Kuutazama Ulimwengu
Infleshoni ya Asilimia Milioni Moja
Kiasi cha infleshoni katika Jamhuri ya Muungano wa Yugoslavia kilipanda kwa asilimia milioni moja katika Desemba 1993, kulingana na Idara ya Tarakimu ya Serikali. Gharama ya maisha ilikuwa mara 2,839 zaidi ya vile ilivyokuwa mwezi mmoja mapema, na mara trilioni 6 zaidi ya vile ilivyokuwa kuelekea mwanzo wa mwaka. Kama tokeo pesa zilizochapwa zinakuwa bure siku kadhaa tu baada ya kutokezwa. Ili kukabili hali hiyo, benki kuu imekuwa ikiondoa sifuri kutoka kwa pesa ya dinar. Katika miezi mitatu tu, dinar trilioni 5 zilishuka thamani na kuwa dinar 5 tu.
Kujihusisha na Dini
Katika uchunguzi mmoja, Wamarekani zaidi ya asilimia 90 walisema waliamini Mungu, na zaidi ya asilimia 40 walidai huhudhuria ibada kanisani kila juma. Mahoji ya Gallup ya 1992 yalionyesha kwamba asilimia 45 ya Waprotestanti katika Marekani na asilimia 51 ya Wakatoliki walihudhuria kanisa katika juma. Hata hivyo, uchunguzi mpya waonyesha kwamba watu wengi wadai kuwa wa kidini na wadai kuwa wahudhuriaji wa kanisa walio wa kawaida kinyume cha vile walivyo. Kulingana na kikundi kimoja cha watafiti, ni asilimia 20 tu ya Waprotestanti na asilimia 28 ya Wakatoliki ambao hasa huhudhuria kanisa kila juma. Kikundi kingine kilipata kwamba ni Wamarekani milioni 36 tu walio watu wazima—asilimia 19—wanaodhihirisha dini yao kwa ukawaida na kwamba karibu theluthi moja ya Wamarekani wenye miaka zaidi ya 18 wana mtazamo wa kilimwengu kabisa. “Ingawa dini yaenea barani Marekani, ni wachache tu wanaoichukua kwa uzito,” lasema Newsweek. “Nusu ya idadi ya Wamarekani wasema kwamba dini haina uvutano juu ya mitazamo au tabia zao.”
Upungufu wa Maji Watisha
“Kwa kuwa kiasi cha theluji na mvua ni kilekile kwa kadiri fulani, maji yanayoweza kupatikana tena yana kiasi,” lasema gazeti Science. “Kufikia mwaka 2025, idadi ya watu wanaoishi katika nchi zenye upungufu wa maji itakaribia bilioni 3,” na tayari “kufikia mwaka 2000, nchi za Afrika na Mashariki ya Kati zitaathiriwa sana.” Kulingana na ripoti kutoka Shirika la Usawazishaji wa Idadi ya Watu ya Kimataifa, tayari nchi nyingi zinamaliza ugavi wa maji yaliyo chini ya ardhi, na nchi kadhaa zashindwa kubainisha kati ya maji yasiyoweza kupatikana tena na yale yanayoweza kupatikana tena katika mipango yao ya muda mrefu. Ingawa jitihada zimefanywa kuongeza ugavi wa maji, kufikia sasa jitihada hizo zimezuiwa na ongezeko la idadi ya watu.
Kukataa Wakimbizi
Wakimbizi wameongezeka zaidi ya mara nane katika miongo miwili iliyopita, asema Sadako Ogata, Kamishna Mkuu wa UM Kwa Ajili ya Wakimbizi, na imetokeza “ongezeko lenye kushtua la mitazamo yenye uhasama na kuchukia wageni.” Kufikia mwisho wa mwaka jana, wakimbizi milioni 19.7 waliishi nje ya nchi zao, na milioni 24 zaidi walihamishwa katika mipaka yao wenyewe. Ulimwenguni pote, mtu 1 kati ya kila 125 amelazimika kuacha maisha ya kawaida ya nyumbani kwa sababu ya jeuri, vita vya wenyewe kwa wenyewe, au mnyanyaso. Hilo limelemeza “uwezo wa ulimwengu kuchukua hatua” na “zoea la kibinadamu la kutoa usalama,” laripoti The Washington Post, likizungumzia uchunguzi huo wa kwanza wa ulimwenguni pote juu ya wakimbizi. Nchi kadhaa ambazo tayari zimelemewa na shida za kiuchumi na vita vinavyoonekana kana kwamba haviwezi kusuluhishwa, zimechukua hatua ya kukataa wakimbizi. “Karibu kila vita iliyotokeza wakimbizi ulimwenguni wakati wa . . . 1993 ilitokea ndani ya nchi badala ya baina ya nchi,” uchunguzi huo ulisema, ukitaka kuwe sera ya kimataifa kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wakati uo huo, “hali isiyopendeza” yawakabili wakimbizi.
Papa Aunga Mkono Mahubiri ya Mlango-kwa-Mlango
Wakikubali himizo la John Paul 2, idadi fulani ya waumini wa harakati ya kuongoa kupitia Katekisimu ya Katoliki wamekubali kuhubiri mlango kwa mlango na katika barabara za Roma na viungani mwalo. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti La Repubblica, hao “washindani wenye kusema sana wa Mashahidi wa Yehova” “watasimulia hadithi ya maisha ya Yesu.” Kikundi cha kwanza kina familia 15 tu, lakini papa atumaini kwamba mradi huo “huenda ukatokeza matunda mengi kotekote.” Kwa nini jitihada hiyo mpya? Baraza la uongozi la Katoliki lang’amua kwamba “limepoteza uwezo walo wa kunasa watu, kuvutia watu kidini,” asema mwanasosholojia Maria Macioti, naye papa atia moyo harakati hizo “za kupata waongofu kupitia uvutio wa kihisiamoyo wenye nguvu.” Mwandikaji Mkatoliki Sergio Quinzio aongeza: “Ni kana kwamba hataki kupoteza fursa yoyote, hali akitumaini, au akiwa na ndoto, kwamba chochote chaweza kufanikiwa.”
Msiba wa Kimazingira Katika Urusi
“Viktor Danilow-Daniljan, Waziri wa Mazingira wa Urusi, ametangaza asilimia 15 ya eneo la Urusi kuwa eneo la msiba wa kimazingira,” laripoti gazeti la habari la Ujerumani Frankfurter Allgemeine Zeitung. Kulingana na ripoti hiyo, nusu ya eneo la ukulima katika Urusi haifai kwa ukulima, na watu zaidi ya 100,000 huishi katika maeneo ambako kiasi cha nururishi kiko juu sana. Isitoshe, makumi ya maelfu ya watu waripotiwa kuwa walikufa kwa sumu za viwandani ambako silaha za kemikali zilikuwa zikitengenezewa. Lew Fjodorow, msimamizi wa Shirika la Usalama wa Kemikali, alisema: “Kwa maoni ya kitiba, maandalizi yetu kwa ajili ya vita ya kemikali yalikuwa na matokeo yenye msiba.”
Watoto Wajeuri
Watoto wanaoua kimakusudi, kuiba, kunajisi, na kutesa wapatikana katika nchi nyingi, na visa vya jeuri na ukatili vyaongezeka. Hesabu ya uuaji-kimakusudi uliofanywa Marekani na vijana wa chini ya miaka 18 ilipanda kwa asilimia 85 katika miaka mitano iliyopita. Jambo lenye kutia wasiwasi pia ni mtazamo wa kiburi ulioonyeshwa na wakosaji wengi. Ni nini kinacholeta mabadiliko hayo? “Jamii yetu yenye kutaka vita, pamoja na viwango vyayo vilivyopotoka, imefanya jeuri ikubaliwe,” lasema gazeti la Ujerumani Der Spiegel. “Viwango vya waziwazi juu ya mambo yanayofaa na yasiyofaa, mema na mabaya . . . haviko wazi tena.” Hilo laongeza: “Wakosaji wachanga ni wadhulumiwa pia. Wao huiga watu wazima katika ulimwengu wanaokulia. . . . Kila mtoto mjeuri ametazama na kufyonza jeuri nyingi sana.” Kupitia televisheni, watoto huona “jeuri ya ulimwenguni pote.” Wao huongozwa vibaya na vidio zenye jeuri, michezo ya kompyuta, na nyimbo zinazotukuza uuaji na matendo mengine ya jeuri. Programu za televisheni huchochea jeuri kuwa njia ifaayo ya kusuluhisha matatizo na kumaliza ugomvi. “Tumekuwa jamii ya kinyama,” asema profesa wa akili Stefan Schmidtchen wa Hamburg, “na watoto wetu wanakua wakiwa hivyo, pia.”
Kulala Pamoja na Kitoto
“Si kwamba tu tungeweza kupunguza SIDS (Sudden Infant Death Syndrome, au Kifo cha Ghafula cha Mtoto Mchanga), bali pia tungeweza kulea vitoto vyenye afya zaidi na vyenye furaha zaidi ikiwa akina mama wangefanya jambo moja tu: Kulala pamoja na vitoto vyao katika mwaka wa kwanza, badala ya kuvitenga katika vijitanda vyao,” asema James McKenna, profesa wa Chuo Kikuu cha Pomona katika California. Kulala huku kitoto kikigusa mzazi “husaidia kufanya viungo vya kitoto vifanye kazi kama kawaida usiku kucha,” laripoti The Dallas Morning News. Majaribio yamethibitisha kwamba kitoto kilalapo kando ya mama yacho, “kadiri ya kupumua [ya kitoto], kadiri ya mpigo wa moyo na utaratibu wa usingizi hufuata ule wa mama yacho.” Na kwa kuwa mara nyingi mama na mtoto hutazamana, kitoto chaweza kunyonya kwa urahisi kama kipendavyo. “Vitoto vilivyo peke yavyo katika vijitanda hupatwa na upweke,” asema Bw. McKenna. “Twafikiri hilo laweza kuleta ukosefu wa ukuzi wa kiakili ulio wa maana na labda hali zinazochochea zaidi hatari ya SIDS.” Tarakimu zaonyesha kwamba katika nchi ambako vitoto hulala pamoja na mama zao kidesturi, kiasi cha SIDS ni cha chini zaidi.
Israeli na Vatikani Zatia Sahihi Mkataba
Baada ya miaka mingi ya kukataa na miezi 17 ya mazungumzo, Vatikani imetia sahihi mkataba wa kibalozi na Israeli. Wajumbe wa pande zote mbili walivaa kofia ndogo ya kugandama na kichwa huku Waziri Msaidizi wa Nchi za Kigeni Yossi Beilin akitia sahihi kwa ajili ya Israeli na Katibu Mkuu wa Taifa Askofu Claudio Celli akitia sahihi kwa ajili ya Vatikani. “Ofisi Kuu ya Roma,” akasema Celli, “imesadikishwa kwamba mazungumzo na ushirikiano wenye kuheshimika kati ya Wakatoliki na Wayahudi sasa utapata nguvu na nishati mpya nchini Israeli na pia kotekote ulimwenguni.” Makubaliano hayo yataka Vatikani ipinge chuki dhidi ya Wayahudi, nayo Israeli yakubali kuipa kanisa uhuru wa usemi na haki ya kuendeleza mipango ya kijamii nchini Israeli. Mambo fulani yangali yahitaji kusuluhishwa, kama vile kodi juu ya mali za kanisa nchini Israeli na kufikiwa kwa mahali patakatifu. Ingawa suala la Jerusalem halikutajwa katika mkataba huo, Vatikani yatumaini kwamba sasa itakuwa na uwezo juu ya yale yatakayopata jiji hilo baadaye.
Mkataba wa Kibiolojia ni Sheria
Mkataba uliotiwa sahihi na mataifa 167 nchini Brazili mwezi Juni 1992 ulikuwa sheria ya kimataifa mwanzoni mwa mwaka huu. Ukiitwa Mkutano wa Mambo Mbalimbali ya Kibiolojia, mkataba huo wataka nchi zilizotia sahihi, zibuni njia za kuhifadhi wanyama, mimea, na vimelea katika mipaka yazo kutia na mazingira yanayofaa. Mataifa yenye kutia sahihi yatakwa yapitishe sheria za kulinda wanyama walio hatarini na kuchochea elimu ya umma juu ya utumizi ufaao wa nyenzo za kibiolojia na uhitaji wa kuhifadhi. Mkataba huo ulichochewa na ufahamu wa kwamba, idadi ya viumbe wanaotoweka ilikuwa ikipanda kwa kadiri ya kusikitisha na hofu kwamba nusu ya viumbe wengine wote wanaobaki waweza kutoweka kufikia mwaka 2050. Watia-sahihi watakutana baadaye mwakani kuamua hasa jinsi mkataba huo utakavyofanya kazi.