Shimo Kubwa Zaidi Ulimwenguni Lililopata Kuchimbwa na Binadamu
RAFIKI mmoja alikuwa ameniambia: “Ukienda Jiji la Salt Lake, hakikisha unazuru migodi ya shaba ya Kennecott katika Bingham Canyon. Utashangaa kwa yale utakayoona.” Mke wangu nami tulikuwa na fursa hiyo mnamo Agosti 1992. Tuling’amua kwamba rafiki yetu hakuwa akitia chumvi.
Tulisafiri kwa starehe kilomita 42 kusini-magharibi kutoka Jiji la Salt Lake, katika joto kavu lenye kuchoma la Utah. Tulipoelekea kwenye safu ya milima iliyo karibu ya Oquirrh, kidogo tukaona pale tulipoelekea—alama kubwa ya udongo wa rangi manjano nyepesi kwenye umbali wa macho, ikitofautiana na rangi iliyoshika sana ya milima mingineyo. Ulikuwa ni uchimbaji mkubwa na mitelemko-telemko ya migodi ya shaba ya Kennecott. Lakini ono hilo halikututayarisha kwa yale tuliyokaribia kuona.
Tulianza kupanda mlima mrefu. Njiani, tulipita malori makubwa ya mchanga, makubwa kama nyumba ndogo, lile kubwa zaidi likiweza kubeba tani 240 hivi za miamba kila safari. Ni makubwa sana hivi kwamba kipenyo cha magurudumu yayo cha mita 3.7 kinapita kimo cha mtu mrefu zaidi. Hatimaye tulifika kwenye sehemu ya umma ya kutazamia. Na ndipo tukaliona—shimo kubwa zaidi lililopata kuchimbwa na binadamu tulilopata kuona!
Tulipotazama chini kwenye sakafu ya shimo hilo, malori hayo makubwa yalionekana kama vitu vidogo vya kuchezea. Tulikuwa tukitazama shimo lenye kina cha zaidi ya kilomita 0.8 na kipenyo cha kilomita nne. Sakafu ya shimo hilo ni zaidi ya mita 1,500 juu ya usawa wa bahari, na sehemu za juu za shimo hilo zafikia mita 2,400. Ni lenye kina kirefu sana hivi kwamba jengo refu zaidi ulimwenguni, Sears Tower katika Chicago, la mita 440, lingefikia nusu tu ya upande wa migodi hiyo. Kampuni inanuia kwenda chini mita zingine 260, ambazo wanakadiria zitawapa kazi hadi angalau mwaka 2020.
Migodi hiyo ilionekana kama jumba kuu la vitumbuizo, likiwa na mitelemko-telemko yenye urefu wa mita 15, iitwazo benchi, ikitelemka hadi kwenye kina cha shimo hilo. Tuliambiwa kwamba migodi hiyo ya shaba yaweza kuonwa kutoka kwa chombo cha kuruka angani. Na bado, yote hayo yalikuwa na mwanzo mdogo sana miaka 130 iliyopita, wakati mlima huo ulipokuwa bado na urefu wa zaidi ya mita 2,400.
Wadhihakiwa kwa Kuchimba Migodi
Uchimbaji migodi ulianza kwanza mwaka 1863, wakati Kanali Patrick Connor kutoka Fort Douglas aliudai kihalali. Hata hivyo, ulikuwa mgodi mdogo na haukuleta faida. Mgodi wa Bingham Canyon ulianzishwa kwanza katika 1906 wakati Kampuni ya Shaba katika Utah ya Daniel Jackling na kampuni yenye ushindani zilipoanza kuchimba mtapo (jiwe lenye madini) uliokuwa na asilimia 2 tu ya shaba. Broshua rasmi hueleza kwamba “walidhihakiwa na watu wa kuchimba migodi wa enzi hiyo waliofikiri kwamba hawangeweza kamwe kupata faida kwa kuchimba mtapo wa hali ya chini.” Wao wangeweza kusema nini leo, wakati asilimia ya shaba kwa mtapo ni asilimia 0.6 tu? “Shaba nyingi imechimbwa Bingham Canyon kuliko migodi nyingine katika historia. Tani bilioni tano za miamba zimechimbwa tangu shimo hilo lilipoanza kuchimbwa.”
Shaba si ndio bidhaa pekee—dhahabu, fedha, na molibdeni (risasi inayotumiwa kuimarisha chuma cha pua) hutokezwa pia, dhahabu ipatayo gramu 14,000,000 na fedha ipatayo gramu 110,000,000 ziki-wa bidhaa za ziada kila mwaka! Basi haishangazi kwamba mgodi huo umeitwa shimo lenye utajiri mwingi zaidi duniani.
Na ikiwa unajiuliza kwa nini shaba ni ya muhimu sana, wazia yale yangetukia ikiwa shaba yote ingeondolewa kwenye waya zote za umeme, katika majenereta yote, transfoma, na vitu vingine vya umeme. Orodha hiyo yaweza kutia ndani friji, ndege, magari, na kadhalika. Shaba ni ya muhimu katika shughuli za maisha ya kisasa, kama vile ilivyokuwa nyakati za kale. Shaba hutajwa mara 166 katika Biblia—Mwanzo 4:22; Kutoka 27:1, 2.
Kusindika Shaba—Si Kazi Rahisi
Yale tuliyoona katika shimo hilo kubwa ni mwanzo tu wa kazi inayotokeza shaba ya thamani. Migodi ni mahali ambapo kupekecha, kupiga baruti, kupakia, na kupeleka hutukia. Kisha mtapo hupelekwa kwa kifaa cha kuponda kilicho shimoni, ambapo mfumo wa upelekaji husafirisha mtapo uliopondwa hadi kwenye kiwanda cha utenganishaji na ueleaji kilicho umbali wa kilomita nane. Mfumo wa usindikaji huongeza kiasi cha shaba ya mtapo kutoka asilimia 0.6 hadi asilimia 28 kwa kuondoa vitu visivyotakiwa.
Kisha kazi ya uyeyushaji hufuata, inayoondoa vitu visivyotakiwa, kama vile chuma na kiberiti, ikitokeza myeyusho wa shaba ambao sasa ni safi kwa asilimia 98. Huo humwagwa katika vitu vyenye pembe nne viitwavyo anodi na kisha hupozwa. Hatua ya mwisho ni kazi ya kusafisha. Broshua moja hueleza: “Anodi hutiwa umeme na shaba husafishwa kuwa safi kwa asilimia 99.98.” Ni wakati wa kazi hiyo kwamba dhahabu na fedha hupatikana zikiwa bidhaa za ziada. Badiliko hilo hugeuza shaba kuwa kathodi kubwa, mabamba ya shaba ya kilo 150 yanayouzwa kwa watengenezaji wa bidhaa za shaba, shaba nyeupe, na shaba nyeusi.
Yote hayo yasikika kuwa rahisi kidogo. Lakini kwa kweli, shughuli yote ni tata sana na huchukua nafasi kubwa. Kwa vyovyote, tani moja ya mtapo hutokeza kilo 5 tu za shaba. Kwa hiyo utakapoona waya ya shaba au kifuniko au birika la shaba, kumbuka huenda ilitoka kwa shimo kubwa zaidi ambalo binadamu amepata kuchimba.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Juu: Shimo lina kina cha kilomita 0.8 na kipenyo cha kilomita nne
Juu kushoto: Kiwanda cha kuyeyushia chenye mojawapo dohani ndefu zaidi ulimwenguni
Picha ya ndani: Kathodi ya shaba ya kilo 150, iliyotiwa alama kuonyesha jinsi shaba hutumiwa kwa asilimia
Chini kulia: Lori la diseli linalochukua tani zipatazo 240 za mtapo
[Hisani]
Picha (juu na ukurasa 25 juu): kwa hisani ya Kennecott Utah Copper
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Picha kwa hisani ya Kennecott Utah Copper