Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 3/22 kur. 3-6
  • Kupenda Fedha—Shina la Uovu Mwingi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupenda Fedha—Shina la Uovu Mwingi
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mamlaka ya Fedha Katika Familia
  • Fedha, Fedha Kila Mahali
  • Hali Tofauti-Tofauti
  • Maoni Yenye Usawaziko Kuhusu Pesa
    Amkeni!—2015
  • Je, Pesa Ndio Chanzo cha Uovu Wote?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Pesa
    Amkeni!—2014
  • Jinsi ya Kupanga Matumizi ya Pesa
    Unaweza Kuwa na Familia Yenye Furaha
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 3/22 kur. 3-6

Kupenda Fedha—Shina la Uovu Mwingi

HUENDA kila kizazi kikatoa hoja ya kwamba muda wao ndio umepita vizazi vyote kwa utafutaji wa kile kitu kitafutwacho zaidi duniani—fedha! Kila kimoja chaweza kuonyesha vita walivyopigana ili kutafuta utajiri na mali, mara nyingi urefu wa vita hiyo ukiamuliwa na muda ambao fedha hizo ziliendelea kuwapo.

Ulimwenguni pote, mamilioni ya watu wameuawa kwa ajili ya fedha. Watoto wa wazazi matajiri wametekwa nyara na kuzuiliwa kwa kusudi la kutoza fidia—fedha ambazo wazazi wao watalipa ili warudishwe wakiwa salama. Watu wasio na habari wamepokonywa na walaghai akiba za fedha walizoweka maisha yao yote. Nyumba za watu zimesakwa-sakwa na wakora na kuvunjwa zikitafutwa fedha. Wajasiri wasiojali hatari wamebandikwa jina la “Adui Namba Moja wa Umma” kwa sababu walivamia benki. Hakuna kizazi chochote kimoja tu kiwezacho kusema ni hicho tu kimepatwa na vitendo hivyo vya aibu. Kwa kielelezo, hakuna kizazi ambacho kimeshuhudia utafutaji wa fedha kwa pupa nyingi kuliko kile kilichoona haini wa kudharaulika akimsaliti rafiki yake mkubwa zaidi, yule mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi, kwa vipande 30 vya fedha.

Hata hivyo, ufuatiaji wa kinunuaji hicho ambacho huwapiga watu chenga daima, kilichoitwa na mwandikaji mmoja Mwamerika “dola ya uweza-yote, kile kitu maarufu kitafutwacho kwa bidii nyingi ulimwenguni pote,” umeharibika zaidi. Hakuna kizazi kingine chochote ambacho kimeshuhudia manyang’anyo ya benki yenye kujasiria sana kama hiki—mamilioni ya dola yamepokonywa kutoka kwa wafanyakazi wa kaunta za benki kwa kuelekezewa bunduki, si na wanaume na wanawake tu bali hata na vijana. Wizi wa jinsi hiyo umeenea sana hivi kwamba hautajwi sana katika vyombo vya habari. Taasisi nyingi za kifedha zimefilisika kwa sababu wamiliki-mali wenye pupa wamenyonya mamilioni ya fedha za waweka-akiba kwa utumizi wao wenyewe binafsi, hivyo wakakausha rasilmali za benki na kuacha waweka-akiba wengi wakiwa wameishiwa.

Yaweza kusemwa nini juu ya makarani ambao huchota mamilioni ya dola kutoka kwa waajiri-kazi wao ili kujaribu kuonja mitindo-maisha ya walio matajiri na mashuhuri? Vibunda vya karatasi vingeweza kuandikwa juu ya watu ambao hunyemelea katika barabara zisizomulikwa vizuri ili wawanyang’anye wapitaji vitu vilivyo katika pochi na vibeti vyao. Na namna gani yale manyang’anyo yashuhudiwayo na watu wengi yakifanyika peupe mchana tu, huku watu wasio na hatia wakiuawa na kunyang’anywa fedha zao? Katika maeneo fulani ya ujirani, wakaaji huomboleza hivi: “Swali si kama nitavamiwa barabarani bali ni mara ngapi nitafanywa hivyo.” Watu fulani hata huchukua ‘fedha za mvamiaji’ ili kumtuliza mnyang’anyi, ambaye naye huenda akaachilia uhai wao. Kwa kusikitisha, kizazi hiki cha umalizio cha karne ya 20 kinapatwa na utafutaji wa fedha ulio wa kikatili zaidi ambao umepata kuwapo ulimwenguni.

