Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/8 kur. 4-7
  • Wafungwa wa Umaskini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wafungwa wa Umaskini
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Njaa na Utapiamlo
  • Afya Mbaya
  • Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa na Malipo ya Chini
  • Uharibifu wa Mazingira
  • Elimu
  • Makao
  • Idadi ya Watu
  • Jitihada za Kumaliza Umaskini
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Majibu ya Maswali ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Umaskini Unaoongezeka—Tisho kwa Wote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Mwisho wa Umaskini Wakaribia
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/8 kur. 4-7

Wafungwa wa Umaskini

KATIKA mwaka wa 33 W.K., Yesu Kristo aliwaambia wafuasi wake hivi: “Sikuzote mna maskini pamoja nanyi.” (Mathayo 26:11) Alimaanisha nini? Je, alikuwa akisema kwamba umaskini haungeshindwa kamwe?

James Speth, msimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, alitaarifu: “Hatuwezi kukubali kwamba [umaskini] utakuwapo sikuzote. Ulimwengu wa kisasa una mali, ufundi na ustadi wa kuondosha umaskini, na kuufanya kuwa kitu cha kale.” Lakini je, ulimwengu wa kisasa waweza kuondoa umaskini?

Kwa wazi Kamati Kuu ya Umoja wa Mataifa yatumaini kwamba jitihada za binadamu zaweza kuondoa umaskini, kwa kuwa iliitangaza miaka ya 1997 hadi 2006 kuwa miaka ya kwanza ya “Mwongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuondoa Umaskini.” Umoja wa Mataifa ulipendekeza kufanya kazi pamoja na serikali, watu, na mashirika ili kuendeleza maendeleo ya kiuchumi, kuboresha njia za kupata huduma za msingi, kuboresha hadhi ya wanawake, na kutokeza mapato na kazi za kuajiriwa.

Ni miradi ya juu sana! Lakini, je, jumuiya ya ulimwengu itapata kuifikia? Fikiria baadhi ya vipingamizi ambavyo huzuia jitihada za binadamu za kuondoa umaskini.

Njaa na Utapiamlo

Ayembe, anayeishi Zaire, ana washiriki wa familia 15 ambao humtegemea. Nyakati nyingine familia inaweza kufaulu kula mara moja kwa siku—uji wa mahindi uliokolezwa kwa majani ya mhogo, chumvi na sukari. Nyakati nyingine hawana chochote cha kula kwa siku mbili au tatu. “Mimi hungoja mpaka watoto walie kabla ya kupika,” asema Ayembe.

Hali yao ni ya kawaida. Katika nchi zinazositawi, mtu 1 kati ya 5 hulala njaa kila usiku. Ulimwenguni pote, karibu watu milioni 800—milioni 200 kati yao wakiwa watoto—hawapati chakula cha kutosha daima. Watoto hawa hawakui kwa njia ya kawaida; mara nyingi huwa wagonjwa. Wao hufanya vibaya shuleni. Wakiwa watu wazima, hupatwa na matokeo ya mambo haya. Hivyo, mara nyingi umaskini huongoza kwenye utapiamlo, ambao nao pia huchangia umaskini.

Umaskini, njaa kali, na utapiamlo umeenea sana hivi kwamba hushinda jitihada za kisiasa, kiuchumi, na kijamii kuuondoa. Kwa kweli, hali haiboreki bali yawa mbaya zaidi.

Afya Mbaya

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, umaskini ndio “maradhi yenye kufisha zaidi ulimwenguni” na “kisababishi kikuu zaidi cha kifo, maradhi na kuteseka.”

Kitabu An Urbanizing World: Global Report on Human Settlements, 1996 kilisema kwamba angalau watu milioni 600 katika Amerika ya Latini, Asia, na Afrika waliishi katika makao yaliyo mabaya sana—bila maji ya kutosha, usafi wa kutunza afya, na uondolewaji wa maji machafu—hivi kwamba maisha na afya yao yalitishwa daima. Ulimwenguni pote, zaidi ya watu bilioni moja hawana maji safi. Mamia ya mamilioni hawawezi kugharimia mlo kamili. Mambo haya yote hufanya iwe vigumu kwa maskini kuzuia maradhi.

Mara nyingi maskini pia hushindwa kutibu maradhi. Maskini wanapokuwa wagonjwa, huenda wasiweze kugharimia dawa zinazofaa au matibabu. Maskini hufa wakiwa wachanga; wale wanaoendelea kuishi huenda wakaishi wakiwa na magonjwa ya kudumu.

Zahida, mchuuzi mmoja wa sokoni katika Maldives asema: “Umaskini humaanisha afya mbaya, ambayo hukuzuia kufanya kazi.” Bila shaka, ukosefu wa kazi, huongezea umaskini unaopita kiasi. Tokeo huwa mzunguko wenye ukatili na wenye kufisha ambapo umaskini na ugonjwa huchocheana.

Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa na Malipo ya Chini

Upande mwingine wa umaskini ni ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Tufeni pote, watu wapatao milioni 120 wawezao kufanya kazi hawawezi kupata kazi za kuajiriwa. Wakati uleule, karibu watu wengine milioni 700 mara nyingi hufanya kazi kwa muda wa saa nyingi kwa malipo ya chini sana yasiyoweza kutosheleza mahitaji yao ya msingi.

Rudeen ni dereva wa tuk-tuk katika Kambodia. Asema: “Kwa upande wangu umaskini humaanisha kufanya kazi kwa zaidi ya saa 18 kwa siku, lakini bado sichumi pesa za kutosha kujilisha mwenyewe, mke wangu na watoto wangu wawili.”

Uharibifu wa Mazingira

Jambo linaloambatana na umaskini ni kuharibiwa kwa mazingira. Alionelea Elsa, mtafiti katika Guyana, Amerika Kusini: “Umaskini ni uharibifu wa asili: msitu, bara, wanyama, mito na maziwa.” Huu ni mzunguko mwingine wenye kuhuzunisha—umaskini huongoza kwenye uharibifu wa mazingira, ambao huendeleza umaskini unaozidi.

Kulima shamba ambalo lafaa kukuza mazao mpaka linapokosa rutuba au kutumiwa kwa kusudi jingine ni zoea la zamani za kale. Ndivyo na—ukataji wa misitu kwa ajili ya mbao au fueli au kwa ajili ya kupanda mazao. Kwa sababu ya ongezeko la watu duniani, hali imefikia viwango vya hatari.

Kulingana na Hazina ya Kimataifa ya Maendeleo ya Kilimo, katika miaka 30 iliyopita, karibu asilimia 20 ya udongo ulio juu ya ardhi wa kukuzia mazao haufai tena kutumika, hasa kwa sababu ya ukosefu wa pesa na tekinolojia inayohitajiwa ili kutekeleza hatua za kuhifadhi. Wakati wa kipindi hicho hicho, mamilioni ya ekari yamekuwa ardhi kame kwa sababu ya kujengwa vibaya na kutodumishwa kwa mifumo ya unyunyiziaji wa maji. Na mamilioni ya ekari za misitu inakatwa kila mwaka ili kutokeza ardhi kwa ajili ya mazao au kupata mbao kwa ajili ya magogo au fueli.

Uharibifu huu huhusiana na umaskini katika njia mbili. Kwanza, mara nyingi maskini hulazimishwa kuharibu mazingira kwa sababu ya mahitaji yao ya chakula na fueli. Mtu awezaje kuzungumza kuhusu ukuzi unaotegemea maliasili au hali-njema ya vizazi vya wakati ujao, kwa wale walio na njaa na maskini na ambao hulazimika kuharibu maliasili ili kujiendeleza kwa sasa? Pili, mara nyingi matajiri hutumia kwa kujifaidi mali za mazingira za maskini. Kwa hiyo kuharibiwa kwa maliasili na matajiri na maskini huongeza umaskini.

Elimu

Alicia, mfanyakazi wa jamii wa mjini katika Filipino, alitaarifu: “Upande mwingine wa umaskini ni mwanamke kuwatuma watoto wake barabarani kuomba-omba badala ya kuwapeleka shuleni kwa sababu kama sivyo hakutakuwa na chochote cha kula. Mama huyo ajua anarudia mzunguko uliomnasa, lakini hakuna njia ya kuponyoka umaskini anayoweza kuona.”

Watoto wapatao milioni 500 hawapati nafasi za shule. Watu wazima bilioni moja hawana elimu ya kutosha. Bila elimu ni vigumu kupata kazi nzuri ya kuajiriwa. Kwa hiyo umaskini hutokeza ukosefu wa elimu, ambao hutokeza umaskini zaidi.

Makao

Kuna ukosefu wa makao katika mataifa maskini, na hata katika mengine yaliyo na mali. Ripoti moja husema kwamba karibu robo milioni ya wakazi wa New York City wamepata kuishi katika makao ya wasiokuwa na makao kwa muda fulani katika miaka mitano iliyopita. Ulaya pia ina maskini wake. Katika London karibu 400,000 wamesajiliwa kuwa hawana makao. Katika Ufaransa watu nusu milioni hawana makao.

Kotekote katika nchi zinazositawi, hali ni mbaya zaidi. Watu humiminika mijini na majijini, wakivutiwa na ndoto za chakula, kazi za kuajiriwa, na maisha bora. Katika majiji fulani, zaidi ya asilimia 60 ya watu huishi katika mitaa ya vibanda. Hivyo umaskini wa mashambani huchochea umaskini wa mjini.

Idadi ya Watu

Jambo linalozidisha matatizo haya yote ni ukuzi wa idadi ya watu. Idadi ya watu ulimwenguni imeongezeka zaidi ya maradufu katika miaka 45 iliyopita. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba tarakimu hiyo itapaa kufikia bilioni 6.2 ufikapo mwaka wa 2000 na kufikia bilioni 9.8 katika mwaka wa 2050. Sehemu zilizo maskini zaidi ulimwenguni ndizo zina viwango vya juu zaidi vya ukuzi wa idadi ya watu. Kati ya karibu watoto milioni 90 waliozaliwa katika mwaka wa 1995, milioni 85 walizaliwa katika nchi ambazo zina uwezo wa chini sana wa kuwaandalia.

Je, waamini kwamba jamii ya kibinadamu itashirikiana kwa ghafula kuondoa umaskini milele kwa kutatua matatizo ya njaa, ugonjwa, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, uharibifu wa mazingira, ukosefu wa elimu, makao mabaya, na vita? Labda huamini hivyo.

Je, hilo lamaanisha kwamba hakuna tumaini kabisa? La, kwa sababu utatuzi waonekana na utakuja kwa hakika. Lakini si kwa jitihada za kibinadamu. Jinsi gani basi? Na namna gani maneno ya Yesu aliposema: “Sikuzote mna maskini pamoja nanyi”?

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Maskini Zaidi Kati ya Walio Maskini

Katika mwaka wa 1971 maneno “nchi zisizositawi zaidi” yalitungwa na Umoja wa Mataifa ili kufafanua “mataifa maskini zaidi na yaliyo dhaifu zaidi kiuchumi kati ya nchi zinazositawi.” Wakati huo, kulikuwako nchi 21 za namna hiyo. Sasa, kuna nchi 48, ambazo 33 zimo Afrika.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Mamilioni hufanya kazi kwa muda wa saa nyingi kwa malipo ya chini

[Hisani]

Godo-Foto

[Picha katika ukurasa wa 6]

Anasa na umaskini zikiwa sambamba

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mamilioni huishi katika makao ya hali ya chini

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki