Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/22 kur. 9-11
  • Utendaji Unapokuwa Uzoelevu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Utendaji Unapokuwa Uzoelevu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uzoelevu wa Kazi
  • Uzoelevu wa Televisheni
  • Shurutisho la Kucheza Kamari
  • Kuacha Uzoelevu
  • Je, Biblia Inaweza Kukusaidia Kushinda Uraibu wa Dawa za Kulevya?
    Habari Zaidi
  • Nimenaswa! Naweza Kuachaje Kucheza Kamari?
    Amkeni!—1993
  • Wazoezwaji Wapya wa Uchezaji Kamari—Vijana!
    Amkeni!—1995
  • Kushinda Uzoelevu wa Vitu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/22 kur. 9-11

Utendaji Unapokuwa Uzoelevu

UZOELEVU wa vitu na uzoelevu wa utendaji waweza kulinganishwa na magari-moshi mawili yanayoelekea upande mmoja katika reli moja.a Kila uzoelevu unaelekea upande mmoja au una kusudi lilelile: la kubadili hisia na kuficha hisia zenye kuumiza. Ebu tuone baadhi ya vielelezo vya uzoelevu wa utendaji.

Uzoelevu wa Kazi

Uzoelevu wa kazi umeitwa aina nzuri ya uzoelevu.[2] Kwani wazoelevu wa kazi ni wafanyakazi bora zaidi. Hata hivyo, huenda wao wakahisi hawatimizi chochote. Kazi yaweza kuwa kikengeusha kutoka hisia zenye kuumiza au yaweza kuwa tamaa kubwa sana ya kutaka atambuliwe.

Tabaka ya barafu juu ya maji humkinga mtelezaji juu ya barafu asizame majini; utendaji humlinda mzoelevu wa kazi asizame katika hisia zake. Kama ilivyo na mtelezaji juu ya barafu, mzoelevu wa kazi aweza kustaajabisha wengine kwa kazi yake nzuri. Lakini hayo ni ya juujuu tu. Ni kitu gani ambacho hujificha ndani? Mshauri wa afya ya akili Linda T. Sanford aandika hivi: “Mzoelevu wa kazi asipojishughulisha mno na kazi, yeye aweza kuzamishwa na hisia zenye kuogofya za kushuka moyo, wasiwasi, ghadhabu, kutamauka na utupu.”[3]

Lile shurutisho lenye kukazwa sana ndani ya wazoelevu wengi wa kazi laonyesha kwamba hilo ni tabia ya tangu zamani, labda linaloanza wakati wa malezi ya mtu. Ndivyo lilivyokuwa kwa mwanamke tutakayemwita Mary. Kutokea umri wa miaka sita alijaribu kumfanya baba yake ampende kwa upishi na kazi za nyumbani. “Likawa shurutisho,” yeye asema. “Nilihisi kwamba nikifanya kazi zaidi au nikifanya vizuri zaidi, angenipenda. Yeye alinichambua tu.”

Akiwa mtu mzima Mary angali anang’ang’ana na mawazo yake yasiyofaa. “Kwa ndani bado nahisi kwamba sifai kitu,” yeye akiri. “Ningali nahisi kwamba ni lazima nifanye kitu ili nipendwe, kwamba sifai kitu mpaka niwe ninafanya kitu fulani. Katika vikusanyiko vya kirafiki, mimi hujichosha sana nikipika na kutumika, kana kwamba najaribu kufanya kazi ili nistahili kuwa huko.”[5]

Kwa watu kama Mary, ni muhimu kuwa na maoni yenye usawaziko kuhusu kazi. Biblia husifu kazi yenye bidii. (Mithali 6:6-8; 2 Wathesalonike 3:10, 12) Yehova Mungu mwenyewe ni mwenye matokeo katika kazi. (Zaburi 104:24; Yohana 5:17) Lakini hashurutishwi. Yehova aliona kazi zake za uumbaji kuwa ni njema wakati zilipomalizika na hata wakati zilipokuwa zikiendelea kufanywa.—Mwanzo 1:4, 12, 18, 21, 25, 31; linganisha Mhubiri 5:18.

Mfanyakazi Stadi wa Yehova Mungu, Mwana wake, Yesu, vilevile alionyesha uradhi wake binafsi kwa kazi yake. (Mithali 8:30, 31) Yesu aliahidi wafuasi wake kwamba wao pia wangepata faraja wakifanya kazi pamoja naye. Wakiwa pamoja walifanya mgao uliokuwa muhimu sana. Lakini huo haukuwazuia wasipumzike.—Mathayo 11:28-30; Marko 6:31; linganisha Mhubiri 4:6.

Labda mzazi mmoja alidokeza kwamba ustahili wako ulitegemea kazi zako ama kwamba hungependwa mpaka ulipofanya kazi fulani. Utafurahi kujua kwamba Yehova hana maoni kama hayo juu ya malezi yafaayo. Neno lake lashauri hivi: “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa [“wasihisi kuwa wa hali ya chini,” The Amplified Bible].”[6] (Wakolosai 3:21) Yehova hamnyimi mtu upendo mpaka aufanyie kazi. Upendo wake hauonyeshwi baada tu ya mtu huyo kuanza kumpenda na kumtumikia. Kwa kweli, Biblia yatuambia kwamba “alitupenda sisi kwanza,” naam, hata “tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Mungu alichukua hatua ya kutupenda. (1 Yohana 4:19; Warumi 5:6-8) Na zaidi, Yehova hachambui jitihada zetu zenye unyoofu za kufanya mapenzi yake. Kwa hiyo, utumishi wetu kwake ni wonyesho halisi wa jinsi tunavyompenda.

Uzoelevu wa Televisheni

Wengine huita kutazama televisheni kupita kiasi uzoelevu. “Kama dawa za kulevya au kileo,” aandika Marie Winn katika The Plug-In Drug, “televisheni humfanya mtazamaji aondoke kabisa katika maisha halisi na kuingia katika hali ya kimawazo yenye kufurahisha na yasiyotenda.”[7]

Bila shaka, hakuna ubaya wowote wa kukengeushwa akili kutoka madaraka ya maisha—kwa muda tu. Lakini watazamaji wengine hawarudi kamwe kwa maisha halisi. Mume mmoja ambaye kwa ghafula hangeweza kutazama televisheni wakati televisheni yake ilipoharibika alikiri hivi: “Nahisi kwamba akili yangu ilipotoshwa kabisa kwa miaka hiyo yote. Nilikuwa nikitazama televisheni sana na kwa njia fulani nilishindwa kuiacha.”[8] Kijana aitwaye Kai aeleza juu ya shurutisho kama hilo: “Sitaki kutazama televisheni kwa kadiri ninavyoitazama lakini nimeshindwa kuiacha. Imenidhibiti.”[9]

Kutazama televisheni kupita kiasi hupunguza uwezo wa kufikiri. Biblia yapendekeza kufikiri kwa kutafakari, jambo linalohitaji kadiri fulani ya upweke. (Yoshua 1:8; Zaburi 1:2, 3; 145:5; Mathayo 14:23; Luka 4:42; 5:16; 1 Timotheo 4:15) Upweke huo huogopesha watu wengi. Wao huwa na wasiwasi sana kunapokuwa na ukimya. Wao huogopa kutafakari wakiwa peke yao. Wao hutafuta kwa bidii kufanya jambo lolote la kujazia upweke huo. Televisheni huwa kitu cha kujazia upweke huo upesi. Hata hivyo, televisheni iwe bora kadiri gani, hiyo si maisha halisi.

Shurutisho la Kucheza Kamari

Kucheza kamari hutokana na pupa. Lakini, shurutisho la kucheza kamari latia ndani mambo mengi kuliko fedha tu.b “Nilitaka ule ‘msisimko’ wa kuepa hali halisi ya maisha,” asema Nigel. “Ilikuwa sawa kabisa na kutumia dawa ya kulevya.”[10] Kwa mcheza kamari mwenye ushurutisho, kucheza kamari kwenyewe huthawabisha pia. Haidhuru matokeo yawe nini. Nigel alipoteza rafiki zake. Wengine hupoteza familia zao. Wengi hupoteza afya yao. Na karibu watu wote hupoteza fedha zao. Lakini ni wachache wanaoacha kucheza kamari, kwa sababu jambo kuu si kushinda wala kupoteza fedha. Ni kucheza mchezo huo—ule mwendo—kunakogeuza hisia za mtu na kumfanya asisimke kana kwamba ametumia dawa ya kulevya.

Kucheza kamari kwaweza kuwa kikengeusha kutoka kwenye matatizo ya maisha, lakini hakutasuluhisha matatizo hayo. Mtu aliyejeruhiwa vibaya ahitaji mengi kuliko dawa ya kutuliza uchungu. Ni lazima majeraha yake yatibiwe. Kama kuna majeraha yaliyomfanya mtu acheze kamari, apaswa kuyatambua na kuyatibu. Hilo lahitaji moyo-mkuu, lakini hatimaye kufanya hivyo huthawabisha.

Kuacha Uzoelevu

Ili kuacha uzoelevu wa aina yoyote, ule uchungu wa moyo ambao mara nyingi huchochea uzoelevu hauwezi kupuuzwa. Ni lazima mzoelevu huyo ajaribu kusuluhisha tatizo hilo kwenye chanzo chalo. Hilo ni jambo gumu sana. “Si rahisi kuacha kutumia dawa za kulevya na kileo baada ya kuzitumia kwa miaka 30,” asema mtu mmoja aliyekuwa mzoelevu, “hasa kama uzoelevu wako ulikuwa ukifunika tatizo fulani la ndani.”[12]

Lakini, yafaa kutia bidii hiyo katika kuacha uzoelevu. Mary, mwenye ushurutisho wa kufanya kazi aliyetajwa mapema, afafanua jambo hilo vizuri. “Kwa miaka mingi,” yeye asema, “Nilikuwa nikitoroka mambo niliyoogopa kukabili. Lakini kwa vile sasa nimeyakabili, inashangaza jinsi yamekuwa mambo madogo-madogo tu.”[13]

Hilo limekuwa ono la watu wengi ambao wamefanikiwa kushinda uzoelevu. Badala ya kuendelea kuwa “watumwa wa tabia zenye uharibifu,” wao wamesali wapate “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida” ili wafanikiwe wanapokabili ugumu wa kushinda uzoelevu.—2 Petro 2:19, Today’s English Version; 2 Wakorintho 4:7, NW.

[Maelezo ya Chini]

a Kuna mjadala mkubwa juu ya yale yanayoweza kuitwa uzoelevu na yale yasiyoweza kuitwa uzoelevu. Wengine hupendelea kuita utendaji utokezao uzoelevu “mashurutisho.” Katika makala hizi tumekuwa tukichunguza fungu la uzoelevu ukiwa “njia za kuepuka” matatizo ya kihisia-moyo. Kwa kuwa utendaji waweza kutumiwa pia kuwa njia za kuepuka matatizo ya kihisia-moyo, hapa tutaurejezea kuwa “uzoelevu.”

b Tofauti na kazi na kutazama televisheni, Wakristo huepuka kamari ya aina yoyote ile. (Linganisha Isaya 65:11.) Kwa habari zaidi, ona Amkeni!, Juni 8, 1992, kurasa 3-11, Kiingereza.

[Blabu katika ukurasa wa 9]

‘Neno uzoelevu laweza kutumiwa kwa aina zote za tabia zenye kushurutisha.’ Dakt. J. Patrick Gannon.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kwa mtu mwenye uzoelevu wa kazi, kazi huonekana kuwa ya maana kuliko familia

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kucheza kamari kwaweza kubadili hisia ya mtu na kumfanya asisimke kana kwamba ametumia dawa ya kulevya

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki