Ikiwa Mimi Nilipunguza Uzito, Yeyote Aweza!
JE! WEWE huchukia mizani yako ya chumba cha bafu? Mimi niliichukia. Nakumbuka nikiikodolea macho kwa kuchukizwa mwaka jana mshale ulipokuwa ukipanda kufikia kilele kipya—karibu kilo 110. Nikafikiri mwenyewe, ‘Nina uzito zaidi ya bingwa wa ndondi wa ulimwengu wa uzani mzito na zaidi ya wengi wa wachezaji futiboli wa kulipwa Waamerika. Hili ni jambo baya, si la kuchekesha. Linakuwa hatari!’
Labda wamjua mtu kama mimi—mwanamume mfanyakazi ofisini mwenye umri wa mwanzo-mwanzo wa makamo, aliyekuwa mtendaji wakati wa ujana wake lakini sasa afanya mazoezi mara kwa mara kati ya vipindi virefu ya kusoma magazeti. Msongo wa damu uko juu kukaribia kuwa hatari, kolesteroli katika damu iko juu “kidogo,” ana kilo 20 zaidi ya uzito anaopaswa kuwa nao, na angali aamini kwamba tatizo si hatari sana.
Tatizo hilo ni hatari. Watu kama mimi tu wanakufa kutokana na maradhi ya moyo kila siku—watu wengi sana wanapatwa na maradhi ya moyo. Ningeweza kutaja tarakimu kuhusu hatari za kila kilogramu ya ziada, lakini tatizo si tarakimu. Tatizo, kusema waziwazi, ni wajane na mayatima. Tatizo ni watoto, kama wasichana wangu wawili wadogo, wakikua bila baba yao.
Fikirieni hilo, enyi akina baba.
Mara nilipokwisha kuamua kupunguza uzito, nilikumbuka ile habari bora katika mfululizo katika Amkeni! (Kiingereza) la Mei 22, 1989 ‘Je! Kupunguza Uzito ni Pigano Unaloshindwa?”—hasa zile “Njia Nne za Kushinda” pigano juu ya kitambi. Hizo njia nne zilizodokezwa ni (1) chakula kifaacho, (2) katika wakati ufaao, (3) kwa kiasi kifaacho, (4) pamoja na mazoezi yafaayo.
Miongozo hiyo hufanya kazi! Nilipunguza kilo 30 kwa kuifuata, na wewe waweza kupunguza uzito pia. Wakati huohuo, nilijifunza mambo machache ambayo huenda ukayaona kuwa yenye kusaidia.
Kupunguza Uzito Huanza kwa Njia Yako ya Kufikiri
Wengi wetu wenye uzito kupita kiasi tulipata uzito wetu polepole, kilo chache kila mwaka, mara nyingi kuanzia miaka yetu ya 30. Pindi kwa pindi, tulikuwa tukipunguza ulaji wetu na kupunguza kilo chache, kisha kupata tena kilo nyingi zaidi ya tulizopunguza. Hilo liliponipata, lilitokeza namna fulani ya hisia ya kuwa hoi—hisia ya kwamba hakuna jambo litakaloleta matokeo, hivyo sababu gani kujaribu?
Njia ya kuondoa hali hiyo ya kuhisi kuwa hoi ni kuanza kupunguza ulaji wako, si kwa kuangalia ukubwa wa kiuno chako, bali kufikiri kwako, kubadili njia ufikiriayo chakula. Hilo huenda likataka unyoofu wenye kuumiza, lakini bila huo kupunguza ulaji wako labda kumeshindwa tokea mwanzo.
Katika kisa changu, kuweka orodha ya kila kitu nilichokula na kunywa kwa juma moja kulinipa ufahamu. Ni kweli, kwa kawaida nilikula kwa kiasi wakati wa milo, lakini kutafuna-tafuna vitu mfululizo jioni kuliharibu wema wowote uliokuwa umefanywa na kujidhibiti kwangu wakati wa mchana. Nilipojumlisha kalori za jibini, nju-gu, siagi ya njugu, na biskuti nilizokula baada ya chakula cha jioni, nilishtuka. Lililo baya zaidi, vitu hivyo nilivyotafuna-tafuna vilijaa mafuta na sukari. Kwangu mimi kuangalia ulaji wangu hakungekuwa na matokeo yoyote nisipoacha kutafuna-tafuna vitu jioni. Je! hilo ndilo tatizo lako pia?
Jambo lenye kuumiza nililofuata kung’amua lilikuwa kwamba singepunguza uzito na niendelee kuupunguza nisipoondoa kileo chote katika ulaji wangu. Kileo kina kalori nyingi na hugeuzwa kwa urahisi kuwa mafuta na bilauri moja ya divai jioni ndiyo tu inayodhoofisha kujidhibiti kwangu na azimio langu la kutotafuna-tafuna vitu. Bilauri ya divai si bilauri ya divai tu. Kwangu mimi, yamaanisha pia kula biskuti sita na bakuli la njugu! Niligundua kwamba chai ya mitishamba ingeweza kuwa kitu kilicho bora badala ya divai. Sasa, hata baada ya kufikia lengo la uzito wangu, nanywa kileo kidogo zaidi ya hapo mbeleni.
Makadirio hayo ya unyoofu yalinisadikisha juu ya thamani ya miongozo miwili thabiti wakati wa kipindi changu cha kupunguza uzito cha chakula changu..
1. Epuka kutafuna-tafuna kitu chochote jioni.
2. Epuka vinywaji vyote vyenye kileo.
Ujue Vyakula Vitakavyokinza Ulaji Wako wa Uangalifu!
Wafaransa wana mithali, En mangeant, l’appetit vient, ambayo humaanisha kwamba kadiri ulavyo zaidi, ndivyo uwavyo na njaa zaidi. Kwa wengi wetu, hilo ni kweli kihalisi. Huenda tusihisi njaa tuketipo kula mlo tuupendao zaidi, lakini jambo fulani hutukia ghafula ndani yetu tuanzapo kula, na ghafula tunakuwa na njaa tele. Hivyo tunakula kupita kiasi mpaka chakula chote kiishe au, baada ya kujipakulia mara nne, matumbo yetu yenye kuumia na hatimaye kutuomba tuyarehemu. Kulitukia nini?
Katika kisa changu tatizo lilikuwa mkate, hasa mkate uliookwa nyumbani. Mke wangu mstahimilivu, aokaye mikate mitamu sana, alilazimika kuacha kuoka kwa muda fulani. Mtu aweza kustahimili jaribu kwa muda fulani tu! Kwako wewe huenda tatizo likawa chokoleti au kitu kingine. Jambo la maana ni, umjue adui wako. Weka orodha ya vyakula ambavyo hukufanya uhisi njaa unapovila nawe uviepuke. Kuna machaguo mengine mengi. Niliona kwamba saladi na mboga zilizopikwa kwa mvuke huwa na ladha nzuri na hunishibisha bila kutokeza hamu hiyo ya kutaka zaidi.
Kupita Hatua Muhimu
Kupunguza ulaji na kisha kuurudia-rudia, kupunguza uzito na kuupata tena tu, ni mchezo wa mtu adanganyikaye kwa urahisi ambao hautumikii kusudi jingine ila kutajirisha waendelezaji wa programu za kupunguza uzito ambao husitawi sana katika nchi tajiri za Magharibi. Baada ya kupunguza ulaji na kuurudia-rudia, niliazimia wakati huu itakuwa tofauti. Lakini jinsi gani?
Usiaibike kuomba msaada. Ongea na daktari wako. Pata watu ambao watakusifu na kukuthawabisha kila juma kadiri upunguzavyo kilo hizo. Huyo huenda akawa rafiki anayepunguza ulaji pia, mshiriki wa familia, au watu kwenye kliniki yenye sifa njema ya upunguzaji uzito. Kufanya kazi mkiwa kikundi na kuongezewa nguvu kutakusaidia upite hatua muhimu—upite pale ambapo jitihada zako za kupunguza uzito zilivunjikia hapo mbeleni. Kufikia wakati huo utakuwa ukihisi vizuri, na watu wataanza kukupongeza kwa ajili ya sura yako. Kuanzia hatua hiyo na kuendelea, fikira zako zitakuunga mkono, badala ya kukupinga.
Ufunguo mwingine wa kupita hatua muhimu ni kuwa na ulaji uliopunguzwa ambao ni wenye kiasi na haukufanyi kuhisi njaa au kwamba unajinyima chakula. Nilipata kuona kwamba shauri zuri zaidi kuhusu kupunguza ulaji ambalo ningeweza kupata liliongezea tu mambo yaliyosemwa katika Amkeni! ile ya Mei 22, 1989, juu ya vyakula vifaavyo. Ulaji wangu uliopunguzwa ili kupunguza uzito ni wa nafaka zenye kiasi kidogo cha mafuta au vitumbua vyenye kalori chache na nusu limau kwa kiamshakinywa, saladi nyingi yenye kiungo chenye kiasi kidogo cha mafuta kwa chakula cha mchana, na mboga zilizopikwa kwa mvuke na nyama isiyo na mafuta kwa chakula cha jioni, bila mkate au vyakula vya kumalizia mlo. Kwa kalori 1,200 hadi 1,500 kila siku, ulaji uliopunguzwa ni mgumu lakini hauumizi hata kidogo. Tofaa moja huwa kitu cha kutafuna mchana chenye kufaa, na kwa ajili ya pindi hizo chache wakati michomo ya njaa haiwezi kupuuzwa, sikuzote mimi hutumia mojapo silaha zangu za siri, siri ajabu unayopaswa kujua ya mpunguzaji uzito.
Silaha za Siri
Siri hiyo ni nini? Ni kitu ambacho chakufaa sana, hukushibisha karibu mara hiyo, hakina kalori hata kidogo, na kinagharimu kidogo tu! Maji. Inashangaza kuona yale yatimizwayo na bilauri sita au nane za maji ili kukusaidia kufanikisha kupunguza ulaji wako. Mara mwili wako ujifunzapo kwamba bilauri ya maji ndiyo azimio lako la kuitikia michomo ya njaa tumboni, inaanza kupungua. Maji, zaidi ya kingine chochote, yalinisaidia kushinda zoea langu la muda mrefu la kutafuna-tafuna vitu jioni.
Silaha nyingine ya siri kwa ajili ya kudhibiti uzito kwa muda mrefu ni mazoezi ya ukawaida. Bila shaka, kila mtu amesikia kwamba mazoezi husaidia kupunguza uzani, hivyo siri ni nini? Katika kisa hiki siri ni ule ufahamu wa kiakili uupatao wa kuhisi vizuri zaidi na kuonekana vizuri zaidi. Thawabu hiyo hulipia ule ukosefu wa vyakula fulani. Hukusaidia kuendelea, hata bila kuwa na tamaa wakati kila mtu karibu nawe anapokula chokoleti nawe unakula zabibu zilizogandishwa kwa barafu.
Kupunguza ulaji na mazoezi hukamilishana kikamilifu. Kupunguza uzito hakumaanishi kwamba lazima uonekane mgonjwa. Mazoezi ya ukawaida yatakupa sura yenye afya na kuweka misuli yako ikiwa imara na yenye nguvu. Kwa kweli, umbo zuri zaidi katika misuli yangu iliwapa wengine wazo la kwamba nilikuwa nikipunguza uzito kwa haraka zaidi ya nilivyokuwa nikipungua kwa kweli! Niliona kwamba nilihitaji michezo kadhaa ambayo ningefurahia pamoja na mtu mwingine, kama vile tenisi, na mazoezi ambayo ningeweza kufanya peke yangu wakati wowote, kama vile kuinua vyuma. Kama vile mazoezi yalivyofanya ulaji uliopunguzwa uonekane kuwa na matokeo zaidi, ulaji uliopunguzwa ulifanya mazoezi yaonekane kuwa na matokeo zaidi kwa kufunua misuli iliyokuwa imefunikwa na nyama kwa miaka kumi. Uzito wangu ulipopungua kutoka kilo 110 kufika 80, nilijipata nikitazamia kufanya programu yangu ya mazoezi pamoja na matineja wenyeji wenye afya nione kama wangedumisha mwendo wangu!
Ikiwa umekuwa na uzito kupita kiasi kwa muda mrefu kama nilivyokuwa, huenda ukawa ulizoea kuhisi umelemewa na umechoka kila asubuhi ulipokuwa ukiamka, ukijikokota siku kutwa, na kusinzia ukiwa kwenye kiti chenye starehe usiku. Kuchukua kilo 20 au 30 za ziada ni kama kuishi maisha yako ukiburuta tufe la chuma lililofungwa kwenye miguu yako kwa mnyororo! Kihalisi mimi sikukumbuka anavyohisi mtu arukapo kutoka kitandani asubuhi akiwa na hamu ya kuamka, akiwa na nishati ya ziada siku kutwa. Sasa najua anavyohisi mtu.
Vita Isiyokoma Kamwe
Kufikia lengo la uzito wako ni kama kushinda sehemu fulani tu ya vita. Lakini ingawa huenda ukawa umeshinda hiyo vita ya kwanza, ile vita halisi ndipo tu imeanza. Wale kati yetu wenye umri wa makamo na wana kazi wanazofanya wakiwa wameketi sikuzote tutakuwa waangalifu kuhusu aina ya chakula tulacho ikiwa tutaendelea kuzuia kurudi kwa uzito tuliong’ang’ana kupunguza. Ufunguo ni kufikiria ulaji wako kuwa mradi wa maishani. Waweza kurekebishwa ili kudumisha uzito badala ya kupunguza uzito, lakini haukomi kabisa. Ukirudia yale mazoea yako ya zamani, uzito wako wa ziada utakurudia.
Ufikiapo lengo la uzito wako, kwa nini usisherehekee kwa kununua mavazi mapya. Halafu fikiria kuyaondoa hayo mavazi ya zamani. Kuweka mavazi hayo ya zamani, ambayo ni makubwa mno kwa uwezekano wa kupata uzito wa ziada tena ni kama kupangia ushinde. Vaa mavazi ambayo si mapana mno, nayo yatakujulisha kwa haraka ikiwa uzito usiotakikana unaanza kurudi. Ingawa ulaji wako wa kudumisha uzito wako utakuwa wa namna-namna zaidi ya ulaji wa kupunguza uzito, hakikisha kwamba umefanya badiliko la kudumu, la maisha la kula vyakula visivyo na kiasi kingi cha mafuta na visivyo na kiasi kingi cha sukari. Pia usikome kufanya mazoezi yako kwa ukawaida. Huo ni ufunguo wa kukufanya uhisi vizuri.—Imechangwa.