Ile Harakati ya Muhula Mpya Ni Nini?
HIYO si tengenezo, na bado mamia ya matengenezo huendeleza mafundisho yayo. Haina uongozi wa mahali fulani hususa, lakini labda ina maelfu ya wanafalsafa na walimu. Haina kitabu fulani rasmi cha kanuni za imani na itikadi, na bado wafuasi waweza kukuza itikadi yao katika karibu kila maktaba katika ulimwengu wote. Haina mungu mwenye utu wa kuabudiwa, na bado mara nyingi huendeleza wazo la mungu awezaye kupatikana popote pale.
Hiyo ni nini? Ni ile harakati ya Muhula Mpya: mchanganyiko mlegevu wa mawazo ya kidini, kitamaduni, kijamii, kisiasa, na kisayansi, uliounganishwa na kuvutiwa na umafumbo wa siri za Mashariki, mambo yapitayo yale ya kibinadamu, mafumbo ya kishetani, na hata aina fulani za saikolojia ya ki-siku-hizi. Mchanganyiko huo watia ndani kuamini unajimu, kuzaliwa upya katika umbo tofauti, maisha ya ulimwengu wa nje, mageuzi, na maisha baada ya kifo. Kuhangaikia mazingira na afya ni mambo makuu pia yanayohusika.
Yeyote aweza kujiunga na harakati hiyo. Hakuna desturi rasmi ya kuingizwa humo wala ubatizo. Wala watu hawalazimiki kuacha mahusiano yao ya kidini ili wawe wa harakati hiyo. Kwa upande mwingine, wengi huchukizwa kutambulishwa pamoja na hicho kibandiko cha “Muhula Mpya” eti kwa sababu tu wao huamini baadhi ya mawazo yafuatwayo na harakati ya Muhula Mpya au hufurahia baadhi ya ule uitwao usanii au muziki wa Muhula Mpya.
Ni mara haba wafuasi waliojitoa kujitambulisha kuwa Wana-Muhula-Mpya. Kwa kweli, usemi “Muhula Mpya” hutumiwa sana-sana na vyombo vya habari. Siku hizi, vitabu, maduka, warsha, na programu za Muhula Mpya mara nyingi huepuka mtajo huo. Jarida Library Journal laeleza kwamba “utangazaji mwingi mno wa vyombo vya habari mwishoni mwa miaka ya 1980 ulikuwa na matokeo mabaya juu ya itikadi na njia za kutiliwa shaka zinazohusika na falsafa ya Muhula Mpya (vitu visivyotambulikana vyenye kuruka angani, uwasiliani-roho, matufe maangavu ya uaguzi, n.k.); hii yaonekana katika jambo la kwamba mashirika mashuhuri ya uchapishaji wa vitabu . . . na hata wachapishaji wa habari za Muhula Mpya wanazidi kuutupilia mbali mtajo Muhula Mpya.”[4] Hivyo, huenda watu wengi wakawa chini ya uvutano wa mawazo ya Muhula Mpya bila hata kung’amua hivyo.
Ni Jambo Gani Jipya Kuhusiana Nao?
Harakati ya Muhula Mpya yafikiriwa na wengi kuwa ajabu ya ki-siku-hizi. Kulingana na Profesa Carl Raschke wa Chuo Kikuu cha Denver, njia ya kufikiri ya Muhula Mpya hasa ni “baki la ile tabia ya Miaka ya Sitini ya kuupinga utamaduni.”[5] Wachanganuzi wengine pia waelekeza kwenye miaka ya 1960, iliyokuwa na mahipi wenye kutafuta uhuru na kweli, kuonyesha kwamba ndiyo iliyokuwa mwanzo wa harakati ya Muhula Mpya. Wengi waliokuwa mahipi, sasa wakiwa katika miaka yao ya 40 na 50, wangali wakitafuta kweli yenye kuwaponyoka. Lakini sasa utafutaji wao haupuuzwi kuwa ni msisimuko wa matineja usio wa kiakili. Wengi wao ni wataalamu katika nyanja zenye kusifika za ujuzi, ni watendaji kisiasa, na sasa huonwa kuwa washirika wenye akili nzuri katika jumuiya.
Wakati wa miaka ya 1970 na 1980, walitumia nguvu zao za kiakili na kifedha kuendeleza utafutaji wao. Matokeo? Mchanganyiko wao wa itikadi umepokea ukubali na staha mahali pengi. Na vyombo vya habari viliweza kufuatana nao haraka, tokeo likawa ni kufahamisha watu juu ya falsafa ya Muhula Mpya.
Kwa kweli, mambo mapya ni machache sana kuhusu itikadi za Muhula Mpya. Kwa kielelezo, falsafa yao ina msingi wa umafumbo wa siri za Mashariki, ambayo imekuwako maelfu ya miaka. Fikiria mawazo machache tu ya Muhula Mpya.
Tumaini la Muhula Mpya
Mwaka 2000 ukiwa karibu sana, wazo la kupata wakati mzuri zaidi, mileani nzuri zaidi, linazidi kupendwa na wengi. Itikadi kubwa moja ni kwamba jamii ya ki-siku-hizi kama tuijuavyo itaondolewa kuwe na jamii ya Utopia.a Kulingana na walimu wa Muhula Mpya, hilo litatimizwa kwa kubadili kabisa ile fikira ya kawaida kwa njia ya ujuzi wa kifumbo ambao umekuwa ukifichika au kupuuzwa mpaka miaka ya majuzi. Wao husema kwamba muhula mpya huo wenye upatano utafungulia kwa wingi majaliwa ya uwezo wa kibinadamu na kuleta amani ya kiroho ulimwenguni pote.
Tumaini hilo laelekea kuwa hasa na msingi wa matabiri ya wanajimu waelekezao kwenye siku yetu kuwa ndiyo ukingo kati ya muhula unaopita wa Samaki (Pisces) na muhula unaokuja wa Mbebamaji (au Ndoo [Aquarius]). Watetezi wa nadharia hiyo hudai kwamba ishara hiyo ya nyota ya utabiri ya Samaki imekuwa na tokeo baya juu ya ainabinadamu kwa karibu miaka 2,000. Wao husema Jumuiya ya Wakristo ndiyo mlaumiwa mkuu katika kufanyika kwa jamii ifuatiayo vitu vya kimwili na yenye kubaki nyuma kimaendeleo. Jumuiya ya Wakristo hulaumiwa juu ya kuzuia maendeleo ya kweli. Lakini kweli leo yasemwa kuwa yapatikana katika mafumbo ya kishetani na itaonyeshwa wazi wakati wa ule muhula unaokaribia sana wa Mbebamaji (Ndoo), ule muhula wa kuangaziwa nuru kiroho, ule muhula mpya.[6]
Wana-Muhula-Mpya wamegawanyika maoni juu ya kama jamii mpya hiyo itatokezwa na nguvu fulani za nje ya dunia hii zisizo na utu au na jitihada ya kibinadamu. Nadharia moja hudai kwamba “jamii yenye kubadilika ghafula ya Ainabinadamu wa Muhula Mpya, ambayo yatokana na mbegu za urithi zilizopandwa na wakale walioangaziwa nuru miaka 3,500 iliyopita, itavuvumka karibuni na kuuokoa ulimwengu kutoka kwenye pupa.”—The Wall Street Journal, Januari 11, 1989.[7]
Hata hivyo, tumaini la jinsi hiyo la muhula wa ufanisi bora, Utopia, au ulimwengu mpya, si jambo jipya. Ngano zinazohadithiwa na karibu kila utamaduni mkubwa hutia ndani tumaini la kuwako jamii ya Kiutopia ya wakati ujao.[8] Hadithi za Kisumeri, Kigiriki, Kiroma, na Kiskandinevia zilihusisha itikadi hiyo.[9] Encyclopedia of Religion husema: “Hamu ya kutaka utopia ambapo mtu hana shida na ambapo amani na ufanisi ni kemkemu imekuwa ni sehemu kuu ya dini ya Kichina tangu nyakati za kabla ya Ch‘in (kabla ya 221 KWK).”[10] Kitabu kitakatifu kilicho cha kale zaidi sana, Biblia, husema juu ya mileani ambapo ainabinadamu italetwa kwenye ukamilifu, kisha vita, uhalifu, maumivu, na kifo vitamalizwa.—Ufunuo 21:1-4.
Dini ya Ubinafsi
Katika filamu ya tawasifu yake Out on a Limb, mwigizaji wa kike na mtungaji mashuhuri wa vitabu vya Muhula Mpya Shirley MacLaine, yeye aonekana amesimama kwenye ufuo uliofagiwa na upepo akinyoosha mikono yake na kupaaza sauti hivi: “Mimi ni Mungu! Mimi ni Mungu!”[10b] Kama yeye, Wana-Muhula-Mpya wengi huendeleza kujitafutia utu wa cheo cha juu zaidi na wazo la kuwa wana mungu fulani ndani yao. Wao hufundisha kwamba wanadamu wakiweza tu kuongeza ufahamu wao wataupata umungu wao.
Wao hudai kwamba, hilo likiisha kufanywa, uhalisi wa kuhusiana kwa vitu ulimwenguni pote hueleweka wazi—kila kitu ni mungu, na mungu ni kila kitu.[11] Hilo si wazo jipya hata kidogo. Dini za kale za Mesopotamia na Misri ziliamini katika uungu wa wanyama, maji, upepo, na anga.[12] Hivi majuzi zaidi, Adolf Hitler asemekana aliwatia wengine moyo wakubali ile “itikadi imara, yenye maoni ya kupita kiasi kwamba Mungu yumo katika Maumbile, Mungu yumo katika watu wetu wenyewe, katika mwisho utakaoyafika maisha yetu, katika damu yetu.”[13]
Utamaduni wa Muhula Mpya umekolewa na fasihi, warsha, na programu za mazoezi za uwezo wa kujiendeleza na kujiboresha. Shime moja ya kawaida huwa juu ya “kujifahamu jinsi nilivyo kwa ndani.” Watu hutiwa moyo wajaribu kitu chochote kile kiwezacho kuwasaidia kufungulia mambo yote ya kujiendeleza mbele. Kama vile mwandikaji mmoja alivyoeleza wazo hilo katika gazeti Wilson Quarterly, “fundisho kuu la harakati hiyo ni ‘kwamba waweza kuamini kitu chochote bora tu kiwe na matokeo mazuri kwako.’”[14]
Margot Adler, mwendelezaji wa Muhula Mpya, aeleza kwamba wengi wa wanawake wajiungao na harakati za Muhula Mpya za wanawake hufanya hivyo “kwa sababu za kibinafsi sana. . . . Wao huchukia miili yao, hujichukia wenyewe. Wao huingia katika vikundi hivi ambavyo hasa huwa vikikuambia, ‘Wewe ndiwe mungu-mke, wewe mzuri ajabu.’”[15]
Gazeti la New York laeleza jinsi kikundi kimoja kijitafutiavyo utu wa cheo cha juu zaidi: “Mwanamke hurefusha sauti yake akisema, ‘Sisi ndio walimu wa lile Pambazuko Jipya. Sisi Ndio Wenyewe.’ Washiriki wengine, wakiwa wamevaa vitambaa vya kichwa vyenye pembe, vificha-uso vyenye manyoya, na mavazi mepesi sana, hucheza dansi wakipita msituni, wakigunaguna na kutoa-toa ishara, wakiomboleza na kupiga viyowe.”[16]
Mafumbo ya Kishetani Yaliyotakaswa
Mawazo fulani ya Muhula Mpya huendeleza maoni mapya, ya kutakasa mafumbo ya kishetani. Ushetani haushirikishwi tena na mambo ya kishetani katika akili za Wana-Muhula-Mpya wengi. Mwandikaji mmoja katika gazeti Free Inquiry hutaarifu hivi: “Kuna idadi inayoongezeka ya wazoeaji uchawi, na hakuna wowote kati yao walio na itikadi zinazohusisha Ushetani.”[17]
Uchunguzi wa hivi majuzi katika Ujerumani ulionyesha kwamba katika nchi hiyo kulikuwa na wachawi wa kike 10,000 walio watendaji. Hata watoto wanavutwa kwenye mafumbo ya kishetani kwa njia za hila.[18] Kitabu cha Kijerumani Der Griff nach unseren Kindern (Uvutio kwa Watoto Wetu) chaeleza kwamba kupitia “kaseti za drama za watoto, watoto wanazoelea sura mpya ya mchawi wa kike kuwa ni mwanamke wa kawaida atumiaye mizungu ya kishetani kwa makusudi mema.”[19] Kitabu hicho chaongezea hivi: “Uangalifu wa hata wadogo wadogo huvutwa hivyo kwenye njia ya Muhula Mpya iwezayo kuwaongoza kwenye mambo ya nguvu zisizo za kibinadamu.”[20]
Katika vitabu vyake, Shirley MacLaine huendeleza wazo la kwamba mafumbo ya kishetani ni ujuzi uliofichwa tu na kwamba kufichwa kwao hakumaanishi kwamba si kweli.[21] Falsafa hiyo imenasa watu wengi sana katika mtego wa kujaribia mazoea ya kigeni ya kuwasiliana na roho, kama vile uaguzi, unajimu, uwasiliano wa kutumia hisia za kufahamu mambo yazidiyo nguvu za kibinadamu, na kuwasiliana na roho. Hilo la mwisho limejulikana kwa maelfu ya miaka kuwa njia ya kuwasiliana na roho waovu. Lakini Wana-Muhula-Mpya huliita kupitishiana-habari. Nadharia yao hudai kwamba roho za wafu huchagua watu fulani mmoja-mmoja kuwa vipitishio vyao vya kuwasilisha habari kwa ainabinadamu.
