Je! Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine Ndio Ufunguo wa Mafumbo ya Maisha?
Je! umepata kuishi awali?
Je! utaishi tena katika namna fulani ya maisha baada ya kufa?
Maswali haya yaweza kukumbusha juu ya fundisho la kuzaliwa upya katika mwili mwingine.
The New Encyclopædia Britannica hufasili “kuzaliwa upya katika mwili mwingine” katika njia ifuatayo: “Itikadi ya kuzaliwa tena kwa nafsi katika mfuatano mmoja au zaidi wa maisha, ambao waweza kuwa binadamu, mnyama, au, katika namna fulani, mmea.”[1]
Kuzaliwa upya katika mwili mwingine huonekana kuwa jambo la maana kwa dini za Mashariki, hasa zile zilizoanzia India, kama vile Dini ya Buddha, Dini ya Hindu, Dini ya Jaini, na Dini ya Sikh. Kwa mfano, miongoni mwa Wahindu katika India, uhai huonwa kuwa mzunguko wa kifo na kuzaliwa tena.
Hata hivyo, nyakati za karibuni, wazo la kuzaliwa upya katika mwili mwingine limevutia watu wengi wanaoishi kwenye Kizio cha Magharibi, kutia na idadi kadhaa ya vijana. Kulingana na mwandishi mmoja akiandika katika Sunday Star la Kanada, sababu ya kupendezwa kwingi huku “ni tokeo la pigo la dini za Mashariki kwa jamii yetu ya Magharibi, lililoanza katika miaka ya 1960.”[1A]
Sababu nyingine ya kupendezwa katika kuzaliwa upya katika mwili mwingine ni kwamba watu fulani maarufu wamesema peupe na wamedai kwa nguvu kwamba wameishi mara moja au zaidi maisha yaliyopita. Pia, redio, televisheni, magazeti, na vyombo vinginevyo vya habari vimeonyesha kupendezwa na kuzaliwa upya katika mwili mwingine, pia wastadi mbalimbali kama vile madaktari na walimu.
Yote hayo yametokeza udadisi mwingi. Hivyo, kulingana na hesabu fulani ya watu, karibu robo ya watu katika Kanada na Marekani wamedai kukubali wazo la kuzaliwa upya katika mwili mwingine.
Madai Kuhusu Maono ya Maisha ya Awali
Mwigizaji wa kike Shirley MacLaine alidai katika mahojiano na Phyllis Battelle katika jarida Ladies’ Home Journal kwamba amekuwa na “maono ya kinjozi” kadhaa katika kipindi cha maisha yake. “Nakumbuka mambo mengi ya maisha yangu ya awali—wakati mwingine nilikuwa mwanamume, nyakati nyingine mwanamke,” yeye asema.[2]
Katika kitabu Coming Back, Dakt. Raymond Moody alielezea uchunguzi alioongoza miongoni mwa wanafunzi wake na wengine. Yeye alisema kwamba kwa kuwekwa katika hali ya usingizi aliwachukua hadi wakati wa kabla ya kuzaliwa kwao, nao wakadai kuwa walikuwa na kumbukumbu la maisha yao ya awali. Mtu mmoja alisema kwamba aliishi akiwa Mweskimo katika jamii ya Waeskimo.[3] Mwingine alidai kwamba aliishi wakati wa ‘ile enzi ya kutumia zana za mawe,’ maelfu ya miaka iliyopita.[4]
Dakt. Moody mwenyewe alidai kwamba ameishi aina tisa za maisha ya awali. Kuanzia maisha kwenye vilele vya miti akiwa aina fulani ya “mwanadamu wa kale wa kabla ya historia” hadi maisha katika siku za Milki ya Roma, aliposema, alishambuliwa na kuuawa na simba katika uwanja wa michezo.[5]
Kuweka watu katika hali ya usingizi ili kuwapeleka wale wenye udadisi huko nyuma eti kwa wakati ambao hawakuwa wamezaliwa kumefafanuliwa pia kuwa hufaa wengine. Madaktari wameutumia kwa kutibu matatizo ya hisiamoyo. Inasemekana kwamba woga usioelezeka umepunguzwa kwa kuchunguza tatizo huko nyuma kwa tukio fulani la maisha ya awali. Wazo hili ni la kweli kadiri gani?
Maono ya Kunusurika Kifo Yaelezwa
Maono ya kunusurika kifo yameelezwa na watu ambao wameendeleza wazo la kuzaliwa upya katika mwili mwingine. Katika kitabu Life After Life, Dakt. Moody aripoti utafiti wake wa maono ya kunusurika kifo kutoka kwa watu wapatao 50.[6]
Ijapokuwa maono yao yalitofautiana, Moody afikiri kwamba yanafanyiza muundo fulani. Watu hawa walikuwa na hisi ya kusafiri kupitia shimo refu lenye giza. Walihisi kana kwamba wametenganishwa na miili yao, wakielea bila kushikilia kitu. Walihisi kana kwamba walikuwa wakipita kwa kasi sana kwenye shimo hilo kuelekea mwangaza mkali sana, na mwisho wa shimo hilo, waliona washirika wa familia waliokufa awali. Mwishowe, wakaamka katika miili yao wenyewe. Hata hivyo, si wote ambao wameona hatua zote hizo.[7]
Inadaiwa kwamba maono kama hayo yamekuwa na athari chanya kwa wale walioyaona. Ikiwa ndivyo, ingepaswa kuwasaidia wasiwe na woga wa kifo na kuwapa uhakika kwamba kuna maana ya maisha. Lakini haijawa hivyo sikuzote. Wengi wanazidi kuogopa kifo na kukosa uhakika katika kuwapo kwa maana halisi ya maisha.
Wale wanaoamini kuzaliwa upya katika mwili mwingine wanasema kwamba kupitia maono hayo wanapata utegemezo wa wazo la kwamba nafsi ya binadamu inazaliwa katika namna tofauti za maisha. Lakini je, fundisho hilo lastahili kwa njia yoyote? Je! kweli kuzaliwa upya katika mwili mwingine kwatoa ufunguo wa mafumbo ya maisha? Je! twaweza kupata jibu lolote kwa maswali, Je! umepata kuishi awali? Je! utaishi tena? Je! wanadamu wana nafsi inayoacha mwili wakati wa kifo? Maswali haya yatazungumziwa katika makala zifuatazo.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine ni fundisho la msingi la dini za Mashariki
[Picha katika ukurasa wa 4]
Gurudumu la Hindu la maisha