi.”
Kwa upande ule mwingine, hata wakati serikali zinapokuwa na nyenzo za kuinua hali ya maskini, mara nyingi hazifanyi hivyo. Tatizo lililo katika mataifa mengi ni kwamba ingawa serikali za wilaya huandaa makao na utumishi mwingineo, serikali kuu haitolei serikali za wilaya uwezo wala nyenzo za kufanya kazi hizo.
Miji ya Wakati Ujao
Kulingana na vile mambo yamekuwa yakienda katika miongo ya karibuni, wastadi wanatabiri wakati ujao wenye giza kwa maskini wa mijini katika nchi zinazositawi. Wao wasema kwamba ukuzi wa haraka wa mijini utaendelea, na serikali zitashindwa kuandalia wakazi wengi wa miji maji ya mfereji, mifumo ya maji machafu, mitaro, barabara, matibabu, na utumishi wa dharura.
Majengo yatazidi kujengwa kwenye sehemu hatari, kama vile kwenye pande za vilima, nyanda zenye mafuriko, au sehemu zilizochafuliwa. Watu watazidi kuugua kutokana na magonjwa kwa sababu ya msongamano wa watu, na hali zisizofaa. Maskini wa mijini watazidi kuishi wakiwa na tisho la kila wakati la kuhamishwa kwa nguvu.
Je! hiyo inamaanisha kwamba hakuna tumaini kwa wakazi wa mitaa ya hali ya chini kama yule msichana mwenye machungwa aliyesimuliwa mwanzoni mwa mazungumzo haya? La Hasha!
Badiliko Lenye Kutazamisha Linakuja
Neno la Mungu, Biblia, huonyesha kwamba badiliko lenye kutazamisha litakaloleta mambo mazuri litakuja—hivi karibuni. Badiliko hilo litakuja, si kupitia jitihada za serikali za kibinadamu, bali kupitia Ufalme wa Mungu, serikali ya kimbingu itakayochukua mamlaka ya dunia yote hivi karibuni.—Mathayo 6:9, 10.
Chini ya Ufalme wa Mungu, badala ya kunaswa katika mitaa michafu ya hali ya chini, familia zenye kumhofu Mungu zitakaa katika paradiso. (Luka 23:43) Badala ya wao kuishi wakiwa na tisho la daima la kuhamishwa, Biblia husema kwamba “wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake, wala hapana mtu atakayewatia hofu.”—Mika 4:4.
Chini ya Ufalme wa Mungu, badala ya watu kufa wakiwa wachanga katika makao yenye msongamano, wao “watajenga nyumba na kukaa ndani yake, watapanda mizabibu, na kula matunda yake. . . . Maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu.”—Isaya 65:21, 22.
Huenda ikawa vigumu kwako kuamini ahadi hizo, lakini unaweza kuwa na uhakika zitakuwa kweli. Kwa nini? Kwa sababu Mungu hasemi uwongo, na “hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”—Luka 1:37; Hesabu 23:19.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Chini ya Ufalme wa Mungu, umaskini na mitaa ya hali ya chini itabadilishwa kuwa hali za paradiso