Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 7/22 kur. 25-27
  • Yule Nyati wa Majini Mwaminifu na Mwenye Mafaa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yule Nyati wa Majini Mwaminifu na Mwenye Mafaa
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mnyama Mwenye Misuli Apatikanaye Sehemu Tofauti za Ulimwengu
  • Wahamiaji Wenye Kusitawi
  • Mama Aliye Malkia
  • Zaidi ya Trekta Inayoishi
  • Kupunguza Uzani wa Nyati
  • Nyati-Mnyama—Mwenye Ushirikiano
    Amkeni!—1993
  • Paradiso ya Aina Tofauti
    Amkeni!—1998
  • Yellowstone—Chimbuko la Maji, Mwamba, na Moto
    Amkeni!—2000
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 7/22 kur. 25-27

Yule Nyati wa Majini Mwaminifu na Mwenye Mafaa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

‘Kimbieni, kimbieni! Kuna simbamarara!’ wanapaaza sauti hao wavulana. Wanakimbilia nyati wao, kuruka juu ya migongo yao, na kwenda shoti. Kwa ghafula, Saïdjah, mmoja wa hao wavulana, anapoteza usawaziko wake na kutumbukia ndani ya mashamba ya mpunga—yaonekana akiwa windo kwa simbamarara anayekaribia. Hata hivyo, nyati wa Saïdjah, aona kilichotendeka. Anageuka kuja kumwokoa Saïdjah, anamkinga rafiki yake mdogo kwa mwili wake mpana, na kumkabili simbamarara. Huyo paka mkubwa anashambulia, lakini nyati anasimama thabiti na kuokoa maisha ya Saïdjah.

MKABILIANO huu, uliofafanuliwa na Eduard Douwes Dekker, mwandishi wa karne ya 19 aliyeishi katika Asia, unaonyesha tabia yenye kupendeza ya nyati wa majini: uaminifu. Leo, uaminifu bado ni alama yake ya utambulisho. “Nyati wa majini,” asema mtaalamu mmoja, “ni kama mbwa wa familia. Yeye hukupa shauku ya muda wote wa maisha mradi tu unamtendea vizuri.”

Watoto katika Asia, hata katika umri wa miaka minne, wanajua jinsi ya kufanya hilo. Kila siku, wao huongoza rafiki zao wanene hadi mtoni, ambapo wanawaogesha na, kwa vijikono vyao, wanasafisha masikio, macho, na mianzi ya pua za hao wanyama. Nyati, kwa kuitikia hutweta kama tokeo la kuridhika. Ngozi yake nyeusi hufyonza joto jingi, na kwa sababu nyati ana tezi-jasho chache zaidi kwa ulinganifu kuliko ng’ombe, ana tatizo katika kuondoa joto mwilini. Si ajabu kwamba yeye hupenda vibwawa hivi vya kila siku! “Wakiwa wamejizamisha majini au matopeni, wakicheua macho yakiwa yamefunuliwa nusu,” chaonelea chanzo kimoja, nyati “hufanyiza mandhari inayoonyesha burudiko.”

Ingawa hivyo, kupenda kwao maji, ni sehemu moja tu ya tabia zao. Wao wana tabia gani nyinginezo? Kwa nini wao ni wenye mafaa? Kwa kuanza, wao wanafananaje?

Mnyama Mwenye Misuli Apatikanaye Sehemu Tofauti za Ulimwengu

Nyati wa majini (Bubalus bubalis) ana sura ya ng’ombe dume aliyenenepa kupita kiasi na ana uzani wa kilogramu 900 au zaidi. Ana ngozi inayoelekea kutokuwa na manyoya, yenye rangi ya kijivu hivi. Akiwa mwenye kimo cha meta 1.8 mabegani—mwenye pembe zilizotandaa, mgongo ulionyooka, mwili mrefu, shingo iliyoinama, na umbo la kimisuli—yeye ni picha ya nguvu. Mwishoni mwa miguu yake minene mna kivao cha mguuni kinachofaa waendao katika matope: kwato kubwa zenye umbo la kisanduku zilizoshikanishwa kwenye viungo vyenye kunyumbuka. Kunyumbuka huko humwezesha huyo nyati kupinda nyuma kwato zake, kukanyaga vizuio, na kufanya kazi kwa kujitahidi kupitia mashamba yenye matope mahali ambapo ng’ombe hupoteza usawaziko.

