Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Je! Ni Waume Wenye Kupigwa? Mimi nahangaishwa na jambo la kwamba mliandika habari “Waume Wenye Kupigwa” katika “Kuutazama Ulimwengu.” (Julai 22, 1993) “Kutendwa vibaya” si sawa na “kupigwa,” jambo ambalo ni jeuri ya uhalifu. Kwa habari ya kwamba wanawake hukiri kutendwa vibaya kwa asilimia kubwa kuliko vile wanaume wakirivyo, uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba wanawake ni wasema-kweli zaidi juu ya kukiri mambo ya jinsi hiyo kuliko watenda-vibaya wa kiume, ambao huelekea kukana vitendo vyao.
K. K., United States
Twathamini maoni hayo. Habari hiyo iliripoti uchunguzi mmoja unaodai kwamba asilimia 40 ya wanawake walikiri kuwatenda vibaya waume zao, kwa kulinganishwa na asilimia 26 ya wanaume waliokiri kuwatenda vibaya wake zao. Hata hivyo, kama vile habari yetu ilivyokubali wazi, huo uchunguzi ulitumia fasili pana ya “kutendwa vibaya” wala haikutumia neno hilo kuhusiana na kupigwa kimwili tu. Hivyo basi kichwa cha habari yetu kilikosa shabaha kidogo. Kwa habari ya ni namna ipi ya kupiga iliyoenea zaidi, toleo letu la Februari 8, 1993 liliripoti hivi kutokana na gazeti “Parents”: “Zaidi ya asilimia 95 ya visa vilivyoripotiwa vya kuwatenda vibaya wenzi wa ndoa [kwa ukali] vyahusisha mwanamume kupiga mwanamke.”—Mhariri.[1]
Kunusa Sikuzote mimi nimefikiri kwamba kama ningelazimika kupoteza moja ya hisia zangu, ningechagua hisia yangu ya kunusa ndiyo iondoke. Lakini baada ya kusoma makala yenu “Hisi Yetu ya Kunusa Inayobadilika-Badilika” (Julai 22, 1993), nilibadili maoni. Makala zenu juu ya mwili wetu wa kibinadamu ulio mzuri ajabu hunisaidia sikuzote kuongeza kina cha upendo wangu kwa Yehova.
D. H., Trinidad
Miwani Asanteni kwa kuchapisha ile makala “Kuitazama Miwani.” (Julai 8, 1993) Ilikuwa na ushauri mwema. Kabla ya kuisoma makala, nilikuwa na zoea la kuweka miwani yangu huku vioo vikiwa vimelalia chini. Ilikuwa ikijawa na mikwaruzo. Nilijaribu vioo vya mgusano-na-jicho, lakini vikanitia kizunguzungu. Kwa hiyo kwa sababu sina namna ila kuvaa miwani, nitatumia ushauri wenu!
T. C., Italia
Vijiwe vya Figo Ninawaandikia kuwashukuru kwa makala yenu ya wakati ufaao “Vijiwe vya Figo—Kutibu Maradhi ya Kale.” (Agosti 22, 1993) Muda mfupi baada ya kupokea nakala yangu posta, nilipatikana nikiwa na vijiwe vya figo. Kwa sababu ya makala yenu, niliweza kuyaelewa vizuri zaidi maradhi yangu na kujitayarisha kwa ajili ya upasuaji.
V. T., United States
Ubaguzi wa Rangi Hii ni barua fupi ya kuwashukuru tu kwa ajili ya mfululizo huo mzuri ajabu wa makala “Je! Jamii Zote Zitapata Kuungana Wakati Wowote?” (Agosti 22, 1993) Nafikiri mliishughulikia kwa njia bora kabisa habari hiyo yenye kuamsha hisia kwa wepesi. Iliunganishwa kwa busara, na bado hamkumpa mtu yeyote, mtu yeyote kabisa, udhuru wa kujihusisha kwa ubinafsi katika ule ugonjwa wa kuudhi sana wa ubaguzi wa rangi.
D. G., United States
Aliyekuwa Padri Asanteni kwa kuchapa ono la Alinio de Santa Rita Lobo, “Sababu Iliyonifanya Niache Ukasisi Kwa Ajili ya Huduma Bora Zaidi.” (Septemba 8, 1993) Hiyo hadithi ilikuwa ya kuvinjari yasiyokuwa yamejulikana—na tena mwenye kuvinjari alikuwa mtu mwenye kisomo. Katika huduma yetu tukiwa Mashahidi wa Yehova, mara nyingi sisi hujenga uelewevu wa ile kweli, kipande kwa kipande. Lakini katika kisa hicho mtu fulani alifanya kinyume cha hilo—kutenga na kutengua mafundisho ya uwongo, kipande kwa kipande, akitenganisha kweli kutoka kwenye mapokeo yenye msingi wa kanisa. Ilitia imani nguvu sana.
B. C., United States
Kuhama Nchi Nyingine Asante sana kwa ile makala “Vijana Huuliza . . . Je! Nihamie Nchi Yenye Utajiri Zaidi?” (Aprili 22, 1993) Sikuzote nilikuwa nimefikiri kwamba ili kufanya maendeleo, ilikuwa lazima nihame. Sasa nimejifunza kwamba huo ni uamuzi mzito sana na kwamba mambo mengi yapasa kufikiriwa. Makala hiyo ilinifundisha pia kujua mahitaji yangu ya kweli na kwamba mambo tuhitajiyo kwelikweli ili tuwe wenye furaha yaweza kupatikana katika nchi yoyote.
M. R., Jamhuri ya Dominika