Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 9/22 kur. 9-12
  • Siku za Ushetani Zimehesabiwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Siku za Ushetani Zimehesabiwa
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Siku za ile Dunia-Paradiso Zitakuwa Bila Hesabu!
  • Je, Ni Mambo Mema Mno Yasiweze Kuwa Kweli?
  • Watawala Katika Makao ya Roho
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Mungu Ana Kusudi Gani kwa Dunia
    Biblia Inafundisha Nini Hasa?
  • Uasi Katika Makao ya Roho
    Roho za Wafu—Je! Zaweza Kukusaidia au Kukuumiza? Je Ziko Kweli?
  • Ishi Milele Juu ya Dunia-paradiso
    Ni Nini Lililo Kusudi la Uhai?
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 9/22 kur. 9-12

Siku za Ushetani Zimehesabiwa

YEHOVA MUNGU aliumba Adamu na Hawa, akawaweka katika bustani-paradiso, akawaambia waongezeke na kujaza dunia kwa wazao waadilifu. Walipaswa kuitunza bustani, kuisitawisha na kuidumisha, na kuishi milele, yote hayo kwa sharti lile moja rahisi: ‘Hampaswi kula kutokana na mti fulani katikati ya bustani. Mkila kutokana nao, mtakufa.’—Mwanzo 1:27, 28; 2:8, 9, 15-17; Isaya 45:18.

Malaika mwenye uweza aliasi dhidi ya Mungu akawa Shetani, kumaanisha “Mpingaji,” kwa sababu alitaka kubamba udhibiti wa mambo. Alitaka kujipatia ibada ya jamii ya kibinadamu. Alimshawishi Hawa kula lile tunda lililokatazwa, akidai kwamba lilikuwa jema kwa chakula na kwamba hangekufa bali angekuwa kama Mungu, awezaye kujiamulia lililo jema na lililo baya. Uamuzi wake wa kwanza ulikuwa mbaya; aliamua kwamba kula lile tunda lililokatazwa kungekuwa kwema. Hawa alikula, akampa Adamu sehemu fulani ya tunda hilo naye akala, na wote wawili wakafa hatimaye. Hivyo Adamu alileta dhambi na kifo juu ya wazao wao, ambao wamekuwa wakifa tangu hapo. (Mwanzo 3:1-6; Warumi 5:12) Watu wawili wa kwanza wa kibinadamu walichagua kumfuata Shetani wakawa waongofu wa kwanza kwenye ibada ya Shetani. Hadi leo hii, mamilioni wameamua kwamba dini ya wazazi hao wa kwanza ilikuwa na ni njema kuwatosha. “Ikiwa mnafuliza kujitoa nyinyi wenyewe kwa yeyote kuwa watumwa ili kumtii yeye, nyinyi ni watumwa wake kwa sababu mwamtii yeye.”—Warumi 6:16, NW; Yohana 17:15, 16; 1 Yohana 5:19.

Yehova alitangaza kwamba Shetani angeangamizwa hatimaye, lakini alimruhusu aendelee kwa muda. Hii ingempa Shetani fursa ya kuthibitisha dai fulani alilotoa, kwamba Mungu hangeweza kuweka duniani wanadamu ambao wangethibitika kuwa waaminifu Kwake chini ya mtihani—dai lililoonyeshwa kwa njia ya kutazamisha sana na kujibiwa kwa kuutetea upande wa Yehova wa lile suala katika sura mbili za kwanza za kitabu cha Biblia cha Ayubu. Akiwa chini ya mashambulio makatili na maovu sana kutoka kwa Shetani, Ayubu mwenyewe alichagua kushika uaminifu-maadili kwa Mungu, hivyo akithibitisha Shetani kuwa mwongo. (Mwanzo 3:15; Kutoka 9:16; Ayubu 42:7) Waebrania sura 11 yarekodi pia orodha ndefu ya Mashahidi waliojipanga upande wa Yehova wa lile suala la enzi kuu ya ulimwengu wote mzima.

Kristo Yesu ndiye mtu wa kutokeza ambaye kwa wakati wote aliandaa jibu kamili kwa kutetea upande wa Yehova wa lile suala kubwa la enzi kuu ya ulimwengu wote mzima na uaminifu-maadili wa kibinadamu kwa Mungu. Huu ulikuwa ushinde kabisa kwa Shetani. Yesu alikataa toleo la Shetani la kumpa utawala juu ya ulimwengu mzima kwa kubadilishana na tendo moja tu la ibada kwa Shetani. Pia Yesu bila kuyumbayumba alivumilia mateso ya ajabu alipokuwa akifa juu ya mti wa mateso. Alishinda Shetani na ulimwengu wa Shetani pia, akituandalia kiolezo kikamilifu cha kufuata.—Mathayo 4:8-10; 27:50; Yohana 16:33; Waebrania 5:7-10; 1 Petro 2:21.

Kwa sababu ya nyakati za mabaya ambamo tunaishi, huenda ikaonekana kama kwamba Shetani anazidi kuwa na nguvu kuliko wakati mwingineo na kwamba Ushetani wenyewe waongezeka. Hata hivyo, kitabu cha Biblia cha Ufunuo chaonyesha hali tofauti kabisa kwenye sura 12, mistari 7-9, 12:

“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli [Kristo Yesu] na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”

Siku za ile Dunia-Paradiso Zitakuwa Bila Hesabu!

“Akijua ya kuwa ana wakati mchache tu,” Shetani anahimiza utendaji wake wa kishetani katika “siku za mwisho” hizi. (Yakobo 5:1-3) Hata hivyo siku zetu hizi ngumu zina tumaini. Ufunuo 21:1, 3-5 yafunua ni tumaini gani: “Nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.”

Hivyo, Kristo Yesu atatawala kwa miaka elfu, wakati ambao Yehova atatekeleza kusudi lake la awali la kuumba dunia na kuweka wanadamu juu yayo. (Ufunuo 20:1, 2, 6) Utakumbuka kwamba awali wanadamu walipaswa kuijaza dunia kwa wazao waadilifu, waitunze dunia, watunze mimea na wanyama wayo, waishi katika amani, na kupendana. Utimizo wa ahadi hiyo umeshikiliwa kwa muda ili kumruhusu Shetani ajaribu kuthibitisha dai lake kwamba angeweza kugeuza watu wote kutoka kwa Yehova Mungu. Yeye ametumikisha mabilioni ya watu, lakini ameshindwa kuwafanya hivyo mamilioni fulani ya wenye kushika uaminifu-maadili.—Warumi 6:16.

Katika wakati fulani wa mrudisho, rehema ya Yehova kupitia Kristo Yesu itafika hata ndani ya kaburi kuwapa fursa ya uhai wa milele katika dunia-paradiso mabilioni ambao wamekufa muda wa maelfu ya miaka iliyopita: “Msistaajabie hili, kwa sababu saa inakuja ambayo katika hiyo wote wale waliomo ndani ya makaburi ya ukumbusho watasikia sauti yake na kutoka, wale waliofanya mambo mema kwenye ufufuo wa uhai, wale waliozoea kufanya mambo maovu kwenye ufufuo wa hukumu.”—Yohana 5:28, 29, NW.

Wowote wakataao wakati huo kujipatanisha na mazingira maadilifu ya dunia mpya hiyo hawatabaki wachafue au kuharibu dunia hiyo, mimea na wanyama wayo, amani ya wanadamu, wala ibada ya kweli ya Yehova Mungu. Zaburi 37:10, 11, 29 yahakikisha hili: “Bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani. Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.”

Mika 4:2-4 yaahidi amani na usalama wa kweli: “Mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA litatoka Yerusalemu. Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.”

Hali hii ya amani itaenea pia kuwahusisha wanyama, kama Hosea 2:18 isemavyo: “Nami [Yehova] siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini.” Ezekieli 34:25 yasema pia juu ya agano lisilohusisha kuwapo kwa “wanyama wakali.”

Tena, Isaya 11:6-9 yaahidi amani kati ya wanyama katika Paradiso: “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”

Wasikivu watairithi dunia. Watatunza hewa, maji, na udongo. Chemchemi na vijito vya maji zitalowesha nchi zilizo ukame. Misitu itaivika nguo milima ambayo imekombwa uzuri wayo kwa faida ya ubinafsi. Pori zitasitawi sana na yaliyokuwa majangwa yachanue kama waridi. Vipofu wataona, viziwi watasikia, vilema watatembea, na mabubu wataongea. (Isaya 35:1-7) Kuthamini milima na mabonde ya Yehova yenye fahari na miambao yake yenye kupakana na bahari na bahari kuu zenye kuumusha mawimbi hakutairuhusu kamwe pupa ya kibinadamu itokee tena kuiharibu dunia. Litakuwa jambo rahisi, la kiasili, kwa wanadamu wakamilifu, waliojawa na matunda ya roho ya Yehova, kila mmoja, kufurahia kupenda jirani yake kama yeye mwenyewe, na juu ya yote kumpenda Yehova kwa moyo, nafsi, akili, na nguvu zake zote. Ndiyo, wanadamu wote watazaa lile tunda la kiroho la “upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, upole, kujidhibiti.”—Wagalatia 5:22, 23, NW.

Je, Ni Mambo Mema Mno Yasiweze Kuwa Kweli?

Kufikia sasa huenda ikawa wasomaji fulani wanasema, ‘Yote hayo yasikika kuwa mema mno yasiweze kuwa kweli.’ Lakini, sivyo, hali zilizoko sasa ni mbaya mno kuendelea. Tumo katika zile iziitazo Biblia “siku za mwisho.” Tazama kukuzunguka, nawe waweza kuona ndivyo ilivyo. “Siku za mwisho,” lasema Neno la Mungu, “kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao. Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.”—2 Timotheo 3:1-5, 13.

Hata yajapokuwako maelezo dhahiri haya juu ya nyakati zetu, bado wengi watadhihaki. Hilo pia ni la kutarajiwa. Dhihaka yao yenyewe ni kisehemu cha uthibitisho wa kwamba tumo katika siku za mwisho: “Siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. . . . Mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. . . . Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.”—2 Petro 3:3, 4, 7, 13.

Yehova aahidi kwamba, katika ulimwengu wake mpya wa uadilifu, mfumo mwovu huu wa zamani wa ulimwengu wa Shetani hata hautakumbukwa: “Tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo.” (Isaya 65:17, 18) Siku za Ushetani zimehesabiwa, na katika wakati wake Mungu, Shetani mwenyewe ataharibiwa milele.—Ufunuo 20:1-3, 7-10.

Kwa kweli, hali zilizobarikiwa zipasazo kuja katika dunia-Paradiso si njema mno zisiweze kuwa kweli; Yehova huziona hali zilizopo za mfumo huu wa zamani chini ya Shetani kuwa mbaya mno zisiweze kubaki.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Hali zilizobarikiwa zipasazo kuja katika dunia-Paradiso si njema mno zisiweze kuwa kweli

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki