Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/22 kur. 6-8
  • Kushinda Uzoelevu wa Vitu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kushinda Uzoelevu wa Vitu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Bidii Nyendelevu Yahitajika
  • Kutafuta Kisababishi
  • Kukabiliana na Hisia
  • Kusuluhisha Matatizo
  • Kujistahi
  • Je, Biblia Inaweza Kukusaidia Kushinda Uraibu wa Dawa za Kulevya?
    Habari Zaidi
  • Utendaji Unapokuwa Uzoelevu
    Amkeni!—1994
  • Ni Nani Hupatwa na Uzoelevu, na kwa Nini?
    Amkeni!—1994
  • Nini Ikiwa Mzazi Wangu ni Mraibu wa Dawa za Kulevya au Pombe?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/22 kur. 6-8

Kushinda Uzoelevu wa Vitu

KUACHA uzoelevu ni kama kuhama nyumba ulimolelewa. Hata nyumba hiyo iwe imezeeka na kuharibika, ni vigumu kuiacha. Ilikuwa nyumba yako.

Kama wewe ni mzoelevu, yaelekea kwamba uzoelevu umekuwa nyumba yako ya kihisia-moyo. Ingawa bila shaka nyumba hiyo imekuwa yenye vurugu, unaijua vizuri. “Ulevi ni jambo la kawaida kwangu. Si kawaida niwe timamu bila kulewa,” asema Charles, anayejaribu kuacha ulevi.[2] Itakuwa vigumu sana kuacha uzoelevu, lakini jitihada hiyo itafaa.

Hatua ya kwanza ni kuepuka vitu vitokezavyo uzoelevu.a Usikawie au kuahidi tu kwamba utaacha matumizi mabaya ya vitu. Ondoa kabisa vitu vyote na vile vinavyohusika mara moja. Kipindi kifupi cha athari za kuacha matumizi mabaya ya vitu kitafuata, ambacho nyakati nyingine ni bora kikichunguzwa na daktari. Huo ndio mwanzo wa kuacha kitu hicho kabisa. Lakini usifikiri kwamba haiwezekani kuacha kitu hicho maishani mwote. Anza kwa kuweka mradi unaoweza kutimiza: kuacha kwa mwezi mmoja, juma moja, au hata kwa siku moja. Mwishoni mwa kila kipindi, azimia tena bila kurudia vitendo vyako.

Huo ndio mwanzo tu wa kubadili tabia ya uzoelevu. Biblia yatuhimiza “tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho.” (2 Wakorintho 7:1) Uzoelevu ni mbaya zaidi ya kuchafua mwili. Mwelekeo wa kiroho, au kiakili, huathiriwa pia. Ni nini kiwezacho kukusaidia ushinde uzoelevu, kimwili na kiroho?

Bidii Nyendelevu Yahitajika

“Uzoelevu ni uharibifu wa mwili wote,” asema Dakt. Robert L. DuPont.[3] Kwa hiyo, ni lazima mwili wote uhusishwe katika kushinda uzoelevu. Ni lazima ubadilishe mtazamo wako wote. Jambo hilo huchukua wakati. Hakuna njia ya mkato ya kuacha uzoelevu. Ahadi yoyote ya kuacha uzoelevu itatokeza tu hali ya kurudia uzoelevu haraka.[4]

Lile pigano la kufanya lililo sawa ni la kuendelea. Mkristo mtume Paulo aliandika hivi: “Katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na [“inapigana daima na,” Phillips] ile sheria ya akili zangu.” (Warumi 7:23) Yeye aliandika pia kwamba Wakristo wapaswa ‘kukamilisha utakatifu.’ (2 Wakorintho 7:1, NW) Kitabu Word Pictures in the New Testament chasema kwamba hapo neno “kukamilisha” laonyesha, “kupata utakatifu kwa mwendo unaoendelea, wala si kwa ghafula.”[5] Kwa hiyo kushinda uzoelevu ni mwendo wa hatua kwa hatua.

Kutafuta Kisababishi

Kwa watu wengi, uzoelevu ni jaribio la kusahau matukio mabaya yaliyotokea maishani. “Bulimia [tatizo la ulaji] ilikengeusha akili yangu nisikumbuke yaliyopita,” asema Janis. “Hiyo ikawa njia yangu ya kuendeleza maisha yangu.” Kwa habari ya Janis, kusahau yaliyopita yaliongeza tu uzoelevu wake. Kuelewa sababu zilizofanya Janis awe na tabia hiyo kulimsaidia abadili tabia yake ya uzoelevu.[6]

Wengine hubadili tabia za zamani na wanaweza kukabiliana kwa mafanikio bila kukumbuka yaliyopita. Wengine hupata kwamba hisia zinazotokana na mazingira yao ya zamani huendelea kuchochea tamaa yao ya uzoelevu. Wao wanaweza kuhisi kama mtunga-zaburi Daudi, aliyeandika hivi: “Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, unijaribu, uyajue mawazo yangu; uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, ukaniongoze katika njia ya milele.”—Zaburi 139:23, 24.

Kukabiliana na Hisia

Je! umepata kutoka ndani ya jumba lenye giza na kuingia katika mwangaza wa jua? Unakunja uso wako kwa sababu ya uangavu wa ghafula. Vivyo hivyo, unapoanza kukabiliana na uzoelevu, unaweza kuona kwamba unashambuliwa kwa ghafula na kwa uchungu sana na hisia nyingi. Upendo, hasira, kiburi, wivu, hofu, chuki, na hisia nyinginezo ambazo zimekuwa zikijificha sasa hujitokeza sana.[7]

Hangaiko laweza kukufanya urudie lile giza ambalo umezoea la matumizi mabaya ya vitu. Lakini usipuuze hisia zako. Zinaweza kuwa chanzo bora cha kukupasha habari. Mara nyingi hisia huwa ni ishara tu kwamba jambo fulani lahitaji kuangaliwa. Kwa hiyo ikihitajika fikiria hisia zako. Zinakuambia nini? Ujumbe usipokuwa wazi au kama hisia zaonekana zakushinda, basi zungumza na rafiki mkomavu. (Ayubu 7:11) Si lazima ukabili hisia zako peke yako.—Linganisha Mithali 12:25.

Kumbuka kwamba si lazima hisia zako ziwe adui zako. Yehova Mungu mwenyewe ana hisia zenye nguvu, na binadamu—aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu—vilevile ana hisia. (Mwanzo 1:26; Zaburi 78:21, 40, 41; 1 Yohana 4:8) Kama ule mwangaza wa jua, hisia zaweza kuwa zenye uchungu mara ya kwanza. Lakini baadaye hizo pia zitakuwa, kama jua, chanzo cha mwongozo na joto.

Kusuluhisha Matatizo

Kutembea kwenye kamba iliyonyooshwa juu kwaogofya sana mtu anayeogopa vimo vya juu. Kwa mzoelevu anayeanza kuacha, maisha yaweza kuonekana kama kutembea kwenye kamba iliyonyooshwa juu kunakoogofya sana. Madaraka ya kuwa na maadili ya hali ya juu yanaweza kuleta woga kama ule wa vimo vya juu. Kutazamia kwamba hutafaulu kwaweza kukufanya ufikirie hivi: ‘Bado nitarudia hali hiyo. Mbona nisiirudie sasa?’[9]

Lakini kumbuka kwamba matatizo hayakushambulii wewe binafsi. Hizo ni hali zinazohitaji kushughulikiwa tu. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi. Suluhisha matatizo yako moja-moja. Jambo hilo litakufanya uyaone matatizo yako kwa njia ifaayo.[10]—1 Wakorintho 10:13.

Kujistahi

Marion, anayeacha ulevi, alilazimika kushughulikia hisia yake ya kutojistahi. “Kindani,” yeye asema, “nyakati zote nilihisi kwamba nikiruhusu [watu] wanijue nilivyo hasa, hawawezi kunipenda.”[11]

Kuacha uzoelevu kwalazimisha kwamba ujifunze—labda kwa mara ya kwanza—ustahili wako ukiwa mtu. Hilo ni jambo gumu kama maisha yako yameharibiwa na uzoelevu. Ni nini kinachoweza kusaidia?

Biblia ni kitabu kinachofariji watu walioshuka moyo. Yaweza kukusaidia ujistahi ifaavyo. (Zaburi 94:19) Kwa kielelezo, mtunga-zaburi Daudi aliandika kwamba wanadamu wamevikwa taji la “utukufu na heshima.” Yeye alisema pia kwamba: “Nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.” (Zaburi 8:5; 139:14) Hayo ni maelezo mazuri kama nini ya kujistahi ifaavyo!

Thamini mwili wako, nawe utautunza kwa namna andiko hili lisemavyo: “Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza.” (Waefeso 5:29) Naam, waweza kukabili ugumu wa kuacha uzoelevu.b

Hata hivyo, uzoelevu waweza kutia ndani mambo mengi zaidi. Utendaji waweza kufuatwa kwa bidii ileile na kwa kusudi lilelile la kufuatia dawa za kulevya, kileo, na chakula. Baadhi ya utendaji huo utazungumzwa sasa.

[Maelezo ya Chini]

a Bila shaka, watu wenye matatizo ya ulaji hawawezi kuacha chakula. Lakini, wao waweza kuacha kutumia chakula kikiwa kitu cha kubadili hisia zao. Mielekeo ya kula kupita kiasi, kutokula, kujitapisha kimakusudi, na kufikiria chakula mno kwaweza kubadilishwa na ulaji ufaao.

b Ili kuendelea kujiepusha na kufanya maendeleo katika kuacha uzoelevu, watu wengine wametafuta msaada wa programu za kuwasaidia kuacha uzoelevu. Kuna vituo vingi vya matibabu, hospitali, na mashirika mengine yanayoandaa programu hizo. Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa. Ni vizuri wale wanaotaka kuishi kulingana na kanuni za Biblia wawe waangalifu wasijihusishe na utendaji uwezao kuvunja kanuni za Kimaandiko.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Kuacha [matumizi mabaya ya vitu] kwamaanisha hasa kubadili kabisa mtazamo wa [mtu].” Dakt. Robert L. DuPont.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Hatua ya kwanza ni kuepuka vitu vitokezavyo uzoelevu

[Picha katika ukurasa wa 8]

Hisia zinapokushinda, zungumza na mtu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki