Chile-Nchi Isiyo na Kifani, Mkusanyiko Usio na Kifani
WALIKUJA Santiago wakiwa maelfu na makumi ya maelfu, jiji kuu la Chile. Hata katika idadi ya watu ambao ni zaidi ya milioni nne, miminiko hilo lilionekana wazi—wageni hao walivaa beji za buluu zenye kutangaza “Ufundishaji wa Kimungu” Mkusanyiko wa Mashahidi wa Yehova wa 1993.
Zaidi ya 400 walitoka Japani mbali kule-e; zaidi ya 700 kutoka United States. Zaidi ya elfu moja walimwagika ndani kwa ndege na magari kutoka Arjentina iliyo jirani. Gazeti la kila siku La Tercera lilitaarifu hivi katika ripoti yalo baada ya mkusanyiko: “Nyuso nyeupe, za kahawia, ‘za manjano,’ na nyeusi zilitoa uthibitisho wa wazi sana juu ya rangi tofautitofauti na mataifa yaliyowakilishwa katika National Stadium. Kwa kuongezea, wanaume na wanawake kutoka Meksiko, Brazili, Peru, Bolivia, Venezuela, Uhispania, na Japani walionekana wazi sana katika mavazi yao ya kitamaduni.”[1] Wajumbe walitoka Australia, Kanada, Paraguay, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Uswisi, na nyingi za nchi nyinginezo za Amerika Kusini. Zaidi ya wageni 4,500 wa kutoka nchi nyinginezo walitiririka kuingia Santiago juma la Novemba 15, 1993. Halafu mambo yakanoga kukiwa na Mashahidi Wachile 30,000 waliosafiri umbali mkubwa kufika Santiago. Kwa nini walifanya hivyo?
Chile—Nchi Isiyo na Kifani
Wajua, Chile ni nchi maalumu sana kijiografia. Ni nini huifanya ipambanuke na kukosa kifani? Itazame ramani kidogo nawe utaona nchi yenye urefu wa zaidi ya kilometa 4,310 lakini inayopungua kilometa 440 kwenye sehemu iliyo pana zaidi.[1a] Kwa kweli upana wayo wa wastani wazidi kidogo tu kilometa 180.[2] Jiji kuu, Santiago, liko karibu na katikati ya nchi. Mambo hayo yamaanisha kwamba Mashahidi wengi Wachile walilazimika kusafiri mamia ya kilometa pamoja na familia zao ili kufika kwenye mkusanyiko wa kimataifa—wakiwa na uwezo haba wa kiuchumi katika visa vingi. Na bado waliwasili wakiwa maelfu, nyuso zao zikiwa zimepambwa tabasamu.
Chile ni nchi yenye unamnanamna wa kuvutia sana, kuanzia Jangwa la Atakama lililo na ukame kaskazini hadi kwenye mashamba ya mizabibu yenye usitawi mwingi ya jimbo linalozunguka Santiago hadi kuteremkia kusini ambako milima Andes yenye misitu huinama na kuingia katika Pasifiki. Mwisho, kuna ile mito ya barafu na vijito vya bahari ambavyo huishia kwenye jimbo la Antarktika.[3]
Wageni wa kutoka nchi nyinginezo walivutiwa sana na jiji la Santiago. Mjumbe mmoja alieleza hivi: “Niliona shamrashamra za daima, na bado watu walikuwa wenye fadhili na urafiki. Katika maisha yangu nilikuwa sijapata kuona mabasi mengi hivyo barabarani. Mashirika mengi ya mabasi hushindania kupata wateja. Teksi ndogondogo zilikuwa zikipita kukurukakara kila mahali. Ubaya mmoja tu ulikuwa ule uchafuzi. Ili kuupunguza, Santiago lina sheria ambazo magari hupokezana zamu za kutopita barabarani siku moja kwa juma, nayo hupokezana kwa kufuata nambari ya leseni ya gari.” Aliongezea hivi: “Upendezi mwingine ulikuwa wale watoto wa shule waliovalia vizuri, wote wakiwa wamevaa mavazi ya shule, bila yeyote aliyekosa kufanya hivyo. Hakika hakukuwa na mashindano na mbano wa marika huko ili mtu awe na nguo maarufu za mtindo wa karibuni zaidi na viatu murua vya aina ya snika! Na hakuna mtu aliyeonekana kavalia kizembe.”[4]
Ukaribisho Mchangamfu kwa Wageni wa Nchi Nyinginezo
Programu ya “Ufundishaji wa Kimungu” ilianza Alhamisi, Novemba 18. Wajumbe wa nchi nyinginezo walishangaa walipowasili kwenye stediamu ya mpira wa miguu ya Estadio Nacional. Walipokuwa wakipiga mwendo ule wa meta 270 kutoka kwenye mabasi yao kwenda kwenye stediamu, walitembea kwa mtiririko mwembamba kupita katika barabara kuu iliyojaa Mashahidi Wachile—wanaume, wanawake, na watoto—wote wakitaka kuwasalimu kwa kutikisa mikono yao na kukaribisha ndugu zao wenye kuzuru. Wengi hata walikuwa wamejifunza vifungu rahisi vya maneno kwa Kiingereza ili kusema: “Karibuni Chile!” Katika muda wa siku nne zilizofuata, urafiki mwingi ulifanyizwa kujapokuwa na vizuizi vya lugha. Kamera na rekoda za vidio zilifanyishwa kazi ya ovataimu. Maelfu ya vizawadi vya ukumbusho, majina, na anwani vilibadilishanwa.
Idadi Kubwa Ajabu
Kilele cha wahudhuriaji walioonekana kuwa wangeweza kuwa kwenye mkusanyiko huu kilikuwa karibu 60,000—wale Mashahidi Wachile 44,000 wale wageni 4,500, halafu wenye kupendezwa. Wazia mshangao wakati hudhurio la Alhamisi na la Ijumaa lilipokuwa tayari limezidi 50,000. Jumamosi umati uliongezeka kutoka 67,865[5] asubuhi kufikia 70,418 alasiri. Asubuhi ya Jumapili, wakati programu ilipohusisha drama yenye kushughulikia mengine ya matatizo yanayokabili Mashahidi leo, hudhurio lilifikia kilele cha 80,981! Stediamu ilijaa pomoni, na mamia zaidi wakawa wakisikiliza vipaaza-sauti nje. Hilo lilikuwa moja la mambo yaliyofanya mkusanyiko huo uwe usio na kifani—hudhurio kubwa kupita mahudhurio yote ya mikusanyiko iliyofanywa kotekote ulimwenguni katika ule mfululizo wa “Ufundishaji wa Kimungu.” Huo ulikuwa mshangao kwa Mashahidi Wachile na kikawa kionyeshi cha uwezekano wa kukua na kuongezeka katika makutaniko yao karibuni sana wakati ujao.
Ule ubao-umeme wa kutangazia mfungano wa mabao ulitumiwa kutangaza kila hotuba kwa Kihispania na Kiingereza. Hata ulionyesha wakati wasikilizaji walipokuwa wakipiga makofi! Kwenye umalizio ulionyesha salamu za kuagana kwa lugha kadhaa, kutia na Kifaransa, Kiholanzi, Kijapani, na Kijerumani.
Ubatizo Wavutia Vyombo vya Habari
Tukio la kutazamisha jinsi hiyo halingeweza kupuuzwa na vyombo vya habari vya Chile. Utangazaji uliofanywa kila siku na magazeti, redio, na televisheni ulikuwa mzuri sana. Ilikuwa hivyo hasa kuhusu ubatizo wa halaiki uliofanywa Jumamosi. Vidimbwi vidogo 12 vilikuwa vimepangwa kwenye mwisho mmoja wa uwanja wa mpira wa miguu. Wakati wa hotuba ya ubatizo, mamia ya wenye kubatizwa walisimama kama ishara ya uamuzi wao kufuata kielelezo cha Kristo kwa kumtumikia Yehova Mungu. Baada ya hotuba, sala, na wimbo, wahudumu 24 waliovalia kaputura na T-shati nyeupe walijipanga mahali pao, wawili-wawili kwenye kila kidimbwi. Wasaidizi wa kike pia walijitokeza kusaidia. Halafu wenye kubatizwa wa kwanza wakaibuka kutoka kwenye vyumba vyao vya kubadilishia mavazi na kutembea uwanjani, wanaume upande mmoja, wanawake upande ule mwingine. Zilionekana kama safu mbili zisizo na mwisho zikipiga msururu kuelekea kwenye vidimbwi vyao. Kila kitu kilienda kwa utaratibu huku wapiga-picha wa magazeti wakijipanga mahali pao. Katika muda wa saa moja ubatizo ukamalizika—Mashahidi wapya 1,282, walio wahudumu Wakristo, wakawa wamezamishwa katika maji, kufuata kielelezo kilichowekwa na Yesu.
Salamu Maridadi za Kuagana
Hali ya hewa ilikuwa imekuwa nzuri sana juma lote. Ingawaje, huo ulikuwa umekuwa msimu wa Chile wa masika, ambapo mvua huwa haitarajiwi. Jumapili halijoto iliongezeka ikawa digrii 20 na kitu Sentigredi. Karibu kila familia ilileta miavuli na viavuli vya kujilinda dhidi ya lile jua lenye kuwaka sana. Yale maelfu ya viavuli vyenye rangi maridadi yalikumbusha mtu juu ya jeshi la vipepeo wenye kutua juu ya maua. Hotuba ya mwisho ilimalizika karibu saa 11 jioni. Baada ya wimbo na sala, ilikuwa kama kila mtu alisimama zizima. Hakuna aliyetaka mkusanyiko uishe. Vikundivikundi vilibobokwa na hiari ya kuimba nyimbo za Ufalme; mawimbi ya makofi yalisambaa kutoka mwisho mmoja wa stediamu hadi mwisho mwingine; vitambaa vya mkononi vilipungwapungwa na viavuli vikatikiswa vuruvuru kwa upatano wa ajabu. Ilikuwa tamasha ya kugusa moyo—stediamu hii iliyopambwa na Milima Andes kama pazia upande wa nyuma—ikiwa imejazana Wakristo wenye furaha na upendo, wakishukuru kwa ajili ya “Ufundishaji wa Kimungu” uliokuwa umebadili maisha zao.
Wakati wa programu ya Jumapili, ndege wakubwa wawili wa Chile, kwelteyusi, au wapigisha-mabawa wa kusini,[6] walitangatanga kuuvuka uwanja, pindi kwa pindi wakila mdudu au mbegu fulani. Pindi kwa pindi waliikatiza programu kwa miito yao yenye kelele kali. Wakati wa hotuba ya mwisho, waliinuka wakienda zao polepole, kama kwamba walihisi programu ilikuwa imemalizika, wakazunguka duara ili wapate nguvu za kupaa, wakarukia mbali. Bila shaka watarudi, hali moja na vile Mashahidi wa Yehova watakavyofurahi kurudi kwenye stediamu hiyo mwaka mwingine kushiriki shangwe na imani yao—katika Chile, un país singular, nchi isiyo na kifani.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Zaidi ya 80,000 walihudhuria mkusanyiko katika Santiago
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 18]