Kuutazama Ulimwengu
Theolojia ya Maadili ya Katoliki na Wanawake Waitalia Vijana
Wanawake Waitalia vijana, wawe au wasiwe ni Wakatoliki, hawamjali sana papa kuhusu maadili ya kijinsia. Kwa kweli, kulingana na matokeo ya utafiti uliochapishwa na gazeti la kila siku la Kiitalia La Repubblica, wengi kufikia asilimia 90.8 ya wanawake vijana wa kati ya miaka 15 na 24 waliohojiwa waliamini kwamba “utumizi wa vizuia-uzazi lazima uhakikishiwe wanawake,” hali asilimia 66.7 walitetea “haki ya kukatiza ‘mimba isiyotakwa.’” Tena, asilimia 80.2 kati yao waliamini kwamba “haki za wagoni-jinsia-moja zapasa kuhakikishwa na kustahiwa.”[1]
Vijisumu Vyapatikana Katika Nywele za Aliyezaliwa Karibuni
Sasa kuna ushuhuda wa kibiolojia kuthibitisha kwamba moshi wa tumbako uliopulizwa na mtu mwingine na kuvutwa na wanawake wenye mimba wasio wavutaji hufika ndani ya kijusu, lasema The Globe and Mail la Toronto, Kanada. Maono mapya kutoka kwa kikoa cha utafiti kilichoongozwa na Dakt. Gideon Koren, mwanafamakolojia wa kliniki kwenye Hospitali ya Watoto Wagonjwa katika Toronto, yaonyesha kwamba sampuli za nywele zilizotolewa kwa mtoto aliyezaliwa karibuni zina nikotini na kitokano chayo, kotinini. Mama hao wasio wavutaji waliwekwa penye moshi uliopulizwa na watu wengine kwa angalau saa mbili kwa siku, ama nyumbani ama kazini. Kulingana na Dakt. Koren, kuvuta kwa kawaida moshi uliotoka kwa mtu mwingine huenda kukawa kama “kuvuta sigareti mbili hadi nne kwa siku.” Utafiti mpya huu “waongeza uzito kwenye uchunguzi mbalimbali wa mapema zaidi uliodokeza kwamba kuwa mahali penye moshi wa tumbaku kungeweza kuathiri ukuzi wa watoto wa kitabia na kiutambuzi,” laongezea The Globe. Dakt. Koren alitahadharisha kwamba “katika mwelekeo wa sasa wa watu kufanyiana-fanyiana kesi, naona kwamba katika miaka 10 hadi 20 ijayo twaweza kuona watoto wakiwashtaki wazazi wao kwa kuzaliwa na kasoro kutokana na uvutaji tumbaku”!
Wizi wa Madukani Wawa wa Kimataifa
“Wahitimu” wa “shule ya wizi” katika Santiago, Chile, ni watendaji katika Montreal na Toronto, Kanada, na majiji fulani ya Marekani, laripoti L’actualité, gazeti-habari la Kanada. “Shule” hiyo hufundisha mbinu za wizi wa mfukoni na wa madukani na kuandaa elimu juu ya sheria za Kanada na njia zitumiwazo na polisi. “Wahitimu” hufanya kazi katika vikundi, huchukua hati bandia, na wana nguo zenye tabaka maalumu na karatasi maridadi za kufungia vitu vilivyoibwa ili vidhaniwe ni zawadi. Polisi wa Jumuiya ya Mji wa Montreal wamegundua mfumo huo na kukamata nguo kadhaa zilizoibwa tangu 1991. Kitu kikubwa zaidi walichogundua hivi majuzi ni kibebeo kilichojaa mavazi ya kupelekwa Chile. Hata hivyo, mfumo huu wa kimataifa wa wizi ulioratibiwa hutatiza sana polisi na wenye maduka pia. Kachero mmoja wa Montreal aliyenukuliwa katika L’actualité alisema kwamba ni vigumu kuwafanya polisi wa kimataifa wasaidie katika jambo hili, kwa kuwa “hilo silo shughulikio la kwanza kwao.”
