Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 6/8 kur. 5-7
  • Maajabu ya Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine Yaelezwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maajabu ya Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine Yaelezwa
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uvutano wa Hali Kama ya Usingizi
  • Maono ya Kunusurika Kifo
  • Hakuna Kumbukumbu
  • Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine
    Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
  • Je! Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine Ndio Ufunguo wa Mafumbo ya Maisha?
    Amkeni!—1994
  • Je! Neno la Mungu Hufundisha Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine?
    Amkeni!—1994
  • Je, Uliwahi Kuishi Katika Mwili Mwingine?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 6/8 kur. 5-7

Maajabu ya Kuzaliwa Upya Katika Mwili Mwingine Yaelezwa

MOJAPO hoja za fundisho la kuzaliwa upya katika mwili mwingine ni kwamba watu walio wengi duniani hawakumbuki hata kidogo kuwa wamepata kuishi awali. Zaidi ya hilo, hata hawafikirii kwamba huenda waliishi maisha ya awali.

Ni kweli kwamba wakati mwingine tuna hisia za kumtambua mtu tunayekutana naye kwa mara ya kwanza. Huenda nyumba fulani, mji, au sehemu za michezo ikawa twaifahamu, ingawa twajua kwamba ni mara yetu ya kwanza kuwa hapo. Hata hivyo, mambo hayo yaweza kuelezwa bila kukimbilia fundisho la kuzaliwa upya katika mwili mwingine.

Kwa kielelezo, mahali pengine penye maeneo yaliyotengana kwa umbali yanaweza kufanana, hivi kwamba tunapotembelea mahali papya, huenda tukahisi tumekuwa huko awali, ingawa bado. Nyumba, ofisi, maduka, miji, na sehemu za michezo nyingi katika sehemu fulani za ulimwengu hufanana na zile nyingine zilizo sawa nazo mahali pengine. Sababu ya kwamba zinafanana na zile tumeona haithibitishi kwamba tumekuwa mahali hapo katika maisha yaliyopita. Zinafanana tu na mahali tunapopafahamu.

Hilo ni kweli pia kuhusu watu. Wengine wanafanana sana na wengine kwa maumbile, hata lile linalosemwa kuwa mtu anayefanana na mwingine anayeishi. Mtu anaweza kuwa na vitabia ambavyo vyatukumbusha mtu mwingine ambaye bado anaishi au amekufa. Lakini tumejua watu hao wakati wa maisha ya sasa, si katika kuwapo kwa awali. Kufanana huko kwa sura au utu hakumaanishi kwamba watu hawa walijulikana kwetu katika maisha yaliyopita. Labda sisi sote tulimdhania mtu mmoja kuwa mwingine. Lakini watu hao wawili wamekuwa hai wakati uleule kama wewe na si kwa maisha ya awali. Haihusiani kwa vyovyote na kuzaliwa upya katika mwili mwingine.

Uvutano wa Hali Kama ya Usingizi

Hata maono yanayoonwa chini ya uvutano wa hali kama ya usingizi yaweza kuelezwa bila kugeukia fundisho la kuzaliwa upya katika mwili mwingine. Akili yetu isiyotambulika vizuri ina hifadhi ya habari inayoweza kufahamika zaidi ya tujuavyo. Habari hiyo hufikia hifadhi hii kupitia vitabu, magazeti, televisheni, redio, na kupitia maono mengine na machunguzi.

Habari zilizo nyingi huhifadhiwa katika pembe fulani iliyojificha ya akili yetu isiyotambulika vizuri kwa sababu hatuitumii moja kwa moja au mara moja. Akili yetu isiyofahamika ni kama vitabu vya maktaba ambavyo havihitajiki kwa sasa na hivyo vimewekwa kando kwenye safu ya faragha.

Hata hivyo, ukiwa katika hali kama ya usingizi, ufahamu wa jambo unabadilishwa hivi kwamba kumbukumbu zilizosahaulika zaweza kuonekana. Watu fulani hufasili kumbukumbu zilizosahaulika kuwa maisha ya awali, lakini hizo ni maono ya maisha ya sasa tu ambayo tuliyasahau kwa muda.

Hata hivyo, kuna visa vichache ambavyo vyaweza kuwa vigumu kueleza kwa njia ya asili. Kielelezo kimoja ni mtu aanzapo kuongea “lugha” nyingine akiwa chini ya uvutano wa hali kama ya usingizi. Wakati mwingine lugha hiyo huwa yenye kuweza kueleweka, lakini sivyo mara nyingi. Wale wanaoamini katika kuzaliwa upya katika mwili mwingine huenda wakasema kwamba hii ni lugha ambayo mtu huyo aliongea katika maisha yake ya awali.

Hata hivyo, inajulikana vizuri kwamba hizo ndimi pia zipo wakati watu wamo katika hali ya kifumbo au msisimko wa kidini. Wale walio na maono hayo wanasadikishwa kwamba hayahusiani na maisha ya awali bali kwamba wanachochewa na uvutano wa roho fulani isiyoonekana katika maisha ya sasa.

Maoni yatofautiana kuhusu uwezo huo kuwa ni nini. Katika tangazo la muungano la Fountain Trust na Church of England Evangelical Council, ilisemwa kuhusu kuongea kwa ndimi: “Twajua pia kwamba maajabu hayohayo yaweza kutokea chini ya mafumbo/uvutano wa kimashetani.”[1] Kwa hiyo kuwazia kwamba maajabu hayo ni uthibitisho wa kwamba tumeishi maisha ya awali kungekuwa kufanya uamuzi usiokomaa ulio bandia.

Maono ya Kunusurika Kifo

Vipi, basi, juu ya maono ya kunusurika kifo ambayo watu wanasema kwamba wamekuwa nayo? Haya yamefasiliwa na watu fulani kuwa uthibitisho wa kwamba mtu ana nafsi ambayo huishi baada ya kifo cha mwili. Lakini maono hayo yanaelezwa ifaavyo katika njia kadhaa za asili.

Katika gazeti la kisayansi la Kifaransa Science & Vie toleo la Machi 1991, hatua tofauti-tofauti za maono ya kunusurika kifo yanaitwa “mfano halisi wa ulimwenguni pote wa mawazo bandia yasiyo halisi” ambayo yamejulikana kwa muda mrefu. Si wale wanaonusurika kifo tu wanaopatwa na maono hayo. Yanaweza vilevile kutokea kuhusiana na “uchovu, homa, kupatwa na kifafa, utumizi mbaya wa dawa za kulevya.”[2]

Mpasuaji wa nuroni wa kwanza, Wilder Penfield, aliyepasua wenye kifafa ambao walipewa dawa na nusukaputi wa mahali pao, alifanya uchunguzi wenye kupendeza. Alipata kwamba kwa kuchochea sehemu tofauti-tofauti za ubongo kwa elektrodi, angefanya mgonjwa awe na hisia za kuwa nje ya mwili wake mwenyewe,[3] akisafiri kupitia shimo refu la chini, na kukutana na watu wa ukoo waliokufa.[4]

Jambo lenye kupendeza kuhusiana na jambo hili ni kwamba watoto ambao wamepata maono ya kunusurika kifo hawakutani na watu wa ukoo wao waliokufa, bali na wanashule wenzao au walimu—wale ambao bado wapo hai.[5] Hilo laonyesha kwamba maono hayo yana uhusiano wa utamaduni fulani. Yanayoonwa yanahusiana na maisha ya sasa, si baada ya kifo.

Dakt. Richard Blacher aandika kwenye gazeti The Journal of the American Medical Association: “Kuelekea kufa, au kupatwa na hali mbaya zaidi ya kimwili ni mfuatano wa tendo; kifo ni hali.” Ukiwa mfano, Blacher azungumza juu ya mtu ambaye kwa mara ya kwanza anasafiri kwa ndege kutoka Marekani hadi Ulaya. “Safari ya ndege si [kuwa katika] Ulaya,” yeye aandika. Mtalii anayeondoka Ulaya, lakini ambaye ndege yake inageuka na kurudi dakika kadhaa baada ya kuondoka, hawezi kuambia watu mengi kuhusu Ulaya kuliko mtu yeyote anayerudi anapoamka kutoka hali ya kukosa fahamu anavyoweza kuambia yeyote juu ya kifo.[6]

Wale ambao wamenusurika kifo, kwa maana nyingine, huwa kwa kweli hawajafa kamwe. Waliona jambo fulani walipokuwa wangali hai. Na mtu bado huwa hai hata sekunde chache kabla ya kifo chake. Walikuwa wanakaribia kufa lakini hawakuwa wamekufa bado.[7]

Hata wale ambao moyo wao umesimama kwa muda na ambao wamehuishwa hawawezi kukumbuka chochote cha wakati huo wa kukosa fahamu wakati ambao wangesemekana “wamekufa.” Wanalokumbuka, likiwapo lolote, ni jambo lililotukia walipokuwa wanafikia mkatizo huo wa muda mfupi, si wakati wenyewe.

Maono yaliyochapishwa ya kunusurika kifo sikuzote huelezwa kuwa yafaayo, ingawa inajulikana kwamba maono yasiyofaa pia yapo. Msaikoanalisti Mfaransa Catherine Lemaire aeleza jinsi hii: “Wale ambao [hawajanusurika kifo] kulingana na mtindo wa IANDS [Shirika la Kimataifa la Masomo ya Kunusurika Kifo] hawapendezwi kusema ono lao.”[8]

Hakuna Kumbukumbu

Ukweli ni kwamba hatuna maono ya maisha kuliko yale tunayoishi sasa, wala ya awali wala maisha ya baada ya kifo. Hivyo, hatuna kumbukumbu halali za chochote isipokuwa za maisha ambayo tumeishi.

Wale ambao wanaamini katika kuzaliwa upya katika mwili mwingine wanasema kwamba maana hasa ya kuzaliwa tena ni kupata nafasi ya kuboresha hali yetu. Ikiwa tuliishi maisha ya mapema, na hali tulikuwa tumeyasahau, kupoteza kumbukumbu huko kungetokeza kasoro kubwa sana. Ni kwa kukumbuka makosa yetu ndipo tunapoweza kufaidika kutokana nayo.

Pia, wale wanaoshikilia matibabu ya kuzaliwa upya katika mwili mwingine wanahisi kwamba unaweza kukabili matatizo ya sasa, kwa kuwekwa katika hali ya usingizi, unaweza kukumbuka maisha za awali. Fundisho lasema kwamba twazaliwa tena ili kuboresha kitu fulani, hali tumesahau kitu hicho chenyewe ni nini.

Kupoteza kumbukumbu katika maisha ya sasa kwafikiriwa kuwa ni kasoro. Ni lazima iwe vivyo hivyo kuhusu kisa hiki. Kupinga kwa kusema kwamba usahaulifu haujalishi, kwa kuwa watu wazuri tu ndio wanaozaliwa tena wakiwa wanadamu, si hoja timamu katika siku hii na enzi hii wakati uovu umeutawala ulimwengu kuliko wakati mwingine wowote. Ikiwa watu wazuri tu ndio wanaozaliwa wakiwa wanadamu, watu wote waovu walitoka wapi? Je! hakungepaswa kuwa watu wachache zaidi walio waovu? Ukweli ni huu: Hakuna mtu yeyote, mzuri au mwovu, anayezaliwa upya katika mwili mwingine ili aanze maisha mengine akiwa mwanadamu au kitu chochote kile kwa upande huo.

Hata hivyo, huenda ukasema, ‘Je! kuzaliwa upya katika mwili mwingine si fundisho la Biblia?’ Acheni tufikirie swali hili katika makala ifuatayo.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Akili yetu isiyotambulika vizuri ni kama maktaba iliyo na habari ambayo imewekwa kando lakini yaweza kukumbukwa baadaye

[Blabu katika ukurasa wa 7]

“Kifo ni hali,” si mfuatano wa tendo.

—Dakt. Richard Blacher katika The Journal of the American Medical Association

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki