Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 6/22 kur. 25-27
  • Bustani za Japani—Mifano Midogo ya Asili

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Bustani za Japani—Mifano Midogo ya Asili
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Miti Inayotumiwa Katika Bustani ya Japani
  • Kulengeta na Kutunza Miti
  • Bustani za Familia
  • Upendo Wetu kwa Bustani
    Amkeni!—1997
  • Kutazama Baadhi ya Bustani Maarufu
    Amkeni!—1997
  • Miti Inayodumu Muda Mrefu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Kuuvumbua Ulimwengu wa Miti Maridadi
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 6/22 kur. 25-27

Bustani za Japani—Mifano Midogo ya Asili

Na mleta habari za Amkeni! katika Japani

UNAPOTAZAMA nje ya dirisha lako, unaona bahari, yenye ukingo wa mchanga mweupe na miti ya misunobari yenye rangi ya kichanikiwiti. Ukisimama kwenye sebule yako, unaona milima yenye fahari ikiwa na maporomoko ya maji. Na kwa kadiri unavyoweza kuona, kila kitu ni mali yako. Je! hiyo ni ndoto isiyoweza kutimia kwa watu wa kawaida? La, si kama una bustani ya Japani. Kufananisha asili katika mfano mdogo hutimiza ndoto hiyo inayoonekana kuwa haiwezi kutimizwa.

Ili kufanyiza fahari ya asili, miamba, maji, mimea, na nyakati nyingine mchanga hutumiwa. Bila shaka, akili kidogo inahitajiwa, lakini ulinganifu mzuri ukitumiwa, mambo ya ajabu hufanyizwa. Kidimbwi huwakilisha bahari au ziwa, na mawe ya kukanyagia, visiwa. Mawe makubwa yanakuwa milima, na maji yanayotiririka kati ya mawe, maporomoko ya maji.

Miti Inayotumiwa Katika Bustani ya Japani

Kwa sababu rangi ya kijani-kibichi huonekana zaidi katika mandhari ya asili ya Japani, miti badala ya maua hutumiwa sana katika bustani. Miti haiwekwi tu kivivi-hivi na kuachwa ikue ovyoovyo. Nafasi kati ya miti hupangwa vizuri, na ukuzi wayo kudhibitiwa. Kwa kweli, miti ina sehemu muhimu sana. Inaleta hali ya utulivu ambayo huonekana sana katika bustani za Japani.

Aina ya miti yenye rangi-rangi hutumiwa lakini kwa kiasi kidogo. Inaongeza mandhari tofauti-tofauti za bustani msimu mmoja hadi msimu mwingine. Mizambarau, cheri, na magnolia hutumiwa kwa ajili ya rangi zayo mapema katika masika. Katika Aprili na Mei, michipuko yenye uangavu ya azalea hutokeza hali nyangavu kwa mazingira hayo ya utulivu. Vichaka vya azalea mara nyingi hupogolewa viwe mipira laini yenye umbo la mviringo, mikubwa kwa midogo. Katika vuli, majani ya mti maple wa Japani hutokeza rangi nyekundu. Hata hivyo, rangi ya kijani-kibichi ndiyo huonekana sana katika bustani ya Japani.

Vichaka vya kuvutia vya mianzi huongeza ile mazingira ya Kimashariki. Mteashuri na mierezi hupandwa na kupogolewa, ikitoa hali nzuri kwa bustani hiyo. Mti holi (inu-tsuge) wa Japani unapendwa wakati wote, kwa sababu mambo mengi yaweza kufanywa nao. Unaweza kupata mti holi umepogolewa ufanane na keki ya arusi, kasa, au korongo anayesimama juu ya mguu mmoja. Hata hivyo, kati ya miti yote inayotumiwa katika bustani, misunobari yenye fahari hutumiwa zaidi.

Kulengeta na Kutunza Miti

Miongoni mwa misunobari ya aina mbalimbali ya Japani, ule mweusi na mwekundu ndio hutumiwa zaidi kwa kulengetwa. Ule mweusi huitwa “wa kiume” na ule mwekundu “wa kike” kwa sababu ya hali zao zinazoonyesha nguvu na upole. Kati ya miti hiyo miwili, ule ugumu wa msunobari mweusi huufanya uwe rahisi kukuzwa na kuzoezwa. Ebu tuchu-kue msunobari kuwa kielelezo na tuone jinsi miti katika bustani ya Japani hulengetwa na kutunzwa.

Mtunza bustani ataanza kazi yake kwa miche. Akichunguza jinsi itakavyokua, anaifanyiza kwa uangalifu miche hiyo ikue katika mitindo kadhaa inayopendwa zaidi. Huenda akapenda ukuzi wenye kukingama ambao ukiwekwa katika lango la nje unafanyiza tao la msunobari lenye kupendeza. Au anaweza kujaribu mtindo wa kufanya matawi yaelekee chini na hivyo kutoa hali ya kuteremka chini. Kusimama wima rasmi kwaweza kutumiwa pia. Mtunza bustani hulengeta umbo na ukubwa unaotakikana?

Anaweza kupanda mche wake kwa mwinamo fulani na atumie fito za mianzi kuwa viegemeo. Anafunganisha fremu au magango na fito za mianzi za kwenda upande kwa kutumia uzi mweusi usioweza kuoza uliotengenezwa kwa gamba la mchikichi. “Uzi huo,” aeleza mtunza bustani wa kizazi cha nne, “hubadilishwa muda baada ya muda ili usiache alama zisizopendeza kwenye matawi.” Fito huachwa kwa mwaka mmoja au miwili mpaka umbo jipya litashika bila fito hizo.

Kisha kuna ile sehemu muhimu zaidi ya kuzoeza miti—kupogoa. “Mtunza bustani hujaribu kusawazisha majani na matawi yanayokua bila mpango na yale yaliyopogolewa kufikia kiwango ambacho udhibiti wa mwanadamu waonekana sana,” chasema kitabu Japanese Gardens for Today. Anajaribu kukazia sehemu zinazovutia zaidi ya mti kwa kukata kila kitu kinachoizuia sehemu hiyo. Je! anataka kueneza mti huo kwa upande mmoja? Ndipo hupogoa matawi yanayoelekea juu. Matokeo yanakuwa kwamba utomvu wenye lishe utaelekea kwenye matawi ya upande na hivyo kugeuza umbo la mti.

Hata hivyo, mambo zaidi yanahitajiwa. Kila masika vichwa vya michipuko mipya hukatwa. Hilo huacha mchipuko wenye urefu wa milimita kama ishirini na tano kwenye miisho ya kila kitawi ili kuenea kwa matawi kudhibitiwe. Majani ya misunobari yenye umri wa mwaka mmoja pia hung’olewa kwa mikono kila mwisho wa Septemba. Hilo hutokeza sura ya miti ya misunobari ya Japani inayoonekana kuwa yaelea na yenye mabawa.

Misunobari inaweza kuishi kwa mamia ya miaka ikitunzwa vizuri. Ili kuihakikishia maisha marefu yasiyo na magonjwa, mtunza bustani huendelea kufanya kazi ya kuiweka ikiwa na afya nzuri. Njia moja anayotumia isiyo ya kawaida ni kufunga shina kwa bandeji ya jamvi la majani makavu. Kipupwe kinapoanza, vidusia (wadudu) vinavyoishi mtini hutafuta sehemu zenye joto na kwa hiyo hushuka chini na kujiingiza pamoja na mayai yao kwenye jamvi. Katikati ya kipupwe, kabla siku zenye joto hazijatoa wadudu hao nje, jamvi hilo huondolewa na kuchomwa pamoja na vidusia hao. Majamvi yanapowekwa kwenye urefu wote wa miti, kama vile michikichi, yanalinda miti hiyo kutokana na theluji na kuifanya isigande. Mbali na kuweka miti ikiwa na joto, suti hiyo maridadi ya majamvi huangazia pia mandhari isiyopendeza ya kipupwe.

Kazi hiyo yote ni ustadi ambao si rahisi kufahamika wala kuigwa. Kwa kweli, ili kutunza baadhi ya miti hii yenye kuishi muda mrefu, kunahitaji vizazi vya watunza bustani.

Bustani za Familia

Zikilinganishwa na bustani nzuri zaidi katika sehemu za umma, bustani za familia za Japani si za rasmi sana lakini zenye hali ya kuvutia zaidi. Kuna fursa nyingi za kuchanganya na kupatanisha rangi ya kijani-kibichi kulingana na mapendezi na mawazio ya mtu.

Familia nyinginezo hufanyiza mifano yao midogo ya mandhari ya milima ikiwa na maporomoko ya maji mengi au kijito chenye kupinda-pinda kwa ukimya kwa kutumia miamba mikubwa na miti midogo. Hata kama nyumba ina nafasi ya meta kidogo tu ya bustani katika kona fulani, kanuni zilezile za mifano midogo zinazotumiwa katika kupanda sehemu zilizo kubwa zaweza kutumiwa. Na kwa msaada wa miti iliyochongwa kwa ustadi sana, tazama! ile ndoto inatimizwa.

Hata uwe unaishi wapi duniani, kanuni zilezile zinazotumiwa katika kutengeneza bustani nzuri ya Japani zinaweza kuleta fahari ya asili katika bustani yako.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Miti ya cheri huongeza rangi wakati wa masika

[Picha katika ukurasa wa 26]

Miti hulengetwa kuwa maumbo mbalimbali

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki