“Kutalii Majiji Yote”
ALIPOKUWA duniani Kristo Yesu ‘alianza kutalii majiji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao na kuhubiri habari njema ya ufalme.’ (Mathayo 9:35, New World Translation) Wale wanaotamani kufuata katika hatua zake walitakwa vilevile wahubiri katika majiji ya ulimwengu. Humo wangekabili matatizo yaliyo kawaida ya majiji na iwabidi kushindana nayo.
Utalii wa kihistoria wa majiji waonyesha nyakati mbaya na nzuri za maelfu ya miaka ya kuwapo kwa binadamu, shangwe na maumivu ya jitihada za binadamu ili kupata furaha. Kutazama majiji kwa unyoofu hukazia ndani yetu uhakika wa kwamba jamii nzima ya kibinadamu ni familia moja tu, inayokabili matatizo yaleyale. Leo hakupaswi kuwa na msingi wowote wa kuwa na kiburi cha kitaifa au chuki ya kikabila.
Kwa kusikitisha, watu wengi hawajui mengi juu ya majiji, hata mahali yalipo. Wakati wanafunzi wa chuo kikuu cha U.S. walipoulizwa katika miaka ya katikati ya 1980 waonyeshe mahali majiji fulani yalipo, baadhi yao walionyesha Dublin (Ailandi) kuwa katika United States na Lima (Peru) kuwa katika Italia.
Mtihani uliofanywa miaka michache kabla ya hapo katika chuo kikuu kingine ulifunua kwamba karibu nusu ya wanafunzi walishindwa kuonyesha mahali London lipo katika ramani ya ulimwengu. Wengine waliliweka katika Aisilandi, wengine katika Kontinenti ya Ulaya. Profesa aliyetayarisha mtihani huo aliomboleza kwamba asilimia 42 ya wanafunzi “walishindwa” kabisa kupata London. Jambo linaloaibisha hata zaidi ni kwamba, asilimia 8 “walishindwa” kupata jiji la Amerika ambamo mtihani huo ulikuwa ukifanywa!
Lakini yaonekana si Waamerika tu walio dhaifu katika ujuzi wa kijiografia. Mwishoni mwa miaka ya 1980, mtihani wa wanafunzi katika mataifa kumi ulionyesha kwamba Waswedeni hufanya bora zaidi na Waamerika hupata nafasi ya sita. Chuo Kikuu cha Sayansi cha ile iliyokuwa Muungano wa Sovieti kilipata kwamba asilimia 13 ya wanafunzi Wasovieti waliochunguzwa walishindwa kuonyesha hata mahali ambapo nchi yao wenyewe ipo katika ramani ya ulimwengu. Mshiriki wa chuo kikuu Vladimir Andriyenkov alisema kwa aibu: “Matokeo hayaaminiki.”
Vipi wewe? Ujuzi wako wa jiografia kwa ujumla na hasa wa majiji ni mzuri kadiri gani? Vipi ukijitahini kwa kutumia mtihani ulio kwenye ukurasa 10? Waweza kujifunza mambo fulani ya kupendeza kwa “Kutazama Majiji kwa Ukaribu Zaidi.”
Katika makala ifuatayo ya Amkeni!, tutatazama kwa ukaribu zaidi majiji matano. Hayo ni aina ya majiji ya kipekee ambayo kwa maelfu ya miaka hayakujulikana kabisa. Lakini kufikia mwisho wa karne hii, yakadiriwa kwamba kutakuwa na angalau 20 ya aina yayo. Zaidi ya nusu ya majiji hayo yatakuwa katika Asia. Hilo laweza kuwa jiji la aina gani?
[Sanduku katika ukurasa wa 10, 11]
Je! Waweza Kutambua Jiji Lenyewe?
Linganisha maelezo yafuatayo na jiji lifaalo.
1. Jiji kuu lililoinuka zaidi ya mengineyo ulimwenguni.
2. Jiji kubwa zaidi katika nchi yenye watu wengi zaidi ulimwenguni.
3. Ingawa halitumiwi sana, jina lalo rasmi lina maneno 27, sehemu ya kwanza yalo ikiwa na maana ileile ya Los Angeles; limo ndani ya sehemu ikuzwayo mchele. Lina mahekalu ya Kibuddha zaidi ya 400.
4. Lina idadi ya watu ambayo—isipokuwa majiji mengine manne—iko juu mara mbili zaidi ya jiji jingine lolote ulimwenguni.
5. Lilipoteza karibu raia robo milioni katika msiba wa 1976.
6. Jiji hili lilikuwa na fungu la maana katika mvuvumko wa viwanda, likiwa kitovu cha eneo la ufumaji la taifa lalo.
7. Wakati mmoja likionwa kuwa mojawapo majiji ya Ulaya yenye uchafu zaidi, leo jiji hilo ni mashuhuri ulimwenguni kwa ajili ya marashi yaitwayo kwa jina lalo.
8. Karibu lugha 60 husemwa katika jiji hili la bandari la Asia. Lilikuwa jiji kuu la nchi yalo kuanzia 1833 hadi 1912.
9. Jiji kuu lililofanyizwa ili kutosheleza uhitaji, lililopangwa kwa muda mrefu, lilikamilika katika 1960.
10. Limo mwishoni mwa hori yenye urefu wa kilometa 100, kwa mweneo ni mojawapo majiji makubwa zaidi ulimwenguni.
11. Likiwa karibu liharibiwe kabisa na tetemeko la dunia katika 1755, lina hali ya maisha ya chini zaidi ya jiji kuu jinginelo katika Jumuiya ya Ulaya.
12. Lilianzishwa rasmi kufikia 1873, wakati jumuiya katika pande zinazokabiliana za Mto Danube zilipoungana chini ya jina moja.
13. Wavumbuzi Wareno walikosea kiingilio cha ghuba lalo kuwa mwisho wa mto, hivyo wakilipa jina linaloitwa sasa.
14. Likianzishwa katika 1788 likiwa eneo la gereza, hilo ni mojawapo jiji la kusini zaidi la ukubwa walo ulimwenguni.
15. Likiwa na vyanzo imara vya kidini, jiji hili lilikuwa mashuhuri kwa ajili ya uasi usio wa kawaida wa kutumbukiza majani-chai baharini.
16. Katika 1850, Mfalme Kamehameha 3 alilitangaza kuwa jiji kuu la ufalme wake; jina lalo lamaanisha “Ghuba Iliyolindwa,” na hali-hewa yayo ya baridi-baridi mwakani hulifanya lipendwe na watalii.
17. Nyakati nyingine likiitwa jiji lenye upepo mwingi, wakati mmoja lilikuwa karibu kuharibiwa kwa moto; leo lina jengo refu zaidi ulimwenguni.
18. Kabla ya 1966, liliitwa Léopoldville.
19. Likiwa la kale kama yule mtawala wa Ugiriki aliye mashuhuri zaidi, jiji hili lakumbukwa na wanafunzi wa Biblia kuwa mahali ambapo tafsiri mashuhuri ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania ilifanywa.
20. Ukuzi walo wa haraka ulitokana na kupatikana kwa dhahabu viungani, na ni la kipekee katika maana ya kwamba ndilo jiji pekee la ukubwa walo ulimwenguni lisilo kwenye pwani au ufuo wa ziwa au mto.
Alexandria, Misri
Bangkok, Thailand
Boston, U.S.A.
Brasília, Brazili
Budapest, Hungari
Calcutta, India
Chicago, U.S.A.
Cologne, Ujerumani
Hong Kong
Honolulu, Hawaii, U.S.A.
Johannesburg, Afrika Kusini
Kinshasa, Zaire
La Paz, Bolivia
Lisbon, Ureno
Manchester, Uingereza
Oslo, Norwei
Rio de Janeiro, Brazili
Shanghai, Uchina
Sydney, Australia
Tangshan, Uchina
[Sanduku katika ukurasa wa 11, 12]
Majibu:
1. La Paz, lililoko kati ya meta 3,250 na 4,100 juu ya usawa wa bahari, lilianzishwa na Wahispania katika 1548.
2. “Shanghai” lamaanisha “Juu ya Bahari,” na pamoja na kuwa mojawapo bandari kubwa zaidi ulimwenguni, ni kitovu cha Uchina cha elimu ya juu na utafiti wa kisayansi.
3. Sehemu ya kwanza ya jina rasmi la Bangkok ni Krung Thep, linalomaanisha “Jiji la Malaika”; katika Kihispania, “Los Angeles” lamaanisha “wale malaika.” Ingawa Bangkok limesitawisha barabara zalo, mifereji yalo mingi iliyo mashuhuri imefunikwa ili kutengeneza barabara.
4. Hong Kong, lenye watu 96,000 kwa kila kilometa ya mraba, lafuatwa na Lagos, Naijeria (55,000); Dacca, Bangladesh (53,000); Djakarta, Indonesia (50,000); na Bombay, India (49,000).
5. Katika 1976, Uchina ilipatwa na mojawapo matetemeko ya dunia mabaya zaidi katika historia ya kisasa, yenye kipimo cha Richter cha 7.8. Tangshan lilikuwa karibu kufanywa tambarare; watu wapatao 240,000 waliuawa.
6. Manchester, lililoko kilometa 240 kaskazini mwa London, lilikuwa kitovu cha kibiashara kwa mwendo wa kasi sana hivi kwamba kati ya mwaka 1821 na 1831, idadi ya watu walo ilikua kwa asilimia 45.
7. Mwanzoni mwa karne ya 19, Cologne lilijulikana kuwa mojawapo majiji machafu zaidi ulimwenguni—Calcutta, Constantinople, na Cologne—sababu iliyofanya askari-jeshi wa Ufaransa waliokuwa humo “wafunike nyuso zao kwa vitambaa vilivyoloweshwa kwa Eau de Cologne (marashi) ili kukinza harufu ya mkojo iliyoenea jijini.”—Kölner Stadt-Anzeiger.
8. Calcutta ni jiji la tatu la India kwa ukubwa na mahali palo pa kuwa jiji kuu palichukuliwa na New Delhi.
9. Likipendekezwa katika 1789 na kukubaliwa katika Katiba ya 1891, wazo la kuwa na jiji kuu katika bara la Brazili lilikuwa halisi katika 1960 kwa kuanzishwa kwa Brasília. Ujenzi walo wa kuanzia mwanzo ulitoa fursa isiyo ya kawaida ya kutimiza kikamili “muundo wa jiji kamili lenye utaratibu kwa habari ya jinsi lilivyofanyizwa, ufundi, na makazi ya kibinadamu.”—Encyclopædia Britannica.
10. Oslo, jiji kuu la Norwei, limo kwenye eneo la kilometa za mraba 453, sehemu kubwa yalo ikiwa ni vilima vyenye miti na maziwa.
11. Makanisa yalijaa asubuhi ya Novemba 1, 1755, wakati wa kusherehekea Siku ya Watakatifu Wote, wakati Lisbon lilipoharibiwa na mojapo matetemeko ya dunia yaliyo makubwa zaidi yaliyopata kurekodiwa, lililoua karibu watu 30,000.
12. Katika 1873 mji wa Pest, ulioko upande wa mashariki wa Mto Danube, na Buda, pamoja na Óbuda na Kisiwa Margaret, kilichoko upande wa magharibi, ziliungana kuwa Budapest, mojawapo majiji ya Ulaya yenye kuvutia sana, wakati mmoja likiitwa Malkia wa Danube.
13. Maneno ya Kireno kusema “mto” na “Januari”—wavumbuzi waliwasili mnamo Januari 1, 1502—yaliunganishwa kufanyiza jina Rio de Janeiro.
14. Katika Januari 1788 karibu wafungwa 750 waliwasili kutoka Uingereza kuwa msingi wa eneo la gereza; leo Sydney ni jiji la kale zaidi na kubwa zaidi la Australia.
15. Kwa karibu karne tatu, ni majiji machache yaliyoathiri maisha katika United States zaidi ya vile Boston lilivyoyaathiri, lilianzishwa na Wapuriti waliotoroka Ulaya kwa sababu ya mnyanyaso wa kidini. Katika 1773 raia walo walisaidia kuanzisha Mapinduzi ya Amerika ambapo, wakijifanya kuwa Wahindi wa Amerika, walitupa shehena tatu za chai katika bandari ya Boston wakiteta juu ya kulipa kodi kwa Uingereza bila kuwakilishwa serikalini.
16. Mwanzoni likiwa msingi wa wafanyabiashara wa sandali na wavua nyangumi, likifuatiwa kukaliwa na Warusi, Waingereza, na Wafaransa, Honolulu lilirudishwa kwa Mfalme Kamehameha 3. Katika 1850 alilitangaza kuwa jiji kuu la ufalme wake. Hawaii lilikuwa eneo la U.S. katika 1900 na kupata kuwa taifa katika 1959.
17. Watu fulani huita Chicago jiji la kawaida la U.S., likionyesha mambo mazuri na mabaya ya nchi hiyo. Sehemu ya kati ya jiji hilo iliharibiwa na moto katika 1871, ikisemekana kwamba ng’ombe wa Bi. O’Leary aligonga taa iliyowashwa zizini. Watu wapatao 250 walikufa, na 90,000 wakaachwa bila makao. Jengo la Sears Tower la Chicago, likiwa na urefu wa meta 443, ndilo jengo refu zaidi ulimwenguni.
18. Katika 1960, Léopoldville, lililoitwa kwa jina la mfalme Leopold 2 wa Ubelgiji, lilikuwa jiji kuu la Jamhuri ya Kongo baada ya kumalizika kwa Kongo ya Ubelgiji. Katika 1971 jina la nchi hiyo lilibadilishwa kuwa Zaire; katika 1966 jiji kuu liliitwa Kinshasa.
19. Aleksandria lilipata jina lalo kutoka kwa lile la Aleksanda Mkuu, aliyeamuru lijengwe katika 332 K.W.K. Miaka iliyopungua mia moja baadaye, wakazi Wayahudi—labda katika utawala wa Ptolemy 2 Philadelphus (285-246 K.W.K.)—walianza kutafsiri Maandiko ya Kiebrania katika Kigiriki ili kutokeza Septuagint.
20. Johannesburg, ambalo halimo pwani, wala penye ziwa, wala penye mto, lawia cheo chalo cha kuwa jiji kubwa kwa kule kupatikana kwa dhahabu katika 1886. Lilikua kutoka idadi ya watu wapatao 2,000 katika 1887 hadi 120,000 kufikia 1899 na lina zaidi ya milioni 1.7 leo.
[Ramani katika ukurasa wa 8, 9]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
[Picha katika ukurasa wa 8]
Rio de Janeiro, Brazili
[Picha katika ukurasa wa 9]
Bangkok, Thailand
[Hisani]
Shirika la Utalii la Thailand
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kushoto: Sydney, Australia
Chini: La Paz, Bolivia
[Picha katika ukurasa wa 11]
Shanghai, Uchina
[Picha katika ukurasa wa 12]
Kushoto: Honolulu, Hawaii
Kulia: Hong Kong