Mamlaka ya Fedha Katika Familia

Ebu angalia jinsi waume na wake hugombania fedha kila siku. “Fedha ni sumaku ambayo huvuta mivurugiko yote ya hisia na kuiingiza katika maisha zetu,” akaandika mtafiti mmoja. “Ni lazima uelewe jinsi wewe na mwenzi wako wa ndoa mwonavyo fedha na kuzitumia ndiyo mweze kuacha kuzipigania,” akasema mwanamke huyo. Wastadi walio wengi wakubali kwamba wenzi waliofunga ndoa hupigania fedha hasa, familia hizo ziwe ni tajiri au maskini au ziko hapo katikati tu. “Mimi hustaajabu,” akasema mtafiti mwingine, “ni mapigano mangapi yahusuyo kutumia au kuweka akiba ya fedha.”[3] Kwa kielelezo, fikiria walio matajiri kupindukia. Mara nyingi mwenzi wa ndoa mwenye tabia ya kubana sana fedha zake hutafuta kuhifadhi fedha hizo, hali yule mtapanyaji hutafuta kuzitumia. Wajapokuwa na utajiri ule, mapambano huanza—si kwa sababu ya ukosefu wa fedha bali kwa sababu ya wingi wazo. Kuna wale ambao hufunga ndoa kwa ajili ya fedha, hufurahia mitindo-maisha waliyokuwa hawajapata kamwe kuwazia wangekuwa nayo, na punde si punde hutalikiana ili walipwe ridhaa ya kiasi kikubwa sana.

Katika mfumo huu wa mambo ulio na kichaa cha fedha, mtu kutajwa kuwa ni mwenye fedha huonyesha ana mamlaka na hali ya kujistahi. Mara nyingi hilo hutokeza udhia wakati mke achumapo kiasi kingi kuliko mwenzi wake wa ndoa. Afanyapo hivyo, mume wake huenda akahisi kwamba mamlaka yake na hali ya kujistahi vimepotea. Hapo wivu hujitokeza—si kuhusu mwingilia-ndoa fulani wa siri—bali kuhusu ile dola ya uweza-yote itamaniwayo sana ambayo imethubutu kuwagawanya. Kutokeapo pambano la kuamua kati ya fedha na upendo, mara nyingi sana fedha ndizo hushinda.

Basi mambo huendelea hivyohivyo. Kwa kweli “shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha.” (1 Timotheo 6:10) Hata hivyo, ukosefu wa fedha umewaletea maumivu na mateso makubwa wale ambao wamedhulumiwa na wale wenye kuifuatia mbiombio.

Fedha, Fedha Kila Mahali

Husemwa mara nyingi kwamba ili kupata fedha nyingi zaidi ni sharti mtu awe na fedha. Ebu angalia yale mapesa—mamilioni kwa mamilioni—yatumiwayo kumnasa atakaye kuwa mnunuzi ili anunue bidhaa ambazo watangazaji huchuuza kwa bidii nyingi. Ebu angalia barua zako zinazoingia—huenda ikawa zamu yako ‘kushinda dola milioni kumi.’ Hakuna mtu huelekea tena kupendezwa na dola milioni moja tu; sasa ni kuanzia milioni kumi kwenda juu. Watu kadhaa hujiandikisha wawe wakipata magazeti wasiyoyataka, na labda hawatayasoma kamwe, wakihofu kukosa donge nono la fedha za ghafula. Ile ahadi itangazwayo kwamba “Si lazima ununue kitu ndiyo ustahili kushinda” huonekana kwa wengi kuwa ya kutiliwa shaka.

Ebu ona ni majimbo mangapi katika Amerika ambayo sasa yana bahati-nasibu zenye malipo yawezayo kuwapa washindi mamilioni ya dola! Milioni chache huonwa kuwa “visarafu tu.” Siku hizi, kuanzia dola milioni 50 hadi milioni 100 zaweza kushindwa kwa droo moja tu. Yaonekana fedha haziishi katika mashine za kamari. Katika nchi nyingi, michezo ya kitaifa ya pata-potea imekuwako kwa vizazi vingi. Watu wametumia fedha za matumizi ya juma zima kubahatisha mchezo mmoja tu ili washinde donge nono la fedha. Familia zimekaa bila chakula na mavazi ya kutosha—badala ya kutumia fedha kwa vitu hivyo, wao hujinyima ziwe za “mungu wa Bahati Njema.”—Isaya 65:11, New World Translation.

Waangalie mamilioni ambao huwazia kushinda madonge manono katika michezo ya nasibu. Fikiria wale wajaribuo kutimiza fantasia zao za kushinda wakicheza kamari katika kasino sehemu zote za ulimwengu. Wao hutumainia kutimiza ndoto zao kwa kukoroga dadu na kuitupa mara moja, kuchagua karata moja tu, kufyatusha kikono cha mashine ya kamari mara moja tu. Hata hivyo, sikuzote mambo huelekea kuwaendea mrama sawasawa na kujaribu kubana mafuta yenye utelezi mkononi.

Na hivyo ndivyo ile mbio ya kufuatia dola yenye kupiga chenga huendelea kasi bila kukoma, mbio ya kufuatia upepo. Hata ingawa watu fulani wamekusanya fedha nyingi, wamepata kwamba kwa ghafula, kwa dakika moja isiyotazamiwa, zimekwisha fyu. Basi maneno ya Mfalme Sulemani mwenye hekima yapasa kuwa na maana kubwa kwao: “Fedha zenu zaweza kwisha kwa mmweko mmoja, kama kwamba zimemea mabawa na kurukia mbali kama tai.”—Mithali 23:5, Today’s English Version.

Hali Tofauti-Tofauti

Haiwezi kukanwa kwamba kuna wale ambao wamejiletea wenyewe na familia zao mateso makubwa kwa kutumia vifedha vyao kwa mchezo wa bahati-nasibu. Mara nyingi hao ni watu maskini, wasiojiweza sana, wenye kuchuma kitonge tu cha riziki. Wengine ni wavivu na hupendelea kucheza kamari ili watafute fedha ambazo hawakufanyia kazi. Hata hivyo, leo wengi wa maskini wa ulimwengu wamepatwa na hali hizo za umaskini bila kupenda kwao wenyewe. Wale ambao elimu yao hata haiwawezeshi kuandika majina yao wenyewe vizuri ni mamilioni mengi ajabu. Kwa wengine wengi, uchumi wenye kuharibika katika maeneo ya kwao umefanya mapato yao yahesabiwe kuwa katika kiwango cha walio maskini. Hata wale wenye digrii za chuo wamelazimika kukataliwa maombi yao ya kuajiriwa kazi. Mashirika makubwa yapunguzapo utengenezaji wa bidhaa zao kwa sababu zimezidi uhitaji, maelfu zaidi hujikuta hawana kazi. Wao hukabilije hali?

Fursa za kupata kiasi fulani cha fedha bila haki huenda zikawavutia. Huenda wakawaza kwamba mbinu mbaya ya kupata kitu ni sawa mradi tu kitu chenyewe kipatikane. Mtazamo wa kawaida miongoni mwa wale wanaokabili shida kubwa za fedha ni kwamba “Mimi nitafanya lolote lile ili kuilisha familia yangu.” Mapito yasiyo ya haki ni mengi, umalaya kwa wanawake, uibaji kwa wanaume. Je! kukosa haki, kuiba, au kucheza kamari—ule ufuatiaji wa dola ambayo haijachumwa—hufaa wakati wowote? Ulimwengu umejawa na watu wenye kufikiri hivyo.

Je! wewe wamwamini Muumba Mtukufu, Yehova Mungu? Shauri lake ni kwamba umtwike mizigo yako yote ikulemeayo, utegemee msaada wake nyakati za uhitaji. Baada ya miaka kama 25 ya kukaa akiwa Mkristo, mtume Paulo angeweza kuandika hivi: “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” (Wafilipi 4:12, 13) Kwa wazi, Paulo hakugeukia kutumia njia isiyo haki alipopungukiwa na maandalizi, bali alimtumaini Yehova akasaidiwa.

Kwa hiyo ikiwa wewe ni maskini, mwenye shida, usitafute faida isiyo ya haki. Hakika si kosa kuchuma fedha kwa njia ya haki; Yesu mwenyewe alisema kwamba “mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake.” (Luka 10:7) Wala hakuna kosa lolote kuwa tajiri. Lakini usigeukie kamwe kuridhiana kiadili ili kutimiza mahitaji yako. Jenga uhusiano pamoja na Muumba wako Mtukufu, Yehova Mungu, na umtegemee akusaidie kukabiliana na magumu na matatizo ya maisha. “Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”—1 Petro 5:6, 7.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki