Je! Mfanyakazi Astahili Mshahara Wake?
EBU watazame! Wao huonekana wakiweza maisha kwa shida, sana-sana wakiwa katika vijumba vichafu, mara nyingi wakiwa na uhaba wa kuwawezesha kuwa hai tu, hata ingawa wengi wao huishi na kulea familia wakiwa katika taifa lenye utajiri mwingi. Hao ndio wale wafanyakazi wa kuhamahama, ambao ni milioni tano katika United States pekee, wenye kuchuma matunda na mboga kwa ajili ya mashirika yaliyo makubwa zaidi taifani.[1]
Ebu ione miili yao yenye makovu na maumivu makali ikifanya kibarua katika joto kali la kuunguza. Ebu watazame wakijaribu kunyoosha migongo yao baada muda wa saa nyingi za kuinama, wakichuma mboga ambazo zitapamba rafu na masanduku ya maduka ya mbali. Tangu macheo hadi machweo, siku sita na saba kwa juma, watakuwa hapo. Ebu waone watoto, wakifanya kazi kando ya wazazi wao na mara nyingi kando ya mababu na manyanya zao wakongwe. Wengi wa hao vijana hutolewa shuleni wakiwa na umri mdogo kwa sababu wazazi wao huhamahama kufuata mazao mapya ya kuvunwa, msimu baada ya msimu. Eti wajiambulie angaa kitu cha kusukuma maisha tu.
Je! ile kelele ya daima ya ndege inayoruka ikiwa kimo cha chini yakuhangaisha wewe uwatazamapo vibarua hao wakitoka jasho mashambani? Je! zile dawa zenye kudhuru za kuua wadudu zinazonyunyizwa kutoka kwenye virija vya ndege hiyo zasababisha macho yako yawashe na ngozi yako iume na kunyeza? Je! wewe waziogopa hatari za muda na za kudumu ziwezazo kukupata? Wafanyakazi hao waziogopa. Ule mnyunyizo huwa daima juu ya nguo zao, katika matundu ya pua zao, katika mapafu yao. Wameziona kemikali hizo zenye kudhuru sana zikiumiza watoto wao na wazazi wakongwe. Wameona washirika wa familia na wafanyakazi wenzao wakiwa wasiojiweza katika umri mdogo kwa sababu ya kutiwa sumu na dawa za kuua wadudu.
Mtoto mmoja, ambaye sasa yumo katika miaka yake ya utineja wa mapema, alizaliwa akiwa na kiuno kilichoteguka, bila msuli wa kifua upande wa kuume, na upande mmoja wa uso wake ukiwa umepooza. Baba yake huamini kwamba kasoro ya umbo lake ilisababishwa na dawa za kuua wadudu zilizonyunyiziwa mashamba ya zabibubua mama yake akiwa mjamzito.[2] Imeripotiwa kwamba kukosa kinga dhidi ya dawa za kuua wadudu peke yake huathiri wafanyakazi 300,000 kwa mwaka na kwamba wafanyakazi wahamaji hudhoofika mara tano kuliko wafanyakazi katika shughuli nyingine yoyote.[3][4]
Ikiwa hisiamoyo zako haziguswi kuwahurumia sana kwa kule tu kuwaona wakifanya kibarua kigumu mashambani au kwa kuona hali za maisha yao fukara, basi yasikilize maneno yao. “Kazi hii huchosha mtu akawa hoi kabisa,” asema mama mmoja mwenye watoto saba akihema kwa uchovu baada ya kushinda mchana kutwa katika kazi ngumu shambani.[5] “Labda nitaoga nikalale tu. Asubuhi ya leo nililala sana nikaamka baada ya saa 10 na sikupata wakati wa kutayarisha chakula cha mchana, hivyo basi sijala chakula. Sasa nimechoka mno nisiweze kula.”[6] Mikono yake ina malengelenge ya kuchubuka. Kushika kijiko au uma kungefanya kula kuwe maumivu.
