“Ee, Yehova, Msaidie Msichana Wangu Mchanga Aendelee Kuwa Mwaminifu!”
NILIZALIWA mnamo 1930 katika Alsace, Ufaransa, katika familia iliyopenda sanaa. Wakati wa jioni, baba, akiketi katika kiti chake chenye starehe, alikuwa akisoma vitabu fulani kuhusu jiografia au astronomia. Mbwa wangu alikuwa akilala mguuni pake, na baba alikuwa akishiriki na mama mambo makuu ya usomaji wake huku mama akifumia familia vitu. Nilikuwa nikifurahia jioni hizo kama nini!
Dini ilikuwa sehemu kubwa ya maisha yetu. Tulikuwa Wakatoliki wenye bidii sana, na watu waliokuwa wakituona tukienda kanisani Jumapili asubuhi walikuwa wakisema: “Ni saa tatu. Akina Arnold wanaenda kanisani.” Nilikuwa nikienda kanisani kila siku kabla ya kwenda shuleni. Lakini kwa sababu ya tabia mbaya ya kasisi, mama alinikataza nisiende kanisani peke yangu. Nilikuwa na umri wa miaka sita wakati huo.
Baada ya kusoma vijitabu vitatu tu vya Bibelforscher (Wanafunzi wa Biblia, sasa wanaitwa Mashahidi wa Yehova), mama yangu alianza kuhubiri nyumba kwa nyumba. Baba alikasirika sana juu ya jambo hilo. Akaweka sheria ya kwamba mazungumzo yoyote ya kidini yasifanywe mbele yangu. ‘Hakuna kusoma takataka hizo!’ Lakini mama alikuwa na shauku sana juu ya kweli hivi kwamba akaamua kusoma Biblia nami. Alipata tafsiri ya Biblia ya Kikatoliki na kuisoma kila asubuhi bila kutoa maelezo juu yayo ili kumtii baba.
Siku moja alisoma Zaburi 115:4-8: “Sanamu zao ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadamu. . . . Wazifanyao watafanana nazo, kila mmoja anayezitumainia.” Aliyalinganisha na amri ya pili, isemayo: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga.” (Kutoka 20:4-6) Nikaamka mara hiyo na kuharibu altare yangu binafsi niliyokuwa nayo chumbani mwangu.
Nilikuwa nikienda shuleni na kushiriki na wanadarasa wenzangu Wakatoliki juu ya mambo niliyojifunza katika usomaji wangu wa Biblia wa kila siku. Hilo lilileta mvurugo mkubwa shuleni. Mara nyingi sana watoto wangenifuata katika barabara ya mtaa na kuniita “Myahudi anayenuka!” Hayo yalitukia katika 1937. Hali hiyo ilimfanya baba yangu achunguze mambo niliyokuwa nikijifunza. Alijipatia kitabu Creation, kilichotangazwa na Mashahidi wa Yehova. Alikisoma na mwenyewe akawa Shahidi!
Mara tu jeshi la Ujerumani lilipoingia Ufaransa kupitia mpaka wa Ubelgiji, tulianza kuona alama za swastika katika bendera zilizokuwa juu ya makanisa, hata ingawa bendera ya Kifaransa ilikuwa ingali ikipepea juu ya jumba kuu la jiji. Serikali ya Ufaransa ilikuwa imefunga Jumba la Ufalme letu na kupiga marufuku kazi ya Mashahidi wa Yehova, na tayari tulikuwa tukifanya kazi kichini-chini Wajerumani walipokuja. Lakini jitihada za kumaliza Mashahidi ziliongezeka sana. Nilibatizwa miaka miwili baadaye nikiwa na umri wa miaka 11.
