Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 9/22 kur. 16-19
  • Tamasha ya Maua-Mwitu ya Australia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tamasha ya Maua-Mwitu ya Australia
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maua, Yasiyo na Kifani na ya Namnanamna
  • Biashara Huchanua Pia
  • Yafuate Mapito Yaendayo Kwenye Maua-Mwitu
  • Ebu Sasa Tuelekee Kaskazini
  • Je, Ni Maua ya Mwituni au Magugu?
    Amkeni!—2005
  • Je, Mna Kipepeo-Madoido Katika Shamba Lenu?
    Amkeni!—1995
  • Kutafuta Okidi Katika Ulaya
    Amkeni!—1995
  • Mfumo Tata wa Viumbe
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 9/22 kur. 16-19

Tamasha ya Maua-Mwitu ya Australia

NA MLETA-HABARI ZA “AMKENI!” KATIKA AUSTRALIA

Kila mwaka kuanzia Agosti hadi Novemba—wakati wa masika katika Kizio cha Kusini—maelfu ya wageni, kutia na wataalamu-mimea na wanasayansi wengine, humiminikia mkoa wa Magharibi mwa Australia. Basi za utalii hufanya kazi sehemu ya kati ya kusini-magharibi na kaskazini. Magari-moshi ya pekee yaliyojaa watazama-mandhari husafiri polepole kuingia vitongojini. Wakaaji wengi wa hapa husafiri sehemu za mashambani pia. Ni nini huleta miminiko hilo la ghafula la watalii? Ni ule wakati wa kutazama maua-mwitu Magharibi mwa Australia—tamasha kwelikweli ya maua-mwitu!

HAPA moja la maonyesho yaliyo ya kuvutia zaidi ulimwenguni ya maua asili laweza kuonwa katika mazingira yayo ya asili, na kwa miezi mitatu maeneo makubwa ya nchi huwaka uzuri wa maua-mwitu ya kienyeji. Kwa kweli, onyesho hili limepandishwa hadhi katika vyombo vya habari kuwa “mojapo tamasha zilizo maarufu zaidi za maua-mwitu ulimwenguni.” Kwa nini mkao wa tamasha hii ni tofauti na nchi nyingineyo yote?

Maua, Yasiyo na Kifani na ya Namnanamna

Sababu moja ni kwamba bahari kuu na bahari za kawaida zimetenganisha kontinenti ya Australia na kontinenti nyinginezo. Labda mkao huu usio na kifani ndiyo sababu ya wataalamu-mimea wengi kusadiki kwamba kontinenti hii ya kisiwa kikubwa ina maua ya unamnanamna mwingi zaidi ulimwenguni. Hakuna mahali pengine ambapo unamnanamna huu usio na kifani huonekana wazi kuliko Magharibi mwa Australia, ambapo nchi huvuvumka maua yachanuayo umaridadi wa kuteremesha sana wakati wa masika.

Magharibi mwa Australia ndilo jimbo kubwa zaidi la kontinenti. Lina eneo la kilometa za mraba milioni 2.5—kubwa kama Ulaya Magharibi na zaidi ya mara tatu ukubwa wa Texas, Marekani. Tokeo ni kwamba, lina unamnanamna mwingi wa mandhari na tabia-nchi. Baada ya mvua nzuri za wakati wa baridi, huchipuza aina-aina za maua yanayoanzia adesi-jangwa ya Sturt iliyo ya kibahameli na iliyotakata, hadi lile ua la dumu-daima la msambao.

Yaliyo mengi ya maua-mwitu huchanua Agosti na Septemba. Hata hivyo, spishi fulani huhitaji ujotojoto ili zikue na hazichanui mpaka Oktoba au Novemba. Spishi nyingi ajabu kufikia 8,000 zajulikana kutokea jimboni. Spishi ni nyingi kuanzia mmojapo miti mikubwa zaidi ya mbao ngumu, ule wa karri, hadi mmea-kimelea ulio mdogo zaidi, Pilostyles. Unamnanamna huo watia ndani pia okidi ambayo ndiyo ya pekee ulimwenguni kwa kutambaa kikamili chini ya ardhi, Rhizanthella gardneri. Halafu kuna baadhi ya maua ya samawati ya utakato safi kabisa—moja liitwalo Lechenaultia biloba, na jingine liitwalo Dampiera, lililopewa jina kulingana na haramia wa baharini William Dampier. Pia kuna mimea myeusi kadhaa ichanuayo maua kama lile la kiguu-kangaruu-cheusi. Spishi mpya zinaendelea kupatikana—tena kwa wingi sana hivi kwamba mtaalamu-mimea mmoja mwenye msisimko alitoa dokezo la kupita kiasi kwamba huenda ikawezekana kupata spishi mpya kila siku!

Biashara Huchanua Pia

Haishangazi kwamba biashara ya maua-mwitu imekua ikachanua wakati wa tamasha hii ya kila mwaka. Angalau misherehekeo 14 ya maua-mwitu hufanywa kila mwaka. Watalii hutembezwa safari za miguu, wakulima-mifugo hufungua nyanja zao za ndanindani zitazamwe na wageni, watengeneza-johari hutengeneza maumbo ya maua-mwitu, na wachoraji huchora mimea watayarishapo vielezi vya vitabu vitakavyochapishwa karibuni. Pia biashara hiyo hufanya mipango kuuza katika soko la kimataifa maua-mwitu yaliyochumwa. Lakini yaweza kuwekwaje yakiwa mabichi-mabichi?

Mbinu ya pekee imesitawishwa kudumisha muundo na mnukio asili wa maua-mwitu. Mbinu hiyo yahusisha umajimaji wa siri upunguzao mwendo wa kukua na kuoza kwa maua hayo. Hii huwezesha wafanyakazi kuyachuma maua-mwitu kabla tu ya maua kuchipuza vitumba kisha kuyasafirisha ng’ambo ambako ule umajimaji utumiwao kabla ya mavuno hupunguziwa nguvu kwa kuchovya majini maua hayo ya kukatwa, hivyo kuyawezesha yaanze tena kuendelea kuchipuka.

Ingawa ni kweli kwamba huenda biashara ikawa inachipuka, si kila mtu afurahiaye wakati wa maua-mwitu. Kwa kielelezo, wasumbuliwao na mafua ya ungamaua huenda wasitazamie miezi hii kwa kuwa wao hupiga chafya vibaya hadi kiangazi. Nyakati nyingine, pia, ile chavuo hutokeza mambo ya ajabu. Fikiria lililotendeka 1992. Baada ya mvua nzito na halijoto za kadiri ndogo, wakaaji katika miji fulani waligutuka kunyeshewa na miminiko la mvua ya manjano nyangavu. Ilifunika magari, ikajaa kando za barabara kama kwamba ni zulia, na kuanguka kandokando ya mitaro. Mvua hii ya manjano ilitambulishwa na wajuzi wa mazingira kuwa chavuo ya maua-mwitu. Yaonekana ile mvua ya chavuo ilikuwa imevuma kuingia kutoka maua-mwitu yenye kuchipuka magharibi-kati. Hata hivyo, yajapokuwa magumu haya, walio wengi watakubali kwamba uzuri na manufaa za ile tamasha ya kila mwaka ni nyingi kuliko masumbufu yayo.

Yafuate Mapito Yaendayo Kwenye Maua-Mwitu

Andamana nasi sasa katika utalii wa kuvumbua maua-mwitu. Pito la kwanza la maua-mwitu latupeleka kusini mwa jiji kuu la jimbo hili, Perth, hadi Mbuga ya Kitaifa ya Serpentine. Mbuga hiyo iko kwenye uwanda wa juu wa bondeni nayo ina vilima kwelikweli. Mto wayo, utiririkao kupitia mivo iliyoinama na sehemu zilizochongoka sana za graniti, humwagika hatimaye kwenye poromoko la maji la meta 15. Kangaruu na vikangaruu hulisha kati ya miti jarra na wanduu, huku ndege wapiga-mluzi wa kidhahabu, reni wa kuvutia sana, na midomo-miba wakicheza dansi ya pamoja katika vichaka vitambaaji. Vidimbwi vya miambani vina mimea ipendayo utopetope na vina okidi maridadi za samawati, na hapo karibu pana hadasi-asali za graniti za urujuani-kijivu zilizojitanda kama manyoya ya bata, pakiwa na vitungamano vya trimaliamu ndogo za manjano-kijivu na michanganyiko ya kuvutia ajabu ya kalitriksi ya urujuani na andasonia ya samawati.

