Watunza-Nyumba Wadogo Walio Hodari Sana
Na mleta-habari za Amkeni! katika Afrika Kusini
MAPENGO katika misitu ya Afrika yenye mvua hujaziwa mara nyingi na mti wenye matawi yaliyo na matundu uitwao barteria.[1] Ili ufikie kimo chao cha juu zaidi, ni lazima mti huo ushindane na mingine ambayo hung’ang’ania kufikia kilele cha msitu huo. Ili kufaulu katika shindano hilo, barteria huhitaji msaada ili ujiondoe kwenye mbano wa mimea mitambaaji yenye kuusonga na kutoka kwenye vijanimaji ambavyo huzuia nuru isifikie majani yao. Hapo ndipo siafu weusi husaidia sana wakiwa watunza-nyumba.[2] Uhusiano ulio kati ya siafu na mti ulipigwa picha ya filamu katika Korup, msitu-mvua wa Cameroon, hiyo ikiwa ni sehemu ya sinema fupi ya TV ihusuyo shughuli za kijamii iitwayo African Rainforest: Korup, iliyotayarishwa na Phil Agland na Michael Rosenberg.[3]
Hiyo sinema fupi ihusuyo shughuli za kijamii huonyesha siafu mpya aliye malkia akitafuta mti barteria. Kwa silika, malkia huyo ajua kwamba matawi yenye matundu ya mti huo ndipo mahali pafaapo kabisa kuanzisha jamii yake. Baada ya kutoboa tundu katika tawi moja, malkia ataga mayai yake humo ndani. Hayo matawi yenye matundu ni makao pia ya wadudu wadogo wa kusawazisha mazingira ambao hula utomvu wa mti huo. Wale siafu huwatunza wadudu hao kama mifugo na kuwakama maziwa ili kupata kinywaji cha kujenga mwili.
Mara tu ile jamii ya siafu ikiisha kuwa kubwa vya kutosha, hiyo huanza kufukuza wakaaji wengine watoke katika makao hayo na kusafisha ule mti. Inasisimua kama nini kuwatazama watunza-nyumba wadogo hao wenye maarifa mengi! Baadhi yao hushuka chini ya mti huo na kushambulia mimea mitambaaji ambayo hutisha kuusonga pumzi. Wadudu hao hutafunatafuna kupenya ndani kabisa ya mashina na hivyo kuiua miti mitambaaji. Siafu wengine waweza kuonwa wakiondoa majani ya takataka, vijanimaji, na kuvumwani. Hata kiwavi apatikanaye amefichika chini ya jani fulani huondoshwa.
“Kwa uangalifu mwingi,” yaeleza hiyo sinema fupi ya TV ihusuyo shughuli za kijamii, “wale siafu hufanya usafi kwa kuondoa kila kipande cha takataka. Barteria ukiisha kuondolewa wadudu na mitambaaji yote yenye kudhuru, sasa waweza kushindana kwa mafanikio pamoja na miti mingine, kwa kulindwa na siafu wao. Siafu hao nao huwa waweza kutumia matawi ya barteria yenye matundu ili kuchunga wadudu wao wenye kusawazisha mazingira—chanzo chao cha pekee cha chakula—tena kulea watoto wao.”
Lo, siafu hao ni wafanyakazi wenye bidii iliyoje! Mithali moja ya kale husema hivi: “Ewe mvivu, mwendee chungu [siafu, ZSB], zitafakari njia zake ukapate hekima.”—Mithali 6:6.