Hatukuunga Mkono Vita ya Hitler
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA FRANZ WOHLFAHRT
BABA yangu, Gregor Wohlfahrt, alitumikia katika jeshi la Austria wakati wa Vita ya Ulimwengu 1 (1914 hadi 1918) na alipigana dhidi ya Italia. Kwa ujumla, mamia ya maelfu ya Waaustria na Waitalia walichinjwa. Maogofyo ya ono hilo yalibadili kabisa maoni ya Baba kuelekea dini na vita.
Baba aliona mapadri Waaustria wakibariki vikosi vya vita, na alipata habari kwamba mapadri Waitalia kwa upande ule mwingine walifanya vivyo hivyo. Hivyo basi aliuliza: “Kwa nini askari Wakatoliki wanahimizwa kuua Wakatoliki wengine? Je, Wakristo wapaswa kupigana wao kwa wao?” Mapadri ha wakuwa na jibu lenye kuridhisha.
Majibu kwa Maswali ya Baba
Baada ya vita Baba alioa na akaishi kwenye milima ya Austria iliyo karibu na mipaka ya Italia na Yugoslavia. Nilizaliwa huko mnamo 1920, kifungua mimba kwa watoto sita. Nilipokuwa na miaka sita, tulihamia maili kadhaa mashariki mwa St. Martin karibu na mji wa kitalii wa Pörtschach.
Tukiwa tungali tunaishi pale, wahudumu wa Mashahidi wa Yehova (walioitwa Wanafunzi wa Biblia wakati huo) waliwatembelea wazazi wangu. Katika 1929 waliacha kijitabu Prosperity Sure, kilichojibu mengi ya maswali ya Baba. Kilionyesha kutoka kwa Biblia kwamba ulimwengu ulidhibitiwa na mtawala asiyeonekana aitwaye Ibilisi na Shetani. (Yohana 12:31; 2 Wakorintho 4:4; Ufunuo 12:9) Uvutano wake kwenye dini, siasa, na biashara ya ulimwengu huu ulikuwa na daraka la maogofyo Baba aliyoyaona katika Vita ya Ulimwengu ya 1. Hatimaye Baba alikuwa amepata majibu aliyokuwa amekuwa akitafuta.
Huduma ya Bidii
Baba aliagiza fasihi kutoka Watch Tower Bible and Tract Society naye akaanza kuzigawa kwa watu wa ukoo halafu nyumba kwa nyumba. Kijana jirani wa miaka 20 tu, Hans Stossier, mara akajiunga naye katika huduma ya nyumba kwa nyumba. Muda mfupi baadaye, watano wa watu wetu wa ukoo wakawa Mashahidi pia—kakaye Baba Franz, mkeye Anna, baadaye mwanao Anton, Maria dada mdogo wa kike wa Baba, na mumeye, Hermann.
Hii ilitokeza msisimuko kweli kweli katika mji wetu mdogo wa St. Martin. Shuleni mwanafunzi alimuuliza mwalimu wetu Mkatoliki, “Padri Loigge, Yehova ni mungu mpya yupi ambaye Wohlfahrt anaabudu?”
“La, la, watoto,” padri huyo akajibu. “Huyu si mungu mpya. Yehova ndiye Baba wa Yesu Kristo. Ikiwa wanaeneza ujumbe huo kwa kuchochewa na upendo kwa Mungu huyo, hiyo ni vyema sana.”
Nakumbuka baba yangu mara nyingi akiondoka nyumbani saa saba usiku akiwa amejisheheni na fasihi za Biblia na mkate uliopachikwa nyama ndani. Saa sita au saba baadaye, alikuwa akifika alifika eneo lake la mahubiri, la mbali zaidi, karibu na mpaka wa Italia. Katika ziara za karibu nilikuwa nikiandamana naye.
Ijapokuwa huduma yake ya peupe, Baba hakupuuza mahitaji ya familia yake ya kiroho. Nilipokuwa na miaka kumi, alianzisha funzo la Biblia la kawaida kila juma pamoja na sisi sote tukiwa sita, akitumia kitabu The Harp of God. Wakati mwingine nyumba yetu ilijaa majirani waliopendezwa, pamoja na watu wa ukoo. Muda mfupi baadaye kukawa na kutaniko lenye wapiga-mbiu wa Ufalme 26 katika mji wetu mdogo.
Hitler Akwea Mamlakani
Hitler alikwea mamlakani katika Ujerumani mnamo 1933, na muda mfupi baadaye mnyanyaso kwa Mashahidi wa Yehova ukaongezeka. Katika 1937, Baba alihudhuria mkusanyiko katika Prague, Czechoslovakia. Wahudhuriaji walitahadharishwa juu ya majaribu yaliyokuwa mbele, kwa hiyo Baba aliporudi alituhimiza sisi sote tujitayarishe kwa ajili ya minyanyaso.
Kwa wakati ule, nikiwa na miaka 16, nilianza kuzoezwa kama mpaka-rangi wa nyumba. Niliishi na mpaka-rangi stadi na nilihudhuria shule ya mazoezi. Padri mzee-mzee aliyetoroka Ujerumani ili kuepuka utawala wa Nazi aliongoza darasa la maagizo ya kidini shuleni. Wanafunzi walipomwamkua kwa salamu ya “Mwokozi ni Hitler!” alionyesha kutopendezwa na akauliza: “Imani yetu ina kasoro gani?”
Nilitumia fursa hiyo ifaavyo kuuliza kwa nini Wakatoliki walitumia vyeo kama “Ewe Mwadhamu” na “Baba Mtakatifu,” kwani Yesu alisema wafuasi wake wote ni ndugu. (Mathayo 23:8-10) Padri huyo alikiri kwamba kufanya hivyo ni kosa na kwamba yeye alikuwa matatani kwa kukataa kumwinamia askofu na kumbusu mkono. Ndipo nikauliza: “Inawezekanaje kuua Wakatoliki wenzenu kwa baraka za Kanisa?”
“Hii ni aibu kubwa kabisa!” padri huyo akapaaza sauti. “Haipaswi kutokea kamwe tena. Sisi ni Wakristo na Kanisa halipaswi kujiingiza vitani.”
Mnamo Machi 12, 1938, majeshi ya Hitler yaliingia Austria bila kizuizi chochote na upesi wakaifanya kuwa sehemu ya Ujerumani. Haraka makanisa yakajipanga pamoja naye. Kwa hakika, kwa muda unaopungua juma moja baadaye, maaskofu wote sita Waaustria kutia ndani Kardinali Theodore Innitzer walitia sahihi “julisho zito” la kusisimua walimosema ya kwamba katika uchaguzi ujao “ni lazima na ni wajibu wa kitaifa tukiwa Wajerumani, kwetu sisi Maaskofu kuupigia kura Utawala wa Ujerumani.”(Ona ukurasa 9.) Kulikuwa na upokewaji mkubwa katika Vienna ambapo Kardinali Innitzer alikuwa miongoni mwa wa kwanza kumsalimu Hitler kwa saluti ya Nazi. Kardinali huyo aliamuru makanisa yote ya Austria yapeperushe bendera ya swastika, yapige kengele zao, na yasali kwa ajili ya dikteta huyo wa Nazi.
Kwa ghafula hali ya kisiasa katika Austria ilibadilika. Vikosi-jeuri vikiwa na sare za hudhurungi na utepe wa Swastika begani huku vilivuvumuka kote kama uyoga. Padri yule aliyekuwa amesema mbeleni Kanisa halipaswi kujihusisha katika vita alikuwa miongoni mwa wale wachache waliokataa kusema, “Mwokozi ni Hitler!” Juma lililofuata padri mpya alichukua mahali pake. Jambo la kwanza alilolifanya alipoingia darasani ni kupigisha chini wayo wake kijeshi, kupiga saluti, na kusema: “Mwokozi ni Hitler!”
Mkazo ili Kujipatanisha
Kila mtu alipatwa na msongo wa Wanazi. Niliposalimu watu kwa “Guten Tag” (Siku njema) badala ya “Mwokozi ni Hitler,” walikasirika. Mara karibu 12 niliripotiwa kwa Gestapo. Wakati mmoja kikundi cha askari-jeuri wa Nazi kilimtisha mpaka rangi stadi niliyekuwa nikiishi naye, kikisema ya kwamba ikiwa singepiga saluti na kujiunga na chama cha Vijana wa Hitler, ningepelekwa kwenye kambi ya mateso. Mpaka rangi huyo, akiwa mfuasi wa Nazi, aliwaomba wafadhili wa Nazi wanistahimili kwani alikuwa na uhakika hatimaye ningebadilika. Alieleza ya kwamba hakutaka kunipoteza kwa sababu nilikuwa mfanyakazi mzuri.
Nazi ilipochukua mamlaka, kulikuwa na maandamano makubwa yaliyoendelea mpaka usiku sana, na watu kwa ushupavu walipaaza shime za kivita. Kila siku redio zilijaa hotuba zilizotolewa na Hitler, Goebbels, na wengine. Unyenyekeo wa Kanisa Katoliki kwa Hitler uliongezeka zaidi, kadiri mapadri walivyosali kwa kawaida na kumbariki Hitler.
Baba alinikumbusha uhitaji wa kuchukua msimamo thabiti kwa kuweka wakfu maisha yangu kwa Yehova na kubatizwa. Pia alinizungumzia kuhusu Maria Stossier, dada mdogo wa jirani yetu Hans, aliyekuwa amechukua msimamo upande wa kweli ya Biblia. Maria nami tulikuwa tumekubaliana kuoana, na Baba alinihimiza niwe kitia-moyo kwake kiroho. Maria nami tulibatizwa katika Agosti 1939 na Hans kaka yake.
Uaminifu-Maadili Bora wa Baba
Siku iliyofuata Baba aliitwa kwa utumishi wa jeshi. Ingawa alikuwa na afya mbaya, kutokana na magumu yaliyomfika wakati wa Vita ya Ulimwengu 1, bado tu ingalimzuia kutotumikia, Baba aliwaeleza waliomhoji ya kwamba akiwa Mkristo hangehusika tena katika vita kama alivyotenda akiwa Mkatoliki. Kwa sababu ya maelezo hayo alishikwa kwa uchunguzi zaidi.
Majuma mawili baadaye Ujerumani ilipovamia Poland, na hilo likaanzisha Vita ya Ulimwengu 2, alipelekwa Vienna. Akiwa angali ameshikwa huko, meya wa wilaya yetu aliandika akidai ya kwamba Baba alikuwa na daraka la kukataa kwa Mashahidi wale wengine kujiunga na Hitler na kwa hivyo Baba alipaswa kuuawa. Kama tokeo, Baba alipelekwa Berlin na muda mfupi baadaye alihukumiwa kukatwa kichwa. Alifungwa kwa minyororo mchana na usiku katika jela ya Moabit.
Kwa wakati huohuo niliandikia Baba kwa niaba ya familia nikamwambia ya kwamba sisi tumeazimia kufuata kielelezo chake bora cha uaminifu. Kwa ujumla Baba hakuwa mtu mwenye hisia nyepesi, lakini tungeweza kuona jinsi alivyohisi katika barua yake ya mwisho kwetu iliyokuwa na alama za machozi. Alifurahi sana kwamba tulielewa msimamo wake. Alipeleka maneno ya kitia-moyo, akitutaja kila mmoja wetu kwa jina na akituhimiza tukae tukiwa waaminifu. Tumaini lake katika ufufuo lilikuwa lenye nguvu.
Licha ya Baba, karibu Mashahidi wengine dazani mbili walikuwa wameshikwa katika jela ya Moabit. Maofisa wenye vyeo vya juu wa Hitler walijaribu kuwashawishi ili waache imani yao lakini bila mafanikio. Katika Desemba 1939, Mashahidi 25 wengine waliuawa. Alipopata habari ya kuuawa kwa Baba, Mama alionyesha jinsi alivyokuwa na shukrani kwa Yehova kwamba yeye alikuwa amempa Baba nguvu za kubaki mwaminifu hadi kifo.
Majaribu Yangu Yaanza
Majuma machache baadaye, niliitwa kwenye kazi ya utumishi lakini mara nikafahamu kazi yenyewe ilikuwa mazoezi ya kijeshi. Nilieleza kwamba singetumikia katika jeshi lakini ningefanya kazi nyingineyo. Hata hivyo, nilipokataa kuimba nyimbo za mapigano za Nazi, maofisa walikasirika sana.
Asubuhi iliyofuata nilitokea nikiwa na vazi la kiraia badala ya sare ya kijeshi tuliyokuwa tumepewa. Ofisa msimamizi alisema ya kwamba hakuwa na jingine ila kunitia katika shimo la gereza. Nilimoishi kwa mkate na maji. Baadaye niliambiwa ya kwamba kutakuwa na sherehe ya kusalimu bendera, na nilitahadharishwa ya kwamba tokeo la kukataa kushiriki lingekuwa kupigwa kwa risasi.
Kwenye uwanja wa mazoezi walikuwako 300 walioingizwa jeshini na pia maofisa wa kijeshi. Niliamriwa kwenda bega kwa bega pamoja na maofisa hao na bendera ya swastika na nimpigie saluti Hitler. Kwa kupata nguvu za kiroho kwa Biblia kutoka kwa masimulizi ya wale Waebrania watatu, nilisema tu, “Guten Tag” (Siku njema), nilipokuwa nikipita. (Danieli 3:1-30) Niliamriwa nipite tena. Wakati huu sikusema lolote, nilitabasamu tu.
Maofisa wanne waliponirudisha kwenye jela ya chini, waliniambia kwamba walitetemeka kwani walitarajia nipigwe risasi. “Yawezekanaje,” wakauliza, “kwamba ulikuwa unatabasamu nasi tukiwa na wasiwasi sana?” Walisema walitamani wangekuwa na moyo mkuu kama wangu.
Siku chache baadaye, Dakt. Almendinger, ofisa wa cheo cha juu kutoka makao makuu ya Hitler katika Berlin, aliwasili kambini. Niliamriwa kukutana naye. Alieleza kwamba sheria zilikuwa zimekuwa kali zaidi. “Huna habari kabisa juu ya magumu utakayoyakabili,” alisema.
“Enhee, ninajua,” nikajibu. “Baba yangu alikatwa kichwa majuma machache tu yaliyopita kwa sababu hiyo hiyo.” Alipigwa na butwaa akanyamaza.
Baadaye ofisa mwingine wa cheo cha juu kutoka Berlin aliwasili, na jaribio zaidi la kubadili akili yangu likafanywa. Baada ya kusikia kwa nini singevunja sheria za Mungu, alishika mkono wangu na, huku machozi yakimtiririka usoni, akasema: “Nataka kuokoa uhai wako!” Maofisa wote waliotazama waliguswa sana. Ndipo nikarudishwa kwenye lile shimo la gereza nilimokaa kwa jumla ya siku 33.
Jaribio na Kifungo
Mnamo Machi 1940, nilihamishwa hadi jela moja katika Fürstenfeld. Siku chache baadaye mchumba wangu, Maria, na ndugu yangu Gregor walinitembelea. Gregor alikuwa mchanga zaidi kwa mwaka mmoja na nusu tu kwa umri, na alikuwa amechukua msimamo thabiti kwa kweli ya Biblia shuleni. Nakumbuka akiwahimiza ndugu zetu wachanga wajitayarishe kwa mnyanyaso, akisema kuna njia moja tu, kumtumikia Yehova! Saa iliyopita tuliyotumia kutiana moyo ilikuwa wakati wa mwisho niliomwona akiwa hai. Baadaye, katika Graz, nilihukumiwa miaka mitano ya kazi ngumu.
Katika vuli ya 1940, nilitiwa katika gari-moshi iliyoelekea kwenye kambi ya kazi ngumu katika Czechoslovakia, lakini nilifungwa Vienna nikatiwa ndani ya jela huko. Hali zilikuwa mbaya. Si kwamba tu niliumia na njaa, bali wakati wa usiku niliumwa na kunguni wakubwa walioniacha nikitokwa na damu na kuwashwa vikali. Kwa sababu nisizozijua kwa wakati ule, nilirudishwa kwa jela katika Graz.
Kulikuwa na upendezi kwani Gestapo waliwafafanua Mashahidi wa Yehova kuwa wafia-imani washupavu waliohitaji hukumu ya kifo ili waweze kupata thawabu ya ufufuo wa kimbingu. Kama tokeo, nilikuwa na fursa nzuri ya kuzungumza kwa siku mbili, mbele ya profesa mmoja na wanafunzi wanane kutoka Chuo Kikuu cha Graz, nikieleza ya kwamba ni watu 144,000 tu ambao wangechukuliwa mbinguni ili kutawala na Kristo. (Ufunuo 14:1-3) Tumaini langu, nilisema, lilikuwa kufurahia uhai wa milele katika hali ya paradiso duniani.—Zaburi 37:29; Ufunuo 21:3, 4.
Baada ya siku mbili za kuhojiwa, profesa huyo alisema: “Nimeng’amua ya kwamba miguu yako miwili ipo hapa duniani. Si tamaa yako ufe ili uende mbinguni.” Aliona huruma kwa jinsi Mashahidi wa Yehova walivyonyanyaswa na akanitakia mema kwa yajayo.
Mapema mnamo 1941, nilijikuta ndani ya gari-moshi likielekea Rollwald kambi ya kazi ngumu katika Ujerumani.
Maisha Makali Kambini
Rollwald ilikuwa katikati ya majiji ya Frankfurt na Darmstadt na ilikuwa na wafungwa wapatao 5,000. Kila siku ilianza saa 11:00 asubuhi kwa kuita majina, kulikochukua muda wa saa mbili maofisa wakichukua muda wao ili kurekebisha orodha yao ya wafungwa, tulitakwa kusimama tuli, na wafungwa wengi walicharazwa sana kwa kutosimama tuli.
Kiamsha-kinywa kilitia ndani mkate, uliofanywa kwa unga, uvumbi wa mbao, na kwa kawaida viazi ambavyo mara nyingi vilikuwa vimeoza. Kisha tulienda kufanya kazi katika ziwa la matope, tukichimba mitaro ili kuondoa maji kwa minajili ya kilimo. Baada ya kufanya kazi katika ziwa la matope siku nzima bila viatu vinavyofaa, miguu yetu ilifura kama sifongo. Wakati mmoja miguu yangu ilikuja kupatwa na lililoonekana kuwa kidonda kisichopona, na nilihofia kwamba ingehitaji kukatwa.
Wakati wa mchana kazini, tuliandaliwa mchanganyiko wa changanyo lililoitwa supu eti. Lilikolezwa kwa mboga au kabeji na wakati mwingine lilitia ndani mizoga ya wanyama waliokufa. Vinywa vyetu na koo viliwashwa sana, na wengi wetu tulipatwa na majipu makubwa. Wakati wa jioni tulipata “supu” zaidi. Wafungwa wengi walipoteza meno yao, lakini nilikuwa nimeelezwa umuhimu wa kufuliza kutendesha meno kazi. Ningetafuna kipande cha mti wa msonobari au vitawi vya mfito, nami sikupoteza yangu kamwe.
Kukaa Imara Kiroho
Katika jitihada ya kuvunja imani yangu, walinzi walinitenga na Mashahidi wale wengine. Kwa sababu sikuwa na fasihi ya Biblia, ningekumbuka maandiko niliyoyakariri, kama vile Mithali 3:5, 6, linalotuhimiza ‘tutumaini katika Yehova kwa moyo wetu wote,’ na 1 Wakorintho 10:13, linaloahidi kwamba Yehova ‘hataacha tujaribiwe kupita tuwezavyo.’ Kwa kurudia maandiko kama hayo akilini na kwa kumwegemea Yehova kwa sala, nilitiwa nguvu.
Nyakati fulani niliweza kuona Shahidi aliyekuwa kuhamishwa kutoka kambi nyingine. Ikiwa hatukupata fursa ya kuongea, tungetiana moyo kusimama imara kwa kuashiriana kwa mtikiso wa kichwa chetu au mkono uliofumbatiwa na kuinuliwa. Mara kwa mara nilipokea barua kutoka kwa Maria na Mama. Katika mojapo nilipata habari kuhusu kifo cha ndugu yangu mpendwa Gregor, na katika nyingine, mwishoni mwa vita, kuhusu kufishwa kwa Hans Stossier, ndugu yake Maria, ameuliwa.
Baadaye, mfungwa mmoja alihamishwa hadi kambi yetu aliyemjua Gregor walipokuwa pamoja katika jela ya Moabit katika Berlin. Kutoka kwake nilipata kujua kwa mapana yaliyotokea. Gregor alikuwa amehukumiwa kifo cha kukatwa kichwa, lakini katika jitihada ya kuvunja uaminifu-maadili wake, kile kipindi cha kidesturi cha kungojea kufishwa kilikuwa kimerefushwa kuwa miezi minne. Wakati huo misongo ya kila aina iliwekwa ili kumfanya aridhiane—minyororo mizito mikononi na miguuni, na ni nadra sana alilishwa. Hata hivyo, hakuyumbayumba. Alikuwa mwaminifu hadi mwisho—Machi 14, 1942. Ingawa nilihuzunishwa na habari hizo, nilitiwa nguvu nazo ili kubaki mwaminifu kwa Yehova, viwe viwavyo.
Baada ya muda nilipata kujua pia ndugu zangu wadogo Kristain na Willibald na dada zangu wadogo Ida na Anni walipelekwa kwenye makao ya kitawa yaliyotumiwa kutia nidhamu katika Landau, Ujerumani. Vijana hao walipigwa sana kwa sababu walikataa kusalimu Hitler.
Fursa za Kutoa Ushahidi
Wengi wa waliokuwa katika kambi niliyoishi walikuwa wafungwa wa kisiasa na wahalifu. Mara nyingi nilitumia wakati wa jioni kuwatolea ushahidi. Mmoja alikuwa padri Mkatoliki kutoka Kapfenberg aliyeitwa Johann List. Alifungwa kwa sababu alisema kwa kutaniko lake aliyoyasikia kwenye Shirika la Utangazaji la Uingereza.
Johann alikuwa na kipindi kigumu sana kwani hakuzoea kazi ya sulubu. Alikuwa mtu mzuri, nami ningemsaidia afikie fungu la kazi alilogawiwa ili asiingie matatani. Alisema aliona haya kwa kufungwa kwa sababu ya siasa bali si kwa uaminifu kwa kanuni za Kikristo. “Hakika unateseka ukiwa Mkristo,” alisema. Alipoachiliwa huru mwaka mmoja baadaye, aliahidi kumtembelea Mama yangu na mchumba wangu, akatimiza ahadi hiyo.
Maisha Yawa Bora Kwangu
Mwishoni mwa 1943, tulipata kamanda mpya wa kambi kwa jina la Karl Stumpf, mwanamume mrefu, mwenye nywele nyeupe aliyeanza kuboresha hali katika kambi yetu. Jumba lake lilikuwa tayari kupakwa rangi, na alipojua ya kwamba mimi nilikuwa na ujuzi wa kupaka rangi, nilipatiwa kazi hiyo. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kuitwa kutoka kwenye kazi katika ziwa.
Mke wa kamanda aliona vigumu kufahamu kwa nini nilikuwa nimefungwa, hata ingawa mumeye alieleza kwamba nilikuwa pale kwa sababu ya imani yangu nikiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alinihurumia kwani nilikuwa nimekonda sana na alinilisha. Alinipangia kazi zaidi ili niweze kujengwa kimwili.
Wafungwa kutoka kambini walipoitwa kwenye nyanja za vita mwishoni mwa 1943, uhusiano wangu mzuri na Kamanda Stumpf uliniokoa. Nilimweleza kwamba ni heri ningepatwa na kifo kuliko kuwa na hatia ya damu vitani. Ingawa hali yangu ya kutokuwemo ilimtia katika hali ngumu, aliweza kuliondoa jina langu katika orodha ya walioitwa.
Siku za Mwisho wa Vita
Wakati wa Januari na Februari ya 1945, eropleni za Kiamerika zilizoruka kichini-chini zilitutia moyo kwa kuangusha vikaratasi vilivyosema vita vilikaribia mwisho. Kamanda Stumpf aliyekuwa ameokoa uhai wangu, alinipatia nguo za kiraia na pia nyumba yake kama maficho. Kwa kuacha kambi hiyo, nilijionea makubwa. Kwa kielelezo, watoto wakiwa na sare za kijeshi na machozi yakiwatiririka nyusoni walikuwa wakiwatoroka Waamerika. Nikihofia kukimbilia askari wa Nazi ambaye angeniuliza kwa nini sikuwa na bunduki, niliamua kurudi kambini.
Muda si muda kambi yetu ilikuwa imezingirwa kabisa na vikosi vya Kiamerika. Mnamo Machi 24, 1945, kambi ilijisalimisha kwa kuinua bendera nyeupe. Ilinishangaza kama nini kujua kwamba Kamanda Stumpf alikuwa amesimamisha mauaji ya Mashahidi wengine kambini pia! Tulifurahi kama nini kukutana! Kamanda Stumpf aliposhikwa, wengi wetu tuliwaendea maofisa wa Kiamerika na kuwaeleza kibinafsi na kwa barua kwa niaba yake ili wamwachilie. Kama tokeo, siku tatu baadaye aliachiliwa huru.
Kwa kushangaza, nilikuwa wa kwanza kati ya wafungwa 5,000 kuachwa huru. Baada ya miaka mitano ya kifungo, nilihisi kana kwamba ninaota ndoto. Nikiwa na machozi ya shangwe, nilimshukuru Yehova kwa kunihifadhi hai, Ujerumani haikujisalimisha hadi Mei 7, 1945, karibu majuma sita baadaye.
Nilipoachiliwa, mara moja niliwasiliana na Mashahidi wale wengine katika eneo hilo. Kikundi cha funzo la Biblia kilipangwa, na wakati wa majuma yaliyofuata, nilitumia saa nyingi kutoa ushahidi kwa watu katika eneo lililozunguka kambi hiyo. Wakati ule ule, nilipata kazi kama mpaka rangi.
Narudi Nyumbani Tena
Mnamo Julai, niliweza kununua pikipiki, kisha nikaanza mwendo wangu mrefu kuelekea nyumbani. Safari ilinichukua siku kadhaa, kwani mengi ya madaraja ya barabara kuuyalikuwa yamelipuliwa. Hatimaye nilipofika nyumbani katika St. Martin, niliendesha kwa kupanda barabara nikamwona Maria akivuna ngano. Hatimaye aliponitambua, alikuja kwa kukimbia. Unaweza kuwazia huo muungano wenye furaha. Mama alirusha mundu chini naye pia akaja kwa kukimbia. Sasa, miaka 49 baadaye, Mama ana miaka 96 na ni kipofu. Akili yake bado ni timamu, naye aendelea akiwa Shahidi mwaminifu wa Yehova.
Maria nami tulioana mnamo Oktoba 1945, na miaka ya tangu wakati huo hadi leo, tumefurahia kumtumikia Yehova pamoja. Tumebarikiwa kwa binti watatu, mvulana mmoja, na wajukuu sita, wote wakiwa wanamtumikia Yehova kwa bidii. Kwa muda wa miaka nimepata uradhi wa kusaidia makumi ya watu kuchukua msimamo kwa kweli ya Biblia.
Ujasiri ili Kuvumilia
Mara nyingi nimewahi kuulizwa, niliwezaje nikiwa kijana tu kukabili kifo bila woga. Uwe na uhakika—Yehova Mungu hupa nguvu ikiwa umeazimia kubaki mwaminifu-mshikamanifu. Mmoja hujifunza upesi kumwegemea kikamili kupitia kwa sala. Na kwa kujua ya kwamba wengine, kutia ndani na baba yangu mwenyewe, walivumilia hadi kifo wakiwa waaminifu kulinisaidia kubaki nikiwa mwaminifu-mshikamanifu pia.
Haikuwa katika Ulaya tu ambapo watu wa Yehova hawakujiunga na vita. Nakumbuka kwamba katika majaribio ya Nuremberg mnamo 1946, mmoja wa maofisa wa cheo cha juu wa Hitler alikuwa akiulizwa kuhusu minyanyaso ya Mashahidi wa Yehova katika kambi za mateso. Alitoa mfukoni ukurasa wa karatasi habari ulioripoti ya kwamba maelfu ya Mashahidi wa Yehova katika Marekani walikuwa katika magereza ya Kiamerika kwa sababu ya kutokuwemo kwao wakati wa Vita ya Ulimwengu 2.
Hakika, Wakristo wa kweli kwa ujasiri hufuata kielelezo cha Yesu Kristo, aliyedumisha uaminifu-maadili kwa Mungu hadi alipokata pumzi katika kifo. Hadi leo kila mara mimi hufikiria washiriki 14 wa kutaniko letu dogo katika St. Martin wakati wa miaka ya 1930 ambao, kwa upendo wao kwa Mungu na wenzao, walikataa kuunga mkono vita ya Hitler na hivyo wakauawa. Ni muungano mtukufu kama nini watakaporudishwa tena ili kufurahia uhai milele na milele katika ulimwengu mpya wa Mungu!
[Picha katika ukurasa wa 8]
Baba yangu
[Picha katika ukurasa wa 9]
Chini na kushoto: Kardinali Innitzer akipiga kura kuunga mkono Utawala wa Ujerumani
Kulia: “Julisho Zito” ambalo maaskofu sita walitangaza kwamba ni ‘wajibu wao wa kitaifa kupigia kura Utawala wa Ujerumani’
[Hisani]
UPI/Bettmann
[Picha katika ukurasa wa 10]
Katika 1939, Maria nami tulikuwa tumechumbiana
[Picha katika ukurasa wa 13]
Familia yetu. Kushoto hadi kulia: Gregor (alikatwa kichwa), Anni, Franz, Willibald, Ida, Gregor (baba, alikatwa kichwa), Barbara (mama), and Kristian
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nikiwa na Maria leo