Sasa twasonga mbele kusini zaidi kwenye mahali ambapo labda ndipo papendwapo zaidi kwa maua-mwitu—Mbuga ya Kitaifa ya Masafa ya Stirling. Masafa haya ya kilometa za mraba 1,150 huinuka ghafula hadi Bluff Knoll, kilele cha juu zaidi, kifikacho meta 1,077 juu ya usawa wa bahari. Tabia-nchi (hali ya hewa) hapa yatofautiana na wilaya inayozunguka. Tokeo ni kwamba, zaidi ya spishi 1,500 za mimea ichanuayo hupatikana kiasili hapa, na 60 kati yazo hupatikana eneo hili tu. Halafu, tunapopanda Kilele cha Toolbrunup twaona mandhari nzuri ajabu na mimea ya namna mbalimbali. Kati ya iliyo mizuri zaidi ni Midarwinia, au kengele za milimani. Spishi kumi zimetambuliwa mbugani kufikia sasa, na ni moja tu kati yazo ijulikanayo kuwa hukua nje ya Masafa ya Stirling. Katika Septemba na Oktoba ile kengele-uvuli nzuri hupatikana kwa urahisi katika miitu iliyoshikamana, hali kule juu zaidi miinamoni hukua ile kengele nyekundu-nyeupe ya milimani. Pia twagundua ua la okidi-buibui la kijani lililo haba na kuona kwamba kuna spishi 23 Magharibi mwa Australia.

Kwa kuwa tuko karibu, twaamua kufuata njia ya mkato kwenda Mbuga ya Kitaifa ya Torndirrup. Hapa nchi ya piti (mimea-miozi) yavutia sana. Twauchungulia Banksia praemorsa wenye maua ya rangi nyingi isivyo kawaida ya kahawia—na ebu tazama! Yule pale oposamu-asali mwenye ukubwa wa panya akijilisha baadhi ya maua-mwitu. Hapa, pia, yapo maua-nyundo ya okidi yanayotokeza mnuko mkali wa kujiandaa kama kwamba wao ni manyigu wa kike. Wamvutia nyigu wa kiume thainidi ambaye katika kutafuta mwenzi wa kuingiliana, aichukua mbegu kuipeleka kwenye wa-kike wa haramu. Mapenzi yafanywayo kwa nyigu huyo bila malipo husaidia katika kuchavusha maua mengine.

Ebu Sasa Tuelekee Kaskazini

Tukiisha kuona baadhi ya maeneo makuu ya maua-mwitu kusini mwa Perth, sasa twaelekea kaskazini kulifuata Pito la Maua ya Dumu-Daima—pito litupitishalo katika mbuga kadhaa za kitaifa. Bila shaka maua hayo ya dumu-daima, yaliyo na jina somo kwa safari hii ya utalii, yamechanua kwa maelfu, yakifanya ni kama yanainamisha kichwa kukubaliana na upepo uvumao kuyapita kama kwamba unayapiga papasa za upendo. Twasimama kwenye uwanja wa makaburi ya nchi ambapo maua ya viguu-kangaruu ya kijani na mekundu yapamba mawe ya makaburi ya zamani. Halafu, ile miitu imejaa vichaka-kuni vya banksia, vya wembamba, na kichaka cha Krismasi—ua-kichaka lenye machanuo maangavu ya kidhahabu. Je, wewe umeona okidi za primrozi zikichanua? Ni maridadi wee! Twajivuta kupita vichakani, na ebu tushangae kukiona kichaka cha samawati chenye maua yenye umbo la moshi.

Katika pito hili, kuna spishi 800 zichanuazo maua. Nyingi za spishi za kustaajabisha zaidi zipo kandokando tu ya barabara, zikionekana kutoka kwenye gari letu la mwendesho wa magurudumu manne. Wageni wamesema mara nyingi kwamba baadhi ya maua yaliyo kandokando ya barabara yana rangi zenye upatani sana hivi kwamba ni vigumu kuamini kwamba si mwanadamu aliyeyapanga hivyo. Naam, vifungufungu vya maua ya urujuani umetametao pamoja na vichaka vya manjano vyaonekana na mpangilio mzuri sana, tena vina rangi kemkem za samawati.

Lakini sasa ni wakati wa kuelekea nyumbani. Tumependezwa na kumbukumbu ambazo tumenasa katika kamera zetu; basi, twataka sana kuchuma ua moja au mawili hivi yawe kikumbusho, lakini twakinza kishawishi hicho japo kwa shida. Twakumbuka kwamba umma wakatazwa na sheria kuchuma maua-mwitu, hata yale yakuayo kando ya barabara. Kwa hiyo twaziacha nyuso zilizolala chali za maua hayo zinyunyiziwe na mvua ile nyingine ya masika na kufurahiwa na mvutiwa atakayefuata. Naam, tumejionea mojapo maonyesho ya kuvutia zaidi duniani ya maua. Na mandhari hiyo ibadilikapo kuwa kiangazi kiangavu, twatazamia kwa raha kuhudhuria onyesho hilohilo mwaka ufuatao, tena kwa miaka mingi ijayo.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Picha zote: Kwa Hisani ya West Australian Tourist Commission

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki