“Jiji Limejaa Uonevu”
NABII wa Biblia Ezekieli aliporejezea jiji ambalo “limejaa uonevu,” yeye hakujua lolote juu ya matatizo yanayokumba majiji ya kisasa. (Ezekieli 9:9, An American Translation) Wala maneno yake hayakuwa njia ya kifumbo ya kutabiri matatizo hayo. Hata hivyo, yale aliyoandika yangekuwa ufafanuzi sahihi wa majiji ya karne ya 20.
Kitabu 5000 Days to Save the Planet kilisema: “Yakiwa sahili na yasiyopendeza, majiji yetu yamekuwa yenye kuchukiza kuishi ndani yayo na yenye kuchukiza kwa macho. . . . Majengo ambayo yazidi kuwa mengi katika majiji yetu yamejengwa bila kufikiria wale ambao lazima waishi na kufanya kazi ndani yayo.”
Mambo Hakika Juu ya Majiji
Majiji tisa, yaliyo katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, yamefafanuliwa na nyusipepa na magazeti kama ifuatavyo. Je! waweza kutambua kila jiji kwa jina lalo sahihi?
Jiji A, lililo katika Amerika ya Latini, lajulikana kwa wauaji walo vijana wa kulipwa na kwa mauaji mengi. Pia lajulikana kuwa makao ya kikundi cha wauzaji madawa ya kulevya.
Jiji B ndilo “jiji baya zaidi katika [United States] kwa habari ya unyang’anyi wa barabarani.” Wakati wa miezi miwili ya kwanza ya 1990, mauaji yalikuwa “yameongezeka kwa asilimia 20 zaidi ya kipindi icho hicho” mwaka mmoja kabla ya hapo.
“Kila mwaka watu milioni kadhaa huhamia majiji ya Amerika Kusini, Afrika, na Asia . . . , wakihamia kuelekea kile wanachoona kuwa bara lililoahidiwa.” Wanapokosa kupata bara hilo, wengi hulazimika kuishi katika umaskini, ikiwabidi kuomba-omba au kuiba ili kuendelea kuishi. Nusu ya raia wa Jiji C la Afrika na Jiji D la Asia—na vilevile asilimia 70 ya Jiji E la Asia—yasemekana huishi katika makao ya hali ya chini.
“Ingawa [Jiji F] ni mojawapo majiji yenye usalama zaidi katika Amerika Kaskazini, ukosefu wa kazi unaozidi, kiwango cha uhalifu kinachopanda na chuki za kikabila zimefanya raia zalo wafikirie upande usiofaa wa mafanikio. Uhalifu . . . umefanya raia wa jiji wavunjike moyo. Mashambulizi ya kingono yameongezeka kwa asilimia 19 . . . Mauaji ya kukusudia yameongezeka kwa karibu asilimia 50.”
“Kila siku watu 1,600 huhamia [Jiji G la Amerika ya Latini] . . . Ikiwa [hilo] litaendelea kukua kwa kiasi hiki watu milioni 30 wataishi humo kufikia mwisho wa karne hii. Wao watang’ang’ana katika jiji hilo kwa mwendo wa polepole sana katikati ya magari milioni 11, yaliyosongamana katika milolongo ya magari kwa saa nyingi kwa wakati mmoja . . . Uchafuzi wa hewa . . . ni mkubwa zaidi ya kiasi kinachokubaliwa. . . . Asilimia 40 ya wakazi wote huugua ugonjwa wa mapafu. . . . Wakati wa saa ambazo kuna magari mengi, kiasi cha kelele jijini hupanda hadi kati ya desibeli 90 na 120; desibeli 70 huonwa kuwa isiyovumilika.”
“Kila siku tani 20 za kinyesi cha mbwa hukusanywa kutoka kwenye barabara na vijia vya [Jiji H la Ulaya]. . . . Zaidi ya gharama na udhia, jambo baya hata zaidi limegunduliwa. Kinyesi cha mbwa huwa chanzo cha maradhi yanayosababishwa na kiini Toxocara canis. Nusu ya sehemu za kuchezea za watoto na visanduku vyao vya mchanga vya [jiji hilo] zilikuwa zimeambukizwa na mayai madogo mno yenye kukinza sana ya kiini hicho, ambayo huingizwa nyumbani kwa nyayo za viatu na kwa mafumba ya wanyama-vipenzi wa nyumbani. . . . Uchovu, maumivu ya tumbo, mizio, matatizo ya moyo na arteri ni viishara vya mapema vya maradhi hayo.”
“Ingawa [Jiji I la Asia] limekumbwa na matatizo yote ya jiji lililositawi kupita kiasi katika nchi ambayo haijasitawi—umaskini, uhalifu, uchafuzi—limeanza kujiimarisha kuwa mojawapo majiji makuu ya karne ya 21.”
Hali Zisizo za Kawaida au Zilizo za Kawaida?
Je! uliweza kutambua majiji hayo kwa majina yayo yafaayo? Labda sivyo, kwa sababu matatizo yaliyotajwa hayapatikani katika jiji moja pekee. Badala ya hivyo, hayo ni ishara ya hali mbaya katika karibu kila jiji la ukubwa wowote ule katika ulimwengu wote mzima.
Jiji A, kulingana na gazeti la kila siku la Ujerumani Süddeutsche Zeitung ni Medellín, Kolombia. Hesabu ya mauaji ya kukusudia ilishuka kutoka 7,081 katika 1991 hadi 6,622 “tu” katika 1992. Na bado, gazeti la kila siku la Kolombia El Tiempo, liliripoti kwamba katika mwongo uliopita, karibu watu 45,000 wamekufa kutokana na jeuri. Hivyo sasa vikundi mbalimbali vya kijamii vyajaribu sana kumaliza vitendo hivyo jijini na kuboresha sifa yalo.
Labda si ajabu kwa watu ambao wamezuru Jiji la New York katika miaka ya karibuni kwamba The New York Times lililitambulisha kuwa Jiji B, na bila shaka hilo si ajabu kwa raia zalo.
Tarakimu zilizotolewa na gazeti la Ujerumani Der Spiegel kuhusu idadi ya watu wanaoishi katika hali za umaskini katika Nairobi, Kenya (C), Manila, Ufilipino (D), na Calcutta, India (E) zaonyesha kwamba watu wengi zaidi wamesongamana katika makao yasiyofaa kuishi katika majiji hayo matatu pekee kuliko wale waishio katika nchi nzima-nzima za Ulaya zilizo tajiri kama vile Denmarki au Uswisi.
Jiji F—Toronto, Kanada—lilifafanuliwa katika 1991 na gazeti Time katika makala iliyokuwa wazi zaidi ya ile iliyochapwa miaka mitatu kabla ya hapo. Ile ripoti ya kwanza, yenye kichwa “Hatimaye, Jiji Litendalo Kazi,” ilisifu jiji “linalovutia karibu kila mtu.” Ilimnukuu mgeni kuwa alisema: “Mahali hapa paweza kunifanya niamini kwamba majiji yastahili tena.” Yasikitisha kwamba, yaonekana sasa “jiji litendalo kazi” lapatwa na matatizo yaleyale yanayokumba majiji mengine yanayozorota.
Ingawa lilisema juu ya Jiji G kuwa “mojawapo majiji yenye uzuri na yenye mtindo zaidi katika mabara ya Amerika, na mojawapo jiji la hali ya juu sana,” gazeti Time hata hivyo lakubali kwamba hilo ni “Jiji la Meksiko la matajiri, bila shaka, na la watalii.” Wakati uo huo, kulingana na World Press Review, watu maskini husongamana “katika mojawapo vijiji vya hali ya chini 500 vya jiji hilo kuu” katika makao “yaliyojengwa kwa takataka za viwanda, katoni, pande za magari mabovu, na vifaa vya ujenzi vilivyoibwa.”
Jiji H limetambulishwa na gazeti la kila juma la Ufaransa L’Express kuwa Paris, ambalo, kulingana na The New Encyclopædia Britannica, “kwa mamia na mamia ya miaka, kwa utaratibu usiopata kuelezwa kamwe kwa mafanikio, . . . limetokeza uvutio usiopuuzika kwa mamilioni ulimwenguni pote.” Hata hivyo, kwa sababu ya matatizo makubwa, uvutio fulani wa “Paris Yenye Usitawi” umefifia.
Kuhusu Jiji I, Time lasema: “Wakati mmoja likionwa na Magharibi kimahaba kuwa jiji kuu la ile iliyokuwa Siam, lililo tulivu, na la kindoto, ‘Venice la Mashariki,’ jiji la leo la malaika na mahekalu ya dhahabu lisilotabirika ndilo jiji lililositawi karibuni zaidi la Asia.” Hata malaika walo na mahekalu yalo yameshindwa kuzuia Bangkok, Thailand, lisiwe, angalau kwa wakati fulani, “jiji kuu la ulimwengu la biashara ya umalaya.”
Kutazama Majiji kwa Ukaribu Zaidi
Mwongo mmoja uliopita mwandikaji habari mmoja alisema kwamba ingawa majiji makubwa yaonekana kuwa “yakishiriki magumu yaleyale, kila moja yalo lina jambo la kipekee, na hivyo lina njia ya pekee ya kujitahidi ili kuendelea kuwapo.” Katika 1994, majiji yangali yakijitahidi, kila moja katika njia yalo yenyewe.
Si kila mtu anayefikiri jitihada ya kuendelea kuwapo imeshindwa. Kwa kielelezo, aliyekuwa meya wa Toronto, alionyesha hali ya kutazamia mema aliposema: “Sifikiri jiji linatokomea mbali. Linakabili magumu, lakini nafikiri twaweza kusuluhisha tatizo hilo.” Ni kweli, majiji fulani yametatua, au angalau yakaondoa, baadhi ya matatizo yayo. Lakini hilo lilitaka zaidi tu ya kuwa na matazamio mema.
Januari uliopita mwandikaji habari Eugene Linden aliandika hivi: “Wakati ujao wa ulimwengu umefungamanishwa na wakati ujao wa majiji yao.” Vyovyote iwavyo, majiji yameufanyiza ulimwengu wetu, na yaendelea kufanya hivyo. Pia, yawe ni ya kale au ni ya kisasa, yametuathiri kibinafsi—labda zaidi ya vile huenda tukadhani. Ndiyo sababu kuendelea kwayo kuwapo kumefungamanishwa kwa ukaribu na kuendelea kwetu kuwapo.
Basi, kutazama majiji kwa ukaribu zaidi si kwa kusudi la kuongeza ujuzi wa ujumla tu. La maana zaidi, kutatutahadharisha juu ya hali ya mashaka ambayo ulimwengu wajipata sasa ndani yayo. Kwa hiyo acheni tuanze “Kutazama Majiji kwa Ukaribu Zaidi.” Twatumaini mfululizo huu wa sehemu sita wa Amkeni! utapendeza, ujenge, na kutia moyo wasomaji wetu. Kujapokuwa matatizo makubwa ya ulimwengu—yaliyo dhahiri sana katika jitihada ya majiji yetu kuendelea kuwapo—bado kuna tumaini!
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Wakati ujao wa ulimwengu umefungamanishwa na wakati ujao wa majiji yao.”—Mwandikaji Eugene Linden
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kusafiri kutoka jiji moja hadi jingine kwaweza kuwa rahisi, lakini kusuluhisha matatizo yayo si rahisi