“Mti Wenye Mafaa Zaidi kwa Binadamu”
Na mleta habari za Amkeni! katika Kenya
KWA watu wengi mnazi huwa ni mti unaonekana kuwa mzembe—ukiwa wonyesho halisi wa utulivu na starehe. Lakini kwa watu wanaoishi katika Kisiwa cha Mombasa katika pwani ya Kenya, unamaanisha mambo mengi zaidi ya hayo. Watu fulani hurejezea dubwana hilo lenye uanana kuwa “mti wa uhai.” Kwa wakazi hao wa pwani, mnazi una uwezo wenye kustaajabisha wa kuandaa umaridadi na vilevile mahitaji mengi ya msingi ya maisha ya kibinadamu.
Mnazi una matumizi mengi sana. Basi haishangazi kwamba mnazi umepata kuitwa “mti wenye mafaa mengi,” “chupa ya maziwa mlangoni pa binadamu,” na “mti wenye mafaa zaidi kwa binadamu.” Kitabu The Coconut Palm—A Monograph chaeleza hivi: “Labda mti huu hutokeza vitu vingi vya kutumiwa na binadamu kuliko mti mwingine wowote.”
Vyatengenezwa Kutoka kwa Nazi
Watu wa pwani ya Kenya wametumia mnazi kwa njia nyingi zenye akili. Kwa kielelezo, fikiria Kadii, mke wa nyumbani wa sehemu hiyo. Ameishi katika mazingira hayo ya kitropiki tangu utoto wake. “Je! nazi imekuwa na fungu kubwa nyakati zote katika nyumba yako?” twauliza.
Kadii ajibu hivi: “Naweza kukumbuka vizuri nikitumia nazi jikoni nilipokuwa msichana mchanga. Kwa sababu kifuvu chayo huwa kigumu sana na chenye kudumu sana, kilitumika vizuri kikiwa vikombe, vijiko, na pawa. Vile vifuvu vikubwa vilikuwa vikitumiwa vikiwa bakuli za supu na mikamshi. Sehemu ya elimu yetu shuleni ilikuwa ni kujifunza jinsi ya kuunda na kutengeneza vitu hivi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.”
Mume wa Kadii, Mbagah, aliyelelewa pwani vilevile, ana mengi ya kusema kuhusu matumizi ya mnazi nje ya jikoni. “Nikiwa mvulana anayekua,” akumbuka Mbagah, “niliona mti huu kuwa sehemu muhimu ya maisha.”
Kwa kielelezo, kuhusu gogo la mnazi, ambalo ni gumu na lenye nguvu, yeye asema hivi: “Twalitumia kuwa boriti, viegemezo, nguzo, mihimili, na vitu vingine vingi vya ujenzi.”
Na vipi juu ya makuti? “Katika vijiji vingi kuna wanawake wanaopata riziki kwa kusuka majani hayo na kuyatengeneza kuwa vipande vikubwa vya kuezeka nyumba vinavyofanana na vigae,” Mbagah aeleza. Hata ingawa nyumba ya-weza kuwa katikati ya jua kali ya kitropiki, wakaaji watahisi baridi kidogo na starehe ndani ya nyumba hiyo. Paa iliyoezekwa haikingi jua tu bali pia huruhusu upepo mwanana kuingia ndani ya nyumba na kuleta baridi. Ni vigumu kuwazia kama kuna aina ya paa nyingine bora zaidi ya hiyo. Makumba (makuti ya nazi yaliyosukwa) hutumika vizuri yakiwa kuta, ua, na milango.
“Tusisahau makumbi ya nazi,” Mbagah aongezea na tabasamu ya fahari. “Hayo hupatikana kwa kutundika nazi kwenye mchongoko wenye ncha kali wa ubao au chuma iliyotundikwa ardhini. Sisi huchukua nazi kwa mikono miwili, na kuisukuma kwa nguvu chini dhidi ya ule mchongoko na kuizungusha ili makumbi yaachane na nazi yenyewe.” Makumbi hutokeza usumba maridadi wenye rangi ya kidhahabu, unaoweza kutumiwa kutengeneza mikeka ya sakafu, virago, mazulia, brashi, vifagio, na hata kujazia magodoro.
“Tamu kuliko Divai”
Nazi pia ina fungu kubwa katika lishe na huliwa katika karibu kila hali yalo ya ukuzi. Dafu huwa na kinywaji safi, chenye kufaa, na chenye kujenga mwili ambacho kina ladha nzuri sana. Kinywaji hicho chaweza kuandaliwa katika chombo chacho cha asili kwa kutoboa tu shimo juu ya nazi—kinywaji chenye kufaa tu kiu ya kitropiki! Mvumbuzi wa nchi aliye mashuhuri Marco Polo anaripotiwa kuwa alisema maneno haya kuhusu kinywaji hicho: “Umajimaji huo ni safi kama maji, ni baridi na yenye ladha nzuri zaidi, na ni kitamu zaidi ya divai au kinywaji cha aina nyingine yoyote.”
Watalii husema maneno kama hayo wanapoonja kinywaji hicho cha sehemu hizo kwa mara ya kwanza. Na umajimaji huo unapomalizika, sehemu iliyovunjika ya kifuvu hicho yaweza kutumika kuchovya tunda jororo. Hilo ni jororo, tamu, na lenye kuburudisha. Ingawa utamu wa dafu ni jambo jipya kwa wageni, kwa watu wa pwani, hicho ni kinywaji cha kila siku, na hilo huthaminiwa sana wakati kuna uhaba wa maji.
Njia za Kutayarisha Nazi
Sehemu iliyo ya maana zaidi ya nazi mbivu ni tunda layo. Laweza kuliwa moja kwa moja kutoka kwa kifuvu, laweza kukunwa na kutayarishwa kwa njia tofauti-tofauti, au kukamuliwa ili kuondoa tui (maziwa ya nazi) lenye thamani.
Kadii akumbuka hivi: “Nikiwa msichana mchanga, ilikuwa ni lazima nihakikishe kwamba kulikuwa na tui nyakati zote kwa ajili ya kupika.” Tui hutumiwa kidesturi katika kuongeza ladha ya samaki, kuku, maharagwe, wali, viazi, muhogo, na mkate. Hayo pia huongezea mchuzi ladha nzuri. Lakini sisi tuna hamu ya kujua jinsi Kadii alivyokuwa akipata tui.
“Tulikuwa tukitumia mbuzi,” aeleza Kadii. Mbuzi ni kiti kidogo cha mbao chenye kimo cha sentimeta 15 kikiwa kimesimama. Kina ubapa wenye msumeno unaochomoza kutoka ndani yacho, uliotengenezwa hasa kwa ajili ya kukuna nazi kwa mikono. “Ilikuwa inafurahisha sana kwetu sisi tukiwa watoto kuketi kwenye mbuzi. Tulikuwa tukichukua nazi iliyopasuliwa mara mbili na kukuna sehemu ya ndani dhidi ya ule ubapa wenye msumeno mpaka kifuvu kitoe tunda lote la nazi. Hatua iliyofuata ilikuwa ni kuchukua nazi iliyokunwa na kuliweka katika kichujio kirefu kiitwacho kifumbu kilichotengenezwa kwa matawi ya miyaa. Kisha tulikamua tui tamu la nazi.”
Kwa kweli nazi ni tunda halisi, na lapatana kabisa na matunda mengine ya kitropiki. Viungo vya kuonja ladha vya mtu huanza kudondoka mate kwa kufikiria tu chakula cha papai lililotoka kukatwa tu, nanasi, embe, ndizi, chungwa, na tunda la pashoni yakiwa yamenyunyiziwa juu machicha ya nazi yaliyotoka tu kukunwa au hata kumwagiwa tui la nazi.
Methali moja ya kale husema hivi: “Yeye apandaye mnazi apanda . . . chakula na kinywaji, makao kwa ajili yake mwenyewe na urithi kwa watoto wake.” Kwa hiyo mnazi uonekanao kuwa mzembe kumbe si mzembe kamwe. Na ingawa waweza kubishaniwa kama ndio mti wenye mafaa zaidi kwa binadamu au la, bila shaka mnazi waandaa mambo mengi katika sehemu hiyo ya Afrika!