Olimpiki za Barcelona—Utukufu kwa Bei Gani?
Na mleta habari za Amkeni! kutoka Hispania
KATIKA Julai 25, 1992, mpinga mshale aliyekuwa pekee, akizungukwa na nuru ya taa, alivuta upinde wake. Mshale wake wenye kichwa chenye moto ulipaa moja kwa moja na barabara katika anga la usiku. Ulipoanza kushuka, mshale ule ulipita juu ya na kugusa mwenge uliowekwa juu ya stediamu. Mwali wa Olimpiki ukawashwa. Olimpiki za Barcelona zikawa zimeanza.
Wanariadha kumi na moja elfu kutoka nchi 172 walikuwa wamekuja kushindania medali za Olimpiki 1,691. Kupatana na shime ya Olimpiki, washiriki walijitahidi kuwa “wenye mwendo wa kasi zaidi, kuruka juu zaidi, wenye nguvu zaidi,” kuliko wakati mwingine wowote—na baadhi yao walifanikiwa. Watazamaji wa televisheni waliokadiriwa kuwa 3,500,000,000 walishiriki ushindi mbalimbali na kukata tamaa mbalimbali.
Ingawa muda ambao wanariadha huvuta uangalifu wa umma ni mfupi, ushindi wa Olimpiki hutoa uwezekano wa kupata utukufu na utajiri. Olimpiki za Barcelona hazikuwa tofauti. Washindanaji wengine mashuhuri walikuwa tayari wakichuma mamilioni ya dola kwa kuvaa hadharani mavazi ya michezo, viatu vya kukimbia, miwani ya kukinga jua, na hata vifaa vya kielektroni.
Kujitoa —Ufunguo wa Utukufu wa Olimpiki
Ijapokuwa wanariadha wengi—hasa wachezaji wa mchezo wa kuzoeza viungo vya mwili na wapiga-mbizi—hucheza kwa njia ionekayo kuwa rahisi, ni miaka mingi ya mazoezi magumu ndiyo hutokeza ustadi huo. Baadhi yao wamekuwa wakijizoeza tangu walipokuwa na miaka mitano. Na michezo lazima itangulie kinginecho chote ikiwa mwanariadha ataka kufanikiwa.
Mwogeleaji Mhispania Marti̇́n López Zubero, aliyeshinda meta 200 za kuogelea kichali, alisema—labda kwa kutia chumvi kidogo: “Nimetumia theluthi ya maisha yangu ndani ya maji.” Ratiba yake ya mazoezi huanza saa kumi na moja za usiku, naye hukadiria kwamba ameogelea kilometa 8,000 kwa muda unaozidi kidogo mwaka mmoja.
Mazoezi humaanisha kuteseka, si kujinyima tu. Jackie Joyner-Kersee, aliyeshinda medali ya dhahabu ya heptathloni (muunganisho wa michezo saba) katika Seoul na Barcelona, alieleza hivi: “Mashindano ni yenye kusisimua. Mazoezi hayasisimui. . . Muulize mwanariadha yeyote: sisi sote huumia nyakati zote. Mimi natarajia mwili wangu ufanye michezo saba tofauti. Kuutarajia usiume kungekuwa kutazamia mengi mno.” Wachezaji wa kuzoeza viungo vya mwili hasa wapaswa kuwa wavumilivu zaidi. Lazima waendeleze ratiba yao ya mazoezi mara mbili kila siku bila kujali maumivu ya vifundo vya mikono na miguu vilivyoteguka, misuli na kano zilizovutika, na hata miatuko ya mifupa inayosababishwa na mkazo wenye kurudia-rudia. Lakini hatimaye kujitoa kwa namna hiyo ndiko hutokeza washindi na ile tamasha.
Msisimuko wa Olimpiki na Mmeremeto wa Dhahabu
Hakuna shaka juu yalo, tamasha ya Olimpiki inaweza kuwa yenye kuvutia. Huandaa nyakati zenye kusisimua kwa umati na ni mahali pa kuonyeshea matimizo ya riadha yenye kutokeza. Ilikuwa hivyohivyo katika Barcelona.
Vitali Scherbo mchezaji wa kuzoeza viungo vya mwili Mbelarusi alivunja rekodi kwa kushinda medali sita za dhahabu kati ya zile nane ambazo zingeweza kushindwa katika michezo ya wanaume ya kuzoeza viungo. Mchezaji wa kuzoeza viungo vya mwili Mchina Shaosahuang Li alistaajabisha kwa kupinduka hewani mara tatu katika mazoezi ya sakafuni. Karl Lewis alifanyiza historia ya Olimpiki kwa kushinda mchezo wa kuruka mbali kwa mara ya tatu mfululizo. Kwa upande mwingine, mshindi wa medali ya fedha wa kutoka Japani katika mbio ndefu za marathoni za wanawake, Yuko Arimori, alishangiliwa kwa adabu yake. Ujapokuwa uchovu wake, alizunguka stediamu akiinamia umati katika mtindo wa Kijapani, na kisha akamwinamia mshindi.
Uwezekano mbalimbali wa kibiashara wa Olimpiki haukusahauliwa na kampuni za mataifa mengi. Kampuni hizo hulipa pesa nyingi ili zishiriki utukufu wa Olimpiki kwa kudhamini michezo yenyewe au timu za Olimpiki za kitaifa.
Kutumia Dawa za Kulevya Ili Kujipatia Utukufu
Mazoezi yasiyokoma na uwezo wa kiasili—ingawa ni ya maana— siyo funguo pekee za kupata fanikio la Olimpiki. Wanariadha wengi hutegemea dawa za kulevya ziwape nafasi bora zaidi za kushinda. Dawa hizo za kulevya zaweza kuwa ni zile za kujenga misuli au hormoni za ukuzi wa kibinadamu za kujenga misuli (hasa hutumiwa sana na wanyanyuaji vyuma na wanariadha wa uwanjani; dawa zinazozuia ufyonzaji wa adrenalini katika chembe za moyo ili kupunguza mpigo wa moyo (ili kufanyia maendeleo upigaji mshale na ulengaji shabaha); au erithropoietini ili kuchochea utokezaji wa chembe nyekundu za damu (zilizo muhimu kwa mbio za baiskeli na mbio ndefu).
Ijapokuwa wanariadha wanajua hatari, mkazo wa kutumia dawa za kulevya zilizo haramu ni mwingi mno. Mwanariadha Mjerumani Gaby Bussmann, mwanatimu mwenzi wa Birgit Dressel, aliyekufa katika 1987 kwa kutumia dawa za kulevya 20 tofauti-tofauti, hueleza hivi: “Kuna michezo fulani ya pekee ambayo katika hiyo ni vigumu kufuzu kwenda kwenye Olimpiki bila kutumia dawa za kulevya.”
Makocha wa wanariadha kwa kawaida hushiriki sehemu katika kutumia dawa za kulevya kwa wanariadha; hata huenda wakawa ndio wanaopendekeza hilo. Aliyekuwa hapo zamani kocha wa Ujerumani Mashariki Winfried Heinicke hukiri hivi: “Niliwaambia kwamba ikiwa walitaka kwenda kwenye Olimpiki, lazima wafanye hilo [watumie dawa za kulevya].” Kwa wazi, idadi kubwa ya washindani huthamini ushindi zaidi ya unyoofu—hata zaidi ya afya yao. Uchunguzi wa karibuni wa wanariadha mashuhuri ulifunua kwamba asilimia 52 wangetumia dawa ya kulevya ya kuwaziwa ifanyayo maajabu inayohakikisha kuwageuza kuwa washindi hata kama ingewaua baada ya miaka mitano yenye utukufu ya umashuhuri.
Mtimuaji mbio fupi Mwingereza Jason Livingston alirudishwa nyumbani kutoka Barcelona kwa aibu baada ya uchunguzi kuonyesha kwamba alikuwa ametumia dawa za kujenga misuli. Harry Reynolds wa United States, mshikiliaji wa rekodi ya ulimwengu katika meta 400, hakukimbia kamwe katika michezo. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika 1990 uligundua kwamba alikuwa ametumia dawa za kulevya na kuongoza kwenye kusimamishwa kwake asishiriki michezoni kwa miaka miwili, ambako kulimpotezea uwezekano wa kupata medali ya Olimpiki na pia dola milioni moja za kudhaminiwa alizopoteza.
Hata hivyo, watumiaji wengi wa dawa za kulevya hawashikwi. Ijapokuwa michunguzo kari-bu 2,000 kuona kwamba dawa za kulevya hazikutumiwa wakati wa michezo ya Barcelona, wanariadha wasio wanyoofu wangali wangeweza kuepuka kupatikana kwa kutumia dawa za kulevya zisizoonekana katika michunguzo ya mkojo. “Pupa ya kupata ushindi na pesa imetokeza ulimwengu mchafu ambapo inakuwa vigumu kutofautisha kati ya kanuni za mwenendo na ukosefu wa unyoofu,” likaeleza El País gazeti la Hispania.
Bila shaka, washindi wengi wa medali walifanikiwa, si kwa sababu ya dawa za kulevya, bali kwa sababu tu ya miaka mingi ya kujidhabihu. Je! dhabihu hizo zilistahili?
Utukufu Wenye Kudumu
Gail Devers, ambaye hakutarajia kushinda mbio za meta 100 za wanawake, alishangilia baada ya ushindi wake. “Ikiwa mtu yeyote aamini kwamba ndoto hutimia, ni mimi,” akasema. Muda usiozidi miaka miwili mbeleni, hangeweza kutembea hata kidogo, na ilisemekana kwamba miguu yote miwili ingekatwa kwa sababu ya matatizo katika kumtibu ugonjwa wa Graves. Pablo Morales, aliyekuwa amestaafu mashindano ya kuogelea lakini akaanza mazoezi mwaka mmoja kabla ya michezo ya Olimpiki naye akashinda medali ya dhahabu katika mchezo wa kuogelea meta 100 kipepeo, alikubaliana naye. “Ulikuwa wakati wangu hatimaye, ndoto iliyotimia,” akasema.
Bila kuepukika, wanariadha wengi zaidi hawatakuwa mabingwa kamwe. Kweli, baadhi yao huhisi kwamba “jambo la maana katika Michezo ya Olimpiki si kushinda bali kushiriki.” Lakini wanariadha wengine, waliotegemea sana kuwa mabingwa, walirudi nyumbani bila ndoto zao kutimia. Mnyanyua vyuma Ibragim Samadov alikuwa ametamani sana kushinda medali ya dhahabu—lakini alikuwa wa tatu tu katika mchezo huo. “Kwa medali ya dhahabu, ningaliongoza maisha yangu, ningalisomea kazi-maisha, ningalisaidia familia yangu. Sasa sijui la kufanya,” akapiga kite. Na hata washindi huelekeana na wakati wenye kuumiza sana hisia uhodari wao uanzapo kupungua.
Aliyekuwa hapo zamani mchezaji tenisi Anna Dmitrieva alisema hivi: “Shirika la michezo [la Sovieti] halikujali watu. Walifikiri tu: ‘Wewe enda zako nasi tutapata 10 zaidi kama wewe.’” Hali kadhalika, Henry Carr, mshindi wa medali mbili za dhahabu katika Tokyo katika 1964, alikubali hivi: “Hata mtu anapokuwa bora kupita wote, ni danganyo tu. Kwa nini? Kwa sababu haidumu, wala hairidhishi kikweli. Upesi wengine huwa mabingwa na kuwashinda na kwa kawaida wao husahauliwa.”
Utukufu wa Olimpiki wenye kupita kasi hauwezi kulinganishwa na thawabu ya uhai wa milele, ambayo Mungu huahidi wale wamtumikiao. Thawabu hiyo hutaka mazoezi ya kiroho badala ya yale ya kiriadha. Hivyo, Paulo alimwandikia Timotheo hivi: “Kujizoeza kupata nguvu za mwili [kihalisi, “kuzoeza viungo vya mwili”] kwafaa kidogo, lakini utawa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.”—1 Timotheo 4:8.
Michezo ya Olimpiki hutetea manufaa za kuzoeza mwili—ambazo ni za muda hata katika hali bora kabisa. Zaonyesha ulimwengu yale wanariadha wawezayo kufanya kupitia kujitoa na kujinyima. Sifa hizo huhitajiwa pia ili kushinda mbio za Kikristo. Mbio hizo, tofauti na mchezo wowote wa Olimpiki, zitaleta manufaa za kudumu kwa wote wamalizao mwendo. Kwa hiyo, Wakristo wafanya vema kuiga, si wanariadha, bali Yesu Kristo, kwa ‘kumaliza mazoezi yao’ na ‘kupiga mbio zao kwa uvumilivu.’—1 Petro. 5:10, NW; Waebrania 12:1.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Wapiga-mbizi wakishindana katika Olimpiki. Barcelona katika upande wa nyuma
[Hisani]
Picha: Sipa Sport
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kushindana michezo katika fito sambamba
[Hisani]
Picha: Sipa Sport
[Picha katika ukurasa wa 25]
Katika finali za meta 100, mpiga mbio aliye kulia kabisa alishinda dhahab
[Hisani]
Picha: Sipa Sport