Nyati wa ulimwenguni pote milioni 150 wafugwao wanapatikana katika vikundi viwili: ile aina ya bwawani na ile ya mtoni. Kutoka Ufilipino hadi India, nyati wa bwawani, akiwa na pembe zake zilizotandaa kwenda nyuma zenye urefu wa meta 1.2 hadi 1.8, hufanyiza sura ipendwayo sana ya posti-kadi. Wakati hachukui kikao ili kupigwa picha, anapita kwenye matope yafikayo magotini ya mashamba ya mpunga au kuvuta mikokoteni katika njia ambazo ni vigumu kwa madereva wa magari ya kubebea mizigo kupita.

Nyati wa mtoni anafanana na ile aina ya bwawani. Mwili wake ni mdogo kidogo na pembe zake ni za kiasi zaidi—zikiwa zimepindika kwa kukazana au zikiwa zimeinama kwa kunyooka. Lakini akiwa na uzani wa kilogramu 900, huyo pia hupendeza. Katika wakati uliopita, wafanyabiashara Waarabu walileta aina hii kutoka Asia hadi Mashariki ya Kati; na baadaye, Wakrusedi waliokuwa wakirudi waliileta katika Ulaya, ambapo bado inasitawi.

Ingawaje nyati wa majini hawana mbio—wanajikokota kwa mwendo mmoja tu wa kilometa tatu kwa saa—wote nyati wa bwawani na wa mtoni wanapatikana katika sehemu nyingi za ulimwengu. Wamekaa kandokando ya pwani ya magharibi mwa Australia, wametembea pwani za visiwa vya Pasifiki, na hata wanafanya vijia katika msitu wa Amazon. Wako katika msitu wa Amazon?

Wahamiaji Wenye Kusitawi

Watu wanaozuru kujifunza ikolojia wanaoenda Amazon kwa ukawaida mara nyingi huchungua kingo za mito bila mafanikio wakitafuta chui waepaji wa Amerika au chatu wakubwa mno. Hata hivyo, hawahitaji darubini, au hata miwani, ili kuona wapya wa hiyo pori—nyati wa majini, walio kwa maelfu.

Ikiwa wahisi kwamba wahamiaji hawa wa Asia wanaogaagaa matopeni katika Amazon wanahatarisha mfumo wa mazingira, huenda ukafikiria kwenda kuteta polisi kwenye Marajó, kisiwa kilicho katika delta ya mto. Lakini jihadhari! Hautapata usikizi usiopendelea ufikapo kwenye kituo cha polisi, kwani afisa aliye kazini wakati huo huenda ikawa yuko tayari kuondoka kwenda kushika doria akiwa juu ya mgongo wa mfanyakazi wa utangamano mwenye kutisha. Unakisia kwa usahihi, nyati wa majini—na kwa kuongezea ni wa aina ya bwawani! Kwa vyovyote, ni nani atakaye kulalamika?

Kwa hakika, nyati wa majini ni mali kwa eneo la Amazon, asema Dakt. Pietro Baruselli, tabibu wa mifugo afanyiaye kazi moja ya vile vitovu viwili vya utafiti wa nyati wa majini katika Brazili. Yeye aliambia Amkeni! kwamba nyati wana mfumo bora sana wa kumeng’enya chakula ambao huwawezesha kujengwa mwili na malisho ambayo yangewaacha ng’ombe wakiwa wamekonda. Wakulima wa ng’ombe huhitaji kukata misitu daima ili kufanyiza malisho mapya, lakini nyati husitawi kwa malisho ambayo tayari yapo. Dakt. Baruselli asema kwamba nyati wa majini “aweza kusaidia kuhifadhi misitu ya kitropiki.”

Hata hivyo, ili kuendelea kuishi porini, huyo nyati lazima awe mvumbuaji—na ndivyo alivyo. Kitabu The Water Buffalo: New Prospects for an Underutilized Animal chasimulia kwamba katika majira ya mvua, wakati ambapo Amazon hufurikisha malisho, huyo nyati hujirekebisha kulingana na mazingira yake yenye maji. Huku ng’ombe, wakiwa wameachwa juu sehemu isiyo na maji ya ardhi iliyoinuka, wakiangalia kwa macho ya wivu na matumbo matupu, nyati wanaowazunguka, wakitembea majini, wanajilisha kwa mimea ieleayo na hata kula malisho chini ya maji. Malisho yanapotokezea tena, hao nyati huonekana wakiwa laini kama walivyokuwa mbeleni.

Mama Aliye Malkia

Nyati wa majini katika sehemu nyingine za Brazili wananawiri vilevile. Tangu miaka ya mapema ya 1980, kundi la nchi limeongezeka kwa haraka kutoka elfu mia nne hadi mifugo milioni kadhaa. Kwa hakika, nyati wanaongezeka katika kiwango cha juu zaidi kuliko ng’ombe. Kwa nini?

Wanderley Bernardes, mzalishaji wa nyati katika Brazili, aeleza kwamba nyati yuko tayari kujamiiana akiwa na umri wa miaka miwili. Baada ya kipindi cha ujauzito cha miezi kumi, huyo huzaa ndama wake wa kwanza. Miezi 14 baadaye, ndama wa pili huzaliwa. Kukiwa na kiwango cha chini cha kifo miongoni mwa ndama na ukinzaji wa juu wa maradhi, nyati hufurahia maisha marefu yenye uwezo mkubwa wa uzaaji. Muda gani? Wastani wa zaidi ya miaka 20. Uwezo wa kuzaa wa kadiri gani?

“Nitawaonyesha,” asema Bw. Bernardes huku akipiga hatua kuingia katika malisho yaliyowimbika ya shamba lake la hektari 300, yapata kilometa 160 magharibi mwa São Paulo. “Huyu ni Rainha (Malkia),” yeye asema kwa shauku huku akielekeza kidole kwa mnyama ambaye ngozi yake iliyochakaa na pembe ambazo vipande vidogo-vidogo vilivunjika zaonyesha rekodi ya maisha marefu ya nyati. “Ana umri wa miaka 25, nyanya mara nyingi sana, lakini si hilo tu,” yeye aongeza, akifurahi, “ametoka tu kuzaa ndama wake wa 20.” Kukiwa na akina nyanya kama Rainha, si ajabu kwamba wataalamu fulani wanatabiri kwamba katika karne ijayo, kundi kubwa kuliko yote la nyati litakuwa likilisha katika Brazili!

Zaidi ya Trekta Inayoishi

Ingawa hivyo, kwa sasa dai hilo ni la India, makao ya nusu ya nyati wa ulimwenguni pote. Huko na katika nchi nyinginezo za Kiasia, mamilioni ya familia za mashambani ambazo kwa msaada wa nyati wanaendelea kuishi katika bara ambayo mazao yauzwapo hayalipii gharama za utokezwaji. Bila kuhitaji mafuta ya dizeli au speapati, “trekta inayoishi” yao huvuta, kulima, kuchimba, kuvuta mikokoteni, na kutegemeza familia kwa zaidi ya miaka 20. “Kwa familia yangu,” akasema mwanamke fulani aliyezeeka Mwasia, “nyati ni wa maana kuliko mimi. Nifapo, watanililia; lakini nyati wetu afapo, huenda wakaumia kwa njaa.”

