Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 2/8 kur. 26-27
  • Nyungunyungu wa Gini—Siku Zake za Mwisho

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nyungunyungu wa Gini—Siku Zake za Mwisho
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Yule Nyungunyungu Hatari wa Gini
  • Historia Ndefu
  • Matibabu
  • Kumwangamiza Nyungunyungu wa Gini
  • Minyoo wa Ajabu
    Amkeni!—2003
  • Gundi ya Mnyoo Anayeitwa Sandcastle
    Amkeni!—2011
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2011
  • Ghuba Maridadi
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 2/8 kur. 26-27

Nyungunyungu wa Gini—Siku Zake za Mwisho

Na mleta habari za Amkeni! katika Naijeria

SIKU ni yenye joto, kama kila siku. Chinyere afunga mtoto mgongoni pake na kuchukua vibuyu viwili vilivyokaushwa, ajiunga na wanavijiji wengine katika barabara yenye vumbi. Pamoja watembea kupitia mashamba yaliyounguzwa na jua, kwenda kwenye ziwa dogo, ambalo ndilo chanzo pekee cha maji katika eneo hilo. Kwenye ziwa ateremka kwa uangalifu zile kingo za matope zenye kuteleza na kuingia ndani ya maji yenye kufika magotini ili kuteka maji.

Awaona mamba wanaolala kwenye nyasi iliyonyauka kando ya kingo na wale wanaokaa chini tu ya uso wa ziwa, lakini yeye hawaogopi. Kama vile mtu mmoja kwenye kando ya ziwa alivyosema: “Hatuwasumbui, nao hawatusumbui.”

Hakika haiwezi kusemwa hivyo kuhusu viumbe wengine wanaoishi ziwani. Chinyere hawaoni, na hawezi kuwaona; ni wadogo mno. Wamo katika maji yanayoingia ndani ya vibuyu.

Yule Nyungunyungu Hatari wa Gini

Chinyere arudi kwenye nyumba yake ya matope iliyoezekwa kwa nyasi na kumwaga yale maji katika nyungu. Baada ya udongo kutulia, achota maji na kuyanywa. Mwaka mmoja baadaye aona kitu fulani katika sehemu ya chini ya mguu wake ambacho huhisi na kuonekana kama mshipa uliovimba. Lakini si mshipa. Yule kiumbe mdogo awezaye kuonwa kwa darubini tu aliyekuwa katika maji aliyokuwa amekunywa amekua akawa nyungunyungu wa gini mwembamba mwenye urefu wa sentimeta 80.

Upesi nyungunyungu huyo atatokeza lengelenge lenye uchungu ngozini mwake. Kisha, lengelenge hilo litapasuka na yule nyungunyungu wa rangi-krimu ataanza kutoka sentimeta chache kila siku. Itachukua majuma mawili hadi manne—labda muda mrefu zaidi—ndipo atoke kabisa. Katika sehemu kubwa ya wakati huo, yawezekana sana kwamba Chinyere atakua hajiwezi kimwili, na uchungu wake utakuwa mwingi sana. Huenda lengelenge hilo lililopasuka likaambukiwa na bakteria, na kuongoza kwenye ugonjwa wa pepo punda, magonjwa ya bakteria, yabisi, au hata majipu.

Chinyere ana nyungunyungu mmoja tu, lakini si jambo lisilo la kawaida kuambukiwa na nyungunyungu kadhaa, au hata dazeni moja au zaidi, kwa wakati mmoja. Kwa kawaida zinatokea katika sehemu za chini za mwili, lakini nyakati nyingine zinahama na kutokea katika sehemu nyingine za mwili kama vile kichwa, matiti, na ulimi.

Hata hivyo, kwa sababu ya kampeni ya kimataifa ya kumwangamiza, huenda nyungunyungu huyo akaangamizwa karibuni. Ulimwenguni pote, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, sasa nyungunyungu huyo anataabisha watu wanaopungua milioni tatu, ambao karibu wote huishi katika Pakistani, India, na nchi 17 za Kiafrika. Muda ulio chini ya mwongo mmoja wa miaka uliopita, alitaabisha kufikia milioni kumi. Katika Esia, nyungunyungu wa gini sasa anakaribia sana kuangamizwa; katika nchi nyingi zaidi za Kiafrika zinazoathiriwa, huenda kimelea huyo akaangamizwa kufikia mwisho wa 1995.

Historia Ndefu

Nyungunyungu wa gini amesumbua ainabinadamu tangu zamani za kale, hasa katika Mashariki ya Kati na Afrika. Nyungunyungu wa gini aliyekaushwa alipatikana katika msichana wa umri wa miaka 13 ambaye mwili wake uliokaushwa uligunduliwa katika Misri. Kwa huzuni, miguu yake miwili ilikuwa imekatwa, labda ili kukomesha donda ndugu lililotokana na kuambukiwa na nyungunyungu wa gini.

Marejezo ni mengi katika maandishi ya kale. Rejezo lililo la mapema zaidi linalomrejezea nyungunyungu wa gini linapatikana katika maandishi ya Misri. Lilieleza zoea la kumzungusha kwenye kijiti nyungunyungu huyo aliyekuwa akitokea. Katika karne ya pili K.W.K., Mgiriki aitwaye Agatharkedezi wa Cnidus aliandika hivi: “Watu waliougua kwenye Bahari Nyekundu walipatwa na maradhi mengi mageni na yasiyojulikana hapo zamani, miongoni mwao minyoo wengine, nyoka wadogo, waliowatoka, wakiguguna miguu na mikono yao, na walipoguswa walirudi, wakajiviringisha ndani ya misuli, na kutokeza humo uchungu usiovumilika.”

Matibabu

Ile mithali, “Ni afadhali kuzuia kuliko kuponya,” hakika hutumika kuhusu maradhi ya nyungunyungu wa gini. Kwa kweli, hakuna ponyo. Mtu akiisha kunywa maji yenye mabuu, hakuna liwezalo kufanywa kitiba mpaka nyungunyungu huyo akaribie kutokea ngozini, kabla hajatokeza lengelenge. Kwenye hatua hiyo nyakati nyingine daktari stadi aweza kuondoa kimelea huyo baada ya kukata kidogo kando na katikati ya urefu wa nyungunyungu huyo. Kisha atumia chombo kama ndoana ili kutokeza nje kisehemu cha nyungunyungu huyo, na kufanyiza kitanzi juu ya ngozi. Mwishowe avuta kwa uangalifu sehemu inayobaki ya nyungunyungu huyo, ni upasuaji unaokamilishwa katika muda wa dakika kadhaa.

Hata hivyo, mara nyungunyungu akianza kujitokeza mwenyewe, mwasho wa sehemu iliyopasuka huzuia nyungunyungu huyo asivutwe kwa urahisi. Ikiwa hivyo, jambo pekee ambalo mgonjwa aweza kufanya ni kufuata lile zoea la kale la kuzungusha nyungunyungu huyo anayetokea kwenye kijiti kidogo kadiri atokavyo. Lazima tahadhari ichukuliwe nyungunyungu huyo asikatike. Akikatika, ile sehemu inayobaki hurudi ndani ya mgonjwa na hilo hutokeza mwasho, uchungu, na ambukizo zaidi.

Hakuna linaloweza kufanywa kutibu nyungunyungu wa gini akiwa ndani ya wanadamu. Lakini mengi yaweza kufanywa kuangamiza kimelea huyo kabla hajaingia ndani ya mwili wa kibinadamu.

Kumwangamiza Nyungunyungu wa Gini

Njia moja ni kuandalia watu chanzo cha maji safi, kama vile visima vilivyochimbwa, ambavyo haviwezi kuingiwa na mabuu ya nyungunyungu wa gini. Njia nyingine ni kufundisha wanavijiji ama kuchemsha maji yao ya kunywa ama kuyachuja kwa kuyamwaga kupitia kitambaa chembamba. Chaguo la tatu ni kutia dawa katika maji ya ziwa ambayo huua mabuu lakini haidhuru wanadamu au wanyama.

Katika mataifa yote yanayobaki ambako ugonjwa huo umeenea, programu zenye juhudi za kuangamiza zimeanzishwa ili kutafuta-tafuta vijiji ambavyo wakazi wanasumbuliwa na nyungunyungu wa gini na kuwasaidia wazuie kuambukizwa. Kufikia hapo, jitihada hizo zimethibitika kuwa zenye kufanikiwa sana. Sasa yaonekana kama nyungunyungu wa gini ameingia katika siku zake za mwisho. Na hakuna atakayesikitikia kuangamia kwake.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Maji yaliyo na mabuu ya nyungunyungu wa gini hayapasi kunywewa isipokuwa kwanza yachemshwe au kuchujwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki