Mashindano ya Mbio ya Baiskeli—Mazuri na Mabaya Yayo
NIKIJITAHIDI, nikipumua kwa nguvu, na kuendesha baiskeli, bila hata kuhisi uchovu, nilikuwa na hakika kwamba ningepata faida. Baada ya kupanda mlima kwa kilometa 25, kwenye kilele cha Mpitio wa Mlima wa Great Saint Bernard Pass, katikati ya Uswisi na Italia, nilikuwa nikiongoza. Kocha wangu aliniashiria kutoka kwenye gari lake kwamba nilikuwa na uongozi wa dakika chache mbele ya wengine. Tayari nilikuwa nikiwazia kushinda mkondo huo wa mbio na kuvaa fulana ya manjano inayovaliwa na yule anayeongoza.
Nikiwa mbele ya pikipiki na magari, niliteremka mbio kwa mwendo wa kasi katika upande ule mwingine. Nikiwa katikati kuelekea chini, nilipiga kona moja haraka sana. Gurudumu la nyuma likateleza chini yangu, na nikarushwa nje ya barabara. Nilimaliza mkondo huo kwa maumivu makali, na sikupata fulana ya manjano na utukufu. Sikushinda mashindano hayo ya baiskeli ya 1966 Tour de l’Avenir.
Jinsi Tamaa Yangu Ilivyokua
Nilizaliwa katika Brittany mwishoni mwa vita ya ulimwengu ya pili. Katika magharibi mwa Ufaransa, kuendesha baiskeli kunapendwa sana, na eneo hilo limetokeza mabingwa wengi wa ulimwengu. Nikiwa mvulana nilikuwa nikitazama mashindano ya mbio ya mahali petu na sikukosa kutazama yale mashindano ya Tour de France katika televisheni. Nikiona waendesha baiskeli wakijitahidi kupitia mipitio ya milimani ya kustaajabisha na kisha kuteremka kwa kasi kwenye miteremko mikubwa zaidi, nilifikiria walikuwa kama miungu.
Nikiwa na umri wa miaka 17, niliamua nijaribu. Kwa msaada wa mwuza-baiskeli nilinunua baiskeli yangu ya kwanza ya mashindano ambayo ilikuwa imetumiwa. Nilikuwa na programu kamili: nikifanya mazoezi kila Jumapili asubuhi na kabla na baada ya kazi katikati ya juma. Miezi miwili tu baadaye, moyo wangu ukipiga-piga, nilikuwa kwenye mstari wa kuanza mashindano yangu ya kwanza ya baiskeli. Ningeshinda kama kikundi cha waendesha baiskeli hakingenifikia meta 10 kufikia mstari wa kumalizia! Kwa muda wote wa mwaka huo, nilikuwa nikimaliza miongoni mwa wale 15 wa kwanza katika mashindano yangu yote.
Msimu wangu wa 1962 haukuendelea sana. Baada ya miezi mitatu ya mashindano na ushindi kadhaa, niliitwa kwenye utumishi wa kijeshi kwa miezi 18 katika Algeria. Baada ya kurudi Ufaransa, nilitumia 1965 katika kuzoea tena kuendesha baiskeli. Lakini msimu uliofuata wa mashindano, nilikuwa nimeazimia kabisa kupata ile shangwe ya kupata shada la maua la mshindi.
Kutoka Machi 1966 na kuendelea, nilishinda shindano moja baada ya jingine. Kila wakati niliposhinda au kuwa wa pili katika mashindano, nilipata pointi ambazo hatimaye zingeniingiza kwenye mashindano ya tabaka ya juu, ambapo mashindano yangekuwa makali zaidi. Hata hivyo, wakati huo, nilikuwa nikifanya kazi ya kimwili ya kulainisha na kupaka rangi sakafu za mbao. Kazi hiyo ilikuwa yenye kuchosha na ilinizuia kutumia wakati mwingi kwa kuendesha baiskeli jinsi ambavyo ningependelea. Kwa hiyo nilipopata pointi zenye kuniwezesha kubaki katika tabaka langu la mashindano, nilijiridhisha na pesa za ziada nilizopata katika mashindano yaliyobaki, lakini ningeacha wengine wanishinde ili nisiende kwenye tabaka la juu la mashindano.
Maendeleo ya Haraka
Kwa sababu ya matokeo yangu ya mashindano, timu tatu zilitaka kufa-nya nami mkataba wa mashindano. Nilikataa ili nisimwache baba yangu. Hata hivyo, kocha mwenye kusisitiza zaidi alimbembeleza baba yangu anipe likizo la juma moja ili nishiriki katika shindano gumu sana katika milima ya Pyrenees kwenye mpaka wa Ufaransa na Uhispania. Nilifanya vizuri, hivyo tukaenda Uhispania, nilikoshinda shindano la waendeshaji wasiolipwa la Tour of Catalonia. Siku chache baadaye nilishiriki katika shindano la Tour of Balearic Islands, nikashinda mkondo wa kwanza, na kuvaa fulana ya kiongozi, na kuipoteza tu baadaye katika siku ya mwisho ya jaribu la muda wa mwendo kwa sababu timu yetu ilijiondoa.
Kisha likaja shindano la Route de France katika eneo la Nice. Nilifanya vizuri sana katika mikondo mingi na kushinda zawadi ya kuwa mwendeshaji bora zaidi katika milima. Kwa sababu ya matokeo mazuri kama hayo, nilichaguliwa kuwa mmoja wa wale waendesha baiskeli kumi waliokuwa bora na kualikwa kuwakilisha Ufaransa katika shindano la Tour de l’Avenir, aina ya shindano la Tour de France la waendeshaji wasiolipwa.
Kwa muda wa miezi hiyo miwili, habari pekee ambazo familia yetu ilipokea ilikuwa kupitia magazeti kwenye kurasa za michezo. Nikifikiria baba yangu na lile jambo la kwamba alikuwa amenipa likizo ya juma moja pekee, nilikataa toleo hilo na kurudi nyumbani. Lakini kocha wangu na mwandishi mmoja wa habari za michezo alimsadikisha baba yangu kwamba nilikuwa mmoja wa wale ambao walikuwa tumaini la Ufaransa katika mashindano ya baiskeli, kwa hiyo akaniachilia niende. Nilifikiri ninaota! Miezi michache tu iliyopita, nilikuwa mwendesha baiskeli asiyelipwa wa tabaka la tatu au nne, na sasa nilikuwa nimechaguliwa kwa shindano kubwa zaidi ulimwenguni la wasiolipwa! Na kama nilivyotaja mwanzoni, kuanguka kwangu kuliharibu nafasi yangu ya kushinda katika shindano hilo la 1966 Tour.
Katika 1967, nilishinda mashindano ya baiskeli karibu kumi, nikashiriki katika shindano la Paris-Nice, na nikawa wa nne katika shindano la Tour du Morbihan, katika Brittany. Katika 1968, nikiwa na umri wa miaka 24, nilitia sahihi mkataba wangu wa kwanza wa mashindano ya kulipwa, nikijiunga na timu ya mwendeshaji Mholanzi Jan Janssen. Tulishiriki katika shindano la Tour de France, na Jan akalishinda mwaka huo. Kwa muda huo, baada ya jaribu la wakati katika Rennes, Brittany, nilikutana na Danielle, aliyekuwa amekuja kuona shindano la baiskeli kwa mara ya kwanza. Na halikuwa lake la mwisho, kwa sababu tulioana mwaka uliofuata.
Jinsi nilivyopenda siku hizo—kule kuendesha pamoja tukiwa timu, maisha ya kuhama-hama, kuona miji mipya na mandhari kila siku! Sikuwa nikichuma pesa nyingi, lakini sikujali kwa sababu furaha ya mashindano iliniridhisha sana. Nilifanya vizuri katika mashindano mbalimbali na nikawa na tumaini la kushinda moja ya mashindano makubwa. Hata hivyo, nilianza kung’amua kwamba ufa mkubwa ulikuwa ukiwatenganisha waendesha baiskeli wasiolipwa na wale wa kulipwa.
Wale Mabingwa Wakuu . . . na Wengine
Wakati wa msimu wa mashindano wa 1969, nilijiunga na mwendesha baiskeli maarufu wa Ufaransa Raymond Poulidor. Nilishiriki katika yale mashindano ya siku moja—Paris-Roubaix na Flèche Wallonne, katika Ubelgiji. Nilishikamana na waendesha baiskeli bora zaidi katika mipitio ya milima, nikimaliza vizuri katika mikondo kadhaa. Lakini, nilifurahia kushinda mashindano ya kwetu mbele ya umati wa watazamaji katika Brittany kuliko kitu chochote.
Lakini tofauti na matumaini yangu, kama ilivyokuwa na wengine, sikubarikiwa kuwa na uwezo mwingi wa kimwili wa kuwa bingwa mkuu. Katika mkondo mmoja mgumu wa shindano la Tour of Spain, ilinibidi niachie katikati kwa sababu ya theluji na mvua. Huko nilitambua kwamba mabingwa wakuu wana kitu kingine zaidi, kitu cha pekee kinachowawezesha kuvumilia joto kali na baridi kali. Kwa mfano, sikuwa katika tabaka moja ya mashindano na Eddy Merckx, yule bingwa wa Ubelgiji aliyetawala mashindano ya baiskeli wakati huo. Alitushinda sisi sote kwa mbali sana. Kwa kweli nilikuwa nikiona tu mgongo wake wakati wa mashindano aliyoshiriki.
Umoja Miongoni mwa Washindani
Umoja ulikuwako hata miongoni mwa timu zenye kushindana. Mimi mwenyewe nilipata ono hilo wakati wa mojapo mikondo migumu ya shindano la 1969 Tour de France. Usiku uliopita, tulikuwa tumefika kwenye hoteli tukiwa tumechoka baada ya mfululizo wa mipitio migumu ya milima. Saa ya kengele ililia saa moja asubuhi iliyofuata. Kama kawaida kiamsha-kinywa kingi kingetungojea muda wa saa tatu kabla ya mashindano.
Tulikuwa 150 wakati wa kuanza, kila mmoja akisimulia mazuri na mabaya ya siku chache zilizopita, ijapokuwa wanajihadhari wasifunue siri ya mpango wa timu kwa shindano linalokuja. Ingekuwa ni siku ngumu. Mkondo huo ulitoka Chamonix, kwenye mtelemko wa mlima Mont Blanc, kuelekea Briançon, umbali wa kilometa 220 za barabara za milima na mipitio mikubwa mitatu ya milima ya kuvuka.
Tokea mwanzo kabisa, mwendo ulikuwa wa kasi sana. Nilipokuwa nikielekea Mpitio wa Mlima wa Madeleine wenye urefu wa meta 1,984, nilijua kwamba haingekuwa siku njema kwangu. Mvua ilikuwa ikinyesha na tulipoendelea kupanda zaidi, mvua iligeuka kuwa theluji. Kufikia kilele cha mpitio huo, tayari sisi watu sita kutoka kwenye timu tofauti-tofauti tulikuwa nyuma ya wale wanaoongoza kwa dakika kadhaa. Tukiwa tumeganda, tulianza kuteremka, vidole vikiwa vimekufa ganzi sana hivi kwamba hatungeweza kushika breki ila kwa kuweka miguu yetu chini. Kule chini, ofisa mmoja alituashiria kutoka kwenye gari kwamba bila shaka tungeondolewa kwenye mashindano kwa sababu ya kufika tukiwa tumechelewa. Nilishuka moyo sana kwa wazo la kuona shindano langu la Tour de France likiishia sehemu niliyopenda zaidi, milimani.
Ijapokuwa jitihada zetu zilionekana kuwa hazitafua dafu, mwendeshaji mmoja mwenye ujuzi miongoni mwetu alitutia moyo tusiache. Alitupa nguvu zaidi, akafanya kikundi hicho kiende kwa kufuata utaratibu fulani, na kudokeza kwamba tuchukue zamu katika kuongoza. Tulivumilia. Tulipofika kwenye kituo cha ugavi wa chakula, kilikuwa kimefungwa, lakini hatukujali kushiriki kile chakula kidogo tulichokuwa tumebakisha.
Tulipofika tena kwenye bonde, hali ya anga yenye joto ilitupatia nguvu tena. Muda ulikuwa ukipita, na mbele yetu kulikuwa na vizuizi viwili vi-kubwa zaidi kwa siku hiyo—ile mipitio ya milima ya Telegraph na Galibier, Telegraph ukifikia urefu wa meta 1,670 na Galibier ukifikia urefu wa meta 2,645. Wakati wa kupanda, mshangao mkubwa sana ulitungojea. Kwenye kona ya barabara, kupita watazamaji, tungeweza kuona watu wengi wenye mavazi yenye rangi tofauti-tofauti. Naam, tulikuwa tumefikia wengine. Tulipita wengine waliokuwa wamejiuzulu na wengine walioonekana kama hawawezi kusonga. Niliona mmoja aliyekuwa mchanga ambaye alikuwa mmoja wa matumaini makubwa ya Ubelgiji akitembea, huku akisukuma baiskeli yake kwa uchovu. Nilimfikia yule aliyekuwa akiongoza kwenye timu yetu na kumaliza mkondo huo kwa nafasi nzuri.
Mambo hayo yote yalinifunza somo muhimu ambalo sijapata kusahau: Mradi mstari wa mwisho haujavukwa, shindano halina mshindwa wala mshindi. Na zaidi, siwezi kusahau ile roho ya utegemeano iliyokuwako, hata miongoni mwa timu zenye kushindana.
Kusikia Ujumbe wa Biblia kwa Mara ya Kwanza
Katika 1972, nilisikia ujumbe wa Biblia kwa mara kwanza. Mwendesha baiskeli aliyeitwa Guy, aliyekuwa ameacha mashindano ya kulipwa karibuni, alitutembelea na kuongea juu ya imani yake mpya. Nilimwambia kwamba sikupendezwa na kwamba kila mtu anaamini kwamba dini yake ndiyo bora zaidi. Guy alinionyesha mistari michache kutoka kwa Biblia na kujibu upinzani wangu kwa kusema kwamba kwa sababu dini nyingi husema kwamba itikadi zao zatoka kwenye Biblia, basi ni rahisi kujaribu itikadi zao dhidi ya kweli ya Neno la Mungu.
Nilikuwa nimesikia juu ya Biblia, lakini nikiwa Mkatoliki asiyetenda, sikufikiri kama Biblia lilihusika na dini yangu. Lakini, bado nilihisi mazungumzo yetu yalikuja kwa wakati unaofaa kwa sababu mmoja wa watu wa ukoo wa mke wangu, mishonari wa Katoliki, alikuwa anakuja kuzuru, na tungezungumza naye mambo hayo yote.
Mtu huyo wa ukoo wa mke wangu alihakikisha kwamba kwa kweli Biblia ilikuwa Neno la Mungu. Lakini, alituambia tutahadhari kwa sababu, kulingana na yeye, Mashahidi wa Yehova walikuwa watu wazuri, lakini walikuwa wakipotosha wengine. Nilipokutana na Guy tena, nilimwuliza juu ya jambo hilo. Alieleza kwamba tofauti na mambo yale niliyokuwa nimefundishwa kanisani, fundisho la kutokufa kwa nafsi ya kibinadamu halimo katika Biblia. (Ezekieli 18:4) Pia aliuliza ni kwa nini mtu huyo wa ukoo wa mke wangu hakutumia jina la Mungu, Yehova.—Zaburi 83:18.
Nilishtuka kujua kwamba Mungu ana jina. Tulipoonyesha mtu huyo wa ukoo wa mke wangu maandiko hayo, alisema kwamba Biblia haipasi kueleweka kihalisi. Mazungumzo yetu na Guy hayakuendelea zaidi, na Guy akarudi Paris, alikokuwa akifanya kazi.
Guy alirudi Brittany mwaka mmoja baadaye na kututembelea. Alianzisha tena mazungumzo yetu kwa kutuonyesha kwamba Biblia pia ilikuwa kitabu cha kiunabii. Jambo hilo lilitutia moyo tuichunguze kwa makini zaidi. Mazungumzo yetu yakaanza kuwa yenye ukawaida zaidi. Lakini, Guy alihitaji kuwa mwenye saburi sana nami, kwa sababu maisha yangu bado yalikuwa kwenye mashindano ya baiskeli na mambo yaliyohusika nayo—marafiki, mashabiki, na kadhalika. Pia, kwa kuwa mimi ni mwenyeji wa Brittany, eneo lenye kufuatia desturi za kidini sana, familia zetu zilipinga kupendezwa kupya kwetu na Biblia.
Katika 1974, kazi yangu ya mashindano ya baiskeli ilikomeshwa kwa ghafula kwa aksidenti ya barabarani. Aksidenti hiyo ilitufanya tufikiri juu ya nini kilichokuwa cha maana zaidi maishani mwetu. Mke wangu nami tukaamua kuhama kutoka mji wa nyumbani na kutoka kwa uvutano wa familia zetu. Kufikia wakati huo tulianza kuhudhuria mikutano kwa ukawaida kwenye Jumba la Ufalme la Kutaniko la Dinan. Sote wawili tulifanya maendeleo katika kweli, na tulibatizwa katika 1976.
Tangu wakati huo nimekuwa na fursa ya kuzungumza juu ya Biblia na waendesha baiskeli wa wakati wangu. Pia, ninapoenda nyumba kwa nyumba, watu wengi wananitambua na kufurahia kuongea juu ya kazi yangu ya mashindano ya mbio. Hata hivyo, wengine hawana shauku ninapoongea juu ya ujumbe wa Ufalme.
Leo, ninapohisi kuwa na mazoezi mazuri, mimi huendesha baiskeli pamoja na familia yangu. Katika pindi hizo, mimi huthamini ukweli wa maneno ya Paulo aliposema hivi: “Kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.”—1 Timotheo 4:8.—Kama ilivyosimuliwa na Jean Vidament.
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
Shindano la Tour de France
Shindano la baiskeli mashuhuri zaidi ulimwenguni, Tour de France lilianza katika 1903. Lina umbali wa kilometa 4,000 hadi 4,800 na huchukua karibu majuma matatu, sasa likimaliza Paris. Washindani wa kulipwa karibu 200 hushiriki katika shindano hilo, linalopitia eneo la mashambani la Ufaransa na kuingia kidogo-kidogo ndani ya nchi jirani. Umati mkubwa wa watazamaji njiani hushangilia washindani hao.
Kila siku mwendeshaji mwenye kutumia muda mfupi zaidi huvaa fulana ya manjano. Yule anayeongoza katika siku ya mwisho ndiye mshindi.
Baadhi ya mikondo mifupi zaidi ni ya kujaribu wakati wa mwendo ambapo watu mmoja mmoja au timu huenda kwa kasi kujaribu kumaliza shindano kwa wakati mfupi zaidi. Katika sehemu ya kujaribu wakati wa mwendo wa timu, idadi fulani ya waendeshaji wa timu ileile ni lazima wamalize mkondo huo wakiwa pamoja, wote kwa wakati mmoja.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Mike Lichter/International Stock
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Katika 1968, akiwa na umri wa miaka 24, Jean Vidament alishiriki katika shindano la Tour de France
ROUBAIX (start)
PARIS
Tour de France bicycle race
France