Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 11/22 kur. 13-17
  • Umaridadi wa Mbuga za Taifa za Milimani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Umaridadi wa Mbuga za Taifa za Milimani
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kusudi Lake
  • Aina Tofauti-Tofauti za Viumbe vya Asili
  • Mimea ya Milimani
  • Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru
    Amkeni!—2003
  • Paradiso ya Aina Tofauti
    Amkeni!—1998
  • Shamba la Starehe Duniani Pote Jinsi Gani?
    Amkeni!—1990
  • Milima Imo Hatarini
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 11/22 kur. 13-17

Umaridadi wa Mbuga za Taifa za Milimani

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA

MAJI-MANGAVU kabisa yanatiririka katika kijito, majani yakipigapiga kwa uanana katika upepo, anga lisilo na mawingu juu, mwangaza ukipenya katika miti. Hizi ni mandhari na sauti zenye kupendeza zinazotukaribisha, na tuna hakika hizo ni mwanzo tu wa siku nzuri ajabu. Tupo wapi? Tumo katika Mbuga ya Taifa ya Écrins, katika Milima ya Dauphiné, Ufaransa.

Kwenye lango moja la mbuga hiyo katika Ailefroide, ukingoni mwa msitu, vibao vya habari vyaonyesha kwamba utendaji fulani hauruhusiwi katika mbuga hiyo, kama vile kupiga kambi au kuwasha moto. Tunaombwa tupeleke takataka zozote nyumbani kwetu, na tunaona kwamba mbwa hawaruhusiwi, kwani mara nyingi huwatisha au huwasumbua wanyama wa eneo hilo.

Kusudi Lake

Lakini mbuga ya taifa ni nini hasa, na hiyo inatumikia kusudi gani? Mbuga ya kwanza, ile Mbuga ya Taifa ya Yellowstone iliyo katika jimbo la Wyoming, ilianzishwa katika mwaka wa 1872 katika Marekani. Tangu wakati huo, nyingi zimeanzishwa katika kila kontinenti. Katika Ufaransa, kuna mbuga saba za taifa, tatu kati ya hizo ziko katika milima ya Alps iliyo na umbo la mwezi, ambayo imesambaa kutoka Ufaransa hadi Austria. Mbuga ya taifa ya kwanza katika Ulaya ilianzishwa katika mwaka wa 1914 katika mkoa wa Graubünden (Grisons), Uswisi. Kisha, katika mwaka wa 1922, mbuga ya Taifa ya Gran Paradiso, katika Italia, ilifunguliwa. Mbuga nyinginezo katika milima yenye umbo la mwezi zatia ndani Berchtesgaden, katika Ujerumani; Hohe Tauern, katika Austria; Stelvio, katika Italia; na Triglav, katika Slovenia. Mbuga ya taifa ya kwanza katika Ufaransa ilikuwa Vanoise, iliyoanzishwa katika mwaka wa 1963.

Kusudi la msingi la mbuga za taifa ni kulinda mimea na wanyama wa asili. Inapaswa kujulikana pia kwamba kuna mbuga nyinginezo nyingi ambazo hazina hadhi ya kitaifa ambazo zina mradi uleule mmoja. Miongoni mwa hizo ni Mbuga ya Mkoa ya Vercors, katika Ufaransa, na Hifadhi ya Karwendel, katika Austria. Lakini, mbuga za taifa zina hadhi za kipekee ambazo huwakabidhi walinzi wake mamlaka fulani. Wana mamlaka ya kutoza faini wale wasiofuata sheria za mbuga. Kwa kielelezo, kuleta mbwa ndani ya mbuga katika Uswisi kwaweza kusababisha faini ya hadi franka 500 za Uswisi (dola 350 za Marekani).

Labda wengine walifikiria hilo kuwa ni kupita kiasi. Lakini kuna sababu za makatazo na faini fulani. Fikiria. Wakati fulani tulipokuwa katika Mbuga ya Taifa ya Mercantour, katika milima ya Maritime Alps kusini-mashariki mwa Ufaransa, tulimwona paa-mbuzi mdogo aliye mchanga sana. Alionekana kama alikuwa peke yake na bila msaada kabisa. Lakini, hatukumgusa, kwani tulifikiri kwamba harufu zetu zingemfanya mama yake asimkubali tena. Lakini wazia ikiwa tungekuwa na mbwa! Paa-mbuzi huyo angetishwa, hasa ikiwa mbwa huyo angeanza kubweka.

Je, hili lamaanisha kwamba kazi ya walinzi ni kuwa askari tu wa mbuga? Hapana, bila shaka sivyo. Mlinzi mmoja tuliyekutana naye katika Mbuga ya Mercantour alituonyesha mahali kundi la paa-mbuzi lilipokuwa limepita punde tu, wakiacha nyayo zao katika theluji iliyotoka kunyesha. Alionyesha jinsi kwato zilivyoacha nyayo zao. Hili lilitusaidia tuthamini kwamba zaidi ya kutunza usawaziko wa asili katika mbuga, ni jukumu la walinzi kutoa habari na kufundisha.

Aina Tofauti-Tofauti za Viumbe vya Asili

Mbele katika kijia chetu, katika kilima kilicho mbali, twaona paa-mbuzi akichezacheza kwa furaha katika kiwanja cha theluji. Pia twawaona panyabuku wawili wakichezacheza kwa furaha juu ya miteremko ya changarawe. Baadhi ya panyabuku hao ni wapole sana, wakiwakaribia wapanda-milima, wakitumaini kupata chakula.

Makundi ya mbuzi-mwitu huishi katika baadhi ya mbuga za milimani. Wako wengi zaidi katika Mbuga ya Gran Paradiso, katika Italia. Tulisisimka kuona baadhi yao katika Mercantour. Mbuga hii iliyo kusini ya milima ina wanyama wengi sana. Mouflons, aina ya kondoo wa mwitu, huzunguka-zunguka kwa uhuru, na mbwa-mwitu wameonekana tena katika miaka ya majuzi. Hata hivyo, wageni hawapaswi kuogopa, kwa kuwa ni nadra kwa mbwa-mwitu kukaribia vijia nao huwaepuka wanadamu. Zamani, dubu pia walitanga-tanga katika milima ya Alps ya Uswisi, lakini wa mwisho kuonekana hapo aliuawa katika mwaka wa 1904. Katika Ulaya Magharibi dubu wa kikahawia sasa waweza kupatikana katika Pyrenees, katika mpaka wa Ufaransa na Hispania; katika Milima ya Cantabrian, kaskazini mwa Hispania; na katika Mbuga ya Taifa ya Abruzzi iliyoko katikati ya Italia. Kwa upande mwingine, nyakati fulani waweza kumsikia paa dume akipiga kelele katika Mbuga ya Taifa ya Uswisi, ambako wako wengi.

Hata hivyo, mbali na wanyama wakubwa, wapo wanyama wengi wadogo wa kumfurahisha mgeni, kama vile vicheche na sungura wa aina tofauti-tofauti, ambao hubadilika kuwa weupe wakati wa majira ya baridi kali, pia mbweha, panyabuku, na kindi. Kwa kuongezea, wadudu wengi sana, kutia ndani vipepeo maridadi sana na mchwa wenye bidii ya kazi, hukaa katika maeneo haya. Wapenzi wa ndege bila shaka hawatakatishwa tamaa. Waweza kumwona tai akipaa juu ya kichwa chako au hata, katika Mbuga ya Taifa ya Uswisi na katika mbuga za Vanoise na Mercantour, lammergeier, au tai-mzoga mwenye kidevu. Pia ni kawaida sana kusikia sauti za kipekee za gogota akigongagonga mti akitafuta wadudu. Wengi huuliza jinsi ambavyo wakazi hawa wa mlimani huokoka wakati wa majira ya baridi kali katika milima ya Alps. Wanyama hawa ni wenye kubadilikana sana ili wafae hali hii, ingawa hali ngumu husababisha vifo kwa wagonjwa na wazee-wazee.

Mimea ya Milimani

Hata mimea hulindwa katika mbuga hizi. Kwa sababu hiyo, hairuhusiwi kuchuma maua hayo, kutia ndani maua maridadi sana ya yungiyungi ya rangi ya machungwa, ambayo yapo kandokando ya kijia chetu. Labda washangaa kwa nini iko hivyo. Mimea fulani—kama vile ile mimea maarufu gurudumu-meno, anemone ya mlimani, waridi-mlima, bluet ya mlimani na namna fulani za kikoroga-maziwa— ni haba sana, na ni muhimu kuilinda ili kuhakikisha imeendelea kuwapo. Maua ya namna nyingi ni yenye kuvutia sana.

Umaridadi wa asili pia huonekana wazi katika miti ambayo hupamba mbuga hizo. Katika vuli rangi ya kidhahabu ya misonobari huipamba msitu. Kwa upande mwingine, arolla, msonobari wa Uswisi, huokoka ukali wa majira ya baridi kali, ukitoa ugavi wenye kudumu wa chakula kwa ndege ajulikanaye kwa kawaida kuwa mvunja-kokwa. Ndege huyu husafirisha mavuno yake ya mbegu za msonobari katika kifuko chake na kisha huzifukia kwa ajili ya matumizi ya wakati ujao. Kwa kufanya hivyo, huchangia katika kusambaza msonobari katika maeneo ambayo kama sivyo yasingefikiwa. Bila shaka, tungeweza kutumia siku nzima kuangalia umaridadi unaotuzunguka. Lakini ikiwa tunataka kufikia nyumba ya mlimani, ni lazima tuendelee kupanda.

Twaendelea na mwendo wetu na baada ya muda mfupi twafikia sehemu iliyo ngumu zaidi. Paa-mbuzi waonekana kana kwamba wanatungoja msituni, na twaweza kupiga picha kadhaa. Lakini, tukaribiapo zaidi, viumbe hao warembo watoroka, bila shaka wakiogopeshwa na kukaribia kwetu. Twafikiria ahadi nzuri ajabu ya Mungu iliyorekodiwa katika Isaya 11:6-9: “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja. . . . Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu.” Twafurahia tumaini la kwamba hivi karibuni dunia yote itakuwa paradiso iliyo kama mbuga kubwa, ambapo watu na wanyama wataishi pamoja bila hofu.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Paa-mbuzi akiwa amestarehe katika milima ya Alps ya Ufaransa

[Picha katika ukurasa wa 14]

Panyabuku mwenye hadhari katika Mbuga ya Taifa ya Vanoise, Ufaransa

[Picha katika ukurasa wa 14]

Tai katika Mbuga ya Taifa ya Mercantour Ufaransa

[Picha katika ukurasa wa 15]

Paa-mbuzi wakipanda milima ya Alps ya Ufaransa

[Picha katika ukurasa wa 15]

Paa-mbuzi mchanga

[Picha katika ukurasa wa 16]

Waridi la mlimani

[Picha katika ukurasa wa 16]

Artichoke ya porini

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ancolie des Alpes

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mbuzi-mwitu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Yungiyungi ya rangi ya machungwa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Yungiyungi aina ya Turk’s-cap

[Picha katika ukurasa wa 17]

Panicaut des Alpes

[Picha katika ukurasa wa 17]

Panyabuku

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki