Je, Wewe Husaga Meno Yako?
TANGU nyakati za kale watu wamekuwa wakisaga meno yao wanapokuwa chini ya mkazo. Mara nyingi Biblia hutumia kusaga meno kuonyesha hasira kali au maumivu makali. (Ayubu 16:9; Mathayo 13:42, 50) Katika ulimwengu wa leo wenye hasira na wenye kujaa mkazo, mamilioni ya watu husaga meno yao kihalisi, na wengi hawajui kuwa wanafanya hivyo. Wanaweza kuwa wanayachakaza meno yao.
Kwa nini watu fulani husaga meno yao? Sababu za kufanya hivyo ni tata na bado hazijaeleweka kabisa. Lakini katika visa fulani mkazo wa kihisia-moyo huelekea kuwa kisababishi. Ile UC Berkeley Wellness Letter yataja kuwa: “Watu ambao husaga meno yao mara nyingi huripoti kuwa wanapatwa na matatizo ya ndoa au ya kifedha, wanafanya mitihani ya mwisho, wanahofu kupoteza kazi zao, au wako chini ya mkazo.” Mambo mengine ambayo huenda yakasababisha na kuchangia hilo hutia ndani mgusano wenye kasoro kati ya meno ya juu na ya chini, kusumbuka wakati wa usingizi, au unywaji wa alkoholi. Kwa hiyo, Wellness Letter yapendekeza kwamba wanaosaga meno wajaribu kupunguza unywaji wa alkoholi; kuchukua hatua sahili za kujituliza kabla ya kwenda kulala, kama vile kufurahia kuoga kwa maji ya moto; au kuzungumzia matatizo yenye kutaabisha pamoja na rafiki au mshauri anayetumainiwa.
Wakati wa mchana waweza kujipata ukikereza meno au kuyasugua pamoja. Lakini waweza kujuaje ikiwa wafanya hivyo unapolala? Wakati mwingine kusaga meno daima, ambako hujulikana kuwa bruxism, hutoa sauti kubwa iwezayo kumwamsha mtu mwingine mliyelala naye katika chumba kimoja. Waweza kuamka ukiumwa na kichwa kwenye panda zako, au taya zako zaweza kufanya sauti kama ya kupiga kidoko.a Huenda daktari wako wa meno hata akagundua kwamba meno yako yanakwisha. Anaweza kupendekeza hatua za kuandaa kitulizo fulani, kama vile kitu fulani cha kuweka juu ya meno yako usiku. Ijapokuwa kilinda-mdomo kama hiki hakijakusudiwa kufanya uache kusaga meno yako, chaweza kuyalinda meno yako yasipatwe na madhara zaidi. Kwa vyovyote, tulia! Kadiri upunguzavyo wasiwasi wako, ndivyo upunguzavyo kusaga meno yako.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi, tafadhali ona toleo la Amkeni! la Juni 22, 1991, ukurasa wa 20-22 (la Kiingereza).