Wanadamu hao wadhaniwao kuwa wapitisha-habari waweza kuingia katika njozi wakati wowote wajitakiapo na kusema au kuandika ujumbe mbalimbali wa “kuangazia nuru,” ambao husemekana watoka kwa wafu au kwa watu waishio nje ya eneo la dunia. Roho za wafu huchukuliwa kuwa ni wahenga wastadi wanaongoja wakati ufaao ili wavae ubinadamu wakiwa umbo jipya. Kwa sasa, wao husemekana kuwa huongoza ainabinadamu katika muhula mpya.
Wana-Muhula-Mpya wengi hukutana kwa kawaida kusikiliza yale ambayo watu hawa wadhaniwao kuwa wastadi hutaka kusema kwa kutumia wapitisha-habari wao. Na waamini wanaweza kuchagua roho watakao kuwaomba ushauri. Miongoni mwa zile zidhaniwazo kuwa zinasema leo ni roho za John Lennon na Elvis Presley, wakaaji wa nje ya dunia hii walio na majina kama Attarro na Rakorczy, na shujaa mwenye umri wa miaka 35,000 wa kutoka Atlantis ielezwayo katika ngano ambaye jina lake Ramtha.
Muhula Mpya na Afya
Idadi inayoongezeka ya wanatiba huamini kwamba wagonjwa hawapaswi kutendewa kama mashine zilizovunjika tu na kwamba afya ya mtu ya kiakili na kihisia-moyo yapasa kufikiriwa. Mfikio huo wajulikana kuwa utibabu mzima-mzima unaotibu mwili pamoja na akili na hisia zote za mtu, na si lazima uwe umetokea kwa sababu ya lile elekeo la Muhula Mpya. Hata hivyo, Wana-Muhula-Mpya wengi wameukubali kwa moyo huo utibabu mzima-mzima. Kitabu The Cosmic Self hueleza kwamba Wana-Muhula-Mpya, bila hasa kuukataa mfumo wa kitiba, hupendelea kumtibu mgonjwa akiwa mtu mzima-mzima, “kiungo hai kilicho kamili kikiwa na mwili, akili, na roho.”[26]
Wana-Muhula-Mpya hudai kwamba afya njema yaweza kupatikana nje ya tiba ile ya kawaida. “Mahali ambapo watu walio wengi hukuta mawazo ya Muhula Mpya kwa mara ya kwanza ni katika tiba iliyo ya namna tofauti,” lasema gazeti la Uingereza The Herald.[27] Na mawazo yasiyo ya kawaida sana hupelelezwa. Kwa kielelezo, mpasuaji Mwaustralia wa siku nyingi aliye mtungaji wa vitabu pia, Ian Gawler, adokeza kwamba huenda kansa ikaponywa kwa kutafakari.[28] Njia nyingine za kuponya ambazo sana-sana hubandikwa sifa ya kuhusiana na Muhula Mpya ni pamoja na kutafuta ugonjwa kwa kutumia unajimu, kuchanganua wingi wa mng’ao unaotoka katika mtu, utibabu wa kutia mtu katika hali ya usingizi, upasuaji wa ajabu usiokata mwili halisi, na utibabu wa kukumbusha akili ya mtu maisha alizoishi nyakati zilizopita. Njia hizi za kuponya huendelezwa katika magazeti ya pekee yanayoshughulika na afya, dawa za kiasili, vitamini, mazoezi ya mwili, na lishe.
Muhula Mpya na Matufe Maangavu
Njia moja ya kuponya ipendwayo na wengi katika Muhula Mpya yahusisha utumizi wa matufe maangavu na johari za uaguzi, kama vile kwartzi, amethisti, topazi, rubi, opali, na zumaridi. Mtengeneza-vito wa Muhula Mpya Uma Silbey adai hivi: “Katika historia yote utapata vielelezo vya tamaduni zilizoamini kwamba kwartzi ingeweza kuongeza nishati ya kufahamu mambo yasiyo ya kawaida na nguvu za kuponya.” Mwanamke huyo aongezea hivi: “Wasumeri, Wamaya na staarabu nyinginezo zilitumia matufe maangavu ya kwartzi kwa makusudi ya kuponya.”[30]
Matufe hayo maangavu hutumiwaje? Matabibu wa kutumia matufe maangavu hudai kwamba maradhi ya kimwili na kiakili yaweza kuponywa kwa kuweka kwartzi na johari nyinginezo juu ya maeneo fulani hususa ya mwili. Katrina Raphaell, mwendelezaji wa kutumia matufe maangavu katika Muhula Mpya, aeleza kwamba matufe maangavu “yaweza kuwekwa chini ya mto wakati wa kulala ili kuchochea ndoto za mambo matukufu na za kiunabii. Yaweza kutumiwa katika mazoea ya kuponya ili kuimarisha hisia-moyo zilizovurugika, kutuliza akili zenye kusumbuka na kusaidia kuponya kasoro za kukosa usawaziko mwilini. Yaweza kushikwa mkononi wakati wa utungu wa kuzaa na muda wa kujifungua ili kupata nguvu zaidi.”[31]
Muhula Mpya na Mazingira
Ile harakati ya Muhula Mpya ni “safi, huhangaikia kulinda mazingira, ni ya kisasa,” ndivyo isemavyo TSBeat, gazeti la Uingereza kwa matineja.[32] Ushiriki mtendaji katika kuendeleza ufahamu juu ya mazingira na ulinzi wa mazingira umechangia kuleta sifa ifaayo kwa harakati ya Muhula Mpya, na ujumbe huo wenye kuyafaa mazingira umevuta wengi kwenye mafundisho yao. Hata hivyo, mara nyingi mahangaiko ya Muhula Mpya kwa mazingira huonyeshwa yakiwa ibada ya moja kwa moja kwa maumbile, pamoja na desturi za kiibada zifananazo na sherehe za kizamani zilizowekwa wakfu kwa mungu-mke dunia.
Je! wonyesho huu wa ki-siku-hizi wa mafumbo ya kale ndilo jibu kwa matatizo yetu? Je! sayari itaokolewa na hekima ya wachawi wa kike na wakaaji wa nje ya dunia hii? Je! kweli muhula mpya wa amani na ufanisi utakuja wakati fulani?
[Maelezo ya Chini]
a Utopia: “Mahali pakamilifu kimawazo, hasa katika mambo ya kijamii, kisiasa, na kiadili.”—The American Heritage Dictionary of the English Language.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
MacLaine, Muhula Mpya, na Ramtha
“ENEO la kule nje nyotani lilikuwa halisi hata ingawa hatungeweza kuliona wala kulipima kwa vipimo vya marefu. Kuna uhalisi ulio mkubwa kuliko uhalisi ambao sisi twaujua ‘kwa kuhisi.’ Huo ndio umekuja kuitwa muhula mpya wa mawazo. Muhula mpya wa ufahamu. . . .
“Mimi nilitembelea wanaosifika kuwa wapitishaji wa habari zitokazo kwa roho walio katika eneo la nyotani. Nilisitawisha mahusiano na ‘roho hao wenye kuwako.’ . . . Mmoja alikuwa na ufahamu wa kina kirefu kuliko wengine wote. Jina lake lilikuwa . . . Ramtha Mwangaziwa-Nuru. . . . Alisema alikuwa amepata kuwa na umbo la kibinadamu wakati mmoja katika kipindi kile ambacho kisiwa kimoja cha Bahari Kuu ya Atlantiki kilizama na alikuwa amefikia kupata ufahamu kamili muda huo wa maisha. . . . Nilipokuwa nikitazama ndani ya macho ya Ramtha, nilijisikia nikisema, ‘Je! wewe ulikuwa ndugu yangu ulipokuwa na umbo lako la kibinadamu katika kipindi cha Atlantiki?’
“. . . Machozi yalitiririka kutoka machoni mwake. ‘Ndiyo, mpenzi,’ yeye akasema, ‘na wewe ulikuwa ndugu yangu.’”
MacLaine aendelea kusema hivi: “Lengo lake la kunipa mimi elimu ya kiroho lilikuwa kunifahamisha kweli ya kwamba sisi ni Mungu. Sisi tuna uwezo wa kuwa na ujuzi kama yeye.”—Dancing in the Light, cha Shirley MacLaine.[1]
Linganisha Mwanzo 3:5, ambapo Joka (Shetani) alimwambia Hawa uwongo huu: “Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Wale wanaotamani kibali cha kimungu ni lazima waepuke kuhusika kwa vyovyote pamoja na viumbe-roho walio waovu na wadanganyifu. Sheria ya Musa ilitaarifu hivi: “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA [Yehova, New World Translation], Mungu wenu.”—Mambo ya Walawi 19:31.
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Je! Ni “Dawa Nyingine ya Kulevya Katika Jamii Iliyojaa Dawa za Kulevya”?
“HARAKATI ya Muhula Mpya—iliyo nyongeza ya karibuni zaidi kwa historia yetu ndefu ya mitindo ya ajabu-ajabu ya kiroho na dawa-muujiza za kuponya matatizo yote—yatokeza dhihaka na kutia ghadhabu. Kinachotokeza shuku kwamba kuna upunjaji mkubwa wa kidini si kule kushuka kwa tabia za uchaji tu bali pia ubiashara wayo wa wazi sana. . . .[1]
“Hiyo harakati ya Muhula Mpya hujaribu kuunganisha kutafakari, kufikiri kuzuri, kuponya kwa imani, . . . siri za ulimwengu wa roho, yoga, maponyo ya kutumia maji, tiba ya kupachika visindano mwilini, uvumba, unajimu, saikolojia ya Jung’, kurekebisha miendo ya mawimbi ya akili na mapigo ya moyo, ufahamu wa kuhisi mambo zaidi ya yale ya kawaida (ESP), uwasiliani-roho, . . . nadharia ya mageuzi, matibabu ya Reich ya kutumia ngono, ngano za kale, . . . hali ya usingizi [mzugo], na mbinu nyingine zote zilizofanyizwa kuongezea kufahamu mambo, kutia na mambo yaliyotolewa katika mapokeo ya zile dini kubwa. . . .[2]
“Mabadiliko ambayo ule Muhula Mpya umeletea dini hutuliza dhamiri badala ya kuisumbua. Fundisho lao kuu ni kwamba haidhuru unaamini kitu gani, bora tu kiwe na matokeo mazuri kwako. ‘Jambo ni la kweli ikiwa wewe waliamini’: ndiyo shime ya ule Muhula Mpya. . . .[3]
“Suala si kama matibabu ya Muhula Mpya yana matokeo kikweli bali ni kama kazi ya dini yapasa kuwa kutibu tu. Ikiwa kazi yayo ni kutoa msisimuko wa kiroho tu, hapo basi dini imekuwa dawa nyingine ya kulevya katika jamii iliyojaa dawa za kulevya.”—“Ile Harakati ya Muhula Mpya: Hakuna Jitihada, Hakuna Kweli, Hakuna Masuluhisho, Maelezo Kuhusu Imani ya Kwamba ya Mungu Hayajulikani—Sehemu ya 5,” na Christopher Lasch, Profesa wa Historia wa Watson kwenye Chuo Kikuu cha Rochester, New York, U.S.A.[5]
[Picha katika ukurasa wa 7]
Vidhehebu vya Muhula Mpya vyajaribia unajimu, ufahamu wa kutumia hisia zisizo za kibinadamu, kutafakari, na matufe maangavu, miongoni mwa vitu vinginevyo
[Picha katika ukurasa wa 8]
Njia za kuponya za Muhula Mpya zatia ndani utumizi wa matufe maangavu