“[Watoto wetu] hutusaidia nyakati fulani za miisho-juma,” akasema mama mwingine, “nao wajua jinsi ilivyo kufanya kazi katika hayo mashamba. Hawataki kujipatia riziki kwa kufanya kazi hiyo. . . . Mimi ningali na vibanzi vya vijiti katika mikono yangu kutokana na kuchuma machungwa kipupwe kilichopita.”[7] Mume wake alisema: “Sisi hufanya kazi kuanzia macheo hadi machweo siku sita kwa juma. . . . Lakini labda tutakuwa tukifanya hilo maisha zetu zote. Tufanye nini kingine?”[8] Hao wenzi wawili wakiwa pamoja huchuma dola 10,000 tu kwa mwaka—kiwango cha walio maskini kulingana na makadirio ya Amerika.[8A]
Wafanyakazi huogopa kulalamika kwa kuhofu kupoteza kazi zao. “Ukilalamika,” akasema mmoja wao, “hawatakuita tena.” Wengi wa wafanyakazi wahamaji ni waume na mababa waliolazimika kuacha familia zao nyuma ili kuyafuata mazao, kwa kuwa nyumba za kupanga, ambazo mara nyingi ni mabweni yaliyojengwa kwa magogo yaliyochomeka ambayo hukaliwa na wafanyakazi wawezao kufika 300, ni chafu na zenye kusongamana mno zisiweze kutumiwa kwa washirika wengine wa familia yao.[10] “Ingependeza kuishi pamoja na [familia yangu] mwaka wote,” akasema baba mmoja, “lakini sina namna ila kufanya hivi.”[11] “Tayari tumefikia kiwango cha chini kabisa,” akasema mwingine. “Basi hatuna la kufanya ila kujitahidi kuinuka kidogo.”[12] Kwa ubaya zaidi, wengi wa hawa ndio hupata mshahara mdogo zaidi. Kwa watu fulani, dola 10,000 kwa mwaka kwa familia ya wafanyakazi huonekana kama mlima, mshahara wasioweza kuufikia. “Wakuzaji mitunda na wenyeshamba waweza kulipa mishahara midogo sana na kuwafukuza tu wafanyakazi wowote wasiofanya sawasawa na vile waambiwavyo,” likaandika gazeti People Weekly. “Mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake,” Yesu akasema. (Luka 10:7) Ni lazima iwe wafanyakazi wahamaji hushangaa ni wakati gani kanuni hiyo itatumika katika maisha zao.
Wale Wafundishao Watoto Wetu
Sasa, fikiria wale ambao kazi zao zimewafanya wawe na daraka la kufundisha watoto na watu wazima kusoma, kuandika, kuendeleza maneno, hesabu, sayansi ya msingi, mwenendo katika mahali pa kazi—mambo ya elimu ya msingi. Katika taasisi za masomo ya juu zaidi, waelimishaji hufundisha sheria, tiba, kemia, uhandisi, na fundi za hali ya juu, nyanja ambazo ndizo hupata kazi za mishahara minono zaidi katika enzi hii ya kutumia kompyuta na kwenda anga za juu. Kwa sababu ya umaana mkubwa sana wa uwanja wa kufundisha, je, waelimishaji hao hawangestahili sana kupata mishahara ipasayo ule utumishi bora sana wautoao? Walinganishwapo na watu ambao mishahara yao huonekana kuwa mikubwa ajabu kwa kulinganishwa na kazi wafanyayo, ingeonekana kwamba jamii haithamini sana kazi ya kufundisha.
Mwishoni mwa karne hii ya 20, kufundisha kumekuwa kazi hatari sana mahali pengi, si katika shule za sekondari tu bali pia katika shule za msingi. Katika maeneo fulani walimu huagizwa watembee wakiwa na fimbo katika madarasa na nyanja za kuchezea ili kujikinga dhidi ya watoto watukutu. Bunduki na visu hubebwa na watoto wa shule wa marika yote, mwilini mwao na katika vikasha vya chakula.[15]
Walimu, wanaume na wanawake pia, wametendwa madhara ya kimwili na wanafunzi. Katika shule za sekondari miaka ya majuzi, walimu zaidi ya 47,000 na wanafunzi milioni 2.5 walitendwa uhalifu katika U.S. “Tatizo liko kila mahali,” likaripoti gazeti la walimu NEA Today, “lakini mambo ni mabaya zaidi katika maeneo ya mijini, ambako kila mwaka mwalimu huelekeana na uwezekano wa kushambuliwa mara 1 kati ya visa 50 shuleni.”[15A] Utumizi ulioenea sana wa dawa za kulevya na kileo shuleni umeongeza mvurugiko wa hisia za walimu.[15B]
Kuongezea mzigo wao wenye kulemea, katika maeneo fulani walimu hutarajiwa waendeleze kiwango cha elimu yao muda wote wa kazimaisha yao, watumie likizo lao kufanya mitalaa ya juu zaidi au kuhudhuria mikusanyiko au warsha za walimu katika kazi yao.[16] Hata hivyo, je! ingekushangaza kujua kwamba katika majiji makubwa fulani katika United States, mshahara wa watunza-shule—wale walio na daraka la kutunza shule zikiwa safi na kuzitengeneza—waweza kuzidi mishahara ya walimu kwa dola 20,000?[17]
Mishahara ya walimu hutofautiana nchi na nchi, jimbo na jimbo, na wilaya na wilaya. Katika nchi fulani kiwango cha mshahara wa walimu ndicho cha chini zaidi katika taifa.[18] Hata katika nchi zilizo na mali nyingi zaidi, ripoti zaonyesha kwamba waelimishaji hawapati mishahara inayolingana na uzito wa daraka lao.[19]
Kama ilivyoripotiwa katika The New York Times, mchambuzi mmoja wa kiwango cha mshahara wa walimu na waelimishaji alisema hivi: “Kazi ambazo huhitaji kujitoa sana katika United States, kama vile kufundisha . . . , sikuzote zimepewa malipo au thawabu ya hali ya chini sana. Sikuzote umma wamefikiri, ‘ah, hiyo ni [kazi] yao, wao huifurahia.’ Mimi sifikiri hiyo ni haki, wala sifikiri ni jambo la akili hata kidogo.”[20] Kwa kielelezo, fikiria ripoti hii iliyochapishwa katika The New York Times: “Mishahara ya walimu na wasimamizi katika Koleji na Chuo Kikuu katika mwaka wa masomo wa 1991-92 iliinuka kwa kadiri ndogo zaidi katika muda wa miaka 20,” wastani wa asilimia 3.5. “Wakati hilo ongezeko la asilimia 3.5 lirekebishwapo kwa sababu ya infleshoni,” mtafiti mmoja akasema, “mishahara iliongezeka kwa asilimia ndogo sana ya 0.4.”[21] Kuna mahangaiko makubwa kwamba kwa sababu ya mishahara ya chini ambayo waelimishaji wenye madaraka hulipwa, huenda wengi wakalazimika kuacha kazi ya kufundisha ili wakapate kazi zenye mishahara mizuri zaidi.[22]
Halafu Kuna Michezo
Kielelezo cha namna tofauti cha mishahara isiyo na udhibiti ni ulimwengu wa michezo. Wafanyakazi wahamaji walio katika kiwango cha kuhesabiwa kuwa maskini na waelimishaji wasiolipwa mishahara inayolingana na kazi yao huyaonaje mabunda manono ya fedha ambayo wanamichezo hulipwa?
Je! polisi wa wastani mwenye kuzunguka-zunguka katika zamu zake za ulinzi na mzima-moto mwenye kazi ya kuitwaitwa na ving’ora—watu ambao huhatarisha maisha zao kila siku kazini—hufurahishwa na ile mishahara ya kushangaza sana ambayo wanariadha mashuhuri hulipwa kwa sababu wao hushangiliwa kuwa nyota? Katika United States, maofisa wa polisi zaidi ya 700 wameuawa wakiwa kazini katika mwongo uliopita.[23] Wazima-moto wengi wamekufa pia. Hata hivyo, wafanyakazi hao wenye mazoezi ya hali ya juu wamejulikana ulimwenguni pote kuwa hulipwa mishahara ya chini mno. Je! wao hawangetia shaka juu ya thamani ambayo jamii imezipa kazi na maisha zao?
