Kuitazama Miwani
Na mleta habari za Amkeni! katika Uingereza
JE! UNASOMA makala hii kwa kutumia miwani? Naam, si wewe peke yako. Kwa mfano asilimia yapata 60 ya idadi ya Waingereza, sasa huvaa miwani.
Kwa hiyo, kuvaa miwani kumeenea sana hivi kwamba marafiki zako wakitaja neno lolote juu yayo, labda ni kwa sababu umebadili mtindo wa fremu zako au umeamua kutoivaa tena. Wengi wetu tumezoea miwani hivi kwamba tunaivaa na kuivua bila hata kufikiri—ila tu wakati inapoteremka kwenye pua zetu au inapopatwa na ukungu.
Lakini wengi wanaovaa miwani hupendelea miwani ya kuona aina ya 20/20 badala ya fremu zenye mtindo. Miwani yaweza kusumbua. Hata hivyo, watu wasioona vizuri wanasaidiwa sana nayo.
Visaidizi vya Mapema vya Kuona
Inasemekana kwamba ili maliki Mroma Nero aone vizuri michezo ya kuuana, alikuwa na lenzi (kioo cha miwani) iliyotengenezwa kwa emeraldi—njia ghali sana na isiyofaa ya kufanya macho yanayodhoofika kuona vizuri. Katika nyakati za kale lenzi zilitengenezwa pia kutokana na kioo chenye kupenyezwa na nuru, quartz, amethisti, berili, na yakuti ya rangi ya manjano. Hata hivyo, kufikia karibu mwaka wa 1268, mtawa Mwingereza Roger Bacon alieleza jinsi kisehemu cha kioo duara kinavyoweza kutumiwa kusaidia kusoma. Karibu na wakati uo huo, miwani ya kwanza—fremu zenye lenzi zisizotengenezwa vizuri—ilianza kuonekana.
Ni nani aliyeivumbua kwa mara ya kwanza—Waitalia au Wachina? Hilo ni jambo la kubishaniwa, kwa sababu chombo hicho kilianza kuonekana karibu wakati uleule katika nchi hizo mbili. Kwa upande mwingine, kaburi moja katika Florence, Italia, lina maneno haya: “Hapa yupo Salvino ďArmato [wa familia ya Armati] wa Florence. Mvumbuzi wa miwani. Mungu amsamehe dhambi zake.” Hakuna mtu ambaye ana uhakika alikufa lini—1285, 1317, au 1340. Kwa upande mwingine, yule mvumbuzi mkuu wa nchi kutoka Italia Marco Polo alikumbuka kuona watu wengi katika Uchina wakivaa miwani alipofika huko kwa mara ya kwanza katika mwisho-mwisho wa karne ya 13. Kwa kweli, hekaya zinasema kwamba miwani ilikuwa ikivaliwa katika Uchina mapema kama 500 W.K.
Angalau kufikia karne ya 16, biashara ya miwani ilikuwa inaendelea vizuri katika Venice, na vilevile Nuremberg na vitovu vingine vya Ulaya. Miwani imekuwa vipambo vya kutafutwa sana, ikiuzwa katika miji mingi na wachuuzi wa barabarani. Lakini ole, wachuuzi hawakujaribu miwani yao. Kwa hiyo huenda sura ya mnunuzi ingeonekana vizuri lakini si lazima kwamba macho yake yangeona vizuri!
Miwani Leo
Polepole, miwani ikawa bora. Ilishikanishwa masikioni na utepe kwenye pua kwa kutumia kibano cha spring’i. Kufikia mapema karne ya 18, mtu mmoja alitokeza wazo la kushikanisha miwani kwa vitu vya masikio vyenye kukazwa. Njia hiyo ndiyo bado inapendwa zaidi.
Maendeleo makubwa yalifanywa pia katika utengenezaji wa lenzi. Kioo cha macho chenye hali ya juu hatimaye kilianza kutumiwa badala ya vitu vyenye kupenyezwa na nuru na vyangavu. Majaribio ya Bwana Isaac Newton ya karne ya 17 kwa prizimu (kipande cha kioo chenye pande tatu) yalitokeza uelewevu mpya wa kupinda kwa nuru. Kwa hiyo, lenzi nzuri zingeweza kufanywa kwa usahihi wa kisayansi.
Katika 1784, mkuu wa serikali wa Amerika Benjamin Franklin alivumbua suluhisho lenye werevu kwa tatizo alilokuwa nalo na miwani yake. Miwani yake ya kusoma iliharibu uwezo wake wa kuona mbali, na ile aliyokuwa nayo ya kuona mbali haikumfaa katika kusoma. Kwa hiyo badala ya kubadili kila wakati jozi mbili za miwani, aliwazia, mbona nisiweke lenzi za aina mbili pamoja katika jozi moja ya miwani? Hivyo, miwani yenye lenzi mbili ikavumbuliwa. Hata hivyo, ilichukua muda wa miaka mia moja mingine kabla ya njia bora ya kuitengeneza kusitawishwa.
Vioo vya macho vya aina tofauti pia vinapatikana kwa ajili ya mahitaji ya pekee. Lenzi zenye kuongezewa tabaka au kuimarishwa zinaweza kuwekwa kwenye miwani ya kinga ili macho ya wafanyakazi yalindwe kutokana na vitu vinavyoruka. Lenzi nyinginezo hubadilika kwa sababu ya athari ya nuru: Zinapowekwa kwenye jua, zinakuwa nyeusi, na zinapokuwa kwenye kivuli au ndani ya nyumba, zinakuwa nyangavu tena. Na bado lenzi nyinginezo ni plastiki, zinapunguza sana uzito wa miwani na kuwezesha watu wenye lenzi nzito waivae miwani kwa ustarehe.
‘Mimi? Nivae Miwani?’
Ingawa hivyo, labda wewe ni mmoja wa wale wanaoona vizuri sana. Labda si kwa muda mrefu.
‘Wasema kwamba huenda nitalazimika kuvaa miwani siku moja?’ wauliza. Ndiyo, uwezekano ni kwamba labda utavaa, hata ikiwa unaona vizuri sasa. Kwa nini? Sababu moja ni kwamba, utakapofika umri wa miaka 45—au zaidi—labda utaona matokeo ya ugonjwa wa presbyopia. Sasa, usiogopeshwe na neno hilo. Linamaanisha tu kwamba lenzi za ndani ya macho yako hazitabadilika haraka kuona vitu vya mbali baada ya kuona vitu vya karibu kwa mafanikio jinsi zilivyokuwa zikifanya wakati wa ujana wako. Miwani ni mojapo tu bei za kulipwa kwa ajili ya uzee.
Je! wazazi wako huvaa miwani? Wengi huhisi kwamba matatizo ya macho ni ya urithi. Kama ni hivyo, kuvaa kwako miwani siku moja tayari kumethibitishwa na urithi.
Hata hivyo, baada ya muda, umri, chembe za urithi, na tabia zaweza kuanza kukudhuru na kusababisha magonjwa ya macho ya kawaida, kama vile kutoweza kuona vizuri vitu vya karibu (hyperopia), kutoweza kuona vizuri vitu vya mbali (myopia), upindo kwenye ngozi ya jicho, na kengeza. Kama una moja ya magonjwa hayo yanayotajwa hapo juu, ni vizuri kumwona daktari wa macho (kama vile optometristi). Kisha unachagua tu jozi la fremu linalokupendeza zaidi.—Ona sanduku.
Kuitunza Miwani Yako
Miwani inaweza kuwa yenye bei ghali, na huenda unaitegemea kwa kuendeleza shughuli zako za kila siku. Kwa hiyo, uitunze vizuri. Unapoivua, usiiweke kwenye lenzi. Pia hakikisha kwamba huiweki mahali inapoweza kukaliwa au kukanyagwa. Miwani huchafuka haraka, kwa hiyo lenzi huhitaji kupanguswa kila siku kwa kitambaa chororo na ambacho kimekauka, na fremu kuoshwa kwa maji yasiyo moto sana mara kwa mara. Kama una watoto wadogo wanaovaa miwani, utapata kwamba miwani yao itahitaji kupanguswa mara nyingi zaidi.
Lakini namna gani kama miwani yako inapanuka na hivyo isikutoshe vizuri? Uipeleke kwa mfanyi miwani airekebishe badala ya kuifanya kazi hiyo mwenyewe.
Kwa utunzi mzuri, utapata utumishi mzuri wa miwani yako. Ah, huenda ikasumbua kidogo mara kwa mara, lakini inakusaidia uone vizuri—na labda hata kufanya sura yako ionekane vizuri. Kwa sababu hiyo, kwa wazi haijalishi kama inasumbua kidogo, ama sivyo?
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Miwani na Mitindo
‘Miwani itaharibu sura yangu!’ wengi husema wanapoambiwa kwamba watalazimika kuvaa miwani. Hata hivyo, wabuni wa mitindo wametumia ustadi wao sana kwenye mitindo ya miwani hivi kwamba jozi ya miwani inaweza kuwa kama kitu tu cha kurembesha.
Sababu moja ni kwamba watengeneza fremu wanafaidika na plastiki nyepesi, na zenye kudumu, wakifanya kuwa na machaguo mengi sana ya rangi na ukubwa. Pia kwa kutumia lenzi nyepesi zaidi, inawezekana kufanyiza lenzi nzito kuwa nyepesi zaidi. Na zinapopakwa tabaka dogo la rangi ya kuzuia kurudishwa kwa nuru, basi zinakuwa hata vigumu kuonekana.
Ikiwa wewe hufuatia mitindo, unaweza kuchagua fremu za miwani kama vile unavyochagua mavazi. Broshua moja iliyotokezwa na Shirika la Habari ya Macho (Uingereza) inapendekeza kwamba uchague fremu zitakazofaana na umbo la uso wako, zinazokazia sehemu nzuri ya uso wako na kupunguza zile zisizo nzuri sana. Kwa mfano, je, ungependa kufanya uso wako uonekane mwembamba? Basi, broshua hiyo inasema, chagua fremu zenye rangi kwenye sehemu inayolalia pua, na kuendelea kuwa nyangavu kuelekea upande. Je! wewe una macho ambayo ni karibu-karibu? Basi chagua fremu zisizo na rangi nyingi mahali zinapolalia pua na zenye rangi zaidi kuelekea sehemu za nje. Jaribu mitindo aina tofauti, na uchunguze matokeo tofauti-tofauti. Unaweza kupata kwamba inasaidia kuandamana na rafiki mzuri anayeweza kutegemeka katika kutoa maoni ya unyoofu.
Ukipata kwamba miwani inasumbua sana, basi fikiria lenzi za kuwekwa machoni. Zinaweza kuvaliwa na watu wengi kwa starehe siku nzima.