Shida Kubwa ya Wakimbizi Tufeni Pote
Katika 1992, karibu watu 10,000 kwa siku walipata kuwa wakimbizi.[1] Chathibitisha hivyo The State of the World’s Refugees, kitabu kipya kilichotolewa na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kwa Ajili ya Wakimbizi (UNHCR).[2] Kulikuwa na wakimbizi milioni 18.2 ulimwenguni pote 1992, mara nane za waliokuwako miaka 20 mapema zaidi.[3] Watu milioni 24 zaidi wamekoseshwa makao katika nchi zao wenyewe.[4] Kwa jumla, karibu 1 katika kila watu 130 duniani amelazimishwa kukimbia nyumbani.[5] Gazeti Refugees la UNHCR lataarifu: “Ongezeko lisilopungua la idadi—la wakimbizi halisi na wahamiaji wa kiuchumi—limetatiza sana ile haki ya tangu miaka 3,500 iliyopita ya kuwapa himaya wakimbizi, kuifanya ikaribie kumalizika.”[6]
Je, Una Usingizi?
Je, unapata usingizi wa kutosha usiku? Mtafiti mmoja asema kwamba njia moja ya kujua ni kula mlo mkubwa halafu uende kwenye hotuba isiyochangamsha katika chumba chenye ujoto. Ikiwa umepumzika vya kutosha, huenda ukahisi ukikosa upendezi na kukosa utulivu lakini si mwenye usingizi.[1] Kulingana na International Herald Tribune, wastadi wakadiria kwamba Wamarekani milioni 100 hawapati usingizi wa kutosha.[2] Watu walio wengi huhitaji kuanzia saa nane hadi saa nane na nusu usiku za usingizi; watu wa miaka kuanzia 17 hadi 25 wahitaji hata zaidi.[3][4] Ingawa watu wengi huweza kuendelea na usingizi mpungufu kuliko ule wahitajio, watu wasiopata usingizi huelekea zaidi kufanya makosa.[5] Pia wao hurundika “deni la usingizi.”[6] Lataarifu Tribune: “Wazazi husikitishwa na ‘uvivu’ wa matineja wao kwa sababu wao hulala hadi adhuhuri miisho-juma, lakini walio wengi wa vijana hawa wanajaribu tu kulipia kiasi fulani cha deni lao la usingizi wa juma zima.”[7]
Kutendwa Vibaya na Makasisi Kwafichuliwa
Moja la machunguzo makubwa zaidi ya kingono Kanada yanayohusisha Mandugu Wakristo Wakatoliki limekamilishwa. “Wadhulumiwa zaidi ya 700 wamejitokeza kutoka [shule ya] St. Joseph” katika Alfred, Ontario, na shule ya St. John katika Uxbridge, Ontario, laripoti The Toronto Star. Malalamiko yaliandikishwa “dhidi ya wanaume 30, kutia na washiriki 29 wa Mandugu wa Shule za Kikristo. Mashtaka yangaliandikishwa dhidi ya wengine 16 kama wangalikuwa hai bado,” laongezea Star. Wadhulumiwa hao wangali wakumbuka mahangaisho “ya mapigo ya utotoni na mashambulio ya kingono yaliyofanywa na wale washiriki wenye kanzu nyeusi wasimamiao waumini wa Katoliki ya Roma ambao walikuwa wamekabidhiwa kwao.” Star lasema kwamba uchungulizi usipofanywa kwa umma, huenda Wakanada wasipate kamwe kujua ni kwa nini wanaume wadaio kumtumikia Mungu hutenda vibaya wavulana wachanga kingono.
Nyenje wa Themometa
Ikiwa wewe waishi Afrika, sasa waweza kujua kiwango cha halijoto bila msaada wa themometa, kulingana na jarida moja la kisayansi kuhusu zuolojia. Hili laweza kufanywa, kwa kipimo cha Selsio, kwa kuhesabu idadi ya vikelele ambavyo nyenje-miti wa Afrika (Oecanthus karschi) hutoa kwa sekunde sita, na kuongeza 12 kwenye jumla hiyo. Au ikiwa unausikiliza mfululizo wa spishi ya Rasi ya Afrika Kusini (Oecanthus capensis), kwa kuhesabu vikelele vyake kwa sekunde tatu na kuongeza 11 kwenye jumla. Upigaji vikelele wa spishi mbili hizi za nyenje-miti ni wa polepole kutosha kuhesabu. Ni wa sauti ya kusikilika pia, kwa kuwa wao hujiweka majanini kwa njia ambayo ule upigaji kelele hukuzwa kana kwamba kupitia kikuza-sauti. Halijoto ya usiku ishukapo, ule upigaji vikelele hupungua. Laeleza hivi jarida African Wildlife: “Nyenje ni ‘wa damu baridi’ kwa hiyo umetaboli wao huathiriwa na halijoto ya hewa. Hiyo huathiri karibu kila upande wa maisha zao, kutia na kadiri ya kuimba kwao.”
Matatizo ya Miale ya Kiuka-Urujuani
Je, wewe hupenda kutumia likizo zako kujistarehesha chini ya jua? Ikiwa ndivyo, tahadhari! Ingawa miale ya kiuka-urujuani ina manufaa ikiwa ya kiasi, kadiri kubwa mno yaweza kusababisha kansa ya ngozi, maradhi ya macho, kupata mikunjo ya ngozi mapema mno, vivimbe vya ngozi vyenye madhara ya kifo, na kudhoofika kwa uwezo wa mwili kupigana na maradhi.[1] Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, miale ya kiuka-urujuani inaongezeka kwa sababu tabaka ya ozoni inapungua.[2] Sasa, katika sehemu nyingi za ulimwengu, kutia na Australia, New Zealand, na Marekani, matatizo ya afya kutokana na miale ya kiuka-urujuani huongezeka baada ya muda mfupi zaidi na haraka zaidi.[3] Ni jinsi gani ya kujilinda katika sehemu zenye jua? Vaa mavazi ya kujikinga, vaa miwani-jua ya kufyonza miale ya kiuka-urujuani, na ukae ndani ya nyumba adhuhuri, wakati mnururisho wa miale ya kiuka-urujuani huwa na nguvu zaidi.[4]
Biashara Kubwa ya Kidini
Mojapo sehemu chache za uchumi wa Kiitalia zenye kuchuma faida, na labda iliyo ya pekee kufaulu kuuweza mzoroto wa fedha, ni biashara “iendeshwayo kichinichini Kanisani,” yasema nyongeza ya kifedha ya La Repubblica. Kwa kweli, wakati wa Wonyesho wa Bidhaa za Kidini ulio wa sita, uliofanywa Pompeii, mapato ya zile kampuni 1,400 zenye kufanya mauzo “yalihesabiwa kuwa lire bilioni 400 [dola milioni 240 za Marekani], kukiwa na ongezeko la kila mwaka lililokadiriwa kuwa asilimia 15 kwa wingi wa mauzo.” Tena, utalii wa kidini, ambao katika 1993 ulivutia wahaji wapatao milioni 35 mahali mbalimbali pa ibada katika Italia, ulipata kiasi kikaribiacho kuwa mara kumi za hicho kingine. “Biashara ‘zilizobarikiwa’ na kanisa zinavuvumka,” yasema ripoti hiyo, na “jamii ya viongozi wa kidini Wakatoliki wa Italia, Kongamano la Maaskofu na Makao Matakatifu yamejua jambo hilo linatendeka na kulifurahia kwa muda fulani.” Jamii ya viongozi wa kanisa hata imeratibu na kudhamini makongamano—yenye kuhutubiwa hata na maofisa wa kanisa wenye madaraja ya juu—ili kudhibiti hali hiyo.
Kujiua kwa Wingi Australia
Kadiri ya kujiua inaongezeka kwa kadiri ya kugutusha sana Australia hivi kwamba Shirika la Afya ya Umma sasa limetia uzuizi wa ujiuaji katika mwongozo walo wa kitaifa wa afya ya umma. Hesabu ya visa vya kujiua ilipozidi hesabu ya vifo kutokana na aksidenti kwa miaka miwili mfululizo, Shirika la Afya ya Umma liling’amua kwamba lazima hatua thabiti ichukuliwe, tena kwa hima. Gazeti The Australian lanukuu msemaji fulani wa shirika hilo kuwa akisema: “Mpaka sasa, ujiuaji haujashughulikiwa na jumuiya ya afya ya umma, na bado una hali kama zile za mahangaisho mengine ya afya ya umma. Mtukio wao ni mkubwa na madhara yao ni yenye kuenea sana kama matatizo mengine yahangaikiwayo sana kuhusiana na afya na rasilmali za umma.” Visa vya sasa vya kujiua ni hesabu kubwa sana iliyo asilimia 31 kati ya vifo vyote vitokanavyo na magonjwa, na hiyo ni asilimia tatu juu kuliko kadiri ya vifo visababishwavyo na aksidenti za barabarani.