Kwa kielelezo, fikiria mchezo wa besiboli—mchezo upendwao sana na mashabiki wa michezo katika United States, Kanada, na Japani. Wachezaji zaidi ya 200 wa ligi kuu katika United States huchuma dola zaidi ya milioni moja kwa mwaka.[24] Mwishoni mwa msimu wa besiboli 1992, wachezaji 100 walitia sahihi mikataba yenye kuwahakikishia kupata dola milioni 516. Kati ya hao, 23 walitia sahihi mikataba ya dola zaidi ya milioni 3 kwa mwaka. Yenye kuipita kwa mbali mishahara mikubwa hiyo ya wachezaji wasiojulikana sana ni ile mikataba ya wachezaji mashuhuri zaidi, waliotia sahihi mapatano ya kupata dola zaidi ya milioni 43 kwa kucheza miaka sita na dola milioni 36 kwa miaka mitano.[25] Kila mwaka mishahara huendelea kupanda, na viwango visivyo na kifani huwekwa vya wachezaji wenye kulipwa malipo yaliyo ya juu zaidi katika historia ya besiboli. Pia wachezaji wa mpira wa miguu (wa Kiamerika) wamepata ongezeko kubwa la mishahara kwa kulipwa wastani wa dola 500,000 kwa mchezaji.[26]
Mishahara hiyo yatokeza swali hili, Je! msomaji wa wastani aweza kuwazia kupata hundi ya dola 62,500 kila juma? “Lakini hicho hasa ndicho kiasi wapatacho wale makwotabeki [walinda-lango] wote wenye thamani ya mamilioni ya dola kila mwaka katika Ligi ya Kitaifa ya Mpira wa Miguu kila juma katika ule msimu wa majuma 16,” likaripoti The New York Times. “Au namna gani mchezaji besiboli mwenye thamani ya dola milioni 2, ambaye hupata hundi ya malipo ya dola 75,000 kila majuma mawili? Baada ya kulipa kodi zake, hubaki na dola 50,000 ambazo eti ni kitu kidogo tu cha kusukuma mwezi mpaka tarehe ya 15 ambapo atalipwa tena.”[27] Hiyo haitii ndani fedha ambazo nyota wa michezo hulipwa kwa kutumiwa katika utangazaji wa bidhaa za biashara, kwa kutia sahihi yake katika mipira ya besiboli, kwa kutia sahihi yake katika vitabu vya mashabiki, na malipo ya kwenda kujitokeza mbele ya wasikilizaji, ambayo yaweza kujumlika kuwa mamilioni.[28] Hapa tena, yule mwalimu mwenye kulipwa mshahara wa chini atafikiri nini wakati yeye apatapo kwa mwaka mmoja kiasi ambacho ni kidogo kuliko kile ambacho mwanariadha aweza kupata katika mchezo mmoja?[29]
Kwa sababu ya uwezo mkubwa wa televisheni wa kuvutia watu, wachezaji mashuhuri wa gofu, tenisi, mpira wa vikapu, na mpira wa magongo ya barafuni wamepata fedha nyingi sana. Wale walio nyota katika nyanja zao waweza kutumainia kupata mamilioni ya fedha. Mkataba wa dola milioni 42 watiwa sahihi na mchezaji mashuhuri wa mpira ya magongo kwa miaka sita.[30] Mchezaji mwingine wa mpira wa magongo hupata dola milioni 22 kwa muda wa miaka mitano, wastani wa dola milioni 4.4 kwa msimu hata ikiwa hataingia uwanjani kucheza kwa sababu ya majeraha au ugonjwa.[31]
Katika mechi moja ya tenisi kati ya wachezaji wawili mashuhuri sana, mmoja wa kiume na mwingine wa kike—iliyotangazwa kuwa “Pambano Kati ya Jinsia Tofauti”—hao wawili waliwania ushindi uwanjani waking’ang’ania kunyakua lile donge lote la dola 500,000. Ingawa yule mwanamume aliishinda zawadi, yaripotiwa kwamba wote wawili walipata “malipo makubwa ya kujitokeza uwanjani, ambayo hayakutangazwa lakini yalikadiriwa kuanzia kitu kama dola 200,000 hadi dola 500,000 kwa kila mmoja.”[32]
Katika nchi kama vile Uingereza, Italia, Japani, na Hispania, kutaja chache tu, mishahara ya wanariadha mashuhuri imeongezeka mno—mamilioni ya dola za kushangaza.[33] Yote hayo yalisukuma mchezaji mashuhuri mmoja wa tenisi aibandike jina mishahara ya miaka ya ’90 kuwa “michafu [kwa unono].”[34]
Hata hivyo, hiyo si kusema kwamba wanariadha mashuhuri ndio wenye lawama kwa kuwa na mishahara mikubwa hiyo. Wenye timu ndio huahidi kuwapa wachezaji wenye vipawa mishahara mikubwa. Wachezaji huchukua tu kile watolewacho. Wachezaji ndio huvutia mashabiki waje kuziunga mkono timu. Kwa kielelezo, misimu ya 1992 ya besiboli na mpira wa miguu (wa Kiamerika) ulikuwa na mahudhurio makubwa yasiyo na kifani katika stediamu nyingi. Hilo pamoja na haki za kulipwa faida za utangazaji katika televisheni zimewaletea wenye timu mapato mengi zaidi. Kwa hiyo, watu fulani huona kwamba wachezaji huwa wakipokea tu haki yao.
Ile mishahara mikubwa mno ilipwayo kwa kugonga mpira juu ya neti (kama katika tenisi), kwa kuugonga uingie katika tundu dogo (kama katika gofu), au uende nje ya uwanja wa kuchezea (kama katika besiboli), inapotofautishwa na malipo ya kimaskini ya wafanyakazi wahamaji wafanyao kibarua cha jasho muda wa saa nyingi chini ya jua kali ili kuvuna chakula chetu, ni wonyesho wa kusikitisha sana wa kanuni zifuatwazo na jamii yenye mali nyingi.
Fikiria uchunguzi wa tukio jingine tofauti, muhtasari juu ya mtu mashuhuri mwingine. Mwanasayansi Mwamerika Jonas Salk na watafiti wenzake walifanya kibarua cha jasho kwa muda wa saa nyingi katika maabara wakifanyiza dawa mbalimbali za kuchanja, wakizijaribu tena na tena, wakiendesha kazi hiyo kwa kutumia kiasi kinachopungua dola milioni 2 kwa utafiti wa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa kupooza. Katika 1953, Salk alitangaza kwamba dawa ya kuchanja kwa majaribio ilikuwa imefanyizwa. Miongoni mwa walio wa kwanza kupokea jaribio hilo la chanjo walikuwa Salk, mkewe, na wana wao watatu. Chanjo hiyo ilipatikana kuwa salama na yenye matokeo. Leo, ugonjwa wa kupooza ni kama umefutiliwa mbali kabisa.
Salk alipewa heshima nyingi kwa mchango wake wa ajabu katika uzuizi wa ugonjwa huo hatari wenye kulemaza. Hata hivyo, alikataa kutuzwa fedha zozote. Alirudi kwenye maabara yake kuboresha chanjo hiyo.[36] Kwa wazi, thawabu yake halisi haikuwa fedha bali uradhi wa kuona watoto na wazazi wakiwa bila hofu ya hatari kubwa hiyo.
Mwisho, fikiria kufundishwa matarajio ya kuishi milele katika dunia-paradiso, ambapo magonjwa, maradhi, na huzuni vimeondolewa mbali milele. Wazia mishahara minono ambayo walimu wa habari njema hizo wangeweza kutia mfukoni. Hata hivyo, kuna waelimishaji wa jinsi hiyo, nao wanafundisha bila malipo! Hawapewi thawabu ya fedha! Yesu aliposema kwamba ‘wafanyakazi wamestahili kupewa ujira wao,’ hakuwa akiongea juu ya mishahara kwa walimu hao wa habari njema hizo. (Luka 10:7) Alisema kwamba wangepokea mahitaji yao ya lazima. Aliwaambia hivi pia: “Mmepata bure, toeni bure.” (Mathayo 10:8) Thawabu yao itakuwa nini? Kumbe, ni kitu kilekile ambacho Yesu, yule mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi, aliahidi—uhai wa milele katika dunia-paradiso iliyosafishwa. Hata mishahara ya mamilioni ya mamilioni ya fedha haiwezi kulingana na kitu hicho!
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Fedha, Umaarufu, au Dawa za Kulevya —Jambo Jipi?
Ushawishi wa kupata umaarufu na mamilioni ya dola katika michezo ya kuajiriwa umefanya vijana wengi wageukie utumizi wa dawa za kuongeza ukubwa wa misuli yao ili wawe na miili mizito na minofu yenye kutokeza nje kwa muda mfupi isivyo kawaida. Dakt. William N. Taylor, mshirika wa Programu ya U.S. ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Katika Olimpiki, alionya kwamba utumizi wa dawa hizo umefikia “kadiri za kupita kiasi.”[1] Yakadiriwa kwamba katika United States pekee, wabaleghe wapatao 250,000 hutumia dawa za kuongeza ukubwa wa misuli.[2]
“Msongo wa kutumia dawa za kuongeza ukubwa wa misuli katika koleji ni mwingi kwa kiasi kisichoaminika,” akasema mchezaji mmoja wa kuajiriwa wa mpira wa miguu (wa Kiamerika). “Wanariadha hawafikirii miaka 20 ya kule mbele juu ya matatizo ambayo yangeweza kutokea wakitumia dawa za kuongeza ukubwa wa misuli. Hawafikirii siku 20 mapema, hasa wale walio kwenye koleji. Wazo la akili ya mwanariadha, hasa akiwa na umri mdogo, ni kwamba: Nitafanya lolote lile ili niwe mwanariadha mashuhuri.”[3]
“Nikitaka kuwa mchezaji,” akasema mmoja mwenye hamu nyingi ya kuwa mchezaji mashuhuri wa mpira wa miguu, “ni lazima nitumie madawa. . . . Kuna mashindano mengi sana katika kile chumba cha kuinua vyuma vya kujenga misuli na ukakamavu. Wataka kuwa mkubwa zaidi na mwenye nguvu zaidi kila mwaka, nawe waona jamaa wale wengine wakijenga kwelikweli, basi wewe pia wataka ujenge. Fikira hiyo iliyokazwa akilini huja kutawala mtu.”[4] Hata hivyo, ijapokuwa alikuwa na hisia hiyo, mwanariadha huyo alikuja kuwa kile alichojitahidi kuwa pale mwanzoni, bila kutumia dawa za kuongeza ukubwa wa misuli—mchezaji mashuhuri wa mpira wa miguu (wa Kiamerika). Yeye aamini kwamba dawa za kuongeza ukubwa wa misuli ni “hatari zaidi kwa mchezo huo kuliko yale madawa yatumiwayo kiharamu barabarani.”[5]
Mengi mno yameandikwa si na madaktari tu bali pia na wale ambao wamepatwa na madhara makubwa sana ya dawa za kuongeza ukubwa wa misuli na dawa nyingine za kuongezea mwili umbo. Matokeo mazito zaidi kutokana na utumizi wa madawa hayo yamekuwa kifo.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wafanyakazi wahamaji wakivuna kitunguu saumu kule Gilroy, Kalifornia
[Hisani]
Camerique/H. Armstrong Roberts
[Picha katika ukurasa wa 8]
Je! walimu hawamo miongoni mwa wale wapaswao kutangulizwa katika kustahili mishahara yao?
[Picha katika ukurasa wa 10]
Zaidi ya wachezaji 200 wa ligi kuu ya besiboli katika United States huchuma zaidi ya dola milioni moja kwa mwaka
[Hisani]
Focus on Sports