Maisha ya Jijini Katika Miteremko ya Vilima vya Caracas
Na mleta habari za Amkeni! katika Venezuela
CARACAS, Venezuela. Majengo makubwa ya kisasa ya ofisi yainuka juu ya magari yenye makelele, maduka yenye shughuli nyingi, na mikahawa yenye kujaa watu. Watalii wazurura-zurura barabarani wakiwa na vinyasa na kofia za kukinga jua, huku kamera zikiwaning’inia. Watu wajaa kando-kando za barabara.
Lakini kuna upande mwingine wa Caracas. Nyuma ya majengo hayo makubwa yenye rangi-rangi, yaliyojengwa kwa vyuma na vioo kuna los cerros (vile vilima), jumuiya zisizo za kawaida zilizojengwa kwenye miteremko ya vilima. Jumuiya hizo huishi katika miteremko yenye kuinuka sana izungukayo jiji pande za mashariki, magharibi, na kusini.[2] Watu wapatao milioni mbili huishi katika sehemu hizo, katika mamia ya vijiji viitwavyo barrios.
Jumuiya hizo zilikujaje kuwako? Katika 1958 serikali ilianzisha mpango wa kuwapa wakazi wa jiji wasiokuwa na kazi kiasi fulani cha fedha. Kwa hiyo watu wakaja kwa wingi katika jiji kuu ili kufaidika na maandalizi hayo. Wengi walihama mikoa kuja kutafuta manufaa za jiji—hospitali, shule, vyuo vikuu.
Jeuri ya kisiasa na mshuko wa hali ya kiuchumi katika nchi jirani pia ulifanya watu wahamie Caracas ili kutafuta kazi. Upesi sehemu tambarare ya bonde la Caracas ikajaa watu, jambo lililolazimisha watu wasonge katika maeneo ya juu ili kutafuta mahali pa kuishi. Na hivyo jumuiya hizo za miteremko ya vilima zikaanzishwa.
Safari ya Kuelekea Juu Vilimani
Twaanza safari yetu kwa kujiunga na mlolongo mrefu wa watu. Wao hawangojei basi ila wanangojea gari aina ya jip, ambalo lafaa zaidi katika kupanda mwinuko mkubwa ulioko mbele. Jip ndefu yaja, na watu wapatao 12 wang’ang’ana kuipanda. Watano waketi katika kila benchi ndefu zilizo kwenye pande za jip; wawili washiriki kiti cha mbele chenye kuthaminiwa sana. Upesi twainama ili kuingia kwenye mlango wa nyuma. Twajifinyilia katika nafasi iliyokuwa katika benchi, twakunja miguu yetu kabisa, na kujaribu kuepuka kukanyaga mfuko wa mboga wa mwanamke mmoja.
Twaanza kupanda mwinuko mkubwa. Barabara za mitaa ni nyembamba na mara nyingi zapinda-pinda. Nyakati nyingine hizo zaonekana kuwa ni kama zainuka wima. Dereva aweka muziki aupendao, na upesi miguu yagonga kwa kufuata muziki huo wa Kilatini. Kwa ghafula mtu fulani apazia dereva sauti: “¡Donde pueda!” (Popote uwezapo!) Yaonekana kuwa njia isiyo ya kawaida ya kumwambia asimame. Lakini ni bora kutegemea uamuzi wa dereva. Jip ikisimama katika mojapo sehemu zilizoinuka sana za barabara, huenda isiweze kwenda tena—angalau haitaenda mbele! Abiria wachache wenye kufujika waondoka kupitia mlango wa nyuma, baada ya kukanyaga vidole kadhaa wanapoondoka.
Upesi twajikuta nyuma ya gari linaloenda polepole na kutiririsha maji kutoka kila upande. Ni lori ya maji, ikipeleka mzigo wayo wenye thamani kwa makao ambayo hayana maji ya mfereji. Kwa kawaida watu huweka akiba ya maji katika matangi au mapipa ya mafuta yaliyokwisha kutumiwa.
Jip hiyo yasimama tena katika mojapo vituo vyayo vingi, na twang’amua kwamba ni wakati wa kushuka. Ardhi ngumu yaonekana kuwa ajabu chini ya miguu yetu, na twatua ili kuona tuko wapi.
Makao Katika Miteremko ya Vilima
Nyumba zimejengwa popote pale na kishaghala-baghala. Yaonekana kwamba vyumba vya ziada na hata orofa za ziada zaongezwa tu familia iendeleapo kukua. Makao mengine ni ya mawe ya udongo mwekundu. Lakini mengine yametengenezwa kwa mbao, mikebe iliyotandazwa, au hata vibao vya masanduku ya kupakia zikiwa bado na alama ya maneno “Upande huu juu.”
Sasa kuna ukimya kidogo kwa sababu ile jip sasa imeondoka na makelele yayo na kupotelea mbali. Mandhari ya huko yastaajabisha sana. Kule, chini kabisa, ndiko jiji la Caracas. Kwa ghafula ukimya huo waondelewa na sauti kubwa inayokwaruzika kutoka kwa kipaza sauti: “Naam, kuna vitunguu. Naam, kuna viazi, mihogo, na ndizi.” Tukigeuka, twaona kwamba lori lililokuwa limeegeshwa kwa utulivu karibu na hapo kwa ghafula lilikuwa limekuwa kitovu cha utendaji. Mvulana mmoja atumikia wateja kutoka nyuma ya lori hilo.
Kuna barrios zipatazo 500 katika Caracas.[8] Baadhi yazo zimepewa majina ya “watakatifu,” nyinginezo zimepewa majina ya tarehe za maana au za wanasiasa. Lakini majina mengine yaonyesha mapendezi ya wakazi badala ya mambo halisi. Vielelezo: El Progreso (Maendeleo), Nuevo Mundo (Ulimwengu Mpya), na El Encanto (Mchachawo).
Maisha Katika Barrio
Roho ya kusaidiana husitawi hapo. Mara nyingi, jitihada za pamoja hufanywa ili kuondoa matumizi ya dawa za kulevya au uhalifu katika barrio. Barrios nyingi zina maduka yanayouza bidhaa mbalimbali na vilevile shule, na duka la dawa, ambapo muuza dawa huwa tayari sikuzote kusaidia katika kugundua ugonjwa na kupendekeza matibabu kwa magonjwa madogo-madogo.
Lakini, maisha ni magumu hapa. Matatizo yanasimuliwa hivi na mchunguzi wa uhalifu Dakt. Elio Gómez Grillo: “Kwa wakati huu watu milioni mbili ambao hawawezi kupata mahitaji ya msingi ya maisha huishi katika jumuiya hizi. Kiwango cha uhalifu chaongezeka sana . . . Kujiua, kupigwa, kuvunja mabenki kimabavu, na wizi wa kimabavu unaotokeza mauaji wahangaisha.”[9] Uhaba wa maji na umeme ni mambo ya kawaida.
Katika vipindi vya mvua, los cerros hubadilika kabisa. Ardhi hugeuka kuwa matope, ngazi hugeuka kuwa maporomoko madogo ya maji, na takataka huelea zikiporomoka kupitia mito ambayo hufurika kandokando ya barabara. Kelele za mvua katika mabati huwa kubwa sana; mazungumzo hukatishwa ndani ya nyumba huku wakazi wakizingatia kutafuta mabakuli na ndoo za kuweka katika sehemu zinazovuja. Lakini upesi jua larudi, likikausha paa na barabara zilizoloweshwa. Vivyo hivyo, ile roho isiyoshindwa ya Wavenezuela yarudi. Maisha yaendelea kama kawaida.
Kusonga Mbele na Kupanda kwa Miguu
Safari yetu haijakwisha bado. Bado twahitaji kufikia kao la rafiki yetu. Kati ya nyumba mbili, kuna ngazi ya saruji inayoinuka sana na kupindapinda ipandapo kilima. Kuna ishara nyingi kwenye nyumba zenye kusongamana zinazoonekana kuwa zashindania nafasi: Pego Cierres (Naweka Zipu); Cortes de Pelo (Kinyozi); Se Venden Helados (Barafu-Sukari Yauzwa). Wakazi hubuni njia yoyote ile ya kujipatia riziki. Baadhi yao hupaka magari rangi, wengine hubadili mafuta ya gari, na kurekebisha magari—yote hayo yakifanywa katika barabara moja ya mitaa.
Twatua ili kupumua tufikapo juu ya ngazi, kisha twaingia katika vijia vingi vyembamba vyenye kupitana-pitana kati ya nyumba nyingi. Twatoka nje ya vijia hivyo vingi na kupepesa macho katika jua lenye kuangaza. Kao la rafiki yetu liko kando ya njia hii ya mchanga. Nyumba hazina nambari hapa—wala barua haziletwi milangoni. Manukato ya kahawa iliyotoka tu kutayarishwa yaenea kila mahali. Bila shaka mkaribishaji wetu atatukaribisha kwa kahawa iliyoandaliwa kwa vikombe vidogo sana, pamoja na arepa (aina ya mkate wa mahindi uongezwao ladha kwa vikolezo vingine mbalimbali).
Twakaribishwa
Kama tulivyotarajia, familia hiyo yatukaribisha kwa ukarimu wa desturi yao ndani ya ranchito (jina la nyumba hizo ndogo) yao sahili lakini iliyo safi. “Están en su casa” (Stareheni) ni mojapo mambo wasemayo kwanza.
Huku jua likichoma paa la mabati, twashukuru kwa ajili ya upepo mwanana upulizao kupitia madirisha yasiyo na vioo. Hata hivyo, madirisha hayo yana vyuma kwa kuwa wizi umeenea sana. Watambuapo kwamba twahisi joto jingi, wakaribishaji wetu waleta kipepea-hewa cha umeme ambacho kama ilivyo na friji na televisheni ni vitu vinavyopatikana kwa wingi. Wana sakafu ya simiti. Majirani wao wengi wana sakafu za mchanga tu.
Mume huyo, ambaye ni baba ya watoto wadogo watano, alihamia Caracas kutoka mashambani akiwa tineja akitafuta hali bora ya maisha katika jiji hilo kubwa. Alienda kuishi na kaka yake aliyekuwa ameoa, ambaye kama wengineo waliokuwa mbele yake, alitwaa tu ardhi ndogo iliyokuwa tupu juu kwenye mteremko wa kilima. Rafiki yetu alipokutana na yule ambaye angekuwa mke wake baadaye, ndugu yake alisema kwa ukarimu kwamba wangeweza kutumia ardhi ndogo iliyokuwa kando ya nyumba yake ili wajenge kao sahili. Kwa msaada wa majirani na watu wa ukoo, mume huyo na mke wake walijenga papo hapo nyumba yao ya matufali pole kwa pole.
Familia hiyo yahisi kwamba mahali hapo hapafai, lakini wamelazimika kupatumia. Wao watumia kwa njia bora zaidi kile walicho nacho. ‘Huenda siku moja tutaweza kuteremka chini zaidi ya kilima,’ wao wasema, “si Dios quiere” (ikiwa ni mapenzi ya Mungu).
Twatumia alasiri yenye kufurahisha na familia hiyo maskini lakini yenye fadhili. Mara kwa mara mazungumzo yakatizwa na watoto wadogo wanaokuja kununua peremende kwenye dirisha la mbele. Hiyo ni njia ya mke ya kusaidia kuongezea mapato ya mume wake.
Kushuka
Twataka kuondoka kabla giza halijaingia. Leo ni Ijumaa, na barrio lachangamka wakati wanaume wanarudi nyumbani wakiwa na mishahara yao. Yale maduka yauza pombe nyingi, na sauti ya muziki wa kilatini wa salsa na mdundo wa muziki wa merengue huchangia hali starehe ya mwisho-juma.
Mara tufikapo chini, twatembea kuelekea stesheni ya gari-moshi iliyoko karibu zaidi. Huko gari-moshi la chini ya ardhi lifaalo sana litatupeleka hadi jijini. Twahisi vizuri kidogo kurudi kwenye eneo tunalolijua vema zaidi. Lakini tutazamapo nyuma kwenye los cerros, sasa zikiwa ni taa nyingi zimulikazo gizani, twafurahi kwamba tuliweza kujua zaidi upande mwingine wa Caracas.