Je! Wewe Wahitaji Meno Bandia?
MENO bandia, mara nyingi huwa kitu cha kufanyiwa usheshi, lakini si jambo la kuchekesha kwa wale wayatumiao. Ikiwa wewe una meno yako yote ya asili yakiwa katika hali nzuri, suala la meno bandia huenda likaonekana kuwa si la maana kwako. Lakini hata ikiwa wewe hutalazimika kamwe kukabili suala hilo, yanayosemwa katika makala hii huenda yakakusaidia uthamini baraka ya kuwa na meno yenye afya na kukufanya uazimie kuyahifadhi kama yalivyo—angalau kwa kadiri yakutegemea wewe.
Lakini kwa nini watu wengi waliofikiri kuwa walikuwa wakitunza meno yao kwa kudhamiria hugundua siku moja kwamba meno yao yanalegea? Muulize daktari yeyote wa meno naye atakuambia yafuatayo. Mara watu wakiisha kupita umri wa miaka 30, kisababishi kikubwa cha kupoteza meno ni ugonjwa wa fizi. Hata hivyo, mtu aweza pia kupoteza meno kwa sababu ya aksidenti au kuoza kwa meno.
Lakini je, kweli wewe wahitaji meno bandia ikiwa umepoteza baadhi ya meno yako au yote?a Kwa nini watu wengine huonekana wakifanya vema bila kuwa nayo? Je! meno bandia ni bidhaa nyingine tu ya kibiashara wanalosukumizwa umma?
Kwa Nini Meno Bandia?
Ili kujibu maswali hayo, acheni tuchunguze kazi za meno yetu. Yanafanya mengi zaidi ya kuathiri tu sura yetu. Tutafunapo chakula chetu, kinachanwa-chanwa ili umajimaji wenye kusaidia kuyeyusha uweze kuchanganywa na vipande hivyo vidogo-vidogo, ili mwili uweze kufyonza vilishaji. Lakini ikiwa tuna meno machache au hatuna kabisa, chakula chetu hakitaweza kusagwa vya kutosha. Hata sehemu ngumu za fizi imara sana haziwezi kufanya hivyo vya kutosha. Hiyo ndiyo sababu watu wasio na meno ambao hujaribu kumeza chakula kwa kutumia kahawa, chai, au kinywaji kingine huenda wakawa na matatizo ya kuyeyusha chakula tumboni. Wakati hata meno machache yamepotezwa, ulaji ni wa kiasi kwa sababu chakula kigumu au chenye nyuzinyuzi ambacho hutaka kutafunwa zaidi kwa kawaida huepukwa.
Meno hutusaidia pia kuongea, manufaa ambayo hatufikirii sana mpaka baadhi yayo yawe yamepotezwa. Husaida ulimi na midomo kufanyiza sauti za usemi zilizo muhimu kwa kueleweka. Kwa mfano, sauti za usemi kama vile konsonanti mwishoni mwa silabi haziwezi kufanywa ifaavyo bila meno kuwapo. Yawezekana umeona jambo hilo ikiwa umepata kumsikia mtu asiye na meno akisema. Hivyo, mtu aliye na meno bandia lazima apatanishe ulimi wake nayo ili sauti ziweze kuwa sawa tena. Ijapokuwa huenda jambo hilo likachukua wakati, matokeo kwa kawaida ni afadhali kuliko wakati hakuna meno.
Vipi kuimba au kupiga ala fulani za muziki mtu anapokuwa na meno bandia? Kwa kawaida utendaji huo mbalimbali waweza kufanywa kwa mafanikio kwa kurekebisha meno bandia kwa njia mbalimbali. Waimbaji, wachezaji wa kuigiza, wapigaji wa ala za muziki zenye kutumia upepo, wahudumu, na baadhi ya violezo vya wapigaji picha wangeona kazi zao zikiwa ngumu sana kufanya, au wasiweze kabisa kuzifanywa bila meno.
Sura ya kibinafsi pia huathiriwa na kukosekana kwa meno. Tishu nyororo za mdomo husogeleana na pua na kidevu hukaribiana, jambo hilo lamfanya mtu aonekane kuwa mzee zaidi ya alivyo kwa kweli. Hilo laweza kuwa na matokeo juu ya kujitumaini kwa mtu na huenda hata kukasababisha matatizo ya kisaikolojia kwa wengine.
Kupotezwa kwa jino kwaweza kutokeza kushuka kwa mpangilio wa namna ya tao wa meno. Meno yetu hutegemeana, kama vile mawe katika tao la Kiroma. Hivyo, kupotezwa kwa “jirani” kutafanya yale meno mengine kusogea. Mwendo huo hufanyiza mianya kati ya meno yanayobaki na huenda kukaruhusu visehemu vya chakula kujazana katika maeneo ya ufizi, na hilo mara nyingi hutokeza ambukizo wa ufizi. Mwendo wa meno huenda pia ukaharibu upatano wa meno, hilo likisababisha matatizo ya kutafuna.
Yanavyotofautiana
Tofauti muhimu ya meno asili na ya bandia ni kwamba yale ya asili yana mizizi imara katika mfupa wa taya. Hilo huyawezesha kukata, kubandua, na kusaga chakula chetu kuwa vipande vidogo-vidogo sana. Meno ya chini husogea juu ya meno ya juu kwa ulinganifu na kwa tendo lenye nguvu la kusaga.
Kwa upande mwingine, seti kamili ya meno bandia, hukaa tu juu ya fizi au ukingo wazo. Hushikiliwa mahali payo na nguvu dhaifu zinazotokezwa na ulimi, mashavu, na ushikamano. Kwa kuwa meno bandia hayaimarishwi kama meno asili, yaweza kuondoshwa kwa urahisi.
Kwa hiyo mafanikio ya meno bandia hutofautiana mtu na mtu. Hakuna meno bandia yaliyo na mafanikio kama ya meno asili. Umbo na ukubwa wa taya, namna ya tishu, na hata mtazamo wa kiakili wa mwenye kuyatumia, pamoja na uwezo wa kujifunza kuyatumia, yote huamua juu ya kufanikiwa kwa meno bandia. Kasoro yayo kubwa ni ukosefu wa imara. Hata hivyo, kwa habari ya vile yaonekanavyo, meno bandia yaweza kufanywa yasiweze kutofautishwa na meno ya asili.
Kwa kusikitisha, nyakati nyingine huwa ni baada tu ya kulazimika kutumia meno bandia kwamba mtu hutambua hekima, ubuni, na ufaaji wa meno asili. Wanadamu waweza kuiga ki-vivi-hivi tu kilicho asili lakini hawawezi kamwe kufikia kadiri ileile ya mafanikio ya ajabu.
Huenda hali yako ikakulazimisha ufikirie kwa uzito kama wahitaji meno bandia, ama seti kamili ama kisehemu chayo. Bila shaka, uamuzi ni wako, lakini yaelekea kuwa ni hekima kufikiria manufaa yayo. Huenda yakakusaidia kuzuia yale yawezayo kuwa matatizo ya uyeyushaji wa chakula tumboni, kukusaidia kupata ulishaji ufaao, na kufanya uwezo wako wa kusema uwe bora. Na kwa kweli yaweza kufanya sura ya kibinafsi iwe bora.
Kwelikweli, ijapokuwa watumiaji wa meno bandia kwa kawaida huombolezea kupoteza meno yao halisi, utengenezaji wa meno bandia umechangia kadiri fulani ya uradhi wa kibinafsi na hisi ya hali njema kwa mamilioni ya watu ulimwenguni pote.
[Maelezo ya Chini]
a Katika makala hii, neno ‘meno bandia’ hurejezea vitu vitumiwavyo badala ya meno yaliyopotezwa. Ikiwa meno yote ya asili yamepotezwa, basi seti kamili ya meno bandia yahitajiwa. Lakini, ikiwa baadhi ya meno yanabaki, kisehemu cha seti ya meno bandia chaweza kutumiwa. Makala hii itakaza fikira juu ya seti kamili ya meno bandia na juu ya kisehemu cha seti ya meno bandia kiwezacho kuondolewa.
[Sanduku katika ukurasa wa 19]
Kupunguza Gharama Yako ya Matibabu ya Meno
ZIARA kwa daktari wa meno au mtaalamu wa meno mara ngingi huleta gharama kubwa kwelikweli. Hata hivyo, waweza kutiwa moyo kwa kujifunza mambo yanayoweza kukusaidia kwa habari ya watoto wako.
”Ile hali yenye kuenea sana ya meno yatokeayo mahali tofauti na yapaswapo kutokea na taya zenye muundo mbaya miongoni mwa Waamerika,” laripoti The New York Times, ”huenda yakawa matokeo ya ulaji wetu wa chakula ambacho vitu vingi muhimu sana vimeondolewa.” Inasemeka kwamba ulaji ambao hutaka kutafuna kwa nguvu ”huchochea ukuzi wa taya (ambao hutokeza nafasi kubwa vya kutosha kuyapa meno nafasi bila kusongamana), huongoza kutokea ifaavyo kwa meno yenye kudumu na ukuzi wa uso na kinywa.”
Wanasayansi walijaribu kuthibitisha nadharia hiyo kwa kuwalisha tumbili chakula kigumu na laini. Matokeo yakawa nini? Wale waliolishwa chakula na ”matatizo machache sana ya kujipanga kwa meno.” Hivyo huenda ikawa kwamba chakula kinachomhitaji mtoto wako kutafuna kwa nguvu kitathibitika kuwa njia moja ya kupunguza gharama zako za matibabu ya meno. Njia nyingine ya kufanya hivyo ni kusaidia watoto wako wawe na zoea la kupiga mswaki meno yao na kutumia flosi.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Meno yetu hutegemeana. Yasipokuwa na “majirani” wa kuyasaidia kuyadumisha mahali payo, upesi meno husogea na kuathiri vibaya meno mengine