Nyati-Mnyama—Mwenye Ushirikiano
Na mleta habari za Amkeni! katika Kenya
UNAENDESHA gari kupitia mbuga ya Afrika. Gari lako lalalia upande wa juu wa kilima, na kwa ghafula, umbali wa meta chache tu, watokea mstari wa wanyama wenye kutisha. Ni wanyama wakubwa, kila mmoja akifikia kimo cha meta 1.5 hadi begani na mwenye na uzani wa karibu tani moja. Wakishtuka kwa sababu ya mwendo wako wa kuwakaribia, wanatulia tuli, vichwa vyao vikiwa vimerudishwa nyuma ili wakunuse, macho yao yakikuangalia kwa ukali.
Hata hivyo, macho yako yakazia pembe zao kubwa, zinazopinda chini kisha zatoka nje kuelekea upande. Pembe hizo ni sentimeta 147 kutoka ncha moja hadi ncha nyingine. Kwenye baadhi ya wanyama hao, misingi iliyoinuka ya pembe hizo hupanuka na kushikana utosini, ikifanyiza kitu kama kofia kubwa. Unajiuliza kwamba gari lako laweza kustahimili mapigo mangapi kutoka kwa pembe hizo.
Kwa sababu ya sifa ya wanyama hao, hofu hizo zinaeleweka. Iwayo yote, hawa ni nyati, na wana sifa ya kuwa hatari sana, wakiwa na mwelekeo wa kushambulia kwa udhiko mdogo tu. Kwa kweli, inasemekana kwamba nyati wamejeruhi au kuua watu wengi zaidi—na simba—kushinda mnyama yeyote duniani alaye majani. Si ajabu kwamba unashtuka kwa kuwaona tu! Hivyo mmoja wa wanyama hao akikoroma kwa sauti kubwa, unakuwa chonjo. Lakini kwa mshangao wako wenye kutuliza, hushambuliwi. Badala ya kushambulia, mstari wote wa madume wageuka na kukimbia!
Hukufaulu kuwaogopesha wanyama hao kwa kuwakazia macho. Kwa sababu, ingawa si mnyama wa kuchezewa, kwa kushangaza, nyati ni mnyama mwenye amani kiasili. Chakula chake ni nyasi—si nyama (ya mnyama au binadamu). Sifa yake ya ukali inatokana na hekaya na hadithi zilizotiwa chumvi zilizosimuliwa na wawindaji, wala haitokani na uchunguzi wa kisayansi. Kwa kweli, atakimbia asipigane badala ya kutafuta vita. Na badala ya kuwa mnyama asiyekuwa na mapatano, nyati ni mfano mzuri wa ushirikiano.
Kushirikiana kwa Ajili ya Kuokoka
Nyati ni mnyama wa pekee mwenye ushirika. Akipatikana kotekote katika sehemu kubwa ya Afrika iliyo kusini mwa Sahara, anaridhika na karibu kila aina ya hali ya nchi bora tu awe karibu na maji. Wakati wa misimu ya mvua ambapo maji ni mengi na chakula ni kingi, nyati husafiri katika makundi makubwa. Ingawa katika sehemu fulani-fulani kundi la kawaida lina wastani wa wanyama 350, makundi mengine yanafikia maelfu. Wakati wa ukame, makundi hayo hupungua kutoka 2 hadi 20. Kila siku—mara moja asubuhi na mara moja usiku—kundi husafiri kwenda kwenye chanzo cha maji kilicho karibu. Nyati mmoja atakunywa kufikia lita 30 hadi 40 za maji.
Wakati wa joto la siku, wanyama hao wenye ushirikiano hupenda kulala ndani ya maji na kugaagaa katika matope. Tabia hiyo haiwapoezi tu na kuwaburudisha bali pia inawasaidia kuondoa vidudu vinavyowasumbua. Au wanaweza kulala tu chini ya kivuli wakionekana kana kwamba wanatafakari, huku wakicheua nyasi polepole, vichaka, na majani waliyokula wakati wa usiku.
Hatari inapotokea, ile roho ya ushirikiano inaonekana waziwazi kwa haraka. Nyati mmoja atawatahadharisha wengine kwa kukoroma kwa nguvu. Upesi kundi zima linakimbia kumsaidia. Kwani, nyati wamejulikana kukusanyika pamoja na kumshambulia simba! Silika hiyo ya kulindana si ya kawaida miongoni mwa wanyama walao nyasi, sheria ya kawaida ni kuwa kila mnyama ajilinde mwenyewe hatari inapotokea. Kwa sababu hiyo, nyati walemavu na vipofu wanaweza kuokoka bora tu wawe pamoja na kundi.
Ushikamano uo huo waendelea hata wakati hakuna hatari yoyote. Kwa mfano, kukiwa na utendaji tofauti, kama vile kuacha kula na kisha kulala chini, kundi zima huchukua dakika chache tu kufanya hivyo. Wanasayansi walikuwa wakiamini kwamba kundi lilifuata mnyama fulani mwenye kuwaongoza katika kufanya hivyo, lakini hivi karibuni zaidi imedokezwa kwamba wanafuata mshiriki yeyote yule anayefahamu zaidi ile sehemu fulani hususa waliko. Kwa kawaida huyo atakuwa wa kike aliye na umri mkubwa. Dume hupendelea kutembea peke yao na kuacha kundi. Kwa hiyo, makundi hayanyanyaswi ili kutii kiongozi mwenye kutawala lakini yajionyesha kuwa wenye kushirikiana kiasili.
Dume Atembeaye Peke Yake—Je! Ni Mpweke?
Lakini, ni kwa nini madume hujitenga na makundi? Je! wamekuwa wanyama wasioshirikiana? La hasha. Maisha yao ya upweke yakilinganishwa na ya wengine ni kwa sababu ya miili yao mikubwa. Kwa sababu ni wazito sana hivi kwamba hawawezi kusonga-songa mara nyingi kama kundi linavyofanya, wao huja kupendelea maisha ya kuwa peke yao. Basi kila mmoja huchukua eneo la binafsi—mahali palipo na kivuli, majani ya kuliwa usiku, sehemu ya kunywa maji iliyo karibu. Na bado, anakaa karibu kadiri awezavyo na kijia kinachofuatwa kila siku na kundi linapoenda kunywa maji. Mara kwa mara atakula pamoja na wenzake wa zamani. Maji yaishapo wakati wa ukame, madume kadhaa wataungana pamoja kwa ajili ya safari zao za mara mbili kila siku za kwenda kunywa maji.
Vipi ikiwa kundi linalazimika kuvuka eneo la binafsi la dume? Je! vita kubwa itazuka? La hasha. Dume huyo atakutana na kundi hilo mpakani mwa “mali” yake na yeye mwenyewe atawasindikiza kwenye mpaka wa eneo la dume jirani. Huyo naye achukua uongozi na kuwapeleka hadi eneo lifautalo. Mwendo huo wajirudia mpaka kundi lifike sehemu yalo ya maji. Kundi hilo likitishwa, madume hao watakuwa walinzi wa nyati wa kike na ndama. Mara moja watachukua sehemu ya nyuma—sehemu ya hatari zaidi—na ndio watakuwa wa mwisho kukimbia.
Hivyo, sifa ya nyati kuwa ni mnyama mwenye kutisha haistahili. Baada ya kujua mnyama huyu kwa njia bora zaidi, twaweza kumwona, si kama mnyama mkali na mkatili bila sababu, bali kama mfano wenye amani wa ushirikiano anayestahili kufikiriwa—labda hata kuigwa.
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Nyati wamejulikana kukusanyika pamoja na kumshambulia simba
Ingawa madume huacha kundi, wao huendelea kushirikiana