Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 9/22 kur. 21-23
  • Je! Ninakua kwa Njia ya Kawaida?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Ninakua kwa Njia ya Kawaida?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maumivu ya Ukuzi
  • Wakuzi Wenye Kuchelewa
  • Namna ya Kukabiliana kwa Mafanikio
  • Mbona Nakua Upesi Hivi?
    Amkeni!—1993
  • Mwili Wangu Unapatwa na Nini?
    Amkeni!—1990
  • ‘Kwani Nina Shida Gani?’
    Amkeni!—2004
  • Ninaweza Kukabilianaje na Kubalehe?
    Vijana Huuliza
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 9/22 kur. 21-23

Vijana Huuliza...

Je! Ninakua kwa Njia ya Kawaida?

“Nilikuwa mmoja wa watoto wadogo zaidi katika darasa letu—na nilikuwa na uzani mdogo zaidi. Sikupenda mikono yangu. Nilifikiri mikono hiyo ilikuwa myembamba mno. Hata niliagiza vifaa vya kufanyia mazoezi vilivyokuwa vimetangazwa katika jalada la nyuma la kitabu kimoja cha ucheshi. Hata hivyo vifaa hivyo havikunisaidia.”—Eric.

“Mimi si mrefu vya kutosha. Nina umri wa miaka 13 na nina kimo cha [sentimeta 150] tu. Kila mtu katika darasa letu ni mrefu zaidi! Ndiyo, kuna wavulana ambao ni wafupi kuliko mimi, lakini labda watakua wakati wa kiangazi. Mimi sipendi kamwe kuwa mfupi! Siwezi kuona kitu chochote! Laiti ningekuwa mrefu sasa.”—Kerri.

MREFU mno! Mfupi mno! Mnene mno! Mwembamba mno! Hizo si dhihaka tu za marika wakatili. Vijana wengi hujiona hivyo kila wakati wanapojiangalia kwenye kioo. “Nilipokuwa na miaka 13,” asema mwanamke mdogo wa Kihispania anayeitwa Mari, “Nilichukia sana pua yangu; ilikuwa pana sana hata nikafikiri nahitaji upasuaji! Na nilikuwa nimenenepa kama nini! Dada yangu mkubwa alikuwa na vazi lililomtosha vizuri kwa umbo lake zuri. Nilipojaribu kulivaa, kila mtu alicheka.”

Unapokuwa katika “uzuri wa ujana,” hasa wakati ule wa msukosuko wa ukuzi wa haraka na mabadiliko ya kihisia-moyo unaoitwa ubalehe, ni rahisi ujihisi vibaya. (1 Wakorintho 7:36) Kutokana na unayoyaona, marika wako wanakua haraka kuwa watu wazima warefu na wenye kuvutia. Lakini waweza kuonekana kana kwamba hukui hata kidogo—au unakua kupita kiasi. Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba idadi ya asilimia 56 ya vijana hawajaridhika na miili yao. Watafiti Jane Norman na Myron W. Harris wasema kwamba wengi wa vijana hao ambao hawajaridhika walihisi kwamba walikuwa “wafupi mno” au kwamba “hawakuwa wamekua vya kutosha.”

Vijana wengi huhangaika pia kuhusu ukuzi wa sehemu zao za siri za mwili; wanajiuliza kama hizo zinakua kwa kawaida. Kitabu Growing Into Love, cha Kathryn Watterson Burkhart, chaeleza kwamba “hisia za [vijana] kujistahi, uwezo wa kufanya mambo, na staha ya binafsi zatokana na mwili wao, kwa hiyo ni jambo la maana kabisa kwamba mwili wao halisi uwe umekua ifaavyo.” Basi, haishangazi kwamba vijana wengi mara nyingi huwa na wasiwasi katika hali (kama masomo ya mazoezi ya mwili) ambapo mwili wao waweza kuchunguzwa—au kulinganishwa. “Huwa sihisi starehe kabisa kuoga pamoja na wavulana wengine shuleni,” akakiri mvulana mmoja mdogo.

Je! hupendi jinsi mwili wako unavyokua? Naam, usiwe na wasiwasi! Inaelekea zaidi kwamba wewe ni wa kawaida kabisa.

Maumivu ya Ukuzi

Ubalehe ni njia ya kawaida yenye kufaa. Hata Yesu Kristo aliupitia, ‘akizidi kuendelea katika hekima na kimo.’ (Luka 2:52) Ubalehe watia ndani ukuzi wa viungo vya uzazi.a Hata hivyo, watia ndani pia kukua haraka kwa ghafula, mara nyingi kwa mara mbili kuliko ukuzi wa wastani wa kila mwaka. “Nilianza kukua kwa [sentimeta 10] kwa mwaka,” akumbuka kijana mmoja anayeitwa Danny. “Kufikia umri wa miaka 13 nilikuwa na kimo cha [sentimeta 180].”

Hata hivyo, mara nyingi wasichana huanza ukuzi wao wa ghafula karibu miaka miwili mbele ya wavulana. Kwa hiyo kufikia umri wa miaka 12, msichana aweza kuwa mrefu zaidi ya wanadarasa wenzake waliokuwa wavulana. Inaelekea kwamba atafurahia urefu huo kwa muda mfupi tu. Kwa miaka kadhaa tu, wengi wa wavulana watamfikia kwa kimo na hata kumpita.

Hata hivyo, ukuzi wa haraka una matatizo pia. Mara nyingi sehemu inayopanuka kwanza ni miguu yako. Basi kwa muda miguu yako yakosa kupatana na ukubwa wa mwili wako. Mwandikaji Lynda Madaras anukuu msichana mmoja mdogo akisema: “Nilikuwa na kimo kinachozidi kidogo [sentimeta 150] nilipokuwa na umri wa miaka kumi na moja, lakini nilikuwa [nikivaa viatu] namba nane. Nikafikiri, Ah, isiwe hivyo, miguu yangu ikiendelea kukua, itakuwa mikubwa kwelikweli! Lakini sasa nina miaka kumi na sita, na nina kimo cha [sentimeta 170], lakini ningali [navaa viatu] namba nane.” Ukuzi wa haraka wa miguu yako ya chini, mapaja, na mwili hufuata upesi baadaye.

Hata jambo lenye kuhuzunisha zaidi laweza kuwa ule mwili unaobadilika unaoona kwenye kioo. Aeleza mwandikaji Lynda Madaras katika The What’s Happening to My Body? Book for Girls: “Unapopitia ubalehe, uso wako wabadilika. Sehemu ya chini ya uso wako yaongezeka na uso wako wajaa zaidi.” Hilo ni kweli kwa wote wasichana na wavulana. Huenda ikachukua wakati kabla ya uso wako kuonekana umepatana vizuri.

Kwa sababu sehemu tofauti za mwili hukua kwa viwango tofauti, mikono yako na miguu yako huenda ikaonekana kuwa mirefu kwa njia ya kuaibisha. “Mikono yangu ilionekana kana kwamba inafikia sakafu,” akumbuka Christine, ambaye baadaye alikuja kuwa mtu mzima mwenye kuvutia. Mara nyingi kipindi chenye mashaka hutokea pia kabla mwili wako kuonekana hatimaye ‘umeungamanishwa na kushikamanishwa kwa msaada wa kila kiungo.’—Waefeso 4:16.

Wakuzi Wenye Kuchelewa

Hata hivyo, ubalehe waweza kustaajabisha sana. Nyakati nyingine mtu mwenye umri wa miaka 12 aweza kufikiriwa kuwa mtu wa umri wa miaka 20. Lakini kwa habari ya vijana wengine, hormoni hazionekani kufanya kazi kwa wakati unaofaa. Kijana mmoja anayeitwa Willie alalamika hivi: “Mimi ni mmoja wa watoto wafupi zaidi katika darasa letu, na ninajua jinsi mtu anavyohisi akifanyiwa mzaha.” Ukijikuta kwamba ni lazima usimame kwa vidole vya miguu ili ufikie marika wako kwa kimo, usifadhaike. Mara nyingi, inamaanisha tu kwamba mwili wako unakua kwa mwendo wa polepole kuliko miili ya wanadarasa wenzako.b

Ni kweli kwamba kuwa mfupi au kuonekana kuwa mdogo kuliko marika wako kwaweza kuwa jambo lisilopendeza. “Najua ninaonekana kama mtoto mdogo, na nachukia hilo!” alalamika Allison mwenye umri wa miaka 16. Je! waweza kuongeza mwendo wa ukuzi wako? La, lakini waweza kuusaidia. Katika Ayubu 8:11, Biblia yasema kwamba: “Je! hayo mafunjo yamea pasipo matope? Na makangaga kumea pasipo maji?” Kama vile mmea husitawi katika hali na lishe ifaayo, wewe vilevile wahitaji mapumziko ya kutosha na lishe bora. Kuendelea kujilisha vyakula visivyofaa afya ya mwili kutanyima mwili wako lishe unayohitaji kwa ukuzi unaofaa.

Mbali na utunzi wa kutumia akili wa afya, huwezi kufanya mengi kuhusu ukuzi wako wa kimwili. Lakini baada ya muda ukuzi wako wa ghafula utaanza. Kwa kweli, hata waweza kuendelea kukua baada ya marika wako kufikia kimo chao cha mwisho. “Nilipokuwa katika darasa la nane,” akumbuka kijana anayeitwa John, “nilikuwa mtoto wa pili kwa ufupi zaidi darasani, lakini kupitia kiangazi, nilikua kwa ghafula. Kufikia wakati nilipoanza darasa la tisa, nilikuwa karibu mvulana mrefu zaidi darasani.” Tunakumbushwa juu ya mithali ya kale: “Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.”—Mithali 13:12.

Bila shaka, hakuna uhakikisho kwamba utakuwa mrefu kama mchezaji wa mchezo wa vikapu wa U.S. Kama una wazazi wafupi, inaelekea zaidi kwamba utakuwa na mwili mfupi wewe mwenyewe. Hata hivyo kuwa mfupi kuliko marafiki wako kwaweza kukuletea matatizo.

Namna ya Kukabiliana kwa Mafanikio

Ingawa Mungu haoni mtu kwa umbo lake, wanadamu wenye akili kidogo hufanya hivyo mara nyingi. Uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba vijana wana mwelekeo wa kuwaona wale wanaokua polepole kuwa hawavutii na hawawezi kutimiza mambo kuliko vijana wanaoonekana kuwa wamekomaa. Hata wanaweza kuwafukuza marafiki wa zamani ambao wanaonekana kama hawapatani tena nao kwa sababu wanaonekana kuwa wachanga mno. Jambo hilo laweza kuathiri kabisa kujistahi kwako. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba muda mrefu baada ya vijana wanaokua polepole kufikia wanadarasa wenzao kimwili, hisia za kutofaa zaweza kubaki.

Waweza kukabilianaje kwa mafanikio? Vijana wengine ambao hukua baadaye waweza kujitenga sana. Lakini wengine—hasa wavulana—huwa wenye kujionyesha au wenye kujasiria sana kwa njia yenye kuchukiza katika jitihada mbaya ya kutaka watambuliwe. Lakini mienendo hiyo miwili haitakuletea marafiki wa kweli. Hatimaye watu watakupenda kwa namna ulivyo, lakini si kwa jinsi unavyofanana. Ukionyesha upendezi wa kweli kwa wengine na kusitawisha fadhili na ukarimu, watu wengi watakupenda. (Mithali 11:25; Wafilipi 2:4) Wengine wakiendelea kukufanyia mzaha au kukupuuza, jaribu kuongea tatizo lako na wazazi wako. Wanaweza kuwa na madokezo yanayokufaa.

Ukumbuke pia kwamba Mungu “huutazama moyo.” (1 Samweli 16:7) Biblia yasema kwamba Mfalme Sauli alikuwa mmoja wa watu warefu zaidi na wazuri zaidi kwa sura katika Israeli. Lakini hakufaulu akiwa mfalme na vilevile akiwa mtu. (1 Samweli 9:2) Kwa upande mwingine, mtu mmoja aliyeitwa Zakayo alikuwa “mfupi wa kimo.” Lakini alibarikiwa kwa pendeleo la kumwonyesha ukarimu Mwana wa Mungu. (Luka 19:2-5) Kwa hiyo, ni utu wa ndani ndio wa maana sana. Na kama mwili wako haukui haraka kama ambavyo ungetaka, waweza kufarijika kwa kujua kwamba hilo ni jambo la kawaida kabisa. “Kwa kila jambo kuna majira yake,” na mwili wako hatimaye utaitikia mwito wa ubalehe. (Mhubiri 3:1) Na kwa kushangaza, vijana wengi hulalamika kwamba miili yao hukua haraka mno. Hali yao itazungumziwa katika makala itakayofuata katika mfululizo huu.

[Maelezo ya Chini]

a Ona makala za “Vijana Wanauliza . . .” katika matoleo ya Amkeni! ya Desemba 8, 1990 na Januari 8, 1991.

b Wastadi wengine hupendekeza kwamba ikiwa mbalehe hajapatwa na mabadiliko yoyote ya ubalehe kufikia umri wa miaka 15, apaswa achunguzwe na daktari aangalie kama hakuna tatizo kubwa lolote la kiafya.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mara nyingi wasichana huanza ukuzi wao wa ghafula karibu miaka miwili mbele ya wavulana. Hata hivyo, wavulana wengi hufikia na hatimaye kuwapita wasichana katika kimo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki