Tiba ya Meno Yaliyoota Vibaya—Inahusisha Nini?
MENO yako ni ya muhimu sana! Unayahitaji kwa ajili ya kula na kwa kusema, na pia huchangia sehemu ya maana katika tabasamu au kicheko chenye kupendeza.
Meno yaliyo kombo yaweza kusababisha iwe vigumu kutafuna chakula, yaweza kuchangia maradhi ya ufizi, na yaweza kuchangia kasoro za usemi. Wataalamu pia wameonelea kwamba meno yaliyo kombo yanaweza kuwa kikwazo cha kuwafanya watu fulani wasishirikiane na wengine, kwani wanaweza kuwa na ugumu katika kujieleza kwa uhuru kwa sababu wanaamini kuwa tabasamu yao huharibiwa na meno yao.
Ni nini linaloweza kufanywa ikiwa meno yako hayajanyooka? Ni nani awezaye kukusaidia? Ukiwa na umri gani? Ni aina gani ya matibabu inayoweza kutumiwa? Je, matibabu hayo yataumiza? Je, ni ya lazima sikuzote?
Tawi la Utaalamu wa Meno
Tawi la utaalamu wa meno linaloshughulika na matatizo kama haya linaitwa tawi la tiba ya meno yaliyoota vibaya. Linahusika katika kurekebisha meno yasiyolingana.
Utendaji mkuu wa tawi hili la tiba ya meno yaliyoota vibaya ni upi? Unahusu ubainishaji wa ugonjwa na kuzuia matatizo vilevile, kutengeneza vifaa vya kurekebishia meno.
Meno yaliyojazana, yasiyolingana, na yaliyojitokeza yalikuwa tatizo kwa watu hata katika nyakati za kale, na majaribio ya kitiba yalifanywa huko nyuma angalau katika karne ya nane K.W.K. Kwa kushangaza vifaa vilivyotengenezwa vizuri vya mapema vya tiba ya meno yaliyoota vibaya vimegunduliwa katika vitu vilivyopatikana kiakiolojia vya Kigiriki na Kietruska.
Leo, katika sehemu nyingi za ulimwengu, madaktari maalumu wa meno wanaoitwa madaktari wa meno yaliyoota vibaya hushughulikia matatizo yanayohusiana na meno yaliyo kombo. Wanahitaji kuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu ukuzi na usitawi wa meno na taya na misuli na tishu zinazozingira.
Kile Ambacho Tiba ya Meno Yaliyoota Vibaya Hufanya
Tiba ya meno yaliyoota vibaya yaweza kufasiliwa kuwa “eneo la utaalamu wa meno linalohusika na kuangalia, kuelekeza na kurekebisha ukuzi na maumbile yaliyokomaa ya uso.” Inatia ndani “marekebisho ya uhusiano miongoni mwa na kati ya meno na mifupa ya uso kwa utumizi wa kani na/au kichechemo na kuelekeza upya kani tendaji ndani ya fuvu la kichwa lililo tata.” Ndiyo, fasili ya kiufundi, lakini iliyo sahihi.
Kwa hiyo katika tiba ya meno yaliyoota vibaya, kani hugandamizwa juu ya meno au kwenye maumbile yanayoyazingira. Hili hufanywa kwa njia ya vifaa vya kutengenezwa kwa agizo ambavyo hurekebisha matatizo hususa ya kila mgonjwa, vikisukuma meno na hata mifupa ili iwe mahali panapoifaa.
Kwenye mifupa inayozunguka meno, kuna chembe zinazoitwa osteoclast na chembe nyingine zinazoitwa osteoblast. Likiwa tokeo la kani zinazotokezwa na vifaa vya kubana meno, osteoclast hufanya kazi mahali palipo na kanieneo, hivi kwamba tishu ile yenye mifupa-mifupa hufyonzwa. Katika maeneo ambapo pana nguvu ya kuvutia, pengo huzibwa na mfupa mpya unaofanyizwa na osteoblast. Kwa njia hii meno husonga polepole.
Je, si jambo lenye kukosesha starehe kuwa na kifaa cha nje cha kubana meno kilichotengenezwa na waya, rezini, au labda hata chenye kunyumbulika katika kinywa kwa miezi kadhaa? Wakati vifaa hivi vinapowekwa au vinaporekebishwa, mara ya kwanza vinaweza kumfanya mtu akose starehe; lakini baada ya muda fulani, mtu huvizoea. Kinadharia, mtu yeyote anaweza kuzoea kuvalia vifaa vya kubana meno.
Ni Wakati Gani Ambapo Mtu Apasa Kutibiwa?
Si hali zote zionekanazo kutokeza kasoro za umo, au malocclusion, katika watoto ambazo zitadumu hadi utu mzima. Aina fulani za meno yanayoota mahali pasipofaa huelekea kujirekebisha zenyewe. Kwa kweli, wakati wa badiliko la kung’oka kwa meno au, kutoka meno ya kitoto hadi kwa meno ya kudumu, meno ya kudumu yaliyo katika sehemu ya mbele ya kinywa mara nyingi huelekea kujikusanya kwa wingi, kwa kuwa huwa makubwa kuliko yale meno ambayo yamechukua mahali pake.
Hata hivyo, meno ya kusaga chakula yang’okapo, ambayo mahali pake huchukuliwa na masagego ya kudumu, kunakuwa na badiliko la jinsi meno yatakavyowiana. Kwa kutumia meno na vilevile chini ya uvutano wa maumbile ya kimisuli, meno yanaweza kujilainisha yenyewe. Kwa hiyo ikiwa wewe ni mzazi, usiwe na hofu ikiwa mara ya kwanza unaona meno ya kudumu ya mtoto wako yanaota yakiwa kombo. Daktari wa meno yaliyoota vibaya apaswa kuamua ikiwa jambo lolote lahitaji kufanywa.
Madaktari wa meno yaliyoota vibaya wana maoni yanayotofautiana kuhusu ni wakati gani unaofaa kutibu wagonjwa walio wachanga. Wengine husema katika umri mchanga sana (miaka 4 hadi 6). Wengine husema baadaye, kuelekea mwisho wa ukuzi wakati wa ubalehe (miaka 12 hadi 15). Na bado wengine huchukua msimamo wa hapo katikati.
Si ya Watoto Tu
Ingawa hivyo tiba ya meno yaliyoota vibaya si ya watoto tu. Meno yaliyo kombo husababisha matatizo mengi, hata wakati wa utu mzima. Namna ya tabasamu yako yaweza kusahihishwa ukiwa katika umri wowote ikiwa meno na vifaa vya kulainishia meno ni vyenye afya.
Ni matatizo gani husababishwa na meno yaliyo kombo? Kuna angalau aina tatu: (1) matatizo yanayohusiana na sura; (2) matatizo ya utendaji, kutia ndani kufumba na kufumbua taya (maumivu na ukosefu wa uratibu wa misuli), matatizo ya kutafuna, na matatizo ya utamkaji wazi na kutokezwa kwa usemi; (3) hatari iliyo kubwa zaidi ya kuumia kwa sababu ya meno yaliyojitokeza na pia hatari kubwa ya maradhi ya ufizi na kuoza kwa meno vilevile, kuzorota kwa hali ya meno na uchakavu unaosababishwa na malocclusion.
Kwa kuongezea, wataalamu fulani hushirikisha malocclusion na matatizo ya namna ulivyo uti wa mgongo (hasa katika eneo la shingo) na matatizo ya utendaji wa misuli katika sehemu nyingine za mwili. Lakini matibabu hutolewa jinsi gani? Nao unadumu kwa muda gani?
Muda Unaohusika na Njia za Matibabu
Ikiwa unahisi kwamba wewe ama mmoja wa watoto wako anahitaji kumwona daktari wa tiba ya meno yaliyoota vibaya, unapaswa kuchagua mmoja unayeweza kumwitibari. Muda unaohusika wa matibabu utatofautiana kulingana na uzito wa tatizo hilo na njia itumiwayo, lakini labda itachukua miezi kadhaa, au labda miaka kadhaa.
Ili kusahilisha mambo, twaweza kugawanya vifaa vya matibabu katika vikundi viwili: vifaa vinavyoweza kutolewa na vifaa vya kudumu. Ilhali vifaa vinavyoweza kutolewa vyaweza kutolewa na kuingizwa tena na mgonjwa, vifaa vya kudumu kwa kawaida huunganishwa na meno na hufanyiza misogeo ya meno iliyo tata zaidi.
Utafiti umeendelea sana katika eneo la ujumi, hivi kwamba leo kuna vifaa vingi vinavyoonekana kuwa vya “kiasili.” Vifaa vingine havionekani kwa sababu vina rangi iliyo sawa na ya meno, na vingine, ambavyo huingizwa kwenye sehemu ya ndani ya meno ambayo inajulikana kuwa mahali pa lugha, inayopakana na ulimi, hubaki bila kuonekana. Njia za namna hiyo huitwa tiba isiyoonekana ya meno yaliyoota vibaya.
Katika visa vilivyo vigumu zaidi, wakati daktari wa tiba ya meno yaliyoota vibaya anaposhindwa kupata matokeo yanayotakiwa kwa kutumia vifaa vya kubana meno, huenda hata akatafuta msaada wa daktari-mpasuaji ambaye ni mtaalamu wa matatizo ya kinywa na uso. Anaweza kufanya upasuaji ambao kwa kawaida husogeza mifupa inayofanyiza umbo la uso.
Leo, tiba ya meno yaliyoota vibaya inaweza kutosheleza mahitaji ya wale walio na matatizo ya meno na taya, kutia ndani wale wanaotamani kutabasamu bila kujali sana juu ya meno yao. Bila shaka, kama mtu aamua kutafuta tiba ya meno yaliyoota vibaya au la ni uchaguzi wa kibinafsi.
Kwa wakati uliopo, wanadamu watahitaji kushughulika na kasoro za kimwili, baadhi ya hizo huenda zikatulizwa na hatua za marekebisho. Hata hivyo, tunaweza kutazamia kwa hamu ulimwengu mpya wa Mungu wakati ambao ataondoa kabisa madhara yote ya kutokamilika, kutia ndani yale ya kinywa. Kisha, katika mfumo huo mpya wenye afya kamili, kila mmoja wetu ataweza kutoa kwa uhakika tabasamu changamfu, na yenye urafiki, kwa kila mmoja tutakayekutana naye.
Kuhusu wakati huo, Biblia hutabiri: “Dunia yote inastarehe na kutulia; hata huanzilisha kuimba.” (Isaya 14:7) Hakika, uchangamfu na shangwe ya namna hiyo utaandamana na tabasamu nzuri!
[Picha katika ukurasa wa 25]
Wonyesho wa vifaa vya kubana meno vilivyobuniwa ili (1) kusogeza masagego kuelekea nyuma na (2) kuchochea ukuzi wa taya
1
2
[Picha katika ukurasa wa 26]
Vifaa vya kubana meno vilivyobuniwa ili kufunga umo