Mwezi mmoja baadaye, Septemba 4, 1941, saa nane alasiri, kengele ya mlango ililia. Baba alipaswa kurudi nyumbani kutoka kazini. Nikaruka, nikafungua mlango, na kukimbia kumkumbatia. Mtu aliyekuwa nyuma yake akapaaza sauti, “Heil Hitler!” Nikikanyaga chini tena, nikang’amua kwamba nilikuwa nimekumbatia mwanajeshi wa kikosi cha polisi cha SS! Wakanifukuza niende chumbani mwangu na kumhoji mama yangu kwa muda wa saa nne. Walipokuwa wakienda, mmoja wao alipaaza sauti akisema: “Hutamwona mume wako tena! Wewe na mtoto wako mtaenda kwa njia iyo hiyo!”
Baba alikuwa ameshikwa asubuhi hiyo. Alikuwa ameweka mshahara wake wa kila mwezi mfukoni mwake. Polisi wa SS walifunga akiba ya benki na kumnyima mama yangu kadi ya kufanya kazi—hati ya lazima ili kupata kazi. Sera yao sasa ilikuwa: “Vijidudu hivyo vikose riziki!”
Mnyanyaso Shuleni
Wakati huo mikazo katika shule iliendelea kuongezeka. Wakati wowote mwalimu alipokuja darasani, ilikuwa ni lazima wanafunzi wote 58 wasimame mikono yao ikiwa imenyooshwa na kusema, “Heil Hitler.” Kasisi alipokuja kwa ajili ya mafunzo ya kidini, alikuwa akiingia na kusema, “Heil Hitler—abarikiwe yule anayekuja katika jina la Bwana.” Darasa lingejibu, “Heil Hitler—Amen!”
Nilikataa kusema, “Heil Hitler,” na mkurugenzi wa shule akapata kusikia. Barua ya kutoa onyo iliandikwa ikisema: “Mwanafunzi mmoja hatii sheria za shule, na kama hakuna badiliko lolote kwa muda wa juma, mwanafunzi huyo atafukuzwa shuleni.” Ilisema katika sehemu ya mwisho kwamba mimi, Simone Arnold, nilipaswa kuisoma barua hiyo, kwenye madarasa zaidi ya 20.
Siku ilifika ambapo niliitwa mbele ya darasa letu ili nifanye uamuzi wangu ujulikane. Mkurugenzi huyo aliniongezea dakika tano za ama kusalimu ama kuchukua vitu vyangu vya shule na kwenda. Dakika hizo tano kwenye saa zilionekana kama umilele. Miguu yangu ikawa minyonge, kichwa changu kikahisi ujazo, na moyo wangu ulikuwa ukipiga. Ukimya wa darasa zima ulikatishwa na kelele za “Heil Hitler,” huku darasa zima likizirudia mara tatu. Nilikimbilia dawati langu, nikachukua vitu vyangu, na kukimbia nje.
Nilirudi shuleni Jumatatu iliyofuata. Mkurugenzi aliniambia kwamba ningerudi tu kwa takwa la kwamba nisingemwambia mtu yeyote sababu iliyofanya nifukuzwe shuleni. Wanadarasa wenzangu walinigeuka, wakiniita mwizi, mtoto mtundu, wakisema kwamba hiyo ndiyo iliyonifanya nifukuzwe. Nisingeweza kuwaeleza sababu halisi.
Nilikuwa nimeketi sehemu ya nyuma ya darasa. Msichana aliyekuwa kando yangu alitambua kwamba mimi sisalimu. Alifikiri mimi ni wa kikundi cha Wafaransa waasi. Nikafikiri tu nimweleze sababu iliyonifanya nisisalimu Hitler: “Kulingana na Matendo 4:12, ‘Hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.’ Kristo peke yake ndiye Mwokozi wetu. Kwa kuwa ‘heil’ husimamia wokovu kutokana na mtu fulani, siwezi kuona wokovu huo kuwa watokana na mtu awaye yote, kutia ndani Hitler.” Msichana huyo na mama yake walianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova na wenyewe wakaja kuwa Mashahidi!
Utendaji wa Kichini-Chini
Tuliendelea kuhubiri kichini-chini wakati huo wote. Tulikuwa tukienda nje kila Jumapili ya kwanza ya kila mwezi kwenye mahali fulani milimani ambako tulipata toleo la Mnara wa Mlinzi la Kifaransa na kulitafsiri katika Kijerumani. Mama alikuwa amenitengenezea soksi ndefu za wanawake zenye ukanda zilizokuwa na mifuko iliyofichika ya kubeba Mnara wa Mlinzi. Siku moja tulisimamishwa na wanajeshi wawili na kupelekwa katika shamba moja lililokuwa mlimani, ambako tulipekuliwa. Nikawa mgonjwa hivi kwamba wakaniacha nilalie ukoka, na kwa sababu hiyo hawakupata kamwe Mnara wa Mlinzi. Kwa njia moja au nyingine, nyakati zote Yehova alionekana kutuokoa.
Siku moja nilipata simu ya kwenda kwa “daktari wa akili.” Kumbe wakawa ni polisi wawili wa SS. Watoto wengine wa Mashahidi walikuwa huko vilevile. Nilikuwa wa mwisho kuitwa ndani. “Madaktari” hao wawili waliketi nyuma ya meza, nikaketi kukiwa na taa nyangavu ikimulika uso wangu, na mahoji yakaanza. “Daktari” mmoja angeniuliza maswali fulani ya kijiografia au kihistoria, lakini kabla sijaweza kujibu, yule mwingine angefuatia kwa maswali yanayohusu ile kazi ya kichini-chini. Angeniuliza pia juu ya majina ya Mashahidi wengine. Nilikuwa karibu sana kushindwa wakati ambapo kwa ghafula mlio wa simu ulipokatiza mahoji yao. Msaada wa Yehova ulikuja nyakati zote kwa njia ya ajabu kama nini!
Katika pindi moja darasa la shule yetu lilichaguliwa liende kwenye kambi ya kuzoeza Vijana wa Hitler kwa majuma mawili. Sikumweleza mama yangu juu ya hilo. Sikutaka awe na daraka lolote juu ya uamuzi wangu wa kutoenda huko. Kabla ya siku ya kuondoka kufika, mkurugenzi wa shule alinionya: “Ikiwa hutakuwa umefika kwenye stesheni ya gari-moshi au ofisini mwangu siku ya Jumatatu, nitaagiza polisi wakutafute!”
Kwa hiyo Jumatatu asubuhi nilipita stesheni ya gari-moshi nikienda shuleni. Wanadarasa wenzangu wote walikuwa wakiniita niende pamoja nao, lakini niliazimia niende kwenye ofisi ya mkurugenzi. Nilichelewa kufika huko, kwa hiyo alidhania nimeenda na wengine kwenye gari-moshi. Alighadhabika sana aliponiona. Alinichukua ndani ya darasa na kufanya darasa zima liumie kwa muda wa saa nne. Kwa kielelezo, angeita kila mtoto mbele ya darasa, na badala ya kuwapa vitabu vyao vya kuandikia, angewachapa usoni na vitabu hivyo. Angenielekezea kidole na kusema: “Ni yeye amesababisha!” Alijaribu kufanya watoto 45, wenye umri wa miaka kumi, wanigeukie. Lakini kwenye mwisho wa masomo, walikuja wakinipongeza kwa sababu nilikuwa nimekataa kuimba nyimbo za kijeshi.
Baadaye nilichaguliwa nigawanye karatasi, mikebe, na mifupa. Nilikataa kufanya hivyo, kwa sababu mikebe hiyo ilikuwa ikitumiwa kwa makusudi ya kijeshi. Nilipigwa nikaachwa nimezirai. Baadaye wanadarasa wenzangu wakanisaidia kusimama.
Niliporudi shuleni, nilishangaa kuona madarasa yote yakisimama kwenye ua kuzunguka mlingoti wa bendera, watoto karibu 800. Niliwekwa katikati. Ufafanuzi mrefu wa uhuru na matokeo ya wasaliti ulitolewa, ukifuatwa na milio mitatu ya Sieg heil! (ushindi na wokovu). Wimbo wa taifa uliimbwa nikiwa nimesimama tuli na kutetemeka. Yehova alinitegemeza; nilishika uaminifu-maadili.
Nilihitaji utegemezo. Kwa sababu ya msimamo wa wazazi wangu na msimamo wangu mwenyewe, nilikamatwa, nikajaribiwa mahakamani, na kufungwa na hakimu katika “shule ya kurekebisha tabia.” Hakimu alisema katika hukumu hiyo kwamba ‘alilelewa katika mafundisho ya Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, ambao mafundisho yao yamekatazwa na sheria, naye atakuwa na tabia mbaya na kuhatarisha wengine.’ Hicho kilikuwa ni kisa chenye kuniogofya sana, sasa nikiwa na umri wa miaka 12, katika jumba hilo la mahakama lenye kuogofya! Baadaye, nilipoingia nyumba yetu, nilipata nguo zangu kitandani na barua iliyosema: “Simone Arnold aende stesheni ya gari-moshi kesho asubuhi.”
Kuelekea Shule ya Kurekebisha Tabia
Asubuhi iliyofuata mama pamoja nami tukawa kwenye stesheni ya gari-moshi. Wanawake wawili wakanichukua kunilinda. Kwenye gari-moshi mama alirudia shauri lake kuhusu tabia yangu. “Uwe mwenye adabu nyakati zote, mwenye fadhili, na mpole, hata katika nyakati ambapo unaonewa. Usiwe mshupavu kamwe. Usirudishe maneno au kujibu vibaya. Kumbuka, kuwa imara hakuhusiani na kuwa msumbufu. Itakuwa shule ya maisha yako ya wakati ujao. Ni mapenzi ya Yehova kwamba tupitie majaribu kwa manufaa yetu ya wakati ujao. Umejitayarisha vizuri kwa ajili ya hayo. Unajua kushona, kupika, kufua, na kutunza bustani. Sasa umekuwa mwanamke mchanga.”
Baada ya safari ya gari-moshi ya muda wa saa tano, tulifika kwenye nyumba ya gereza. Jioni hiyo mama nami tukapiga magoti chini, tukaimba wimbo wa Ufalme kuhusu tumaini la ufufuo, na tukawa na sala. Kwa sauti thabiti, mama aliomba dua kwa niaba yangu: “Ee, Yehova, msaidie msichana wangu mchanga aendelee kuwa mwaminifu!” Kwa mara ya mwisho, mama aliniweka kitandani na kunibusu.
Mambo yalienda vyepesi siku iliyofuata, bila kunipatia muda wa kuaga mama yangu. Msichana mmoja alinionyesha kitanda chenye godoro la makapi ya ngano. Viatu vyangu vilichukuliwa, na tulilazimishwa kutembea miguu mitupu mpaka Novemba mosi. Ilikuwa vigumu kumeza chakula cha mchana cha kwanza. Nilipewa jozi sita za soksi nitengeneze; bila kufanya hivyo nisingepewa chakula. Kwa mara ya kwanza nilianza kulia. Machozi yalifanya soksi hizo ziwe maji-maji. Nililia karibu usiku kucha.
Niliamka saa 11:30 asubuhi iliyofuata. Kitanda changu kilikuwa na damu—hedhi yangu ilikuwa imeanza muda mfupi kabla ya mambo hayo yote. Nikitetemeka, nilimwendea mwalimu wa kwanza niliyekutana naye, Bi Messinger. Alimwita msichana mmoja aliyenionyesha jinsi ya kufua shuka yangu katika maji baridi. Sakafu ya mawe ilikuwa baridi, na uchungu ukaongezeka. Nikaanza kulia tena. Kisha Bi Messinger kwa maneno ya kuchoma akasema: “Ambia Yehova wako akufulie shuka yako!” Hayo ndiyo mambo niliyohitaji kusikia. Nikapangusa machozi yangu, na hawakuweza kunifanya nilie machozi tena.
Ilitubidi tuamke saa 11:30 alfajiri kila asubuhi ili kuosha nyumba kabla ya kiamsha-kinywa—bakuli la supu saa 2:00 asubuhi. Shule ilifanywa katika makao hayo kwa ajili ya watoto 37, wenye umri wa kuanzia miaka 6 hadi 14. Alasiri tulikuwa tukifua, kushona, na kutunza bustani kwa sababu hakukuwa na wanaume wa kufanya kazi zilizo ngumu. Katika majira ya kipupwe ya 1944/45, nikiwa pamoja na msichana mwingine, tulilazimika kukata miti yenye kipenyo cha sentimeta 60 tukitumia msumeno wa kukatia miti. Watoto hawakuruhisiwa kuongea kati yao wala hawakuruhusiwa wabaki peke yao, hata kwenda chooni. Tulioga mara mbili kwa mwaka, na kuosha nywele zetu mara moja kwa mwaka. Adhabu ilikuwa ni kunyimwa chakula au kupigwa.
Nikawa ninasafisha chumba cha Bi Messinger. Alitaka niende kila siku mvunguni mwa kitanda chake na kupangusa spring’i. Nilikuwa na Biblia ndogo ambayo nilikuwa nimeingiza nyumbani humo, na niliweza kuitia kati ya spring’i. Baadaye, niliweza kusoma visehemu vya Biblia kila siku. Si ajabu kwamba waliniita mtoto mwenye kufanya kazi polepole zaidi waliopata kuwa naye!
Wasichana wa Kiprotestanti walienda kwenye kanisa lao Jumapili, na wasichana watatu Wakatoliki walienda kwenye lao, lakini nililazimika kupikia watoto wote 37. Nilikuwa mdogo hivi kwamba ilikuwa ni lazima nisimame juu ya benchi na kushika kijiko kwa mikono miwili ili kukoroga supu. Ilinibidi nipike nyama, nioke keki, nitayarishe mboga kwa ajili ya walimu wetu wanne. Katika Jumapili alasiri, ilikuwa ni lazima tupambe vitambaa vya mkono vya mezani. Hakukuwa na wakati wa kucheza.
Miezi kadhaa baadaye, akiwa na furaha ya waziwazi, Bi Messinger alinipatia habari kwamba mama yangu mpendwa alikuwa amekamatwa na sasa alikuwa katika kambi ya mateso.
Katika 1945 vita vilikwisha. Kambi za mateso zilikoma na kutapanya nchini kote wateswa wazo, zikifanya maelfu ya watu watange-tange huku na huku wakitafuta mabaki wowote wa familia zao ambao huenda bado walikuwa hai.
Kupatana Tena Kwenye Kutia Uchungu
Angalau mama yangu alijua nilipokuwa, lakini alipokuja kunichukua, sikumtambua. Si ajabu, kutokana na yale aliyokuwa amepitia! Mama alipokamatwa, alipelekwa kwenye kambi ileile ambayo baba alikuwa amepelekwa, Schirmeck, isipokuwa tu kwamba aliwekwa katika kambi ya wanawake. Alikataa kutengeneza yunifomi (sare) za wanajeshi na kwa hiyo aliwekwa ndani ya kifungo cha peke yake kwa miezi mingi katika chumba cha chini ya ardhi. Kisha, ili kumchafua, alipelekwa akae na wanawake waliokuwa wakiugua kaswende. Alipokuwa akihamishwa kuenda Ravensbrück, akawa mgonjwa wa kukaa kitandani kutokana na kukohoa. Wakati huo Wajerumani wakatoroka, na kwa ghafula wafungwa waliokuwa wakielekea Ravensbrück walikuwa huru, mama yangu akiwa mmoja wao. Alielekea Constance, mahali nilipokuwa, lakini mlipuko wa mashambulizi ya ndege ulikuwa umekata uso wake na alikuwa akitokwa damu.
Nilipopelekwa mbele yake, alikuwa amebadilika sana—akiwa amedhoofika kutokana na njaa, kwa wazi akiwa mgonjwa, uso wake ukiwa na majeraha na damu, sauti yake ikiwa karibu haisikiki. Nilikuwa nimezoezwa kuinama mbele ya wageni na kuwaonyesha kazi zangu zote—yale mapambo ya vitambaa, vitu nilivyoshona—kwa sababu wanawake wengine walikuwa wakija kuchukua mjakazi. Na hivyo ndivyo nilivyomtenda mama yangu maskini! Ni wakati tu aliponichukua kwa hakimu ili apate kibali cha sheria cha kunipeleka nyumbani ndipo nilipong’amua kwamba huyu alikuwa mama yangu! Mara hiyo, yale machozi yote niliyokuwa nimeweka ndani yangu kwa miezi 22 iliyokuwa imepita yakabubujika.
Tulipokuwa tukitoka, taarifa ya mkurugenzi, Bi Lederle, ilikuwa kama mafuta ya kutuliza kwa mama. Alisema hivi: “Nakurudishia msichana wako akiwa na mwelekeo uleule wa akili aliokuja nao.” Uaminifu-maadili wangu ungali ulikuwa imara. Tulipata nyumba yetu na tukaanza kuishi humo ndani. Jambo moja tu ambalo bado lilituhuzunisha lilikuwa kwamba baba hakuwa amepatikana. Aliorodheshwa na shirika la Msalaba Mwekundu kuwa alikuwa amekufa.
Katikati ya Mei 1945, mlango ulibishwa. Tena nilikimbia kuufungua. Rafiki yetu, Maria Koehl, alikuwa mlangoni, naye akasema: “Simone, siko peke yangu. Baba yako yuko chini ya orofa.” Karibu baba ashindwe kabisa kupanda ngazi, na alikuwa amekuwa kiziwi. Alinipita kwa karibu sana na kwenda moja kwa moja kwa mama! Yule msichana mdogo mwenye umri wa miaka 11 mwenye utendaji aliyekuwa amejua wakati mmoja alikuwa amekuwa kijana mwenye haya katika miezi hiyo mirefu. Msichana mgeni ambaye hakumtambua.
Yale aliyopitia yalikuwa yamemwathiri vibaya. Kwanza kwenda Schirmeck, kambi ya kipekee, kisha kwenda Dachau, ambako alipatwa na ugonjwa wa homa kali na akazirai kwa siku 14 zilizofuata kutokana nao. Baadaye alitumiwa katika majaribio ya kitiba. Kutoka Dachau alipelekwa Mauthausen, kambi ya maangamizo iliyokuwa mbaya kuliko Dachau, ambako alilazimishwa kufanya kazi ngumu na mapigo na kushambuliwa na mbwa wa polisi. Lakini alikuwa ameokoka na hatimaye alirudi nyumbani tena.
Nilipofika umri wa miaka 17, niliingia katika utumishi wa wakati wote nikiwa mhudumu wa Mashahidi wa Yehova na kisha nikaenda Gileadi katika United States, ile shule ya Watch Tower Society ya wamishonari. Katika makao makuu ya ulimwengu ya Sosaiti, nilikutana na Max Liebster, Myahudi-Mjerumani aliyekuja kuwa Shahidi katika mojapo kambi za mateso za Hitler. Tulioana katika 1956, na kwa msaada wa Mungu wetu, Yehova, tumeendelea mpaka sasa katika utumishi wa wakati wote tukiwa wahudumu mapainia wa pekee hapa katika Ufaransa.
Maneno aliyoyasema mama katika sala yake kwa ajili yangu miaka hiyo mingi iliyopita wakati alipolazimika kuniacha katika nyumba ya gereza yalikuwa ya kweli kama nini: “Naomba dua kwako, ee, Yehova, msaidie msichana wangu mchanga aendelee kuwa mwaminifu!”
Na Yehova amefanya vivyo hivyo mpaka leo hii!—Kama ilivyosimuliwa na Simone Arnold Liebster.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Simone Arnold Liebster na mume wake, Max Liebster