Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 4/8 kur. 4-7
  • Kutazama Baadhi ya Bustani Maarufu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutazama Baadhi ya Bustani Maarufu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Bustani za Mapema
  • Tokea Bustani za Waarabu Hadi Bustani za Waingereza
  • Mandhari za Mashariki
  • Upendo wa Ulimwenguni Pote
  • Upendo Wetu kwa Bustani
    Amkeni!—1997
  • Chakula Kutoka Shamba Lako
    Amkeni!—2003
  • Bustani za Japani—Mifano Midogo ya Asili
    Amkeni!—1993
  • ‘Wamwachao Yehova Wataangamia’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 4/8 kur. 4-7

Kutazama Baadhi ya Bustani Maarufu

MAONO ya mwanadamu na Paradiso yalianza katika bustani iliyo katika eneo lililoitwa Edeni, labda karibu na Ziwa Van, la Uturuki ya kisasa. Mto uliogawanyika na kufanyiza mito minne ilitilia maji bustani hiyo kwa ajili ya Adamu na Hawa, ambao walipaswa ‘kuilima na kuitunza.’ Ingependeza kama nini kutunza bustani iliyojaa “kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa”!—Mwanzo 2:8-15.

Edeni ilikuwa makao makamilifu. Adamu na Hawa na wazao wao walipaswa kueneza mipaka yayo, bila shaka wakitumia ubuni wa awali wa Mungu ulio maridadi sana kuwa kigezo cha kufuata. Baada ya muda, dunia yote ingekuwa paradiso iliyojaa vizuri watu. Lakini kutotii kimakusudi kwa wazazi wetu wa kwanza kulifanya waondoshwe kwenye himaya hiyo. Kwa kuhuzunisha, wengine wote wa familia ya kibinadamu walizaliwa nje ya makao hayo ya Edeni.

Hata hivyo, mwanadamu aliumbwa na Muumba aishi katika Paradiso. Basi ni kawaida kwamba vizazi vya wakati ujao vingejizingira na miigo ya Paradiso.

Bustani za Mapema

Bustani za Juu za Babiloni zimesifiwa kuwa mojawapo ya maajabu ya ulimwengu wa kale. Hizo zilijengwa na Mfalme Nebukadreza zaidi ya miaka 2,500 iliyopita kwa ajili ya mke wake Mmedi aliyetamani misitu na milima ya kwao. Ujenzi huo wa kimo cha meta 22 wenye ngazi, kuba zilizopinda, zote zikiwa zimepandwa mimea sana, ulikuwa na mchanga wa kutosha kukuza miti mikubwa. Malkia huyo aliyetamani kwao alielekea kufarijika alipotembea-tembea katika eneo hilo lililofanana na Edeni.

Utengenezaji wa mandhari ulitia fora katika Bonde la Naili lenye rutuba katika Misri. “Misri,” chasema The Oxford Companion to Gardens, “ndiyo chanzo cha picha za kale zaidi za bustani na pia mahali penye desturi ya muda mrefu sana . . . ya utunzaji wa bustani.” Plani ya mandhari ya bustani ya ofisa mmoja wa Misri katika Thebes, ambayo ni ya karibu 1400 K.W.K., yaonyesha vidimbwi, barabara zenye miti kandokando, na vibanda. Mbali na bustani za kifalme, bustani za hekalu ndizo zilizokuwa na mimea zaidi, zikiwa na miti, maua, na mimea midogo ambayo ilinyunyiziwa maji kupitia mifereji kutoka kwenye vidimbwi na maziwa yaliyojaa ndege wa majini, samaki, na lili-loto.—Linganisha Kutoka 7:19.

Waajemi pia walikuwa watunza-bustani stadi wa awali. Bustani za Uajemi na Misri zilikuwa zenye kuvutia sana hivi kwamba wakati majeshi ya Aleksanda Mkubwa yenye ushindi yaliporudi kutoka Ugiriki katika karne ya nne K.W.K., hayo yalikuja kama yamejaza mbegu, mimea, na mawazo mapya. Katika Athene, Aristotle na mwanafunzi wake Theophrastus walikusanya mimea hiyo yenye kuongezeka na kuanzisha bustani ya mimea, ili kuchunguza na kuainisha mimea. Matajiri wengi wa Ugiriki, kama ilivyo na Wamisri na Waamedi kabla ya wao, walikuwa na bustani maridhawa.

Wakazi wa jiji la Roma walichanganyisha makao na bustani katika nafasi ndogo ya jijini. Matajiri waliunda bustani za raha katika nyumba zao za mashambani. Hata Nero mkatili alitaka Edeni yake, kwa hiyo kwa ukatili alihamisha kwa nguvu mamia ya familia, akaharibu nyumba zao, na kutengeneza bustani yake ya zaidi ya hektari 50 kuzingira makao yake ya kifalme. Baadaye, karibu na mwaka wa 138 W.K., kwenye nyumba ya Maliki Hadrian katika Tivoli, utengenezaji wa mandhari katika Roma ukafikia upeo. Nyumba hiyo ilikuwa na hektari 243 za bustani, vidimbwi, maziwa, na mabomba ya kububujisha maji.

Waisraeli wa kale pia walikuwa na bustani. Mwanahistoria Myahudi Josephus aandika kuhusu bustani zenye kujaa vijito katika mahali paitwapo Etam, kilometa 13 hadi 16 hivi kutoka Yerusalemu. Bustani za Etam huenda zilikuwa miongoni mwa ‘bustani, viunga, birika za maji na mwitu’ ambazo Biblia yasema Solomoni ‘alijifanyizia.’ (Mhubiri 2:5, 6) Nje tu kidogo ya Yerusalemu kwenye Mlima wa Mizeituni kulikuwa na Bustani ya Gethsemane, iliyofanywa mashuhuri na Yesu Kristo. Hapo, Yesu alipata mahali ambapo angeweza kufundisha wanafunzi wake.—Mathayo 26:36; Yohana 18:1, 2.

Tokea Bustani za Waarabu Hadi Bustani za Waingereza

Majeshi ya Waarabu yalipoenea mashariki na magharibi katika karne ya saba W.K., hayo, kama Aleksanda, yaliona bustani za Uajemi. (Linganisha Esta 1:5.) “Waarabu,” aandika Howard Loxton, “walipata kwamba bustani za Waajemi zilifanana sana na paradiso iliyoahidiwa katika Qurani.” Kama ilivyo na kiolezo cha Kiajemi, bustani ya kawaida ya Waarabu, tokea zile za Wamoor katika Hispania hadi Kashmir, ziligawanywa katika sehemu nne na vijito vinne vilivyokutana katikati kwenye kidimbwi au kwenye bomba la kububujisha maji, inayokumbusha juu ya mito minne ya Edeni.

Kaskazini mwa India, kando ya Ziwa Dal katika Bonde la Kashmir lililo maridadi, watawala walioitwa Mogul wa karne ya 17 walipanda bustani zaidi ya 700 za kiparadiso. Hizo zilifanyiza rangi nyingi zenye kuvutia sana zenye mamia ya mabomba ya kububujisha maji, ngazi, na maporomoko ya maji. Banda la marumaru nyeusi lililojengwa kwenye ufuko wa Ziwa Dal na Shah Jahan (aliyeijenga Taj Mahal) bado lina mwandiko: “Ikiwa pana paradiso duniani, ipo hapa, ipo hapa, ipo hapa.”

Karne kadhaa mapema, Ulaya ilikuwa imepitia Enzi za Kati na kuingia katika Mvuvumko wa karne ya 14. Desturi ya utunzaji wa bustani ya Roma, iliyokuwa imepuuzwa wakati Enzi za Kati zilipoanza katika karne ya tano W.K., ilianza kusitawi tena—wakati huu chini ya utawala wa kanisa. Jumuiya ya Wakristo iliona bustani kuwa ‘paradiso ya muda.’ Plani ya karne ya tisa ya makao ya watawa yaonyesha bustani mbili zilizoitwa “Paradiso.” Bustani za Jumuiya ya Wakristo upesi zikawa kubwa na zenye fahari zaidi, lakini badala ya kuonyesha mambo ya kiroho, nyingi zikawa ishara za mamlaka na mali.

Charles 8 wa Ufaransa aliposhinda Naples, Italia, katika 1495, aliandika hivi barua ya kwenda nyumbani: “Hamwezi kuamini bustani maridadi ambazo ninazo katika jiji hili . . . Inaonekana ni Adamu na Hawa pekee ndio wanaokosekana ili iwe paradiso ya kidunia.” Lakini kama Charles angaliishi hadi karne ya 17, angaliona katika Ufaransa bustani kubwa sana za Mfalme Louis 14. Kitabu The Garden chasisitiza kwamba bustani zilizo kwenye Makao ya Kifalme ya Versailles “bado zaweza kutajwa kuwa kubwa zaidi na bora zaidi ulimwenguni.”

Hata hivyo, ule Mvuvumko ukawa na ufafanuzi mpya wa paradiso: asili inapaswa kudhibitiwa na mwanadamu aliyeerevuka ambaye atatiisha bustani kwa kuiondolea pori. Miti na maua yote yalipangwa kwa njia fulani hususa. Hivyo, sanaa ya Waroma—ya kuunda miti na vichaka kwa kuvipogoa na kuvikunja—ilivuvumka sana.

Kisha, katika karne za 18 na 19, uvumbuzi na biashara zilizofanywa kwa kuabiri zilitokeza mimea mipya na mawazo mapya ya kutunza bustani katika ulimwengu wa magharibi. Uingereza nayo ikajitosa katika uwanja wa kubuni bustani. “Katika Uingereza ya karne ya 18,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “mwanadamu akafahamu zaidi na zaidi ulimwengu wa asili ambamo alishiriki. Badala ya kulazimisha njia yake ya kuunda ulimwengu wa asili, alianza kufikiria kurekebisha maisha yake ili kupatana na huo.” Wanaume kama William Kent na Lancelot Brown walikuwa stadi sana katika kutengeneza mandhari. Brown alitengeneza mandhari za zaidi ya nyumba mia mbili katika Uingereza. Watu wawili waliokuja kuwa marais wa Marekani, Thomas Jefferson na John Adams, walizuru Uingereza katika 1786 ili kujifunza kutokana na bustani za Uingereza.

Mandhari za Mashariki

Desturi ya China ya kutunza bustani imeathiri sana ustaarabu wa Mashariki kama desturi za kutunza bustani za Misri, Ugiriki, na Roma zilivyoathiri Magharibi. Awali Wachina walikuwa waabudu-maumbile, nao waliona mito, majabali, na milima, vyote kuwa roho zilizotwaa umbo la vitu na hivyo vilipaswa kuheshimiwa. Baadaye, Dini ya Tao, Dini ya Confucius, na Dini ya Buddha zikaenea sana na kutokeza aina zazo za bustani.

Kwenye upande ule mwingine wa Bahari ya Japani, bustani za Wajapani zilisitawisha mtindo wazo zenyewe, ambapo umbo lilikuwa la maana kuliko rangi na kila kitu kilikuwa na mahali pake pa pekee. Katika kujaribu kunasa unamna-namna na utulizo wa asili, mtunza-bustani huweka mawe kwa uangalifu na kupanda na kufanyiza bustani yake kwa uangalifu mkubwa. Jambo hilo huonekana wazi katika bonsai (linalomaanisha “mimea iliyopandwa katika chungu”), sanaa ya kuzoeza mti mdogo au labda miti kadhaa katika umbo fulani na uwiano hususa.

Ingawa mtindo wao waweza kutofautiana na bustani ya Magharibi, bustani ya Mashariki pia huonyesha tamaa ya Paradiso. Kwa kielelezo, katika kipindi cha Heian katika Japani (794-1185), aandika mwanahistoria wa bustani za Japani Wybe Kuitert, watunza-bustani walijaribu kutokeza hisia ya “paradiso duniani.”

Upendo wa Ulimwenguni Pote

Kutia ndani na hata makabila ya kuwinda na kukusanya chakula, walioishi katika bustani za “kiasili”—mwitu, misitu, na nyanda—bustani inapendwa ulimwenguni pote. Kuhusu “Waaztec wa Mexico na Wainka wa Peru,” yasema Britannica, “wale washindi waliripoti kuona bustani zenye madoido sana zenye milima iliyo na ngazi, miti, mabomba ya kububujisha maji, na vidimbwi vyenye mapambo . . . vinavyofanana na bustani katika Magharibi.”

Ndiyo, misitu ya kale yenye kuvuka Naili, mandhari za Mashariki, bustani za kisasa za majiji, na bustani za kibotania—hizo zafunua nini? Tamaa ya mwanadamu ya kutaka Paradiso. Katika kutaja “tamaa ya [kudumu] ya mwanadamu ya kutaka Paradiso,” mwandikaji Terry Comito alisema: “Bustani ni mahali ambapo watu huhisi wamestarehe.” Na ni mtu yupi asiyeweza kufurahia kusema, ‘Makao yangu ni kama Bustani ya Edeni’? Lakini, je, Edeni ya duniani pote—na si tu kwa matajiri pekee—ni ndoto tu? Au ni uhakika wa wakati ujao?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mchoro wa msanii unaoonyesha Bustani za Juu za Babiloni

[Picha katika ukurasa wa 7]

Bustani ya kikale katika Japani

[Picha katika ukurasa wa 7]

Versailles, Ufaransa

Katika historia yote, mwanadamu ametamani Paradiso

[Hisani]

French Government Tourist Office/Rosine Mazin

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki