Wanamuziki Wanaoruka wa Ulimwengu wa Wadudu
TUNAKUBALI kwamba sisi ni viumbe wenye kula sana. Na naam, uwezo wetu wa kula waweza kuamsha hasira ya wakulima wanaotuona kuwa balaa kwa kuharibu mimea yao. Hata hivyo, sisi panzi tuna mambo yanayovutia—jinsi tunavyoruka, jinsi tunavyoambaa hewani, jinsi tunavyopanda, na jinsi tunavyofanyiza “muziki.”
Je! ulijua kwa mfano kwamba tuna macho matano? Badala ya kuvaa miwani ya kuona mbali na karibu kama yale ambayo binadamu wengi huvaa, tuna macho matatu madogo mbele ya kichwa chetu kwa ajili ya kuona vitu vilivyo karibu. Macho yale mengine mawili ni makubwa na yamo ndani zaidi kichwani, yakituruhusu tuone yale yanayoendelea kando yetu. Si ungependa kuwa na macho yenye uwezo kama huo?
Uwezo wetu wa kuruka ni mzuri kadiri gani? Tunaweza kuruka mara kumi ya uzito wetu na tutue umbali wa karibu mita moja. Ili binadamu aruke vivyo hivyo, angehitaji kuruka urefu wa jengo la orofa sita. Siri yetu ni misuli yetu yenye nguvu sana kwenye miguu ya nyuma. Hiyo hutupa uwezo wa kuruka ili tutimize matendo hayo ya ajabu.
Hata baada ya mruko wetu wa kwanza kuondoka njiani pako, tunaweza kufanya iwe vigumu hata zaidi kwako kutushika kwa kutumia jozi mbili za mabawa ambazo sote tunazo. Mabawa thabiti ya juu hufanya kazi ileile kama ya mabawa ya eropleni, hali mabawa yale mengine ya chini yasiyo thabiti sana hutumiwa kwa ajili ya kuruka zaidi. Hivyo, kwa kuunganisha stadi zetu za kuruka na kupaa hewani, kwa kawaida tunaweza kuruka mbali vya kutosha kuweza kukukatisha tamaa uwache kutufuata.
Je! wewe huona ugumu kupanda ufito wenye mafuta-mafuta? Sisi hatuoni ugumu. Kwa kweli, tunaweza kukimbia tukipanda kinyasi chenye utelezi bila kuteleza kwa sababu ya jinsi Muumba alivyobuni miguu yetu sita. Vijifumba vidogo kwenye kila mguu vina vijinywele vidogo vinavyotoa umaji-maji wenye kunata, ukitusaidia kushika vitu kwa imara. Isitoshe, kila mguu una kulabu mbili zenye nguvu, zinazotuzuia tusiteleze nyuma kwenye sehemu zinazoinama sana. Naam, muda mrefu kabla wanadamu hawajafikiria juu ya kupanda milima, tulikuwa na vifaa vya kupanda.
Panzi wa kiume wa jamii yetu ndio wanamuziki. Panzi mabibi huvutiwa kwa kufaa na huwaona wao kuwa wenye kipawa sana. Naam, tunaweza kusikia na kuitikia sauti mbalimbali. Masikio yetu yamo kwenye kila pande ya kifua. Hivyo, wanapokuwa tayari, panzi wa kiume husugua kwa wororo mguu wa nyuma juu ya mabawa yaliyoinuliwa kwa njia ileile ambayo mpiga zeze husugua mti wake juu ya nyuzi za zeze lake. Jinsi inavyostarehesha katika siku yenye joto ya katikati ya kiangazi kujilaza kwenye konde la majani na kufyonza nyimbo kutoka kwa panzi na chenene (nyenje) elfu moja. Aa, sauti ya kiangazi!