Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 8/8 kur. 25-27
  • Paradiso ya Aina Tofauti

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Paradiso ya Aina Tofauti
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mbuga ya Aina Tofauti
  • Historia Yenye Kupendeza ya Eneo Hili
  • Mandhari ya Umaridadi
  • Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru
    Amkeni!—2003
  • Umaridadi wa Mbuga za Taifa za Milimani
    Amkeni!—1997
  • ‘Ni Neno Jema Kama Nini Wakati Ufaao!’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Corcovado Mbuga Inayovutia ya Kosta Rika
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 8/8 kur. 25-27

Paradiso ya Aina Tofauti

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA

UNAPOSIMAMA juu ya mwinuko wa mtaro na kutazama chini kwenye sakafu ya bonde, unashangazwa na mandhari ya kustaajabisha—milima yenye miinuko na mabonde marefu. Mbele yako kuna nyasi nyingi sana. Upepo wa ghafula wapita, ukiwa umejaa manukato makali ya majani ya sage, manukato ya uwanda mpana wa majani.

Ebu wazia kwamba miaka mia mbili tu iliyopita, ungesafiri kwa siku kadhaa ukiona kwa mfululizo kundi kubwa la nyati ambao walifunika mbuga kubwa za Kanada na ungeweza kusikia ardhi ikitikisika chini yako kwa mtetemo wa mamilioni ya kwato. Hata kule kuhama kwa wanyama wa Afrika kunakojulikana sana hakungeweza kushinda kule kwa nyati waliorandaranda katika sehemu hii yenye nyasi nyingi.

Sasa, ishara pekee zinazobakia za kuonyesha kwamba kulikuwako nyati wakati fulani ni mawe makubwa ambayo nyati walijisugulia. Unaweza kugusa pembe za mawe zilizo laini na kuona mitaro iliyofanywa kuzunguka mawe hayo na maelfu ya nyati waliosugua ngozi zao zenye kuwasha kwenye mawe hayo. Si pepo zenye nguvu tu zinazovuma kutoka magharibi ambazo husababisha utokwe na machozi bali pia ni hisi yenye nguvu sana ya kicho kwa maajabu ya uumbaji ambayo hukuzunguka na kujaza hisi zako. Upo wapi? Unazuru paradiso ya aina nyingine.

Mbuga ya Aina Tofauti

Wakaribishwa kwenye mbuga ya Grasslands National Park, katika kusini-magharibi ya Saskatchewan, Kanada—mbuga pekee katika Amerika Kaskazini iliyotengwa ili kuhifadhi uwanda usiovurugwa wa nyasi ya aina mbalimbali. Mbuga hiyo hasa inafanyizwa na sehemu ya mashariki na ya magharibi zinazotenganishwa na kilometa 22.5. Hatimaye itatia ndani kilometa 900 za mraba.

Mandhari ni yenye mawemawe na imejaa vizuizi vikubwa. Uvumbuzi hufanywa vema zaidi kwa kutembea kwa miguu au kwa kupanda farasi. Kupiga kambi kwa usiku kadhaa chini ya nyota kunawezekana kwa walio wajasiri, lakini ujitayarishe kubeba maji ya kutosha na maandalizi mengine ya lazima. (Ona sanduku “Uvumbuzi wa Mbuga”) Wakati wa safari yako kupitia kwenye mbuga, hutaona nyumba za kisasa, hakuna barabara za lami, hakuna nyaya za umeme, na hakuna mahali pa marundiko ya takataka, na hakuna mahali pa kuegeshea magari. Huenda hata usikutane na mwanadamu mwingine. Kwa kweli, ni paradiso ya aina tofauti! Uingiapo mbugani, unaingia katika ulimwengu ulio na umaridadi wa kipekee.

Nyanda Kuu za Amerika Kaskazini hufanyiza mojawapo ya mazingira yaliyovurugwa zaidi ulimwenguni. Miaka ipunguayo mia mbili hivi iliyopita, hii ilikuwa pori kamili, ardhi isiyoguswa. Kwa kielelezo, leo, chini ya asilimia 25 ya uwanda wa nyasi za aina mbalimbali katika Kanada bado haujasitawishwa. Wazo la kulinda uwanda huu wa nyasi kwa kuufanya kuwa mbuga liliibuka katika miaka ya 1830. Zaidi ya miaka mia moja baadaye, katika mwaka wa 1957, Saskatchewan Natural History Society ilianzisha kazi ya kutengeneza mbuga ya kitaifa.

Hata hivyo, ni kufikia mwaka wa 1988 kwamba mkataba wa serikali kuu na ya jimbo ulipoanzisha mbuga ya Grasslands National Park. Mbuga hii pamoja na nyinginezo katika nyanda za nyasi za Kanada sasa hulinda mimea 22, mamalia, na ndege ambao wako katika orodha rasmi ya Kanada kuwa zimo hatarini mwa kutoweka. Kwa kuongezea, aina nyingine nyingi zimehifadhiwa, nyinginezo hazipatikani mahali popote ulimwenguni.

Mbuga ya Grasslands ni bara lenye tabia ya nchi ipitayo kiasi. Kwa kuwa iko katikati ya bara, haiathiriwi na athari zozote za bahari za kusawazisha halijoto. Hivyo, halijoto ya majira ya baridi kali yaweza kufikia digrii -50 za Selsiasi, na wakati wa kiangazi, ni kawaida kuwa na halijoto yenye digrii 40 za Selsiasi. Ikiwa na mvua kidogo sana na upepo usiokoma tabia ya nchi haipendezi .

Hata hivyo, ingawa hawaonekani kwa urahisi mara ya kwanza, kuna wanyama wengi sana. Kwa saburi na udumifu, hasa kwenye mapambazuko na wakati wa jioni-jioni, huenda ukafanikiwa kumpiga picha mbawala, mbwa mwitu, paka shume, sungura, kwale, nyoka-kayamba, bundi wafukuaji, mwewe wa kikahawia, tai, aina ya paa (anayedhaniwa kuwa mnyama mkubwa mwenye mbio zaidi wa Amerika Kaskazini), au kikundi kinachobakia cha kindi wenye mikia myeusi katika Kanada. Pia utaona ndege wengine wengi na wadudu na mimea ya sehemu hiyo.

Historia Yenye Kupendeza ya Eneo Hili

Iwapo utaamua kuzuru mbuga hii ya kipekee, twakutia moyo ufanye utafiti fulani kuhusu eneo hili. Utapata eneo hili lina historia yenye mambo mengi. Mathalani, bado kuna ishara zinazoonyesha ile njia ya North West Mounted Police Red Coat. Katika mwaka wa 1874, baada ya kusikia uvumi juu ya msukosuko kati ya Wahindi na Wazungu, serikali ya Kanada ilipeleka kikosi maalumu cha Mounted Police mia tatu kuelekea Magharibi ili kuweka sheria na utengamano. Jambo hili pia liliondoa hofu za wengi kwamba Magharibi ya Kanada ilikuwa karibu kutwaliwa na Marekani. Wakiwa wamevalia mavazi yenye rangi nyekundu nyangavu na kupanda farasi waliopambwa vizuri, kikosi hiki kilivutia sana hivi kwamba mpaka leo hii njia waliyotumia huitwa Red Coat Highway.

Kwa kupendeza, katika mwaka wa 1878 eneo hili lilikuwa makao ya wanavita Wahindi wanaohofiwa zaidi katika Amerika Kaskazini—chifu mkuu wa Sioux aliyeitwa Fahali Aketiye. Baada ya ushindi wa Sioux dhidi ya majeshi ya Custer katika Little Bighorn, maelfu ya Waamerika wa Sioux walikimbilia sehemu hii ya Kanada ili kupata hifadhi kutokana na kikosi cha wapanda farasi Waamerika.

Kuna karibu sehemu 1,800 za kiakiolojia katika mbuga ambazo zina chanzo cha kale hata zaidi. Juu ya vilima vingi, juu ya vilele vya vilima, na vilima vilivyotengwa miamba mikubwa yaweza kupatikana ambayo ilikuwa msingi wa mahema. Pindi fulani miamba hii ilishikilia kingo za hema zilizotengenezwa kwa ngozi ya nyati ili kuzizuia zisipeperushwe na upepo. Pia kuna njia ambazo Wahindi wa Nyanda Tambarare walipitia wakiingiza makundi ya nyati ili wawauwe kwa ajili ya chakula. Karne nyingi zilizopita, eneo hili lilikuwa mahali palipojaa wanyama wa kuwindwa na makabila ya Gros Ventre, Cree, Assiniboin, Blackfoot, na Sioux.

Miaka mingi sana huko nyuma, katika sehemu ya mashariki ya mbuga, mabaki ya dinosau yamepatikana katikati ya vilima vya udongo vilivyomomonyolewa vya Killdeer Badlands.

Mandhari ya Umaridadi

Ikiwa unamnanamna wa mimea na wanyama au historia yenye kupendeza ya bara hili hazitoshi kukustaajabisha, uzuri wa bara na mandhari yake yenyewe yenye kuvutia utakustaajabisha hakika. Kuna sauti tele za aina za ndege, manukato ya sage, na utahisi jua likiwa kali na upepo. Ladha ya chakula kilichopikwa na jiko la kubebwa huongezewa na maono ya mandhari, ambayo huyapendeza macho yako daima. Isitoshe, unaweza kutazama kotekote hadi upeo wa macho bila kuzibwa, hasa kandokando ya Two Trees Interpretive Trail, iliyo katika sehemu ya magharibi ya mbuga. Anga kubwa la samawati nyangavu limerembwa na mawingu meupe ya hapa na pale ambayo huning’inia juu yako kama mlima unaoelea. Mandhari yenye kuvutia hukupa hisi kubwa sana ya uhuru, na wakati uleule, kukufanya ujihisi kuwa duni sana na kutiwa kicho.

Kuhusu uwanda wa majani, jambo kuu si kile uonacho tu bali pia kile uhisicho. Kitakachokuvutia urudi katika paradiso hii ya aina tofauti ni namna uhisivyo kuihusu. Unapoizuru moyo wako unajawa na shukrani. Mawazo yako yanajawa na sifa kwa Muumba Mtukufu, Yehova, aliyeitokeza. Karibuni siku inayongojewa sana itafika ambapo dunia nzima itakuwa paradiso na kutokeza kikamili umaridadi wake wa asili.

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

Uvumbuzi wa Mbuga

Kumbuka

1. Kusajiliwa na wafanyakazi wa mbuga na kupata kijitabu cha habari kabla ya kuingia katika mbuga.

2. Kubeba maji ya kunywa ya kutosha. Maji ya kunywa hupatikana tu kwenye Idara ya Habari ya Mbuga.

3. Kuvaa kofia ya kujikinga na jua na pia viatu imara vyenye kustarehesha ambavyo vitafunika tindi zako ili kujilinda na miiba ya mipungate.

4. Kubeba fimbo ili kuibembeza kwenye njia unapotembea katika nyasi ndefu na vichaka.

5. Kubeba kamera na darubini, ikiwa unazo. Wakati unaofaa zaidi kutazama wanyama ni kwenye mapambazuko na wakati wa jioni-jioni. HADHARI: Epuka kuingiza miguu na mikono katika sehemu usizoweza kuona. Nyoka-kayamba waweza kuuma wanapozingiwa au kushtuliwa. Ni kinyume cha sheria kusumbua au kuwinda wanyama wa pori katika mbuga ya kitaifa.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Picha zote: Parks Canada

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki