Kionyeshi cha Uhuru
UNDP (Programu ya Usitawi ya Umoja wa Mataifa) ilichapisha “Kionyeshi cha Uhuru wa Kibinadamu” kilichoonyesha ni uhuru wa kadiri gani unaofurahiwa na idadi ya watu wa nchi mbalimbali 88. Kikitegemea haki na uhuru mbalimbali 40 uliowekwa katika Tangazo la Ulimwengu Wote Mzima la Haki za Kibinadamu, kionyeshi hicho huipa kila nchi pointi moja kwa kila uhuru.
Kulingana na The Courier gazeti lichapishwalo na Jumuiya ya Ulaya, baadhi ya uhuru uliokadiriwa na UNDP ni: haki ya kukusanyika na kushirikiana kwa amani; uhuru wa kutolazimishwa dini au wazo la serikali katika shule; uhuru wa kuchapisha vitabu kwa kujitegemea; uhuru wa kutonyang’anywa mali ya kibinafsi ovyoovyo; na haki ya kibinafsi ya kufuata dini yoyote. Nchi hutimizaje matakwa hayo?
Ingawa hakuna nchi iliyopata pointi zote 40, Swedeni na Denmarki zilikaribia zaidi zikiwa na pointi 38, na Uholanzi ikawa ya tatu ikiwa na pointi 37. Kuelekea chini ya orodha zilikuwako nchi zilizopata pointi chache kama moja au mbili. Nchi moja iliyokuwa chini kabisa ya orodha haikupewa pointi hata moja. Hata hivyo, yapasa iangaliwe, yasema ripoti ya UNDP, kwamba “kionyeshi hicho chahusu hali katika 1985” na tangu hapo ulimwengu umepata uhuru mwingi zaidi.
Gazeti la Uholanzi Internationale Samenwerking husema kwamba “nchi zenye kusitawi kama vile Kosta Rika (namba 18), Papua New Guinea (namba 20), na Venezuela (namba 22) zilipata pointi za juu zaidi katika orodha kuliko nchi za Ulaya za Ailandi (namba 23) na Hispania (namba 24).”
Ripoti hiyo yamalizia kwamba, kwa kawaida, kuna ufungamano kati ya uhuru na usitawi. Nchi nyingi zaidi zenye kadiri kubwa ya uhuru huonekana zikifurahia kiwango cha juu cha usitawi wa kibinadamu, hali nchi zilizo na uhuru kidogo mara nyingi hulemewa na usitawi mbaya pia. Yasema hivi ripoti hiyo ya UNDP: “Uhuru hufungulia nguvu za ubunifu za watu wanyakue kwa ajili yao wenyewe na jamii zao fursa za kiuchumi.”
Bila shaka, uhuru mbalimbali 40 ulioorodheshwa na UNDP kuwa miradi yenye kutamanika katika jamii ya kibinadamu haukutia ndani uhuru wa kutokuwa na matokeo yenye kuharibu ya ugonjwa, uzee, na kifo. Ni Ufalme wa Mungu tu ukiwa mikononi mwa Mwana wake Yesu Kristo, ambao utatupatia uhuru mbalimbali kama huo. Biblia huahidi kwamba “viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.”—Warumi 8:21.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Kubomolewa kwa Ukuta wa Berlin kulionyesha uhuru mkubwa zaidi katika Ulaya Mashariki