Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 8/22 kur. 16-18
  • Tarumbeta—Yatoka Uwanja wa Vita Hadi Jumba la Muziki

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tarumbeta—Yatoka Uwanja wa Vita Hadi Jumba la Muziki
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hatua za Mwanzo-Mwanzo
  • Ukuzi wa Tarumbeta ya Kisasa
  • Tarumbeta Yenye Vibonyezo
  • Tarumbeta ya Kwanza ya Vilango
  • Yajulikana Sana kwa Matumizi Mbalimbali
  • Tauni za Yehova juu ya Jumuiya ya Wakristo
    Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!
  • Kuitikia Mwito wa Tarumbeta Leo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2020
  • Saa ya Hukumu ya Mungu Imewasili
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Kutazama Ufunuo kwa Njia ya Uchunguzi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 8/22 kur. 16-18

Tarumbeta—Yatoka Uwanja wa Vita Hadi Jumba la Muziki

KATIKA wakati wa Mfalme Abiya, mashujaa wa vita wa Yuda walinaswa katika mtego. Wakiwa wamezingirwa na wanajeshi adui 800,000, wao walishindwa kwa idadi maradufu. Ilionekana kama hawangeokoka. Kwa ghafula, sauti za tarumbeta zikalia kwa nguvu! Adrenalini ilipopitia mishipa yao ya damu, wanaume wa Yuda walitoa sauti kuu za vita na kuingia vitani. Wajapokabiliwa na mambo mengi, Wayudea walishinda adui.—2 Mambo ya Nyakati 13:1-20.

Ni lazima walichochewa kama nini kusikia tarumbeta hizo! Bila shaka hiyo ilikumbusha Wayudea ahadi ya Yehova: “Mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu.” (Hesabu 10:9) Kupigwa kwa tarumbeta kulionyesha kwamba Yuda ilitumaini Yehova, na tumaini hilo lilithawabishwa.

Historia ya tarumbeta yarudi nyuma zaidi sana ya kisa hicho cha Biblia. Tarumbeta ya chuma yaweza kufuatwa hadi Misri karibu miaka 2,000 kabla ya Kristo. Tarumbeta hizo za kale zilikuwa tofauti kabisa na zile tunazojua leo. Ebu fikiria maendeleo ya chombo hiki chenye kuvutia.

Hatua za Mwanzo-Mwanzo

Neno la Kiswahili “tarumbeta” latokana na neno la Kiingereza trumpet lililotokana na neno la Kifaransa cha Kale, trompe, linalorejezea mkonga wa ndovu. Inaonekana kwamba tarumbeta za kale zilifanana na mkonga wa ndovu. Mtungaji michezo ya kuigiza aliye Mgiriki, Aesiklasi (525-456 K.W.K.) alisema sauti ya tarumbeta ni kama “kupasuka-pasuka.” Ilitumiwa tu katika kutoa ishara za vita, mazishi au katika vipindi vya sherehe, mashindano ya riadha, na matukio mengine ya umma.

Ingawa tarumbeta za Israeli zilitumiwa kwa kutoa ishara za vita, pia zilitumiwa kucheza muziki katika hekalu. Wasanii stadi waliajiriwa kutengeneza vyombo vya hali ya juu kutokana na fedha. Katika hekalu, wacheza-tarumbeta walicheza kwa upatano sana hivi kwamba walisemwa kuwa “kama mmoja wakisikizisha sauti moja [kwa upatano kamili, Today’s English Version].”—2 Mambo ya Nyakati 5:13.

Kwa hiyo tarumbeta za Israeli hazikuwa za hafifu hata kidogo, ama kwa kutazamwa ama kwa kusikizwa. Lakini, kama ilivyokuwa na tarumbeta za mataifa jirani, ziliweza kutokeza sauti chache tu. Karne nyingi zikapita kabla ya uwezo wa tarumbeta kuboreshwa.

Ukuzi wa Tarumbeta ya Kisasa

Ili kuongeza uwezo wa tarumbeta kutoa sauti nyingi zaidi, ubuni wayo ulihitaji kurekebishwa. Kwanza ilirefushwa. Ilifikiriwa kwamba chombo kirefu zaidi kingetokeza sauti nyingi zaidi mbalimbali. Tarumbeta moja ya enzi za kati (iliyoitwa buisine) ilikuwa na urefu wa meta 1.8! Kama unavyoweza kuwazia, ilikuwa vigumu sana kuicheza. Hivyo, katika karne ya 14, tarumbeta hiyo ilikunjwa iwe na umbo-S ili ichezwe kwa urahisi. Karne moja baadaye, ilikuwa imekuwa na umbo refu linaloanza kwa ukubwa likirudi kuwa dogo na likiwa na mirija mitatu yenye kuambaana.

Tarumbeta hiyo mpya iliweza kutoa sauti nyingi zaidi lakini zile nyembamba pekee. Ilikuwa vigumu kufikia sauti hizo. Hata hivyo, watu fulani walianza kutunga muziki kwa ajili ya tarumbeta ya clarino, iliyofaa sauti zilizo nyembamba pekee. Mtungaji mmoja mashuhuri wa muziki wa enzi hiyo alikuwa Johann Sebastian Bach (1685-1750).

Hatimaye, mirija yenye mipindo zaidi iitwayo vigoe viliongezwa kwenye tarumbeta. Lilikuwa wazo sahili: Kuongezwa kwa mirija kuliongeza urefu wa sehemu kuu ya kupitisha hewa, hivyo ikiongeza sana uwezekano wa kutoa sauti nyingi zaidi. Vigoe hivyo vilipunguza sauti ya kawaida ya tarumbeta kutoka sauti-F kuwa chini kufikia sauti ya kitelemsho-B.

Kwa hiyo, kufikia wakati wa Wolfgang Amadeus Mozart (1756-1791), tarumbeta za clarino zenye sauti nyembamba zilikuwa zimekwisha. Zomari iitwayo clarinet ikaja kucheza sauti nyembamba bila shida yoyote, nayo tarumbeta ikacheza sauti za katikati.

Tarumbeta hiyo mpya ilianza kutumika kwa njia nyingi. Lakini bado ilikuwa shida kuicheza, kwa sababu kurekebisha vigoe kulihitaji matumizi ya mikono yote miwili. Kwa hiyo, ilifaa ifanyiwe marekebisho zaidi.

Tarumbeta Yenye Vibonyezo

Karibu na mwaka 1760 mwanamuziki mmoja Mrusi aitwaye Kolbel alifanya uvumbuzi wa maana. Aliweka tundu karibu na sehemu ya mwisho iliyo pana ya tarumbeta na kuiwekea kibonyezo kilichofunikwa kilichotumika kikiwa kisimamishi. Kubonyeza kibonyezo hicho kuliinua sauti ya tarumbeta hatua moja na nusu zaidi katika sauti yoyote. Katika 1801, mcheza-tarumbeta kutoka Vienna aitwaye Anton Weidinger aliboresha ubuni wa Kolbel kwa kutengeneza tarumbeta yenye vibonyezo vitano. Hatimaye kukawa na tarumbeta ambayo ingeweza kutoa sauti zote za uimbaji bila kuleta matatizo sana wakati wa kucheza.

Hata hivyo, tarumbeta ya Weidinger ilikuwa na kasoro kubwa sana. Kufunguka kwa vibonyezo kulihitilafiana na mlio wa chombo hicho, kukibadili sana sauti ijulikanayo ya tarumbeta hiyo. Kwa hiyo, tarumbeta yenye vibonyezo haikudumu. Upesi iliachiliwa kwa sababu ya ubuni mpya kabisa wa tarumbeta.

Tarumbeta ya Kwanza ya Vilango

Katika 1815, Heinrich Stölzel wa Silesia alinunua haki ya ubuni uliotumia pistoni, au vilango, katika tarumbeta. Kupitia matundu yayo yaliyowekwa sehemu zifaazo, kila kilango kingebadili njia ya hewa kutoka kwenye mrija mkuu na kuingia katika kigoe kilichoshikanishwa. Kwa hiyo, vigoe kadhaa vyenye urefu mbalimbali vingeweza kutumiwa sawia kwa mchanganyiko wowote wa muziki. Na zaidi, kwa sababu vilango viliwekewa springi, vingeitikia mara iyo hiyo.

Mwanzoni tarumbeta hii ilikuwa na matatizo ya kuweka sauti sahihi ya kuimba. Hata hivyo, miaka ilipopita, kasoro hizo zilirekebishwa, na tarumbeta ya vilango imedumu mpaka leo.

Yajulikana Sana kwa Matumizi Mbalimbali

Tarumbeta inaweza kucheza katika karibu kila aina ya muziki. Hiyo hupatana vizuri sana na sauti na vyombo vingine. Sauti yayo ya kishujaa, iliyo hodari huifanya itumike vizuri sana katika maonyesho ya tarumbeta na katika miendo ya taratibu kama ya kijeshi. Na wakati uo huo, ina sauti nzuri sana ya kuimba na yenye nguvu ifaayo sana maonyesho ya muziki, na jazi ya kisasa. Isitoshe, kwa sababu ya sifa zayo nyingi za kuimba, tarumbeta hufaa sana katika nyimbo za utenzi na mara nyingi hutumiwa kuimba ikiwa peke yayo bila sauti ya kuandama.

Naam, tarumbeta ina historia ndefu. Haitumiki tena ikiwa chombo tu cha kutoa ishara ya kivita mikononi mwa mwanajeshi. Sasa inaweza kutoa usanii halisi wa muziki—angalau katika mikono ya mstadi wa muziki. Bila shaka imekuletea raha usikilizapo, hata uwe unapendelea muziki wa aina gani. Twaweza kumshukuru Muumba wetu kama nini kwa kuwapa wanadamu uwezo wa kuvumbua vyombo vya muziki kama tarumbeta!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Tarumbeta Yenye Vibonyezo na Tarumbeta Yenye Slaidi: Encyclopædia Britannica/11th Edition (1911)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki