‘Jiji Lililokuwa Limejaa Watu’
TOKYO, São Paulo, Lagos, Jiji la Meksiko, na Seoul yafanana na ufafanuzi huo, ingawa nabii wa Biblia Yeremia hakusema juu ya jiji lolote kati ya majiji hayo. Alikuwa akirejezea Yerusalemu muda mfupi baada ya kuharibiwa na Wababuloni katika 607 K.W.K.—Maombolezo 1:1.
Sasa ulimwengu ukiwa na idadi ya watu ipatayo bilioni tano na nusu, si vigumu kupata majiji yaliyojaa watu.[1] Mwendo wa wazi katika nusu karne ambayo imepita umekuwa ukielekea ukubwa. Ingawa kulikuwa na majiji 7 pekee yaliyokuwa na wakazi wapatao milioni tano katika 1950, makadirio yaonyesha kwamba kufikia mwisho wa karne hii, angalau majiji 21 yatakuwa na wakazi zaidi ya milioni kumi, kutia ndani majiji 5 yaliyotajwa juu.[2]
Yalipataje Kuwa Makubwa Hivyo?
Majiji makubwa sana hufanyizwa wakati wakazi wa mashambani wahamiapo jijini kutafuta kazi na wakati wakazi wa jiji wanapohama kutoka katikati ya jiji na kwenda viungani vyalo kutafuta sehemu zenye nafasi zaidi na zenye kupendeza zaidi ambazo wao waweza kupanda gari, basi, au gari-moshi ili kwenda kazini. Upesi viunga hivyo, vikiwa pamoja na jiji lenyewe hujiunga na kufanyiza jiji kuu na viunga vyalo.[6]
Majiji fulani makubwa sana yalikuwa hivyo yakiwa yangali “matineja.” Tenochtitlán—leo twaliita Jiji la Meksiko—lilianzishwa karibu 1325. Kufikia 1519, Wahispania walipofika, tayari jiji hilo kuu la Milki ya Aztek lilikuwa na idadi ya watu ikaribiayo 300,000.[7]
Hata hivyo, kama ilivyo na watu wanaonenepa wakati wa miaka ya makamo, majiji mengine yamepanuka baada ya kuwapo kwa muda mrefu. Seoul, mahali pa Olimpiki za 1988, lilianza zamani hata kabla ya siku za Ukristo, lakini miaka yapata 50 iliyopita, idadi yalo ya watu bado ilikuwa sehemu moja kwa kumi tu ya idadi ya watu ya sasa.[8][9] Sasa hilo ni nyumbani kwa watu wapatao robo ya wakazi milioni 43 wa nchi nzima.[10]
Kama ilivyo na Seoul, jina la Tokyo vilevile lamaanisha “jiji kuu.” Kwa habari ya Tokyo, hilo hasa lamaanisha, “jiji kuu la mashariki.” Zamani likiitwa Edo, jina hilo lilibadilishwa likawa Tokyo katika 1868 wakati jiji kuu lilipohamishwa kutoka jiji la Kyoto lililokuwa upande wa magharibi zaidi. Eneo la Edo tayari lilikuwa na watu katika nyakati za kabla ya Ukristo, lakini msingi wa jiji kubwa sana la leo haukuwekwa hadi 1457, wakati shujaa wa vita mwenye nguvu sana alipojenga huko jumba kubwa la ngome. Jiji hilo lilianzishwa katika kipindi cha karne ya 17, na kufikia katikati ya miaka ya 1800 jiji hilo lilikuwa na watu zaidi ya milioni.[11] Wakati mmoja likitajwa kuwa jiji lenye ishara nyingi zaidi zenye kuwaka taa, Tokyo ni jiji la kisasa sana.[12]
Jiji jingine kubwa sana na la kisasa vivyo hivyo na lenye uzuri wa ujana ni São Paulo, Brazili. Likiwa na barabara zilizo pana sana zenye miti kandokando na majengo marefu ya kisasa, laonekana kuwa changa sana likilinganishwa na umri walo, likiwa limeanzishwa na wamishonari Wayesuiti kutoka Ureno katika 1554. Sasa, katika Januari, wakazi walo—Paulistas—wanasherehekea mwaka walo wa 440 tangu lianzishwe. São Paulo lilibaki likiwa dogo sana mpaka miaka ya 1880, wakati ambapo fedha zinazotokana na biashara mpya ya kahawa ya Brazili zilipotumika kuvutia wahamiaji kutoka Ulaya na baadaye kutoka Asia.[13]
Wareno walikuwa pia na fungu katika kusitawisha jiji moja kubwa sana katika Nigeria. Bila shaka, muda mrefu kabla Wazungu wafike katika mwisho-mwisho wa karne ya 15, eneo la Lagos lilikuwa limekaliwa na moja ya makabila yenye watu wengi zaidi katika Afrika na wenye kuishi kijumuiya zaidi katika eneo la tropiki kabla ya nyakati za ukoloni, Wayoruba. Jiji hilo lilijulikana kwa biashara ya watumwa mpaka miaka ya katikati ya 1800. Lilitwaliwa na Uingereza katika 1861, na katika 1914 lilikuja kuwa jiji kuu la ile iliyokuwa wakati huo koloni ya Uingereza.[14]
“Ukubwa Si Uzuri Tena”
Ukubwa una mafaa. Kwa kawaida, kadiri jiji lilivyo kubwa, ndivyo uwezekano wa wakazi kuishi maisha mazuri zaidi ya kijamii na kitamaduni uendeleavyo kuongezeka. Mambo ya kiuchumi pia hufanya ukubwa ufae, kwa sababu idadi kubwa ya watu hutoa fursa nyingi za biashara na uwezekano wa kupata kazi. Kama sumaku yenye nguvu sana, ufanisi wa kiuchumi wa majiji huvutia watu wanaotafuta hali bora zaidi ya maisha. Lakini wanapokosa kupata kazi na kulazimika kuishi katika mitaa ya hali ya chini, labda wakiomba-omba ili waendelee kuishi, au wanapokosa makao, kwa sababu ya ukosefu wa nyumba, wanavunjika moyo haraka kama nini na kisha uchungu wa maisha waanza![15]
Gazeti National Geographic ladai kwamba kubwa mno ni kubwa mno kwelikweli, likisema: “Miaka michache iliyopita, majiji yalionyesha ukuzi wayo kwa fahari. Ukubwa ulikuwa kitu kizuri, na majiji makubwa zaidi yalijigamba kwa sababu ya ukubwa wayo ulimwenguni. Lakini ukubwa si bora tena. Leo, kutafuta kuwa ‘jiji kubwa zaidi ulimwenguni’ ni kama kijana mwenye afya nzuri aambiwaye kwamba ana ugonjwa hatari. Waweza kutibiwa, lakini hauwezi kupuuzwa.”[17]
Haiwezekani kuzuia watu wasimiminike majijini kwa idadi kubwa isiyotakwa. Kwa hiyo majiji makubwa sana hujaribu kusuluhisha tatizo hilo kwa njia nyinginezo, labda kwa kujenga safu nyingi za majengo yafananayo na yasiyo mazuri yenye kukaliwa na watu wengi, kwa kujenga majengo marefu yanayoonekana kufikia mbinguni, au kwa kutafuta mawazo mapya kabisa. Kwa kielelezo, makampuni ya ujenzi ya Kijapani, sasa yanajaribu wazo la kujenga majengo makubwa chini ya ardhi, ambapo mamilioni ya watu waweza kufanya kazi, kununua vitu, na hata kuishi. “Jiji la chini ya ardhi si ndoto tena,” asema ofisa mmoja wa ujenzi, “twatarajia uanze hasa katika mwanzo-mwanzo wa karne ifuatayo.”[19]
Hata kihalisi, ukubwa si mzuri nyakati zote. Misiba yaweza kutokea—na hutokea—kila mahali. Lakini inapotokea katika majiji, uangamivu wa uhai na mali waweza kuwa mkubwa zaidi. Ili kutoa kielezi: Tokyo imepata misiba mingi sana, ya kiasili na ya kuletwa na binadamu. Katika 1657 watu wapatao 100,000 walikufa katika moto wenye msiba mkubwa, katika 1923 idadi iyo hiyo ya watu walikufa katika tetemeko kubwa la ardhi na moto, na yawezekana kwamba watu wengi wapatao robo ya milioni walikufa wakati wa mashambulizi ya mabomu katika mwisho wa Vita ya Ulimwengu 2.[20]
Matatizo ya ulimwengu huonwa katika majiji yao—idadi ya watu wakaao mijini na msongamano mkubwa wa magari.[21] Matatizo hayo mawili yaonyeshwa waziwazi na Jiji la Meksiko, lililotajwa wakati mmoja kuwa “mfano halisi wa msiba wa jiji.”[22] Magari zaidi ya milioni tatu husongamana barabarani. Magari hayo, pamoja na viwanda vinavyozidi jumla ya viwanda vyote vya Meksiko husababisha uchafuzi mwingi kila siku hivi kwamba kulingana na ripoti ya 1984, “kupumua tu kwakadiriwa kuwa sawa na kuvuta paketi mbili za sigareti kila siku.”[23]
Bila shaka, Jiji la Meksiko si la kipekee. Ni jiji gani la kisasa lenye viwanda lisilokuwa na matatizo yalo ya uchafuzi na msongamano wa magari? Katika Lagos, msongamano wa magari wakati kuna watu wengi zaidi huitwa “mwendo wa pole,” kwa kufaa. Jiji hilo laenea katika visiwa vinne vikuu; madaraja ya kuunganisha bara hayawezi kuwezana na hesabu ya magari yenye kuongezeka yanayoziba barabara, na kusimamisha mwendo wa magari.[24] Kitabu 5000 Days to Save the Planet chasema hivi: “Ni kama wakati umefika ambapo kutembea kungekufikisha haraka zaidi.”[25] Ni kama umefika?
Matatizo Mabaya Hata Zaidi
Majiji makubwa sana yanapatwa na matatizo makubwa hata zaidi. Bila kufikiria makao, shule zenye wanafunzi wengi kupita kiasi, na hospitali zisizo na wafanyakazi wa kutosha, kuna mambo ya kisaikolojia yahusikayo. Dakt. Paul Leyhausen, mstadi mashuhuri wa tabia ya binadamu kutoka Ujerumani, adai kwamba “hesabu kubwa ya mafadhaiko na matatizo ya kijamii husababishwa, kwa sehemu au kikamili, moja kwa moja au njia isiyo ya moja kwa moja, na wingi wa watu kupita kiasi.”[27]
Majiji makubwa sana huwanyang’anya wakazi wayo ile hisia ya kuishi kijumuiya, jambo linalofanya jiji kuwa na idadi kubwa ya watu. Miongoni mwa mamia ya majirani, mkazi wa jijini aweza kuwa mpweke, akitamani marafiki na wenzi ambao hawezi kupata mahali popote. Ile hisi ya upweke iletwayo na hali hiyo huja kuwa hatari zaidi wakati isababishapo watu wa jamii tofauti-tofauti kujigawanya katika vikundi vya jamii moja au kabila moja. Ukosefu wa usawaziko wa kiuchumi na matendo ya ubaguzi—ya kweli au ya kuwaziwa tu—yaweza kuleta msiba, kama vile Los Angeles lilivyokuja kutambua katika 1992 wakati jeuri za kijamii zilipotokeza vifo zaidi ya 50 na majeraha zaidi ya 2,000.[28]
Hatari kubwa zaidi ya maisha ya jijini ni mwelekeo walo wa kuharibu hali yetu ya kiroho. Maisha ya jijini ni ghali, na kwa hiyo wale wanaoishi humo waweza kwa urahisi kukengeushwa na mahangaiko ya maisha. Hakuna sehemu nyingine ambayo ina vitu vingi sana vinavyopatikana kwa urahisi vya kukengeusha watu wapuuze mambo halisi na yenye mafaa ya kudumu. Hakuna mahali popote ambapo fursa za vitumbuizo—vizuri, vibaya, na vichafu—ni nyingi sana hivyo. Ilikuwa ni ukosefu kama huo wa hali ya kiroho uliofanya Yerusalemu, jiji lililojaa watu ambalo Yeremia alitaja lianguke.
Ni Kama Kurekebisha Ndege Hewani
Kwa sababu ya magumu hayo makubwa sana, kitabu 5000 Days to Save the Planet chamalizia kwamba “jukumu la kuandaa kiwango cha maisha kifaacho kwa wakazi wa leo wa jijini, acha vizazi vinavyokuja, laleta matatizo yaonekanayo kama hayawezi kusuluhika.” Kutosheleza tu mahitaji ya sasa “kwaleta mzigo mkubwa sana kwa mazingira na jumuiya.” Na kwa kutazama wakati ujao, kitabu hicho chasema: “Kutarajia kuyasuluhisha wakati majiji yamefurika kwa watu mara tatu kushinda idadi ya sasa ni ndoto tu.”[30]
Hakuna shaka kwamba majiji yamo hatarini. Na majiji makubwa sana yamo katika hatari kubwa zaidi kwa sababu ya ukubwa wayo! Magonjwa yayo yamechangia kuweka ulimwengu wote mzima katika hali mahututi. Je! kuna tumaini la kupata ponyo?
Majiji makubwa sana hutuathiri. Hata majiji madogo yaweza kuwa na uvutano juu yetu, baadhi yayo kwa njia kubwa sana kushinda ukubwa wayo. Kwa vielelezo juu ya jambo hilo, fikiria majiji mengine zaidi yatakayozungumziwa katika toleo letu linalokuja.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Lagos, lajaa watu