Harakati ya Muhula Mpya Ipendwayo na Wengi
TWAISHI katika muhula wa kukata maneno. Kanuni za kiadili na mitindo-maisha hutiliwa shaka daima. Mchanganyiko usiodumu wa dini na siasa hutusukuma kwenye shida moja hadi nyingine. Sayansi na ufundi hazijaleta suluhisho la daima kwa matatizo ya ainabinadamu. Wengi husadiki kwamba hali hiyo haiwezi kusuluhishwa kusipoanzishwa mfumo mpya kabisa wa ulimwengu.
Lakini muhula wa jinsi hiyo utakujaje? Je! ni kwa hatua ya Mungu kuingilia mambo? Ikiwa ndivyo, je! ni lazima tuendelee kungoja? Au sisi wenyewe twaweza kurekebisha mambo? Je! twaweza kuuleta muhula mpya ambao wahitajiwa sana? Mamilioni ya watu kutoka kila namna ya maisha ulimwenguni pote huamini kwamba wao waweza kushiriki utendaji wa kuleta muhula mpya wa amani na udugu. Wao ni wa ile harakati ya Muhula Mpya yenye kutaka mapinduzi makubwa, nao wataka wewe ujiunge nao!
Harakati ya Duniani Pote
Je! wewe umesikia juu ya ile harakati ya Muhula Mpya? Katika nchi nyingi mtajo “Muhula Mpya” umetumiwa hivihivi tu kuhusu namna fulani za fasihi, muziki, na usanii upendwao na wengi. Ho, hata kuna mikahawa ya Muhula Mpya! Majogoo wa michezo na miamba ya kuigiza sinema wa Hollywood huendeleza harakati hiyo. Washirika hufanya makusanyiko na maonyesho ya kawaida. Mtajo “Muhula Mpya” umehusianishwa pia na bidhaa za wanunuzi, kama marashi, virembeshi, vitamini, na vitunza-afya. Vitabu vya Muhula Mpya huuzwa mamilioni kwa mamilioni. Maduka fulani yana sehemu iliyotengwa kwa ajili yavyo. Vingi vya vitabu hivyo vina uvutano imara wa kidini juu ya wasomaji.
Katika kitabu chake The Cosmic Self—A Penetrating Look at Today’s New Age Movements, mtungaji wa vitabu Ted Peters arejezea hiyo harakati kuwa “kilinganisho cha kombora la haidrojeni la kidini ambalo kwa miongo mitatu sasa limeendelea kulipuka.” Aongezea kwamba “manabii wa muhula mpya wanafanya waongofu; na mafundisho yao yanafuatwa . . . na Waprotestanti, Wakatoliki wa Roma, Wayahudi, wasioamini kuwapo kwa Mungu, na pia idadi inayoongezeka ya Wabuddha na Wahindu katika Amerika ya Kaskazini.”[9]
The Times la London laripoti kwamba “Imani ya Muhula-Mpya . . . labda sasa ndiyo imani yenye kukua kwa haraka zaidi sana Magharibi. Yakadiriwa kwamba karibuni asilimia 25 ya Waamerika watakiri kuikubali Imani ya Muhula Mpya kwa kadiri fulani.”[10] Gazeti la Uswisi Fundamentum lilionelea kwamba, katika Uholanzi, karibu wanatheolojia mia moja walikuwa wakikutana kwa kawaida “kuzungumza jinsi fikira ya Muhula Mpya yaweza kuingizwa katika maisha ya kanisa na pia katika mahubiri.”[11] Gazeti jingine latangaza kwamba “nchi za ulimwenguni pote zina maoni tofauti juu ya Muhula Mpya, lakini uvutio ni wa ulimwenguni pote.”[12]
Mashirika ya kibiashara yametumia mamilioni ya dola kwa washauri wa Muhula Mpya na kuandikisha wafanyakazi wao katika programu za Muhula Mpya. Kichapo San Francisco Chronicle charipoti kwamba “fikira ya Muhula Mpya imeenea katika taasisi za kibiashara zilizo kuu Amerika.” Gazeti hilo laongeza kwamba uchunguzi mmoja wa kampuni 500 ulifunua kwamba zaidi ya asilimia 50 zilihusika kwa njia fulani na fikira ya Muhula Mpya.[13]
Lakini hilo elekeo la Muhula Mpya ni nini, na lilitokeaje? Je! kweli litaleta amani na upatano duniani? Hilo hufundisha nini, na lakuathirije wewe?