Je! Magpai Kweli Ni Mwizi?
WAKATI Rossini mtungaji Mwitalia wa karne ya 19 alipoandika ile opera La gazza ladra (Magpai Anayeiba), katika 1817, hakika yeye aliamini kwamba magpai (aina ya kunguru) ni mwizi. Na wengine wana maoni kama hayo juu ya ndege huyu mwenye tabia ya kufikiria wengine. “Wakora-wasumbuaji, magpai ni miongoni mwa maharamia wa Marekani Magharibi,” chasema Book of the North American Birds. Magpai hawa wenye midomo myeusi, ingawa wajulikana mahali penginepo, walivumbuliwa katika Marekani wakati wa ile safari maarufu ya Lewis na Clark ya 1804-06 iliyofungua sehemu za Magharibi. Washiriki wa kikundi hicho walisema kwamba magpai waliingia katika mahema yao na kuiba chakula.
Ikiwa wewe waishi katika Ulaya, Asia, Australia, au Marekani Kaskazini, huenda ukawatambua magpai wa kwenu. Kwa kawaida huyo ni ndege mkubwa, wa kufikia urefu wa sentimeta 56, mwenye umbo dhahiri la rangi nyeusi na nyeupe katika mabawa na mwili wake. Ana mkia mrefu wa kijani ung’aao mchanganyiko wa rangi za kuvutia na mdomo wake ni wenye nguvu. Mara nyingi magpai huishi vikundi-vikundi na kukinga eneo lao kwa uthabiti, hata dhidi ya watu.
Kwa kumtupia jicho mara ya kwanza, huenda magpai wa Uingereza akaonekana kuwa mweusi tu akiwa na tumbo jeupe na vifito vya mabawa, lakini yeye ana rangi fulani nyangavu lakini zisizoonekana wazi sana. Mwili na manyoya yake marefu yana uzambarau uliochanganyikana na mng’ao wa rangi za kuvutia na uangavu wa kijani, na manyoya hayo yana ushaba-mweusi pia kwenye ncha zayo. Mkia wake ni zaidi ya nusu ya urefu wake.
Magpai wa Australia hupendeza waitapo kwa wimbo wenye madaha na madende. Sauti za kuita za magpai na kukabura, waitwao punda wachekaji, ni ishara moja hakika ya kuonyesha kwamba umefika Australia. Mbali na ule wimbo wa kumpambanua magpai, waweza kumtambua kwa viraka vyeupe vilivyo juu ya mgongo, tako na mabawa yake, na chini ya mkia.
Kwa hiyo je, kweli yeye ni mwizi? Kitabu Song and Garden Birds of North America chataarifu hivi: “Katika Marekani ya magharibi magpai mwenye mdomo mweusi amedharauliwa kwa muda mrefu kuwa mwizi na topasi.” Hata hivyo, katika mchomo huo wa mwisho, mna sifa fulani. Kwa nini? Kwa sababu matopasi hufanya usafi kwa kuondoa uchafu katika miili mifu ya wanyama na ndege wengine. Iwe atadharauliwa au atathaminiwa, magpai ni mojapo jamii zaidi ya 9,300 za ndege ambao huongezea uzuri wa dunia yetu na kuirembesha.