Vijana Huuliza . . .
Michezo ya Timu—Je, Yanifaa?
“Mimi hupenda kushiriki michezo. Mimi hufurahia sana. Nami hufurahia kuwa pamoja na rafiki zangu.”—Sandy mwenye umri wa miaka 14.
“FURAHA!” “Msisimuko!” “Ushindi!” Hizi zilikuwa baadhi ya sababu ambazo vijana wa Marekani na Kanada walitoa walipoulizwa ni kwa nini walishiriki michezo ya timu. Kwa wazi, vijana wengi wana msisimuko huohuo.
Kwa kielelezo, chukua Marekani. Kulingana na kitabu Your Child in Sports, kilichoandikwa na Lawrence Galton, “kila mwaka, watoto milioni 20 wa Marekani wenye umri wa kuanzia miaka sita kuendelea hucheza, au hujaribu kucheza, kwenye timu za michezo.” Na ingawa miaka michache iliyopita michezo ya timu ilikuwa ni karibu ya wanaume peke yao, idadi kubwa ya wasichana sasa wanacheza besiboli, mpira wa vikapu, na hata kushindana kwenye uwanja wa mpira wa miguu.
Huenda wewe ni mpenda mchezo nawe wahisi kwamba kujiunga na timu kungefurahisha. Au huenda ikawa unapata kitia moyo kingi—labda hata mkazo—kutoka kwa wazazi, walimu, au makocha ili ufanye hivyo. Viwavyo vyote kujihusisha na timu kwahitaji wakati na nguvu kwa kiasi fulani. Basi, yafaa kwamba tujue baadhi ya faida na hasara. Kwanza, acheni tuone baadhi ya faida.
Michezo—Faida
“Kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo,” yasema Biblia. (1 Timotheo 4:8) Bila shaka vijana nao wanaweza kufaidika kutokana na utendaji wa kimwili. Katika Marekani, idadi kubwa sana za vijana wananenepa kupita kiasi, wana msongo mkubwa wa damu, na kolesteroli. Mazoezi ya kawaida yanaweza kupunguza matatizo kama hayo. Kulingana na makala katika gazeti la American Health, wachanga wanaofanya mazoezi kwa ukawaida “wanapata uwezo mkubwa zaidi wa kupumua na wa mzunguko wa damu kuliko watoto wasiofanya mazoezi. Wanaojizoeza kwa ukawaida wanafanya vizuri zaidi katika michezo na hudhibiti vyema zaidi uzito wao wa mwili.” Wachunguzi pia husema kwamba mazoezi yanaweza kuondoa mkazo, na kupunguza uchovu, na hata kuuboresha usingizi wako.
Kwa kupendeza, kitabu Your Child in Sports chaonelea hivi: “Imekuwa wazi kwamba matatizo mengi ya kiafya ya watu wazima yana vyanzo vyayo mapema maishani.” Hivyo madaktari wengi wanahisi kwamba faida za mazoezi ya ukawaida huenda zikaendelea kufikia utu mzima. Mwandishi Mary C. Hickey aripoti hivi: “Uchunguzi umegundua kuwa watoto wanaoshiriki katika michezo yaelekea watakuwa watendaji zaidi kimwili watakapokuwa watu wazima.”
Wengi wanahisi kwamba kuna faida nyingine zenye umaana za michezo ya timu. Baba mmoja alisema hivi kuhusu mwana wake kucheza mpira wa miguu: ‘Kunamfanya asizurure mitaani. Kunamtia nidhamu.’ Wengine wahisi kwamba kucheza kwenye timu humfundisha kijana kufanya kazi pamoja na wengine—ustadi unaoweza kuwa na faida za muda mrefu. Michezo ya timu pia inamfundisha kijana kutii sheria, kujitia nidhamu, kuweza kuongoza watu, na kushughulikia vizuri mafanikio na kushindwa. “Michezo ni maabara kubwa ya vijana,” anasema Dakt. George Sheehan. “Inawapa wanafunzi uzoefu wa moja kwa moja wa mambo wanayosikia kwa ukawaida kutoka kwa walimu: ujasiri, ustadi, ujitoaji.”—Current Health, Septemba 1985.
Angalau kuwa katika timu inayoshinda kwaweza kuongezea hali ya kujistahi mwenyewe. “Nifungapo bao,” asema kijana Eddie, “mimi hujivuna sana.”
Sifa, Mafanikio, na Umashuhuri
Hata hivyo, kwa vijana wengine, kinachowavutia kwenye michezo ya timu ni kupata kibali na kutambuliwa na marika yao. “Kila wakati ufanyapo jambo zuri,” aeleza Gordon mwenye umri wa miaka 13, “kila mtu anakupongeza.”
Kitabu Teenage Stress, kilichoandikwa na Susan na Daniel Cohen, hukubali hivi: “Ikiwa kuna njia yoyote hakika ya umashuhuri, na hasa wavulana, hiyo ni riadha. . . Ni mara chache sana utakuta mchezaji maarufu wa mpira wa miguu au mpira wa vikapu akisumbukia umashuhuri.” Uchunguzi mmoja ulifunua jinsi wanariadha wanastahiwa sana. Wanafunzi waliulizwa ikiwa walipendelea kukumbukwa kama mwanariadha maarufu, mwanafunzi mwerevu, au mtu apendwaye na wengi. Kati ya vijana, chaguo la kwanza lilikuwa “mwanariadha maarufu.”
Uhakika wa kwamba mchezaji wa mpira wa miguu au mpira wa vikapu hupata staha nyingi kuliko msomi haishangazi sana ufikiripo uangalifu wa kiibada ambao vyombo vya habari humtolea mwanariadha wa kulipwa. Utangazaji mwingi hukazia fikira mishahara yao mikubwa na mtindo maisha wao wa hali ya juu. Haishangazi kwamba vijana wengi, na hasa wale walioko mijini, huenda wakaona michezo shuleni kama jiwe la kukanyagia kupata mafanikio—njia ya kutoka kwenye umaskini!
Kwa ubaya, uhalisi hutofautiana sana na matarajio hayo. Makala katika gazeti Current Health yenye kichwa “Ni Wangapi Wanaofikia Kuwa Wanariadha wa Kulipwa?” ilitoa takwimu za kushangaza. Iliripoti hivi: “Wavulana zaidi ya milioni 1 [Marekani] hucheza mpira katika shule za sekondari; karibu 500,000 hucheza mpira wa vikapu; na karibu 400,000 hushiriki katika besiboli. Kutoka shule ya sekondari hadi kwenye chuo, idadi ya washiriki hupungua sana. Ni kama wachezaji 11,000 tu ambao hushiriki mpira wa miguu, mpira wa vikapu, na besiboli wakiwa kwenye chuo.” Kutoka hapo, hesabu hizo hupungua hata zaidi. “Ni kama asilimia 8 tu [ya wachezaji kwenye chuo] wanaochukuliwa na timu za kulipa, na karibu asilimia 2 tu hufanya mkataba wa kucheza kwa kulipwa.” Kisha makala hiyo yatoa kikumbusha hiki: “Hata kufanya mkataba hakumaanishi kwamba mchezaji atapata kuchezea timu hiyo.”
Basi, kama ilivyoelezwa, “ni mmoja tu kati ya wachezaji 12,000 wa shule ya sekondari atakayekuwa mchezaji wa kulipwa.” Uwezekano huo si mkubwa zaidi ya ule wa kushinda zawadi ya kwanza katika bahati nasibu! Lakini angalau, waweza kuuliza, si mwanariadha anaweza kulipiwa masomo yake kwenye chuo kwa sababu ya jitihada zake? Kwa mara nyingine, mambo si rahisi sana. Kulingana na kitabu On the Mark kilichoandikwa na Richard E. Lapchick na Robert Malekoff, “kati ya mamilioni ya wachezaji walioko kwenye shule ya sekondari . . . , ni 1 tu kati ya 50 atakayepata kulipiwa masomo ili acheze kwenye chuo.” Takwimu nyingine ndogo ni: “Kati ya wachezaji bora wanaopata kulipiwa masomo yao wachezapo michezo yenye pesa nyingi kama vile mpira wa miguu na mpira wa vikapu, wanaopungua asilimia 30 ndio watakaomaliza masomo ya chuo baada ya miaka minne.”
Kwa wachezaji walio wengi, lile wazo la kuwa wachezaji matajiri na mashuhuri ni ndoto tu—jambo lisiloweza kutimizwa.
Wanaojiuzulu
Unapofikiri juu ya matarajio ya afya bora zaidi, ukuzi wa utu, na umashuhuri ulioongezeka, kujiunga na timu ya michezo kwaweza bado kuonwa kuwa jambo la busara kufanywa. Lakini kabla ya kukimbia kufanya majaribio, fikiria lililosemwa katika jarida Ladies’ Home Journal: “Watoto wengi zaidi wanajiunga na timu za michezo leo kuliko kilivyofanya kizazi chochote kilichotangulia. Habari isiyopendeza ni: Wanajiuzulu kutoka programu hizo za michezo kwa wingi.” Dakt. Vern Seefeldt, mtaalamu katika mambo hayo ananukuliwa akisema: “Wanapofikia umri wa miaka kumi na mitano, asilimia sabini na tano ya watoto ambao wamepata kushiriki mchezo fulani tayari wamejiuzulu.”
Fikiria Kanada, ambapo mchezo wa magongo uchezwao kwenye barafu hupendwa na wengi. Katika ligi moja ya mchezo wa magongo ya wachezaji wasiolipwa, asilimia 53 ya wachezaji zaidi ya 600,000 walikuwa wenye umri wa chini ya miaka 12. Hata hivyo, ni asilimia 11 tu waliokuwa na umri wa miaka zaidi ya 15. Sababu ilikuwa nini? Vijana wengi wamejiuzulu kabla ya kufikia umri huo. Kwa nini wengi sana hivyo wanajiuzulu?
Wachunguzi wanasema kwamba wanaojiuzulu hivyo hutoa sababu rahisi na yenye kushangaza ya kuondoka kwao: Michezo hiyo haifurahishi tena. Kweli kweli kucheza kwenye timu kwaweza kuwa mradi wenye kuchosha na wenye kupoteza wakati. Gazeti Seventeen liliwaambia wasomaji walo kwamba kujaribiwa na timu kwaweza kumaanisha kufanya kazi “muda wa saa tatu kwa siku, siku tano kwa juma . . . kwa muda wa juma moja au mawili.” Ukiokoka majaribio hayo na kuruhusiwa kujiunga na timu, muda wa saa nyingi za ukuzi na vipindi vya mazoezi uko mbele yako. Mfano mzuri ni mshiriki wa timu ya mpira wa vikapu ya wasichana ambaye hutumia zaidi ya muda wa saa tatu kwa siku akijizoeza kwa ajili ya mchezo wake. Wakati huo ungeweza kutumiwa kufanya jambo jingine lenye umaana.
Bila shaka, vijana wengi hawajali kuwa na hayo magumu ya mazoezi ya ukawaida. Wao hufurahia raha na magumu wanapokuza uwezo wao wa kucheza. Lakini kuna sababu nyingine zinazowafanya vijana wengi wajiuzulu kutoka kwa timu za michezo. Unahitaji kuzijua ili uamue kujiunga na timu au kutojiunga na timu. Kama vile Mithali 13:16 linavyosema, “kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa.” Hivyo makala ya wakati ujao itaendeleza mazungumzo haya.
[Blabu katika ukurasa wa 14]
‘Wachezaji wengi bora wa vyuo vikuu wanaolipiwa masomo yao hukosa kumaliza masomo’
[Picha katika ukurasa wa 13]
Umashuhuri wa wachezaji huwavutia vijana wengi wajiunge na timu za michezo