Licha ya kuwa mkono wa shambani, nyati ni mwandalizi wa chakula. Asilimia 70 ya maziwa yatokezwayo katika India hutokana na nyati wa majini aina ya mtoni, na maziwa ya nyati hutafutwa sana hivi kwamba inaweza kuwa vigumu kuuza maziwa ya ng’ombe. Kwa nini wengi huyapendelea? “Maziwa ya nyati,” chaeleza kitabu The Water Buffalo: New Prospects for an Underutilized Animal, “yana maji machache, ni mazito zaidi, yana shahamu zaidi, laktosi zaidi kidogo, na protini zaidi kuliko maziwa ya ng’ombe.” Hayo hupa nishati nyingi mno, yana ladha nzuri, na hutumika katika kutengeneza mozzarella, ricotta, na jibini nyingine tamu.

Namna gani nyama ya nyati? “Hatuwezi kutosheleza kutakwa kwayo,” asema mfugaji Bernardes. Katika majaribio ya ladha zenye kupendelewa katika Australia, Venezuela, na Marekani, na nchi nyinginezo, minofu ya nyati ilipendelewa zaidi ya ile ya ng’ombe. Kwa hakika, mamilioni ya watu ulimwenguni pote mara nyingi wanafurahia ladha tamu ya nyama ya nyati huku wakifikiri kuwa wanatafuna-tafuna mnofu wa nyama ya ng’ombe iliyonona. “Mara nyingi watu huwa na wazo la kimbele,” aonelea Dakt. Baruselli, “lakini nyama ya nyati ni tamu kama, na bora mara nyingi kuliko, nyama ya ng’ombe.”

Kupunguza Uzani wa Nyati

Ingawa nyati wanaongezeka katika idadi, wako taabani. “Mafahali wakubwa ambao wangekuwa bora kabisa kwa makusudi ya uzalishaji,” lataja Earthscan Bulletin, “mara nyingi huteuliwa kuwa wanyama wa kuvuta vitu na kuhasiwa, au kupelekwa vichinjioni.” Kwa njia hiyo, tabia za kiurithi za saizi kubwa zapotea, na nyati wanazidi kupungua saizi. “Miaka kumi iliyopita katika Thailand,” wasema wataalamu, “lilikuwa jambo la kawaida kupata nyati mwenye uzani wa kilogramu 1,000; sasa ni vigumu kupata violezo vyenye kilogramu 750.” Je, tatizo hili laweza kutatuliwa?

Ndiyo, yasema ripoti iliyokusanywa na wanasayansi 28 wa wanyama, lakini “hatua ya haraka yahitajiwa . . . ili kuhifadhi na kulinda violezo vyenye kutokeza vya nyati.” Wao wanakubali kwamba kufikia wakati huu, nyati amepuuzwa, lakini “uelewevu mzuri zaidi wa nyati wa majini ungeweza kuwa wenye thamani isivyoweza kukadiriwa kwa mataifa mengi yanayositawi.” Wao wanasema kwamba utafiti zaidi utasaidia “sifa zayo halisi kuzuka.”

Hatimaye, wanasayansi ulimwenguni pote wanagundua kile wakulima wa Kiasia wamekijua kwa karne nyingi: Yule nyati wa majini aliye mwaminifu na mwenye mafaa ni mmoja wa rafiki wakubwa zaidi wa mwanadamu.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Utambulisho Uliokosewa

“KWA kawaida inaaminiwa,” chaonelea kitabu The Water Buffalo: New Prospects for an Underutilized Animal, “kwamba nyati wa majini ni mwenye uhasama na mkali. Ensaiklopedia mbalimbali hutilia mkazo dhana hii.” Hata hivyo, kwa uhalisi, nyati wa majini afugwaye ni “mmoja wa wanyama wanana kuliko wanyama wote wa shambani. Ajapokuwa na sura yenye kutisha, ni sawa sana na mnyama-rafiki wa nyumbani—mwenye kushirikiana, mwanana, na mtulivu.” Ni jinsi gani, basi, nyati wa majini alikuja kupata sifa hii asiyostahili? Huenda akakosa kutofautishwa na nyati wa Afrika (Synceros caffer), ambao kwa kweli ni wenye hasira mbaya ingawa ni wa ukoo wa mbali. Hata hivyo, nyati wa majini hawezi kuzaa nao. Hupendelea kuweka ndugu hao wenye kinyongo mahali walipo—kwa umbali.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki