Vijana Wenye “Nguvu Ipitayo Iliyo ya Kawaida”
WEWE ni kijana. Una miaka 12 tu. Wewe una familia yenu uipendayo. Una rafiki za shule uwafurahiao. Wewe huenda kutembea kwenye ufuo wa bahari na milimani. Wewe huhisi ukistaajabu sana utazamapo anga ya usiku ikiwa imejaa nyota. Una muda mwingi sana wa kuishi kwa sababu wewe ni mchanga.
Na sasa una kansa. Habari hizo ni pigo la kuhuzunisha ukiwa na miaka 60. Ni pigo la kuvunja moyo kabisa ukiwa na miaka 12.
Lenae Martinez
Hivyo ndivyo ilivyoonekana kwa Lenae Martinez wa miaka 12. Tumaini la msichana huyo lilikuwa kuishi milele katika dunia-paradiso. Tumaini hilo liliimarishwa na mazoezi ya Biblia aliyokuwa amekuwa akipokea kutoka kwa wazazi wake, ambao ni Mashahidi wa Yehova.[1] Kwani je, si yeye mwenyewe alikuwa amesoma katika Biblia kwamba dunia ingeendelea milele, kwamba iliumbwa ikaliwe milele, na kwamba wasikivu wangeirithi milele?—Mhubiri 1:4; Isaya 45:18; Mathayo 5:5.
Sasa msichana huyu alikuwa katika Hospitali ya Watoto Bondeni katika Fresno, Kalifornia, Marekani. Alikuwa amelazwa huko kwa lile lililoonekana kuwa ambukizo la figo. Hata hivyo, uchunguzi mbalimbali ulifunua kwamba alikuwa na leukemia. Madaktari wenye kumtibu Lenae waliamua kwamba chembe nyekundu na visahani vya damu vilivyotiwa katika pakiti zitiwe mishipani na utibabu wa kikemikali uanzwe mara hiyo.[2]
Lenae alisema kwamba hakutaka damu yoyote wala vifanyizo vyenye damu, kwamba yeye alikuwa amefundishwa kwamba Mungu hukataza hilo, kama ionyeshwavyo katika vitabu vya Biblia vya Mambo ya Walawi na Matendo. “Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu [roho takatifu, New World Translation] na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati.” (Matendo 15:28, 29) Wazazi wake walimwunga mkono katika msimamo huu, lakini Lenae akakazia kwamba huo ulikuwa uamuzi wake na ulikuwa wa maana sana kwake.[3]
Madaktari waliongea mara kadhaa pamoja na Lenae na wazazi wake. Hata hivyo, walikuja tena alasiri moja. Lenae alisema hivi kuhusu ziara hii: “Nilikuwa nikihisi nikiwa dhaifu sana kutokana na maumivu yote na nilikuwa nimekuwa nikitapika damu nyingi. Waliniuliza maswali yaleyale, ila kwa njia tofauti. Mimi nikawaambia tena: ‘Sitaki damu yoyote wala vifanyizo vyenye damu. Ingekuwa afadhali nikubali kifo, ikiwa lazima, kuliko kuvunja ahadi yangu kwa Yehova Mungu ya kufanya penzi lake.’”[4]
Lenae aliendelea kusema: “Walirudi asubuhi iliyofuata. Hesabu ya visahani ilikuwa ikipungua, na homa yangu ilikuwa ingali kali. Ningeweza kuona kwamba yule daktari alinisikiliza zaidi safari hii. Hata ingawa hawakupendezwa na msimamo wangu, walisema nilikuwa [msichana] aliyekomaa sana wa miaka 12.[5] Baadaye daktari wangu wa magonjwa ya watoto aliingia akaniambia alisikitika kuniambia kwamba hakuna kitu ambacho kingenisaidia isipokuwa ule utibabu wa kikemikali na mitio ya damu mishipani. Aliondoka na kusema angerudi baadaye.[6]
“Alipoondoka, nilianza kulia sana kwa sababu yeye alikuwa amenitunza maisha yangu yote, na sasa nilihisi ni kama alikuwa akinisaliti.[7] Alipoingia baadaye, nilimwambia jinsi alivyokuwa amenifanya nihisi—kwamba hakunijali tena. Hii ilimshangaza, naye akasema alisikitika. Hakuwa na lengo la kuniumiza. Alinitazama akasema: ‘Haya, Lenae, ikiwa lazima itukie hivyo, basi tutaonana mbinguni.’ Akavua miwani yake na, akiwa na machozi makubwa machoni mwake, akasema ananipenda na kunipa kumbatio kubwa. Nilimshukuru na kusema: ‘Asante. Mimi nakupenda wewe pia, Dakt. Gillespie, lakini natumaini kuishi katika dunia-paradiso katika ufufuo.’”[8]
Halafu madaktari wawili na mwanasheria mmoja wakaja, wakawaambia wazazi wa Lenae kwamba walitaka kuongea na Lenae akiwa peke yake, wakawaomba wazazi waondoke, wakafanya hivyo. Muda wote wa mazungumzo haya, madaktari walikuwa wamekuwa na ufikiro na fadhili sana na walivutiwa na njia ya Lenae ya kujisemea waziwazi na usadikisho wake wa kina kirefu.
Walipokuwa peke yao pamoja naye, wakamwambia kwamba alikuwa akifa kutokana na leukemia na kusema hivi: “Lakini mitio ya damu mishipani itarefusha maisha yako. Ukikataa damu, utakufa katika muda wa siku chache.”
“Nikikubali damu,” Lenae akauliza, “hiyo itarefusha maisha yangu kadiri gani?”
“Karibu miezi mitatu hadi sita,” wakajibu.
“Naweza kufanya nini katika miezi sita?” akauliza.
“Utapata nguvu. Waweza kufanya mambo mengi. Waweza kuzuru eneo la maonyesho la Disney World. Waweza kuona mahali pengine pengi.”
Lenae alifikiri kidogo, kisha akajibu: “Nimemtumikia Yehova maisha yangu yote, miaka 12. Yeye ameniahidi uhai wa milele katika Paradiso nikimtii. Sitageuka nimwache sasa kwa muda wa miezi sita ya maisha. Nataka kuwa mwaminifu mpaka nife. Halafu najua atanifufua kutoka kifoni katika wakati wake upasao na kunipa uhai wa milele. Kisha nitakuwa na wakati tele wa kila jambo nitakalo kufanya.”[9]
Madaktari na yule mwanasheria walionekana wakivutiwa. Walimpongeza na kwenda nje na kuambia wazazi wake kwamba yeye yuafikiri na kuongea kama mtu mzima na aweza kufanya maamuzi yake mwenyewe. Walipendekeza kwa halmashauri ya maadili ya Hospitali ya Watoto Bondeni kwamba Lenae aonwe kuwa mtoto aliyekomaa. Halmashauri hii, yenye madaktari na wataalamu wengine wa kutunza afya, pamoja na profesa mmoja wa maadili kutoka Chuo Kikuu cha Fresno State, walifanya uamuzi wa kumruhusu Lenae afanye maamuzi yake mwenyewe kuhusu utibabu. Walimwona Lenae kuwa mtoto aliyekomaa. Hakuna agizo la mahakama lililotafutwa.[10]
Baada ya usiku mrefu, wa magumu, saa 12:30 asubuhi, Septemba 22, 1993, Lenae alilala usingizi katika kifo mikononi mwa mama yake. Fahari na utulivu wa usiku huo vimekazika kikiki katika akili za wale waliokuwapo. Kulikuwako 482 waliohudhuria mkutano wa ukumbuko, kutia na madaktari, wauguzi, na walimu, waliokuwa wamevutiwa na imani na uaminifu-maadili wa Lenae.[11]
Wazazi na rafiki za Lenae walishukuru sana kwamba madaktari na wauguzi na wasimamizi wa Hospitali ya Watoto Bondeni walikuwa na ufahamu mwingi wa kutambua ukomavu wa mtoto huyu na kwamba haikuwa lazima kuwe na kesi ya mahakamani ili kufanya uamuzi huo.
Crystal Moore
Ufikirio wa jinsi hiyo haukupewa Crystal Moore mwenye miaka 17 alipolazwa katika Kituo cha Tiba cha Kipresbiteri cha Columbia katika Jiji la New York. Msichana huyo alikuwa na ugonjwa wa kufura matumbo. Crystal alipolazwa hospitalini, msichana huyo akiwa pamoja na wazazi wake alikazia mara nyingi kwamba alikataa damu. Yeye hakutaka kufa; bali, alitaka utibabu uliopatana na amri ya Biblia ya kujiepusha na damu.—Matendo 15:28, 29.[12]
Kikoa cha wanatiba wenye kumtunza Crystal kilikuwa na uhakika kwamba hali yake ilitaka mtio wa damu mishipani. Daktari mmoja alitaarifu wazi sana hivi: “Ikiwa Crystal hatatiwa damu mishipani kufikia Alhamisi, Juni 15, basi Ijumaa, Juni 16, atakuwa amekufa!” Juni 16, Crystal hakuwa amekufa, na hospitali ilipeleka ombi kwenye Mahakama Kuu ya Jimbo la New York ili ipewe mamlaka ya kulazimisha mitio ya damu mishipani.[13]
Kwenye usikizi wa kesi, ambayo ilifanywa haraka-haraka hospitalini asubuhi hiyo, mmoja wa hao matabibu alishuhudia kwamba Crystal alihitaji yuniti mbili za damu mara hiyo na angeweza kuhitaji angalau yuniti kumi zaidi. Alizidi kutaarifu kwamba kama Crystal angejaribu kukinza mitio ya damu mishipani, yeye angemfunga vifungo kwenye vifundo vya mikono na miguuni ili kutekeleza hatua hiyo. Crystal aliwaambia madaktari kwamba yeye ‘angepiga mayowe na viyowe’ kama wangejaribu kumtia damu mishipani na kwamba kwa kuwa ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, yeye anaona utiaji wowote wa damu kwa njia ya kulazimisha kuwa ni chukizo sana kama kunajisiwa.[14]
Crystal alinyimwa fursa ya kujisemea mbele ya mahakama kuonyesha uwezo wake wa kujifanyia maamuzi, ijapokuwa kwenye kesi wakili wake aliomba mara nyingi kwamba apewe fursa hiyo. Ingawa ni punde tu Cyrstal alikuwa ametoka kupokea tuzo katika Programu ya Kutuza Vijana Bora kwa kutambua ubora wake wa kimasomo na uongozi kwenye shule yao ya sekondari, hakimu wa kusikia kesi alikataa kumruhusu atoe ushuhuda wa kimaandishi kwamba anakataa damu. Hiyo ilikuwa sawa na kumnyima Crystal haki za kutendewa kulingana na sheria, kujiamulia yapasayo kutendwa na mwili wake, faragha ya kibinafsi, na uhuru wa kidini.[15]
Ingawa mahakama ya kusikiza kesi haikutaka kumruhusu Crystal atoe ushuhuda wa kimaandishi, mahakama hiyo ilimzuru Crystal akiwa peke yake katika chumba chake kwa karibu dakika 20. Baada ya ziara hiyo hakimu mwenye kusikiza kesi alisema kwamba Crystal alikuwa “kwa wazi ni mwenye akili sana” na “mwenye kusema wazi sana” na akaeleza kwamba Crystal “hakika alikuwa timamu katika akili” na “mwenye kuweza kujieleza kikamili.” Yajapokuwa maoni haya, mahakama ya kusikiza kesi ilikataa katakata kumpa Crystal fursa ya kujiamulia matibabu.[16]
Asubuhi ya Jumapili, Juni 18, Crystal alihitaji upasuaji wa dharura, naye akauidhinisha, lakini akaendelea kukataa damu. Ni gramu 85 tu za damu zilizopotezwa katika hatua hiyo. Hata hivyo, matabibu walidai kwamba kutia damu mishipani kungeweza kuhitajiwa baada ya upasuaji. Daktari mwingine alishuhudia kwamba hakuna utiaji damu uliohitajiwa. Alikuwa amekuwa na kawaida ya kutibu visa kama hivyo bila damu kwa muda wa miaka 13 iliyopita, na hakuna mitio ya damu mishipani iliyohitajiwa kamwe baada ya upasuaji.[17]
Juni 22, 1989, mahakama ya kusikiza kesi iliipa hospitali haki ya muda ya kumtunza Crystal kwa makusudi ya kumtia damu mishipani ikiwa tu “ni lazima kulinda na kuokoa uhai wake.” Utunzaji huo ulikomeshwa wakati Crystal aliporuhusiwa kutoka hospitalini. Crystal hakupata kuhitaji damu kamwe, na hakuna yoyote iliyopata kutiwa mishipani, lakini inashtusha kuona jinsi mahakama ilivyomtenda Crystal.[18]
Tangu aliporuhusiwa kutoka hospitalini, Crystal alihitimu shule ya sekondari kwa kutunukwa heshima ya mafanikio. Muda mfupi baada ya hapo, akawa mhudumu wa wakati wote akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Akawa mwongoza-watalii kwenye Jumba la Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova katika Jiji la Jersey na kujitolea kuwa mshirika wa kikundi cha wafanyakazi ambao hujenga na kufanya upya Majumba ya Ufalme.[19]
Hata hivyo, madaktari kwenye Kituo cha Tiba cha Kipresbiteri cha Columbia walisema kwamba ikiwa yeye hakutiwa damu mishipani Juni 15, angekuwa amekufa Juni 16 na kwamba kama angekinza kutiwa damu mishipani, angefungwa vifungo kwenye vifundo vya mikono na miguuni. Wakati madaktari wenye kutaka maagizo ya mahakama ili kutia damu watangazapo wazi sana kwamba ikiwa hakimu hatakubaliana nao mara hiyo mgonjwa atakufa, acheni wakumbuke kisa cha Crystal Moore.
Lisa Kosack
Usiku wa kwanza wa Lisa katika Hospitali ya Toronto kwa Ajili ya Watoto Wagonjwa ulikuwa mbaya wee. Yeye aliingia saa 10 alasiri na mara hiyo akafanyiwa mfululizo wa uchunguzi mbalimbali. Hakufika kwenye chumba chake mpaka saa tano na robo ya usiku. Ulipofika usiku wa kati—haya basi, acha Lisa aeleze lililotukia. “Usiku wa kati muuguzi mmoja aliingia akasema: ‘Lazima nikutie kiasi fulani cha damu.’ Mimi nikalia kwa kupaaza sauti: ‘Siwezi kukubali damu kwa sababu mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova! Natumaini wajua hilo! Natumaini wajua hilo!’ ‘Eeh, ndiyo, najua,’ akasema yule muuguzi, na mara hiyo akauvuta mrija wangu wa kutilia damu mishipani na kuupachika pakiti ya damu. Mimi nilikuwa nikilia na nikipiga mayowe ya ajabu.”[20]
Lo, ulikuwa utendeo ulio mkavu wa hisia kama nini tena wa ukatili kwa msichana wa miaka 12 aliye mgonjwa na mwenye hofu nyingi katikati ya usiku katika mazingira ya kigeni! Wazazi wa Lisa walikuwa wamempeleka Hospitali ya Toronto kwa Ajili ya Watoto Wagonjwa wakitumaini kupata madaktari wenye fadhili na ushirikiano. Badala ya hivyo, binti yao alifanyiwa ule mtio wa damu mishipani uliotesa sana hisia zake usiku wa kati, ujapokuwa msimamo wa Lisa na wazazi wake kwamba damu au vifanyizo vyenye damu ni uvunjaji wa sheria ya Mungu na havipasi kutumiwa.—Matendo 15:28, 29.[21]
Asubuhi iliyofuata hospitali ilitafuta agizo la mahakama la kumfanyia mitio ya damu mishipani. Kesi hiyo ilichukua siku tano, ikisimamiwa na Hakimu David R. Main. Ilifanywa katika chumba kimoja kwenye hospitali hiyo, huku Lisa akihudhuria siku zote tano.[22] Lisa alikuwa na leukemia kali iliyotokana na mfanyizo mwingi mno wa chembe nyeupe za damu kabla hazijakomaa, hali ambayo kwa kawaida huua, ingawa madaktari walishuhudia kwamba kadiri ya kuponywa ilikuwa asilimia 30.[23] Walimwandikia atiwe damu mishipani mara nyingi na kufanyiwa utibabu mwingi wa kikemikali—utibabu unaohusisha maumivu na athari za kudhoofika.[24]
Siku ya nne ya kesi, Lisa alitoa ushuhuda. Mojapo maswali aliyoulizwa lilikuwa jinsi ule mtio wa damu mishipani wa kulazimishwa wakati wa usiku-kati ulivyomfanya ahisi. Akaeleza kwamba ulimfanya ahisi kama mbwa mwenye kutumiwa kwa jaribio, kwamba alihisi alikuwa akinajisiwa, na kwamba utoto wake ulifanya watu fulani wafikiri wangeweza kumtenda lolote. Yeye alichukia kuona damu ya mtu mwingine ikimwingia, akishangaa kama angepata UKIMWI au mchochota wa ini au ugonjwa fulani mwingine wenye kuambukiza kutokana nayo. Na hasa, yeye alihangaikia vile Yehova angefikiri juu ya kuvunja kwake sheria yake dhidi ya kuingiza damu ya mtu mwingine katika mwili wake. Alisema kama hilo lingetendeka tena, “angekigonga na kukipiga teke kiguzo cha kushikilia mrija wa damu mpaka kianguke na kuing’oa ile sindano ya kutilia damu hata kama ingeuma namna gani, na kuitoboatoboa pakiti ya damu.”[25]
Wakili wake aliuliza, “Wewe wahisi namna gani, Chama cha Kusaidia Watoto kitoapo ombi la kwamba wazazi wako wanyang’anywe haki ya utunzaji ili wapewe wao?”[26]
“Eeh, yanifanya nihisi hasira sana, tena sana; yanifanya nihisi kwamba wao ni wakatili kwa sababu wazazi wangu hawajapata kamwe kunipiga, wamenipenda nami nawapenda, nami nilipokuwa nikishikwa na homa za kooni au mafua au chochote kile, wao walinitunza. Maisha yao yote yalikuwa ya kunihangaikia, na eti sasa mtu fulani, eti kwa sababu tu hakubaliani nao, aje na kuniondoa hivihivi tu kutoka kwao, naona huo ni ukatili mwingi sana, tena sana, nao waniudhi sana.”[27]
“Je! wewe wataka kufa?”
“La, sidhani mtu yeyote ataka kufa, lakini nikifa sitaogopa, kwa sababu najua kwamba nina tumaini la uhai wa milele katika paradiso duniani.”[28]
Ni macho machache ambayo hayakutokwa na machozi Lisa alipokuwa akizungumza kwa moyo mkuu juu ya kifo chake chenye kukaribia, imani yake katika Yehova, na uamuzi wake thabiti wa kubaki mtiifu kwa sheria yake juu ya utakato wa damu.
“Lisa,” wakili wake akaendelea kusema, “je, kungekuwa na tofauti yoyote ukijua kwamba mahakama yakuagiza ukubali mitio ya damu mishipani?”
“La, kwa sababu bado nitabaki mwaminifu kwa Mungu wangu na kusikiliza amri zake, kwa sababu Mungu ni mkubwa sana kuliko mahakama yoyote au mwanadamu yeyote.”[29]
“Lisa, wewe ungependa hakimu aamue nini katika kesi hii?”
“Eeh, kile ambacho ningependa hakimu aamue katika kesi hii ni kuacha tu nirudishwe kwa wazazi wangu na kuacha wao wawe tena na haki ya kunitunza ili niweze kuwa mwenye furaha, na ili niweze kwenda nyumbani na kuwa katika mazingira yenye furaha.”[30]
Na hivyo ndivyo Hakimu Main alivyoamua. Vifuatavyo ni visehemu vilivyotokana na uamuzi wake.
“L. ameiambia mahakama hii wazi na bila kuficha kwamba, likifanywa jaribio la kumtia damu mishipani, yeye atazuia huo mtio wa damu mishipani kwa nguvu zote awezazo kupata. Amesema, nami namwamini, kwamba atapiga mayowe na kujitahidi sana na kwamba atang’oa ile sindano mkononi mwake na kujaribu kuiharibu damu iliyo kifukoni juu ya kitanda chake. Mimi nakataa kutoa agizo lolote ambalo lingetia mtoto huyu katika hiyo taabu kubwa.”[31]
Kwa habari ya mtio wa damu uliolazimishwa usiku-kati, hakimu alisema hivi:
“Mimi naona wazi kwamba yeye amebaguliwa kwa sababu ya dini yake na umri wake kulingana na kifungu cha 15(1). Katika hali hizi, alipotiwa damu mishipani, haki yake ya kulinda mwili wake kulingana na kifungu cha 7 iliingiliwa.”[32]
Maoni yake juu ya Lisa mwenyewe yanapendeza:
“L. ni mtu wa kuvutia, mwenye akili nyingi ajabu, mwenye kusema waziwazi, mwungwana, mwitikivu na, la maana zaidi, mwenye moyo mkuu. Yeye ana hekima na ukomavu unaozidi sana miaka yake nami naona ni sahihi kusema kwamba ana sifa zote nzuri ambazo mzazi angetaka katika mtoto. Kwa maoni yangu, yeye hawezi kutikiswa wala kubadili imani zake za kidini hata kuwe na ushauri mwingi kadiri gani kutoka kwenye chanzo chochote kile au msongo kutoka kwa wazazi wake au mtu mwingine yeyote, kutia na agizo la mahakama hii. Mimi naamini kwamba L. K. apaswa kupewa fursa ya kupambana na ugonjwa huu kwa fahari na amani ya akili.”[33]
“Ombi limefutwa.”[34]
Lisa na familia yao waliondoka hospitalini siku hiyo. Kweli Lisa alipambana na ugonjwa wake kwa fahari na amani ya akili. Alikufa kwa amani nyumbani, akiwa katika mikono yenye upendo ya mama na baba yake.[35] Kwa kufanya hivyo alijiunga na vijana wengine wengi Mashahidi wa Yehova waliomtanguliza Mungu. Tokeo ni kwamba, yeye, pamoja nao, atafurahia utimizo wa ahadi ya Yesu: “Yeye apotezaye uhai wake kwa ajili yangu ataupata.”—Mathayo 10:39, kielezi cha chini.
Ernestine Gregory
Akiwa na umri wa miaka 17, Ernestine alichunguzwa akaonwa kuwa mwenye leukemia. Alipolazwa hospitalini, alikataa kuidhinisha utumizi wa vifanyizo vyenye damu ili visaidie utibabu wa kikemikali ambao madaktari walitaka kutekeleza. Kwa sababu ya Ernestine kukataa na kuungwa mkono na mama yake juu ya chaguo lake la utibabu usio na damu, hospitali iliripoti jambo hilo kwa maofisa wa masilahi katika Chicago, Illinois, Marekani, nao wakatafuta agizo la mahakama kutumia damu. Usikizi ulipangwa, na huko mahakama ya kusikiza kesi ikasikia ushuhuda kutoka kwa Ernestine, daktari mmoja, tabibu mmoja wa magonjwa ya akili, na wakili mmoja, na pia kutoka kwa watu wengine waliohusika.[36]
Ernestine alimwambia daktari wake kwamba yeye hakutaka damu. Kwamba huo ulikuwa uamuzi wake wa kibinafsi kwa msingi wa usomaji wake wa Biblia. Kwamba damu ikitiwa mishipani kwa agizo la mahakama bila hiari yake, bado huko ni kukosa staha kwa sheria ya Mungu na ni kosa machoni pa msichana huyo, hata kama mahakama itatoa mamlaka ya kufanya hivyo. Kwamba yeye hakupinga matibabu na hakutaka kufa. Kwamba uamuzi wake haukuwa wasia wa kifo, haukuwa kujiua; hata hivyo, yeye hakuhofu kifo.[37]
Stanley Yachnin, M.D., alishuhudia kwamba ‘alivutiwa na ukomavu wa Ernestine, hali yake ya kujitambua,’ na weupe wa moyo wa imani zake za kidini. Pia alisema Ernestine alielewa hali na matokeo ya ugonjwa wake. Kwa sababu ya ufahamu wake, Dakt. Yachnin hakuona uhitaji wa kuita daktari wa magonjwa ya akili au mwanasaikolojia.[38]
Hata hivyo, mmoja wao aliitwa, Ner Littner, M.D., daktari wa magonjwa ya akili, na baada ya kuongea na Ernestine akawa na maoni ya kwamba msichana huyo alikuwa na ukomavu wa mtu aliye kati ya umri wa miaka 18 na 21. Alitaarifu kwamba Ernestine alionyesha uelewevu wa matokeo ya kukubali au kukataa mitio ya damu mishipani. Alisema msichana huyo alikubali hilo, si kwa sababu alikuwa chini ya udhibiti wa mtu mwingine, bali kwa sababu aliliamini yeye mwenyewe. Dakt. Littner alisema Ernestine apaswa kuruhusiwa afanye uamuzi wake mwenyewe katika jambo hili.[39]
Jane McAtee, wakili wa hospitali hiyo, alishuhudia kwamba baada ya kumhoji Ernestine, aliamini kwamba Ernestine alielewa hali ya ugonjwa wake na kwamba ‘alionekana kuwa mwenye uwezo kamili wa kuelewa uamuzi wake na kukubali matokeo yao.’[40]
Mahakama ilivutiwa sana pia na ushuhuda wa Ernestine. Mahakama ilipata kwamba Ernestine alikuwa kijana aliyekomaa wa miaka 17, kwamba uamuzi wa Ernestine ulifanywa bila kutegemea mtu mwingine, na kwamba yeye aliielewa hali yake ya shida kubwa. Hata hivyo, ingawa alionyesha kwamba yeye ni kijana wa kike aliyekomaa mwenye uwezo wa kujifanyia maamuzi ya utibabu kwa kufahamu na kuelewa mambo vizuri kwa kupatana na viwango na masadikisho yake yenye kushikiliwa sana, mahakama hiyo yenye kusikiza kesi ilistaajabisha kwa kutoa agizo la kuruhusu mitio ya damu mishipani.[41]
Agizo la mahakama ya kusikiza kesi lilikatiwa rufani mara ya kwanza kwenye Mahakama ya Rufani ya Illinois. Katika uamuzi wa wawili-kwa-mmoja, Mahakama ya Rufani ilishikilia kwamba Ernestine hangeweza kulazimishwa kukubali mitio ya damu mishipani dhidi ya penzi lake. Mahakama ilisababu kwamba haki ya Ernestine ya kutumia Sahihisho la Kwanza ili kumruhusu awe na uhuru wa kidini pamoja na haki yake ya kuruhusiwa kikatiba atumie faragha yake ililinda haki yake akiwa mtoto aliyekomaa kukataa mitio ya damu mishipani kwa sababu za kidini.[42]
Ndipo maofisa wa masilahi ya watoto walipokata rufani kwenye Mahakama Kuu ya Illinois juu ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani. Mahakama Kuu ya Illinois iliuthibitisha uamuzi, ikikata maneno kwamba hata ingawa Ernestine alikuwa mtoto, yeye alikuwa na haki ya kukataa matibabu asiyoyataka. Mahakama kuu hiyo ilifanya uamuzi kwa msingi wa sheria zilizotungwa kutokana na vikao vya zamani mahakamani kuhusu haki ya mtu kujiamulia jinsi mwili wake utakavyotendewa na jinsi ya kushughulika na mtoto aliyekomaa.[43] Kiwango cha kutumiwa katika visa vya watoto waliokomaa katika Illinois kilitajwa kwa muhtasari na Mahakama Kuu ya Illinois katika taarifa ifuatayo:
“Ikiwa uthibitisho ni wazi na wenye kusadikisha kwamba mtoto amekomaa kadiri inayotosha kuyafahamu matokeo ya matendo yake, na kwamba mtoto huyo amekomaa kadiri inayotosha kutumia uamuzi wa mtu mzima, basi ile kanuni ihusuyo mtoto aliyekomaa yampa haki ya sheria zilizotungwa kutokana na vikao vya zamani mahakamani ili aidhinishe au akatae matibabu.”[44]
Ernestine hakupata utibabu wowote wa kikemikali wala mitio ya damu mishipani, hata hivyo msichana huyo hakufa kutokana na leukemia kama vile madaktari walivyotaka kuaminisha mahakama. Ernestine alisimama imara na kumtanguliza Mungu, kama vijana wale wengine waliotangulia kutajwa. Kila mmoja alipokea “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida.”—2 Wakorintho 4:7, NW.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Hatari za Kutiwa Damu Mishipani
The New England Journal of Medicine, toleo la Desemba 14, 1989, liliripoti kwamba kipimo kimoja tu cha damu huenda kikabeba virusi za UKIMWI za kutosha kusababisha maambukizo hadi milioni 1.75![1]
Katika 1987, baada ya kujulikana kwamba UKIMWI ulikuwa ukipitishwa na ugavi wa damu ya mwenye kujitolea kuchanga, kitabu Autologous and Directed Blood Programs kiliomboleza hivi: “Hili lilikuwa ndilo tokeo-kinyume la kutia uchungu mwingi zaidi ya matokeo-kinyume yote ya kitiba; kwamba zawadi ya damu yenye kupa uhai ingeweza kugeuka kuwa chombo cha kifo.”[2]
Dakt. Charles Huggins, mkurugenzi wa huduma za kutia damu mishipani kwenye hospitali moja ya Massachusetts, Marekani, alisema hivi: “Hicho ndicho kitu hatari zaidi tutumiacho katika tiba.”[3]
Jarida Surgery Annual lilikata shauri hivi: “Kwa wazi, mtio wa damu ulio salama zaidi ni ule ambao haujafanywa.”[4]
Kwa sababu kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kurudi kwa kansa baada ya upasuaji iwapo mitio ya damu mishipani imefanywa, Dakt. John S. Spratt alisema hivi katika The American Journal of Surgery, toleo la Septemba 1986: “Mpasuaji wa kansa huenda akahitaji kuwa mpasuaji asiyetumia damu.”[5]
Jarida Emergency Medicine lilisema hivi: “Mambo tuliyojionea kwa Mashahidi wa Yehova yangeweza kufasiriwa kumaanisha kwamba hatuhitaji kutegemea mitio ya damu mishipani, kwa kuwa yaweza kuleta matatanisho mengi, kadiri ya vile tulivyofikiri wakati mmoja.”[6]
Jarida Pathologist lilirejezea kukataa damu kwa Mashahidi wa Yehova likasema hivi: “Kuna uthibitisho mwingi wa kuunga mkono ushindani wao dhidi ya damu, kujapokuwa na mateto kutoka kwa wahifadhi wa akiba za damu.”[7]
Dakt. Charles H. Baron, profesa wa sheria kwenye Chuo cha Boston cha Shule ya Sheria, alisema hivi kuhusu kukataa damu kwa Mashahidi wa Yehova: “Jamii yote ya Kiamerika imenufaika. Si Mashahidi wa Yehova tu, bali pia wagonjwa wote kwa ujumla, hawataelekea leo kupewa mitio ya damu isiyo ya lazima kwa sababu ya kazi ya zile Halmashauri za Mashahidi za Uhusiano na Hospitali.”[8]