Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 7/8 kur. 3-4
  • Talaka—Magharibi Yashawishi Mashariki

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Talaka—Magharibi Yashawishi Mashariki
  • Amkeni!—1993
  • Habari Zinazolingana
  • Talaka Huwa na Majeruhi
    Amkeni!—1991
  • Ongezeko Kuu la Talaka
    Amkeni!—1992
  • Ndoa-Sababu Inayofanya Wengi Waivunje
    Amkeni!—1993
  • Talaka Matokeo Yayo Mabaya
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 7/8 kur. 3-4

Talaka—Magharibi Yashawishi Mashariki

Na mleta habari za Amkeni! kat ika Japani

“ACHA mimi pia nistaafu niache kazi yangu.” Maneno hayo yalishangaza meneja mmoja aliyekuwa akistaafu kutoka kampuni moja mashuhuri ya biashara ya Japani. Mke wake alitaka kustaafu aache kuwa mwenzi wake na mke wa nyumbani. Nchi yao inapatwa na ongezeko kubwa la talaka ambayo, kwa kushangaza, inakumba watu wenye umri wa makamo na wenye umri mkubwa zaidi. Miongoni mwa wale ambao wamo katika miaka yao ya 50 na 60, hesabu ya talaka imeongezeka mara tatu katika miaka 20. Kuvunja ndoa kwaonekana kuwa fursa yao ya mwisho ya kutafuta maisha yenye furaha zaidi.

Kwenye upande mwingine wa umri, waume na wake wachanga ambao wamepata kujuana vizuri wakati wa fungate yao huamua kupata Narita rikon (talaka ya Narita). Narita ni kiwanja ndege cha kimataifa cha Tokyo, na maneno hayo yanarejezea waume na wake waliotoka kufanya arusi wanaochana na kuvunja ndoa yao wanaporudi Narita. Kwa kweli, 1 kati ya kila waume na wake 4 au 5 hujaribu kupata talaka katika Japani. Wanaona talaka kuwa mlango wa kupata maisha yenye furaha zaidi.

Hata katika Hong Kong, ambako desturi za Kichina za kale bado zinafuatwa sana, kiwango cha talaka kiliongezeka zaidi ya mara mbili katika miaka sita kati ya 1981 na 1987. Katika Singapore, talaka miongoni mwa Waislamu na wasio Waislamu iliongezeka kwa karibu asilimia 70 katikati ya 1980 na 1988.

Ni kweli kwamba maoni ya wanawake katika Mashariki yamekandamizwa kwa muda mrefu. Kwa mfano, zamani katika Japani, mume angeweza kumtaliki mke wake kwa “mistari mitatu na nusu” tu ya maandishi. Kile alichohitaji tu kufanya ni kuandika taarifa yenye mistari mitatu na nusu inayothibitisha talaka hiyo na kumpatia mke wake kikaratasi hicho. Mke wake kwa upande mwingine hakuwa na njia rahisi ya kupata talaka isipokuwa kwa kukimbilia hekalu linalowapa himaya wanawake wanaotoroka waume zao wanaowatesa. Wakiwa hawana njia ya kujiruzuku, wake wamelazimika kuvumilia ndoa zisizo na upendo na hata waume zao wanaofanya ngono nje ya ndoa.

Leo, waume wengi wanaojiingiza mno katika kazi yao ni kama huacha kabisa familia zao. Hawaoni ubaya wa kuishi kwa ajili ya kampuni yao. Wakiwa na ujitoaji kama huo kwa kazi yao, wanapuuza mahitaji ya wake zao ya kutaka kusikilizwa na kuwaona kama wajakazi wasiolipwa wanaowapikia, kuwafanyia usafi, na kuwafulia nguo zao.

Hata hivyo, ongezeko kubwa la mawazo ya Magharibi linabadili namna wanawake wa Mashariki wanavyoona ndoa na maisha ya ndoa. “Ule ‘uhuru’ wa wanawake,” lasema Asia Magazine, “kwa wazi ni sababu moja kubwa zaidi unaotokeza hali inayoongezeka ya talaka katika Esia.” Anthony Yeo, mkurugenzi wa Kitovu cha Mashauri na Utunzaji cha Singapore, alisema hivi: “Wanawake wametia mkazo zaidi juu ya haki zao na kufikiria zaidi juu ya staha yao. Hawataki tena kuketi kitako na kuvumilia kwa ukimya. Wanawake wa leo wana mambo mengi ya kuchagua na hawavumilii kupuuzwa wala kutendwa vibaya. Na talaka ndiyo chaguo halisi la wale ambao hawawezi kupata furaha katika ndoa, hasa wakati ambapo ile aibu inayoshikanishwa nayo imeondolewa kwa kadiri kubwa na aibu hiyo si ile iliyokuwa miaka 25 iliyopita.”

Nchi za magharibi pia zimepatwa na mabadiliko makubwa wakati wa robo karne ambayo imepita. Samuel H. Preston aliyaita mabadiliko hayo “tetemeko kubwa lililoharibu sana familia ya Amerika kwa miaka 20 ambayo imepita.” Katika 1985, karibu robo ya makao yote yenye watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 yalikuwa ya familia zenye mzazi mmoja, hasa kwa sababu ya talaka. Inatabiriwa kwamba asilimia 60 ya watoto waliozaliwa 1984 huenda watakuwa wakiishi katika familia zenye mzazi mmoja kabla wafikie umri wa miaka 18.

Hali ya ndoa ikiwa inadhoofika, je, kweli talaka ndiyo mlango wa kupata maisha yenye furaha zaidi? Ili kujibu, ebu kwanza tutazame kile kilichowafanya watu waone talaka kuwa dawa ya kuponya matatizo yao ya familia.

[Sanduku katika ukurasa wa 4]

Tokeo la “Talaka ya Kuishi Pamoja”

CHINI ya hesabu ya talaka halisi kuna talaka “zisizotumika” zilizofichika. Katika Japani, ambako wanawake wengi bado wanategemea waume zao kiuchumi na kupatwa na ile desturi inayoendelea kudumu ya kutawalwa na mume, mume na mke wanaweza kuishi katika nyumba moja bila kutaka katika hali inayoitwa “talaka ya kuishi pamoja.” Katika hali kama hiyo, wanawake huelekea kutumia nguvu zao zote katika kulea watoto. Akina mama kama hao mara nyingi huwalinda watoto kupita kiasi, likifanya iwe vigumu kwa watoto kujitegemea baadaye.

Kama tokeo, wana wa mama kama hao wanapokua na kuoa, wengi wao hupatwa na “mwelekeo wa usiniguse” (kutotaka kuguswa kwa shauku). Watu hao hawagusi kamwe wake zao kwa upendo, hata baada ya miaka kadhaa ya maisha ya ndoa. Wanaugua kile ambacho kimekuja kuitwa tatizo la “Nampenda Mama” na mara nyingi walioa kwa sababu mama yao aliwaambia wafanye hivyo. Kulingana na Asahi Evening News, Dakt. Yasushi Narabayashi, ambaye ni mtaalamu wa mashauri ya ndoa, anasema kwamba tatizo hilo limekuwa likikua kwa mwongo wa miaka na kwamba kuna makumi ya maelfu ya watu wanaoogopa kutafuta shauri kwa sababu ya kuona aibu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki