Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 11/8 kur. 24-27
  • Michezo ya Olimpiki ya Norway—Je, Ile Miradi Ilitosha?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Michezo ya Olimpiki ya Norway—Je, Ile Miradi Ilitosha?
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Olimpiki na Biashara Kubwa
  • Citius, Altius, Fortius
  • Ulinzi wa Kimazingira, Kazi ya Kupunguza Shida za Wenye Maafa, na Jitihada za Amani
  • Miradi Itakayotimizwa
  • Malengo ya Olimpiki Yanazorota
    Amkeni!—2000
  • Michezo ya Olimpiki Yarudi Nyumbani
    Amkeni!—2004
  • Kutoka Olympia Hadi Sydney
    Amkeni!—2000
  • Olimpiki za Barcelona—Utukufu kwa Bei Gani?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 11/8 kur. 24-27

Michezo ya Olimpiki ya Norway—Je, Ile Miradi Ilitosha?

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA NORWAY

WAKATI Halmashauri ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) ilipoanzishwa miaka mia moja iliyopita, ilikuwa na matazamio makubwa. Shabaha ilikuwa kuongezea udugu na amani kwa kufanya vijana wa ulimwengu wote wakusanyike kila mwaka wa nne kwenye uwanja wa michezo bila faida ya kifedha. Ilitumainiwa kwamba shindano safi lingetokeza ufungamano na upatanisho miongoni mwa vikundi vya watu. Kwa msingi huu ile Michezo ya Olimpiki ya kale ilifufuliwa nyakati za kisasa.

Kutoka mwanzo wa chini katika Athens, Ugiriki, katika 1896, hiyo Michezo ya Kiangazi imesitawi ikawa msherehekeo ulio mkubwa zaidi wa michezo ulimwenguni, ikiwa na kilele cha washiriki 11,000 kutoka mataifa zaidi ya 170. Michezo ya Majira ya Baridi ya kwanza ilifanyiwa Chamonix, Ufaransa, katika 1924, na sikuzote imekuwa “mnuna” wa ile Michezo ya Kiangazi. Hata hivyo, karibu wanariadha 2,000 kutoka mataifa karibu 70 walikusanywa kwa ajili ya Olimpiki za Majira ya Baridi kule Lillehammer, Norway, siku ya Februari 12-27, 1994.a

Lile wazo la udugu na urafiki, kama lilivyofananishwa na yale mapete maarufu ya Olimpiki, na la “akili timamu katika mwili timamu” laonekana kuwa lahitajiwa sasa zaidi ya wakati mwingineo. Miradi hii ilitimiza sehemu gani kwenye Michezo ya Olimpiki katika Lillehammer?

Olimpiki na Biashara Kubwa

Ule utangazaji wa habari nyingi ulitokeza upendezi mkubwa sana wa umma katika Olimpiki. Idadi ya watu wa vyombo vya habari walio mara nne za wanariadha walikuwako Lillehammer, na idadi isiyopata kuonekana ya watu wapatao bilioni mbili waliitazama Michezo ya Majira ya Baridi katika televisheni. Hivyo Olimpiki zimekuwa biashara yenye faida nono kwa shughuli za biashara zenye nguvu, na mifumo ya televisheni na wadhamini hushindania kupata mapendeleo na mikataba maalumu.

Wawakilishi wa kuuza bidhaa na wa viwanda kutoka sehemu zote ulimwenguni waliihudhuria Michezo katika Lillehammer, na wengi wao waliona mkutano huu wa kimataifa wenye tungamo la watu wengi kuwa fursa ya kusitawisha mahusiano ya kibiashara na kupanga warsha na makongamano. Mashirika, madogo na makubwa pia, yalionyesha yana uwezo wa kubuni vitu kwa kuwa na bidhaa nyingi sana tofauti-tofauti za Olimpiki zilizouzwa—kila kitu kuanzia pini na postikadi hadi vyombo vya jikoni na nguo.

Kama kawaida, kwa wenyeji mambo yalipinduka mrama kabisa wakati wa Michezo hiyo. Lile miminiko la wafanyakazi wa Olimpiki, washiriki, na viongozi lilirudufisha idadi ya wakaaji wa Lillehammer, ambayo kwa kawaida hupita sana 20,000. Kwa kuongezea hilo, kulikuwa na “uvamizi” wa watazamaji 100,000. Wengine wa wakaaji wenyeji walichagua kwenda likizoni ili kuutoroka msongamano huo nao walirejezewa kwa mzaha kuwa “wakimbizi wa michezo.”

Namna gani ule upande wa ile Michezo na miradi ya Olimpiki?

Citius, Altius, Fortius

Kwa kupatana na shime ya Olimpiki—Citius, altius, fortius (Yenye mbio zaidi, ya juu zaidi, yenye nguvu zaidi)—mwana-Olimpiki hujaribu kuvunja rekodi na kushinda washindani wake. Ili kutimiza hilo leo, wana-Olimpiki hukuta kwamba kwa kawaida haitoshi kufanya michezo kuwa utendaji wa wakati wa starehe tu. Hiyo ni kazi ya wakati wote na ni riziki kwa wana-Olimpiki walio wengi, kwa kuwa yale mapato yatokanayo na kutumiwa kwao katika matangazo ya kibiashara hutegemea sana matokeo watimizayo. Imekuwa lazima uanamichezo usio na malipo na wa muda tu uupishe ule wa kuchuma fedha na ulio wa wakati wote.

Baada ya hilo, umma nao hupata tamasha na utumbuizo wote watakao. Rekodi kadhaa zilizowekwa wakati wa Olimpiki za majuzi zashuhudia kwamba kumekuwako matimizo yasiyofikirika miongo michache iliyopita. Hii haitokani na mazoezi yaliyoongezeka na kujitaalamisha kwa kadiri kubwa zaidi tu bali yatokana na vifaa vilivyoboreshwa na mastakimu nzuri zaidi pia. Kwa kielelezo, kwenye ile Michezo ya Lillehammer rekodi nne za ulimwengu na rekodi tano za Olimpiki ziliwekwa wakati wa yale matukio matano ya utelezi-kasi wa barafuni kwa wanaume. Sifa fulani ilipewa lile jumba jipya la utelezi, ambapo hatua za kisayansi zilifuatwa kuboresha barafu kabisa kwa utelezi wa wakati wote.

Kwa kusikitisha, wanariadha fulani huonekana wazi kuwa hawashindani “katika ile roho ya kweli ya uanamichezo, kwa fahari ya kucheza tu,” kama vile waahidivyo katika kile kiapo cha Olimpiki. Michezo ya Majira ya Baridi ya mwaka huu ilikuwa na washinde fulani wabaya, na wanariadha wachache walijaribu kuhujumu washindani wenzao. Katika miaka ya majuzi imekuwa lazima kupambana na dawa za kulevya na steroidi. Kule Lillehammer, mshiriki mmoja aliagizwa aende nyumbani ile siku ya kufungua kwa sababu ya kutumia dawa za kuchochea utendaji. Hata hivyo, wakati wa Michezo hiyo hakuna mmoja wa wanariadha aliyepatikana kuwa mtumia-madawa alipopimwa.

Kulikuwako njia fulani mpya za kushughulika na miradi ya Olimpiki kuhusiana na ile Michezo ya Lillehammer.

Ulinzi wa Kimazingira, Kazi ya Kupunguza Shida za Wenye Maafa, na Jitihada za Amani

Shughuli kubwa sana kama Olimpiki, inayohusisha kazi nyingi sana za kusitawisha eneo na kutokeza takataka nyingi, “haifikirii mazingira wala haina urafiki kwa mazingira.” (Miljøspesial, taarifa ya kimazingira kwa Olimpiki za Lillehammer) Watu wengi walihisi hii haikupatana na ile roho ya Olimpiki na wakadokeza kuweka kielelezo kwa kufanya hiyo Michezo ya Majira ya Baridi ya 1994 itunze mazingira kwa njia isiyo na kifani. Wazo hilo lilifuatwa, na ile Michezo ya Lillehammer ikaja kuvuta uangalifu wa kimataifa kuwa “ndiyo Michezo ya Olimpiki ya kwanza kuwa na sura ‘ya kijani-kibichi.’” Hii ilimaanisha nini?

Mahali, utengenezaji, na uendeshaji wa muda mrefu wa sehemu mpya za kufanyia michezo vilifikiriwa ili kupunguza yale matokeo mabaya juu ya mazingira. Katika nyanja zote, vifaa vyenye kutunza mazingira na viwezavyo kutengenezwa upya kwa utumizi mwingine, kama vile mbao, mawe, na bodi za karatasi, vilitumiwa sana, na viwango vya juu vya kimazingira vikawekwa kwa wadhamini na wagawaji wote. Uvutaji sigareti ulipigwa marufuku kabisa ndani ya majengo yote.

Kuchunguza miradi ya Olimpiki kuliongoza pia kwenye uanzilishi wa ile hazina ya Msaada wa Olimpiki ya Lillehammer ya kupunguza shida za wenye maafa. Ilianza ikiwa mkusanyo wa kusaidia watoto katika lile jiji la zamani la Olimpiki la Sarajevo katika Bosnia na Herzegovina, kisha baadaye ikapanuliwa kusaidia majeruhi wachanga wa vita kotekote ulimwenguni. Hazina hiyo iliongezewa kichocheo kikubwa sana baada ya mmojapo washindi wa medali za dhahabu kuchanga fedha zake zote za ushindi kutokana na tukio mojapo (karibu dola 30,000) kwa kuunga mkono. Wale waanzishi watumainia kwamba Msaada wa Olimpiki utaendelea katika Michezo ya wakati ujao.

Yale mafungulia-njiwa ya desturi katika mwadhimisho wa kuanza Olimpiki yalipelekea ulimwengu ujumbe kimya wa amani. Mradi wa amani ulikaziwa fikira zaidi ilipofika ile Michezo ya Majira ya Baridi ya 1994, kwa kuwa Juan Antonio Samaranch, yule msimamizi wa IOC wa kutoka Catalonia, alisema mara nyingi juu ya amani kwa watu wote wa dunia.

Miradi Itakayotimizwa

Miradi ya Olimpiki yaonyesha tamaa iliyotia mizizi sana katika wanadamu wote—tamaa ya udugu, amani, uadilifu, shangwe, na utimamu wa kimwili na wa kiakili. Michezo ya Majira ya Baridi ya mwaka huu ilisifiwa sana kwa kufanya fikira zikazwe tena juu ya ile miradi ya asili ya Olimpiki na ikatajwa kuwa “Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi iliyo mizuri kupita yote.” Hata hivyo, ile harakati ya Olimpiki haikufikia miradi yayo.

Fahari na ubiashara zilielekea kukaziwa kuliko viwango bora vya msingi vya michezo. Mashindano hayo yaligeuka mara nyingi kuwa ushindani mkali uliotokeza kujiona na kutukuza mataifa badala ya udugu na upatanisho.

Je, kuna njia ya kutimiza matamanio ya Olimpiki? Biblia huonyesha kwamba jitihada za kibinadamu za kupata ulimwengu bora kabisa zitashindwa. Hata hivyo, Ufalme wa Mungu utachukua hatua karibuni kuleta hali kamilifu, za paradiso duniani. (Yeremia 10:23; 2 Petro 3:13) Ulimwengu wa jinsi hiyo hautegemei wala msingi wa kusitawisha riadha wala wa kufuata kanuni na mapokeo ya Olimpiki kwa uaminifu-mshikamanifu bali juu ya ujitoaji wa kweli kwa Muumba. Mtume Paulo alisema: “Kwa maana mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa kidogo; lakini ujitoaji kimungu ni wenye manufaa kwa mambo yote, kwa kuwa una ahadi ya uhai wa sasa na ule utakaokuja.” Kwa wale leo wanaojizoeza “ujitoaji kimungu ukiwa shabaha [yao],” tokeo kwa kweli litakuwa utimamu wa akili katika mwili timamu.—1 Timotheo 4:7, 8, NW.

[Maelezo ya Chini]

a Michezo ya Olimpiki ilipangwa katika 1992 pia, lakini hiyo ndiyo mara ya mwisho Michezo ya Kiangazi na ya Majira ya Baridi kufanywa mwaka uleule mmoja. Kuanzia sasa na kuendelea imeratibiwa kubadilishana kila mwaka wa pili

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

Mchanganyiko wa Kidini wa Olimpiki

Michezo ya Olimpiki ina mizizi katika dini ya Kigiriki. Ilizaliwa ikiwa msherehekeo wa kidini kuheshimu Zeu, aliye mkuu zaidi miongoni mwa miungu ya Kigiriki. Sehemu mbalimbali za Michezo ya kisasa zina msisimko wa uanadini: desturi za kustahi kwa uzito ile bendera ya Olimpiki, ule mwali “mtakatifu,” na kile kiapo cha Olimpiki. Ule wimbo wa Kigiriki wa karibu miaka 100 ulioimbwa kwenye ufunguzi wa Michezo hiyo ulitafsiriwa katika Kinorway kwa mwadhimisho wa ufunguzi katika Lillehammer. Wimbo huu wa Olimpiki una madokezo yenye hisia nyingi za kidini. Waeleweka kuwa wimbo kwa Zeu. Maneno yao yatia ndani taarifa zinazofuata: “Roho wa kale usiyeweza kufa,/Baba yao wenye kweli, wazuri na wema,/Shuka, tokea, tuangazie nuru yako/ . . . Huisha na himiza michezo bora hiyo!/ . . . Mataifa yote yasongamana kukucha,/ Ewe roho wa kale usiyeweza kufa!”

Kanisa la Kilutheri la Norway lilipanga, kupitia Halmashauri yalo yenyewe ya Olimpiki, kuwe na programu ndefu ya kimuziki na kidini. Matengenezo makubwa yote ya kanisa yaliwakilishwa katika mradi mkubwa wa tangamano moja la dini mbalimbali. Kasisi wa jeshi aliye rasmi wa Olimpiki na kikoa cha makasisi wa kimataifa na muungano wa makanisa walikuwa katika Kijiji cha Olimpiki kule Lillehammer.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Juu: Mteleza-kasi wa barafuni akienda akashinde medali ya dhahabu katika ile mbio ya meta 10,000

Katikati: Michezo-hewani ya mtindo-huru ilikuwa tukio jipya la Olimpiki

Chini: Kushindana katika mteremko—kwa miendo ya kilometa zaidi ya 120 kwa saa

[Hisani]

Picha: NTB

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki